Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Mwanzo 4, Hesabu 21, Yeremia
13)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com
kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, umeitafakari
njia ambayo Mungu anaitumia kwa kutumia ishara? Mfumo wa huduma ya patakatifu
katika Agano la Kale lote ni ishara ya kile ambacho Yesu atatutendea. Kumwita Yesu
“Mwana-kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu” hututafakarisha ishara
ya kafara ya kondoo kwa ajili ya dhambi zetu. Juma lililopita tulianza kujadili
kwamba Mungu alimfundisha Yeremia kutumia ishara katika mafundisho yake kuhusu
kile ambacho Mungu alitaka watu wajifunze. Juma hili tutazama zaidi katika somo
hilo. Hebu tuone mambo mapya tunayoweza kujifunza kutoka kwenye Biblia na
ishara!
I.
Matunda na Nyoka
A.
Soma Mwanzo 4:1-2. Katika uhusiano wa hawa ndugu
wawili, unadhani kuna umuhimu gani wa Kaini kuwa mzaliwa wa kwanza? (Kwa yeye
kuwa mkubwa, huenda Habili angekuwa akimwangalia Kaini na kufuata nyayo zake. Bila
shaka ndio maana wazazi wa Kaini walimwonesha upendo mkubwa.)
1.
Unazipa umuhimu gani kazi zilizochaguliwa na
hawa vijana wawili? (Mwanzo 3:17-19 inatuambia Mungu aliwaelekeza wanadamu
kutenda jambo kama ambalo Kaini alikuwa akilifanya.)
a.
Lengo la kazi ya Habili lilikuwa ni lipi? (Sio
kutengeneza chakula. Ilikuwa ni hadi baada ya gharika ndipo wanadamu waliambiwa
kuwa wanaweza kula nyama (Mwanzo 9:1-3). Habili alifuga wanyama kwa ajili ya
kutengeneza mavazi ya kujivika (Mwanzo 3:21) na kwa ajili ya kutoa sadaka
(Mwanzo 4:4).)
A.
Soma Mwanzo 4:3-5. Endapo ungekuwa Kaini, ni
sababu gani zitakufanya ulete mazao kama sadaka? (Yanaakisi kile unachokifanya!
Inawezaje kuwa sadaka ikiwa haiakisi juhudi zako kubwa?)
1.
Kwa nini Mungu hakubali juhudi za dhati za Kaini
zinazowakilisha kazi yake? (Sadaka “hazikumhusu Kaini,” bali zilikuwa zinahusu
ishara ya Mungu. Ishara za tunda na Yesu kusulubiwa kwa ajili ya dhambi zetu
hazifanani (hazikaribiani) na kifo cha kondoo.)
A.
Soma Mwanzo 4:6-7. Je, Mungu alikuwa wazi kuhusu
maelekezo yake kwa Kaini? (Hii inathibitisha kuwa Mungu alimwambia “kutenda
kilicho chema,” lakini Kaini alitenda kile alichodhani ni sahihi.)
1.
Tunajifunza nini katika jambo hilo? (Tunaweza
kuwa na sababu zenye mantiki kwa kile tunachokitenda, lakini katika mfano huu
tunaweza kuona kwamba uelewa wa Mungu wa “taswira pana” inamaanisha kuwa
tunatakiwa kumtumaini Mungu na kumstahi.)
A.
Soma Hesabu 21:1-3. Mungu ni wa muhimu kiasi
gani katika ushindi wa watu wake? (Walikuwa wanaendelea kushindwa hadi Mungu
alipoingilia kati kwa ajili yao.)
A.
Soma Hesabu 21:4-5. Kutokana na kile
kilichotokea hivi punde, unaweza kuelezeaje tabia na mtazamo wa watu wa Mungu?
(Ni waasi. Walipoteza imani kwa Mungu. Hawana shukrani.)
A.
Soma Hesabu 21:6-7. Kwa nini Mungu aliwatuma
nyoka?
A.
Soma Hesabu 21:8-9. Je, ishara hii ina mantiki
yoyote? Nyoka ilikuwa sura ya dhambi ya asili (Mwanzo 3:1-4), na sasa nyoka
wanawaua! Kwa nini asimweke kondoo mtini na kuwaambia watu wamwangalie? (Tatizo
ni kwamba, kama ilivyokuwa kwa Kaini, walikuwa hawakabiliani na dhambi zao kwa
kuiangalia nyoka, waliziangalia dhambi zao. Ili dhambi zetu ziweze kusamehewa,
tunatakiwa kuzikiri na kuomba msamaha. Ishara ya kondoo, na kwa kiasi kidogo,
ishara ya nyoka, zilionesha kwamba tunatakiwa kuwa na imani kwa yale
yanayotendwa na Mungu.)
1.
Watu wanatakiwa kufanya nini na hii nyoka ya
shaba? (Wanatakiwa “kuiangalia.”)
A.
Hatimaye watu wa Mungu sio tu kwamba waliitunza
hii nyoka ya shaba, bali pia waliipa jina la “Nehushtani.” Soma 2 Wafalme 18:4
ili uone kile ambacho Mfalme Hezekia alimtendea Nehushtani na kwa nini alifanya
hivyo?
1.
Watu walikuwa wanaifanyia nini Nehushtani?
(Walikuwa wanaiabudu kwa kuifukizia uvumba.)
1.
Kuna fundisho gani katika ishara na ibada?
(Mungu aliwaambia waiangalie na kupata fundisho. Watu walikwenda mbali zaidi na
kuanza kuiabudu nyoka ya shaba. (Ishara ya kitendo hicho ni kuabudu dhambi!)
Hakuna ubaya wowote kwa ishara zinazotukumbusha mapenzi ya Mungu, tatizo ni
pale tunapoanza kuziabudu. Angalia Kutoka 20:3-6.)
I.
Mkanda
A.
Soma Yeremia 13:1-2. Nimejifunza kwamba mara
kadhaa kitani kilikuwa kinatumika kama fedha katika Misri ya kale. Mithali 31:22
inatuambia kwamba mke mwema huvaa “mavazi ya kitani safi na urujuani.” Kutokana
na maelezo haya, unadhani kwa nini Mungu alimwambia Yeremia anunue mshipi wa
kitani? (Nadhani kilikuwa ni kitu ambacho alijivunia kukivaa. Ulikuwa ni mtindo
wa kale wa uvaaji wake.)
1.
Kwa nini hakutakiwa kuutia majini? (Baadhi ya maoni
ya watu yanabainisha kuwa hii inawakilisha upungufu wa jumla wa usafi wa kiroho
wa watu. Angalao baadhi ya watu (na ninakubaliana nao) wanasema kuwa maji yalikuwa
yanahusika katika kuhafifisha (kuharibu) mkanda wenye kupendeza. Endapo ungeoshwa
ungeharibu umbo lake na kuhafifisha mwonekano wake.)
A.
Soma Yeremia 13:3-5. Je, mkanda una matumizi
yoyote kwa Yeremia sasa?
1.
Je, unaweza kuwa na manufaa? (Ikiwa unafichwa,
hii inaashiria kuwa Yeremia ataweza kuutunza na kuutumia katika siku zijazo.)
1.
Kuna mjadala unaoendelea kuhusu tafsiri ya neno ”Frati
(Perath)” (kwa mujibu wa tafsiri ya Biblia ya Kiingereza ya NIV) na “Frati (Euphrates)” kwa mujibu
wa tafsiri nyinginezo. Mojawapo ya tatizo la kutafsiri neno hili kama “Frati
(Euphrates)” ni kwamba Frati (Euphrates) ipo umbali wa maili 200, na safari
kama hiyo inaonekana kutoendana na kile anachokisema Mungu.)
A.
Soma Yeremia 13:6-7. Sina uhakika ni kwa jinsi
gani kuficha mshipi “katika pango la jabali” (Yeremia 14:4) kulimsababisha
Yeremia kuufukia ili kwamba uweze “kuchimbuliwa.” (Yeremia 13:7.) Ikiwa huu ni
ufa uliopo kwenye mwamba pembeni mwa Frati, je, hiyo inaweza kumaanisha jambo
gani? (Mshipi kuloana kwa maji ya mto, au kuloana na kupata uchafu kutoka
shimoni, vyote hivyo havifai kwa mkanda wa Yeremia aupendao sana!)
A.
Soma Yeremia 13:8-10. Jambo gani linakikumba
kiburi chetu tunapozifuata njia zetu wenyewe badala ya kuyafuata maneno ya
Mungu? (Kiburi chetu kinakuwa kama nguo chafu.)
A.
Soma Yeremia 13:11. Utagundua kwamba kuna jambo
jingine la mfano la kujifunza kutoka kwenye mshipi wa kitani. Mungu anasema
kuwa ana malengo gani kwa ajili ya huu mshipi? (Endapo watu wangemfuata Mungu,
badala ya kuifuata miungu yao wenyewe na mawazo yao wenyewe, Mungu “angewashikamanisha”
naye. Wangekuwa karibu na Mungu mkuu wa ulimwengu!)
1.
Mungu ana mtazamo gani dhidi ya watu wake? (Endapo
watu wa Mungu wangekuwa wanamfuata, Mungu angefurahia “sifa na utukufu” na
hadhi yake ingeongezeka. Hii inatia msisitizo kwamba mshipi wa Yeremia ulikuwa
ni kifaa cha nguo ambao aliweza kujivunia!)
1.
Tafakari kile ambacho Mungu anatufundisha. Je,
ni mara ngapi unafanya uamuzi endapo utafuata ushauri wa Mungu kutokana na
jinsi unavyokuathiri wewe, familia yako, au utajiri wako? (Yeremia anawaambia
watu kwa kurudiarudia jinsi ambavyo kumfuata Mungu kutakavyoathiri maisha yao,
lakini nadhani sababu ya msingi kabisa ya kumfuata Mungu ni kwamba ni baraka kwake.
Angalia jinsi tunavyomuwia Mungu kwa kuyaokoa maisha yetu na maisha ya wale
tunaowapenda! Ni heshima na utukufu kwa Mungu pale unapomtii na kumtumaini!)
I.
Divai
A.
Soma Yeremia 13:12. Kuna tatizo gani la dhahiri
katika ujumbe huu? (Kila mtu anafahamu kile unachopaswa kukifanya kuhusu divai.
Ni sawa na kuwaambia watu wasugue meno yao.)
A.
Soma Yeremia 13:13-14. Mungu anatupatia ujumbe
gani katika hii ishara? (Unapokuwa umelewa, unakuwa unapata wakati mgumu
kutafakari jambo unalopaswa kulifanya. Unakuwa umevurugwa akili. Mungu anawaambia
watu wake, ikiwa hamtayasikiliza maneno yangu maisha yatawachanganya zaidi hadi
pale ambapo hamtajua nini cha kufanya. Kitendo hiki kitawaelekeza upotevuni na
kwenye maangamizi.)
A.
Rafiki, je, tumejifunza nini katika hizi ishara?
Tumejifunza kwamba tunapaswa kumtii Mungu, na si mantiki yetu wenyewe ambayo
inakinzana na neno la Mungu. Sio tu kwamba kitendo hicho kitaepusha uangamivu
wetu na wa familia yetu, lakini jambo la muhimu zaidi ni kwamba kitendo hicho
kitampa Mungu utukufu. Je, utadhamiria leo kutia bidii ya kumpa Mungu utukufu
katika kila jambo ulitendalo?
I. Juma lijalo: Mgogoro unaendelea.
No comments:
Post a Comment