Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Yeremia 9, 10 & 26)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com
kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Endapo wewe ni
mzazi wa watoto ambao kwa sasa ni watu wazima, je, kuna kipindi ambacho hukujua
ufanye nini ili kuwasaidia watoto wako? Mimi nilipitia nyakati hizo. Endapo
wewe ni kiongozi wa kanisa, je, kuna nyakati ambazo hujui ufanye nini ili
kutatua matatizo ya kanisa? Hata nilipokuwa mtoto mdogo, kuna mitafaruku ambayo
sikuweza kuisuluhisha katika familia yangu. Je, tunafanya nini katika hali kama
hizo? Jibu la kwanza ni kumgeukia Mungu kwa ajili ya kuomba msaada! Lakini, je,
Mungu anakabiliana na hali kama hizo ambapo hawezi kutatua tatizo kwa kuwa
anatupatia uhuru wa kufanya uchaguzi? Yeremia anaendeleza maonyo yake kwa watu
wa Mungu katika somo letu la juma hili, lakini katika maonyo yake tunapata
mwangaza wa namna ya kutatua matatizo yanayoonekana kutowezekana kutatuliwa.
Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!
I.
Mkanganyiko
A.
Soma Yeremia 9:1. Je, umewahi kuangalia chemchemi
iliyotengenezwa kwa ajili ya umma na kufikiria kwamba pengine ingetengenezwa
ili ifanane na kichwa chako? (Kamwe sijawahi kufikiria hivyo! Lakini, Yeremia
anatafakari hivyo.)
1.
Kwa nini Yeremia anakuwa na mawazo hayo yasiyo ya
kawaida? (Amesikitika sana kutokana na watu waliokufa kwa sababu hawakulifuata
neno la Mungu. Chemchemi zina maji mengi sana, na anatumia ishara hii (fikiria
somo la juma lililopita) kuonesha jinsi ambavyo angependa kulia kutokana na huu
upotevu mkubwa.)
A.
Soma Yeremia 9:2. Yeremia ana mawazo gani mengine
kuwahusu watu wake? (Angependa kuwapeleka jangwani na kuwaacha huko!)
1.
Je, jambo hili linaonekana kutokuwa na mwelekeo kidogo
kwako? Kwa upande mmoja Yeremia anawalilia watu wake, na kwa upande mwingine
angependa kuwatelekeza watu wake jangwani. Je, umewahi kuwa na mawazo kama hayo
kwa watu unaowafahamu?
A.
Soma Yeremia 9:3. Yeremia analalamika kwamba watu
wanasema uongo, wanajiingiza kwenye dhambi za aina mbalimbali, na hawamkiri
Mungu. Endapo hawa wangekuwa watoto wako, je, ungewalilia na pia kutaka
kuwaacha jangwani?
I.
Suluhisho la Mungu
A.
Soma Yeremia 9:7. Suluhisho la Mungu kwa ajili ya watu
hawa ni lipi? Nilikuuliza ungekuwa na mwitiko gani endapo watoto wako wangekuwa
kama watu ambao Yeremia amewaelezea? (Nikiwa kama mzazi, nimekuwa nikishindwa
kutambua jambo sahihi la kufanya katika baadhi ya nyakati. Ninaupenda ukweli
ambapo Mungu anasema, “Nitende nini kwa ajili yao?” Anachokifanya Mungu ni
“kuwayeyusha na kuwajaribu.”)
1.
Unadhani inamaanisha nini “kuwayeyusha na kuwajaribu”
watu? (Mungu anawaletea watu mambo magumu/machungu.)
1.
Hii inahusikaje kwa kwatoto wako? (Katika nyakati
fulani, tunatakiwa kuwaacha watoto wetu wapitie uzoefu wa matokeo ya maamuzi
yao mabaya – na kumwomba Mungu kwamba athari zisiwe za moja kwa moja (za siku
zote).)
A.
Soma Yeremia 9:23-24. Mungu ana lengo gani kwa ajili ya
watu wake? (Watajivuna kutokana na kumjua na kumwelewa Mungu, na sio kujivuna
kutokana na kuwa werevu, matajiri au kuwa na nguvu.)
1.
Jambo hili linanipa wasiwasi kidogo. Unawezaje kujivuna
kwamba unamjua na kumfahamu Mungu? Je, umewasikia watu wanaodai kuzungumza kwa
niaba ya Mungu na ukadhani kuwa, “Hivyo sivyo ambavyo ninamfahamu Mungu?” Je,
wanadamu hawana uwezo wa kutosha kuyafahamu mawazo ya Mungu? (Nadhani jibu
linapatikana kwenye fungu. Tunajivunia wema, utendaji haki na unyofu wa Mungu.
Hii ni tofauti na kudai kwa kiburi kufahamu kwa mahsusi jinsi Mungu
anavyofikiri.)
1.
Tunawezaje kutumia maelekezo haya kutatua matatizo
katika familia zetu na kanisani kwetu? (Tunaweza tusifahamu cha kufanya
(tofauti na kuomba), lakini, tukiwa kama wawakilishi wa Mungu, tunaweza kuwa na
uhakika wa kumwakilisha Mungu kwa kuwa wema, watenda haki na wanyofu.)
I.
Mungu Wetu wa Hali ya Juu
A.
Soma Yeremia 10:1-2. “Ishara za mbinguni”
zilizowaogofya watu ni zipi?
A.
Soma Yeremia 10:3-5. Je, ni upumbavu kiasi gani kuabudu
sanamu? (Ni upumbavu mkubwa sana. Mungu anasema uliitengeneza, haiwezi kusimama
wima, wala kutembea au kuzungumza. Kwa nini utarajiwe kulindwa na kitu ambacho
hakiwezi kujilinda chenyewe?)
1.
Angalia maneno ya mwisho ya fungu la 5: “Hawawezi
kutenda uovu wala hawana uwezo wa kutenda mema.” Je, umewahi kusikia kwamba
baadhi ya watu wanaogopa laana ya sanamu? (Mungu anasema kuwa hupaswi na wala
huna cha kuogopa.)
1.
Jambo gani linafanana na hilo katika zama za sasa? Kama
nilivyokwishabainisha hapo awali, hakuna mtu hata mmoja ninayemfahamu anayekata
mti, kuuchonga na kisha kuuabudu. (Mantiki ya Mungu ni kubwa kuliko kitu
chochote kilichotengenezwa na wanadamu. Ukiwa unakitegemea kitu
kilichotengenezwa na mwanadamu mwenzako, tofauti na kumtegemea Mungu, basi upo
kwenye tatizo lile lile la kimantiki.)
A.
Soma Yeremia 10:6-7. Nani anayefanana na Mungu? (Hakuna
mtu hata mmoja.)
1.
Je, Mungu anastahili kuabudiwa nasi? (Ndiyo! “Hii ni
stahili yako.” Watu wasiomwamini Mungu ni wapumbavu. Wanamnyima Mungu kile
anachokistahili.)
A.
Bila shaka yote ambayo tumekwishayajadili hivi punde
katika maswali haya machache ni dhahiri kwako. Kwa nini Yeremia anaandika
kuyahusu? (Kwa sababu hayako dhahiri kwa watu wa Mungu. Wanaitegemea miti
pamoja na vitu vingine walivyovitengeneza.)
1.
Je, hii inaashiria nini kwetu kuhusu ugumu wa kutatua
matatizo katika familia zetu na katika makanisa yetu? (Watu wengine hawana
akili. Jibu liko wazi kuhusu kuabudu mti. Ndio maana jibu la matatizo mengi
katika familia na kanisani pia liko dhahiri, lakini Mungu pamoja na Yeremia
wanatakiwa kushughulika na watu wasioweza kuona mambo yaliyo bayana – vivyo
hivyo kwetu pia.)
a.
Tunapaswa kufanya nini katika hali zilizo dhahiri
kabisa kama hizi? (Soma Yeremia 10:22. Tunatakiwa kuomba ili Mungu “arekebishe”
hali.)
I.
Hatari
A.
Soma Yeremia 26:1-3. Matumaini ya Mungu ni yapi?
(Kwamba watu watakaposikia kile anachowaambia Yeremia kwa niaba ya Mungu,
watageuka na kuuacha uovu wao.)
A.
Soma Yeremia 26:4-6. Mungu anawapatia watu uchaguzi.
Achana na dhambi nawe utaokolewa dhidi ya janga, au endelea kutenda dhambi ili
uwe mfano. Je, unadhani utafanya nini endapo utakabiliana na hizo chaguzo
zilizo bayana kabisa?
A.
Soma Yeremia 26:7-8. Je, ni uchaguzi gani wa tatu ambao
watu waliuchagua? (Kumnyamazisha Yeremia kwa kumuua.)
1.
Hebu turejee mjadala wetu juu ya kutafuta suluhu ya tatizo
katika familia au kanisani. Je, mara zote mambo yanakuendea barabara? (Kwa
dhahiri, hapana, kama jinsi Yeremia anavyoonesha. Lakini, unatakiwa kuwa na
uhakika kwamba unazungumza kwa ajili ya Mungu (unamzungumzia Mungu).)
A.
Soma Yeremia 26:9. Je, ungejisikiaje endapo ungekuwa
Yeremia – watu wanakuzunguka huku wakipiga kelele kwamba unapaswa kufa?
A.
Soma Yeremia 26:10-11. Mashtaka gani yanatolewa dhidi
ya Yeremia yanayomfanya astahili kufa? (Alisema mambo mabaya kuhusu mustakabali
wa Yerusalemu.)
1.
Unaichukuliaje mantiki ya mashtaka hayo? (Suala sio
kusema ukweli, bali suala ni endapo ninafadhaishwa na kile unachokisema. Tunalo
tatizo hili katika zama za sasa. Kiukweli watu hawaujali ukweli, kwa sababu
ukweli ni chochote kile unachokiamini kuwa ni kweli. Badala yake, suala
lililopo ni endapo mtu anafadhaishwa kwa kile unachokisema.)
A.
Soma Yeremia 26:12-15. Je, Yeremia anaonekana kuogopa?
(Anazungumza kwa ujasiri!)
A.
Soma Yeremia 26:16. Je, kitendo hiki kinakutia hamasa?
(Inaonekana kwamba watu hawa hawakuwa na matumaini yoyote. Lakini, Yeremia
anazungumza kwa ujasiri na watu wanaguswa dhambi zao. Bila shaka Roho Mtakatifu
yupo kazini.)
A.
Rafiki, tunapokabiliana na matatizo ambayo hatujui
namna ya kuyatatua, tunapaswa kumgeukia Mungu kwa ajili ya kupata suluhisho. Mungu
anatuambia kwamba katikati ya matatizo tunaweza kuwaambia watu wengine kuwa
yeye ni mwema na mwenye kutenda haki! Je, utayageuzia matatizo yako kwa Mungu?
I. Juma lijalo: Uongofu wa Yosia.
No comments:
Post a Comment