NENO LA LEO | WAKATI UNAOFAA KUWA KIPOFU NA KIZIWI

Ni nani aliye kipofu, ila mtumishi wangu? au aliye kiziwi, kama mjumbe wangu nimtumaye? Ni nani aliye kipofu, kama yeye aliye na amani [mkamilifu]? naam, kipofu kama mtumishi wa BWANA? Unaona mambo mengi, lakini huyatii moyoni; masikio yake ya wazi, lakini hasikii. Isaya 42:19,20 [KJV].

Ni upofu gani huu? Ni upofu ambao hautayaruhusu macho yetu kutazama sana maovu. Hautayaruhusu macho yetu kutulia juu ya maovu. Hautayashika mambo yale yanayoonekana na kuupoteza umilele katika kumbukumbu zake.... Tunataka kuona ipasavyo, tunataka kuona kama vile aonavyo Mungu; maana Shetani anajaribu daima kuyageuza mambo yale ambayo macho yetu yanayaangalia sana ili tupate kuyaona kwa njia yake aliyoichagua....

Mtumishi wa Mungu aliye hai anaona akiwa na kusudi fulani. Macho hutakaswa na masikio nayo hutakaswa, na wale watakaofumba macho na masikio yao wasiyaangalie maovu watabadilika. Lakini endapo watawasikiliza wale wanaozungumza nao na wanaojaribu kuyaongoza mawazo yao mbali na Mungu na mbali na mambo yao yale ya milele, basi, hapo ndipo fahamu zao zote zitapotolewa kutokana na kile macho yao yanachokiangalia sana. Yesu asema, "Basi... jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru. Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza." Mathayo 6:22,23.

Inaleta tofauti kubwa juu ya kile tunachoilisha mioyo yetu na roho zetu. Tunaweza kuiacha mioyo yetu kutafakari sana hadithi zile za mahaba na ndoto zisizowezekana, je! hayo yatatufanyia nini sisi? Yatatuangamiza, mwili na roho.... Twataka kuwa na nguvu ile itakayotuwezesha kuyafumba macho yetu kwa mandhari [picha] zile zisizokuwa nzuri; zisizotuadilisha tabia zetu, zile ambazo hazitatutakasa na kutufanya kuwa waungwana; na kuziba masikio yetu kwa kila kitu kilichokatazwa katika Neno la Mungu. Anatukataza kuwaza maovu, kusema maovu, na hata kutafakari maovu....

Ndani ya Yesu mimi naona kila kitu kilicho chema, kila kitu kilicho kitakatifu, kila kitu kinachotia moyo na kilicho safi. Basi, kwa nini mimi nipende kuyafumbua macho yangu sana ili kuangalia kila kitu kinachochukiza? Kwa kutazama tunabadilishwa. Na tumtazame Yesu na kuutafakari uzuri wa tabia yake, na kwa kutazama tutabadilishwa tupate kufanana na sura yake.

BWANA AWAPATIE SIKU NJEMA YENYE AMANI NA BARAKA TELE

No comments:

Post a Comment