NENO LA LEO - JE SILAHA ZAKO ZINA UWEZO?

Tafakari: 2Wakorintho 10:3-5
 "Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; maana Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina UWEZO KATIKA MUNGU hata kuangusha Ngome; tukiangusha Mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu;  na tukiteka nyara kila FIKIRA ipate KUMTII Kristo". 

Nakumbuka usemi wa marehemu Baba wa Taifa Mwalimu JK Nyerere, wakati Raisi wa Uganda Idd Amini alipoivamia Tanzania, Baba wa Taifa alisema "Nia tunayo, Sababu tunayo na Uwezo wa kumpiga tunao". Ndipo akatoa Amri ya Kumpiga na Kuivunjilia mbali ngome yake katika nchi yake.

Katika ulimwengu wetu huu uliotekwa na Adui shetani, ni jambo la kawaida kusikia Watu wanajiita ni Wakristo, wengine wanajiita wacha Mungu, wengine wameokoka n.k. Wanauwezo mkubwa hata wa kuimba nyimbo za dini kwa hisia kubwa, lakini jambo la kushangaza, asilimia kubwa unawakuta bado ni watumwa wa yule Adui. 

Mbali na kuonekana watu wema au wacha Mungu machoni pa watu, ndani ya Mawazo yao au Fikira zao, kumejaa Visasi, Uadui, Kutosamehe, Husuda, Wivu. Wakati mawazo, maneno na matendo ya Ngono na Mapenzi yakiendelea kukamata akili za Vijana kwa Wazee, wakipigwa upofu wasione kuwa ni dhambi; Mungu anazidi kutoa wito wa Kushinda vita. 

Wapendwa Ngome kuu za Shetani ziko katika MAWAZO au FIKIRA, huko ndiko zinatakiwa zivunjiliwe mbali, hatimaye mawazo yetu yaunganishwe na Kristo. Hayo yanawezekana tu kwa watu ambao wameruhusu utawala wa Ufalme wa Mungu kuwa ndani yao, kwa njia ya Roho mtakatifu. 

Ni wakati wa kila mmoja kujipima, kuwa je; ni kweli amezivaa Silaha zenye Uwezo wa Mungu? Mawazo na Fikira Je zinapatana na Mungu au zimejaa Uchafu wa yule Adui shetani? Yesu Kristo alikuja kwa ajili ya kutuokoa kutoka katika mateka ya dhambi, na huu ndio uhuru wa Kweli.

NAWATAKIA WOTE SIKU NJEMA YENYE BARAKA TELE NA MAFANIKIO KATIKA MWILI NA ROHO. 

Na: Ev. Eliezer Mwangosi - 0767 210 299.

No comments:

Post a Comment