Tafakari: Marko 11:25 "Nanyi, kila msimamapo na kusali, sameheni,
mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na
ninyi makosa yenu".
Kama kuna dhambi itakayowapeleka wengi motoni, ni hii ya kutosamehe.
Ingelikuwa mtu anapewa kuona yaliyo ndani ya mioyo ya watu;
tungeshuhudia majeraha makubwa yasiyopona, yaliyotokana na kuumizwa na
ndugu au jamaa na wakati mwingine wapenzi wao. Japokuwa hatuwezi kuona,
maneno ya manung'uniko na malalamiko yanafunua mizigo ilioko ndani japo
kwa sehemu ndogo.
Wengi utasikia wanasema "nimemsamehe ila sitasahau" huyo bado
anamaumivu hajasamehe. Wengi wanaenda majumba ya Ibada, wanaimba,
wanahubiri, wanatoa zaka na sadaka, huku wakiwa bado wana mafukuto ya
chuki kwa waliowakosea. Utakuta mtu anajisifia akisema "mimi hata
simsalimii" au "nikimuona nakereka", ndivyo wengi walivyo hata kama
hawasemi. Jiulize ukimuona yule mbaya wako unajisikiaje? Kila mmoja
analo jibu.
Haijalishi umeumizwa kiasi gani; iwe ni kazini, iwe kwenye ndoa au
mahusiano, au katika mazingira yoyote; unapaswa kusamehe kabisa, na
kuachilia roho za kulipa kisasi, manung'uniko, malalamiko, chuki, hasira
na harara. Hayo yote yakidumu moyoni yanafunga kabisa milango ya
mbinguni.
Yesu alirudia kufundisha jambo hili akiwa anawafundisha wanafunzi
wake kuomba akisema - Mathayo 6:12 "utusamehe deni (makosa) yetu, kama
sisi nasi tuwasemehevyo wadeni (waliotukosea) wetu". Kwa maneno hayo,
tunajifunga kitanzi au kuwa huru, kwa kusamehe au kutosamehe.
Wapendwa katika hali ya ubinadamu jambo hili la msamaha ni gumu,
hivyo linahitaji kutoa maisha yetu kwa Yesu Kristo ili atupatie uwezo wa
kutenda yale tusiyoweza, atupatie tabia ya Upendo wa kuwapenda wabaya
na kuwaombea. Msamaha ni mojawapo ya vipimo kama kweli tunaongozwa na
Roho mtakatifu au bado tuko chini ya kongwa la utumwa.
NAWATAKIA WOTE SIKU NJEMA YENYE NURU YA MAFANIKIO NA BARAKA TELE.
By: Ev. Eliezer Mwangosi - 0767 210 299.
No comments:
Post a Comment