JE! UTAUVUMILIA MOTO WA MTU ASIFISHAYE FEDHA?


  Ili  kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo. 1 Petro 1:7. 

1. Dhahabu  husafishwa kwa moto, ili isafishwe na uchafu wote; bali imani iliyosafishwa kwa majaribu, ni ya thamani kuliko dhahabu safi. Basi, na tuyaangalie majaribu kwa njia ya busara. Tusipite ndani yake huku tukiwa tunanung'unika na kuona chuki. Hebu na tusifanye makosa ya kujitoa ndani yake [majaribu]. Katika nyakati za kujaribiwa yatupasa kumshikilia sana Mungu na ahadi zake. 

2. Wengine  wameniambia hivi, "Je! wakati mwingine wewe hukati tamaa unapokuwa chini ya majaribu?" Nami nimewajibu hivi, "Ndiyo, kama kwa kukata tamaa mnamaanisha kuhuzunika au kushushwa moyo." "Je! hukuongea na ye yote juu ya hisia zako?" "La; kuna wakati wa kunyamaza, yaani, wakati wa kuuzuia ulimi kama kwa lijamu, nami niliamua kutosema neno lo lote lenye kuleta mashaka au giza, yaani, kutoleta kivuli cho chote chenye utusitusi kwa wale nilioshirikiana nao. Nimejiambia mwenyewe hivi, Nitavumilia moto wa mtu yule asafishaye fedha; Sitateketezwa kabisa. Nisemapo, basi, itakuwa  juu ya nuru; itakuwa juu ya imani na tumaini kwa Mungu; itakuwa juu ya haki, juu ya utu wema, juu ya upendo wa Kristo Mwokozi wangu; itakuwa juu ya kuyaongoza mawazo ya wengine kuelekea mbinguni na juu ya mambo yale ya mbinguni, juu ya kazi yake Kristo anayofanya huko mbinguni kwa ajili yetu, na juu ya kazi yetu tunayofanya hapa duniani kwa ajili yake. ----- RH, Feb. 11, 1890.  

3. Tanuru  lile la moto usafishao linaondoa uchafu tu. Yule Asafishaye [Kristo] anapoiona sura yake ikiakisiwa [ikiangaza] kikamilifu  ndani yako, atakuondoa katika tanuru hilo. Hutaachwa kuteketezwa wala kuvumilia mateso ya moto huo kwa muda mrefu kuliko ilivyo lazima kwa utakaso wako. Lakini ni jambo la maana kwako kujiweka chini ya njia ile anayokuchagulia yule Asafishaye [Malaki 3:1-3], ili upate kuakisi sura ya Mungu, yaani, ili upate kusafishwa, kutakaswa, na kila waa na doa kuondolewa kwako  ----- lisibakie hata kunyanzi moja katika tabia yako ya Kikristo. Bwana na akusaidie... kuchagua mapenzi na kazi ya Mungu ipate kutimilika ndani yako.... Tazama juu! Yesu wako yu hai. Yesu anakupenda. Yesu anakuhurumia, naye atakupokea pamoja na mzigo wako wa masumbufu na shida kama wewe utakuja kwake na kumtwika mzigo wako. Yeye ameahidi kwamba hatawapungukia kabisa, wala hatawaacha kabisa wale wanaoliweka tumaini lao kwake. ----- Letter 2, 1870.

No comments:

Post a Comment