Somo La 9 | Nira Ya Yeremia

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

(Yeremia 16, 27 & 28)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Unapokuwa huna uhakika na mapenzi ya Mungu, je, huwa unafanyaje? Unasali, sawa? Unasoma na kujifunza ili uone kama Biblia inatoa mwelekeo, sawa? Je, huwa unajichunguza ili kubaini kama vipaumbele na matamanio yako binafsi yanaweza kuwa yanaingiliana na juhudi zako za kuyatafuta na kuyatenda mapenzi ya Mungu? “Mimi niko radhi kuyafanya mapenzi ya Mungu, ili mradi tu mapenzi ya Mungu ni kwa mimi kutenda ninachotaka kukifanya!” Nina uhakika hili lilikuwa tatizo katika siku za nyuma maishani mwangu. Wakati Mungu anaweza kubadilika kwa urahisi katika nyanja ambazo maisha yetu yanazipitia, mbaraka wetu mkubwa kuliko yote unatokana na kuifuata njia ambayo Mungu anatamani tuifuate. Somo letu juma hili linaelezea kwamba ikiwa kweli tunataka kuyaelewa mapenzi ya Mungu, basi tunaweza kuyaelewa. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

I.                   Kutokuoa
A.                Soma Yeremia 16:1-4. Kwa nini Mungu anamwambia Yeremia asioe na kupata watoto? (Kwa sababu watauawa kwa maradhi, upanga au njaa.)
1.                  Nakumbuka nilikuwa nina wasiwasi juu ya aina ya maisha watakayokabiliana nayo watoto wangu. Sasa ninajiuliza aina ya maisha watakayokuwa nayo wajukuu wangu. Ikiwa unaona kwamba mustakabali wa siku zijazo unatisha sana, je, unapaswa tu kutooa?
a.                   Endapo ungekuwa Yeremia, je, ungeuchukulia huu kama mzigo mwingine uliotwishwa na Mungu au rehema nyingine aliyokupa Mungu? (Kuna masomo mbalimbali kuhusu upotevu wa fedha na upotevu wa mali. Watu wanajuta mara mbili zaidi kwa kupoteza kitu fulani kuliko kabla hawajawa nacho (hawajakipata). Sina uhakika jambo hilo linahusikaje kwa watoto, lakini ni heri nisiwe na watoto kuliko kuwashuhudia wakifa kifo cha kutisha.)
A.                Soma Yeremia 16:14-15. Katikati ya hizi habari mbaya, Mungu anawapa watu matumaini gani? (Kwamba Mungu atawarejesha katika nchi yao.)
1.                  Kwa nini Mungu anafanya hivi? Kwa nini anatoa huu ujumbe wa matumaini? (Inaonesha kwamba bado Mungu anawapenda watu.)
A.                Soma Yeremia 16:16-18. Mungu anasema kuwa atawalipa “mara mbili zaidi.” Unadhani hii inamaanisha nini? (Mungu anasema kuwa adhabu ni mbaya zaidi kuliko dhambi. Yumkini Mungu anaufahamu mtazamo wa kiakili unaohusiana na kupoteza mali. Hivyo, anasema utajutia kile ulichokitenda kwa sababu hasara itaonekana kuwa mbaya mara mbili zaidi.)
1.                  “Kuwalipa mara mbili zaidi” inafungua lango la fikra ya Mungu. Mungu anasema kuwa anafahamu uhusiano wa jinsi dhambi na adhabu unavyoendana. Je, hiki ndicho ambacho mahakimu wa kibinadamu wanakizingatia? (Ndiyo. Nadhani lengo ni kufanya adhabu ya kosa la jinai iendane na kosa lenyewe.)
1.                  Wakristo wanaoielewa Biblia wanatambua kuwa wanaokolewa kwa neema, na si kwa matendo yao. (Warumi 8:1-4). Hiyo inamaanisha kwamba “mtu mwema” anayetenda mambo mema atapotea na kufa kifo cha milele ikiwa hataipokea kafara ya Yesu kwa ajili yake. Je, Wakristo wengi wanaamini kuwa hatima ya wale waliopotea ni ipi? (Mateso ya milele katika jahannamu.)
a.                   Je, hii inaleta mantiki yoyote kwa Mungu anayezingatia kanuni ya usawa? Kuna mtu “mwema” ambaye alipingana na msukumo wa Roho Mtakatifu, na mtu huyo anaungua milele? (Kitendo hicho kinaonekana kutokuwa na usawa kabisa.)
I.                   Manabii wa Aina Mbili
A.                Soma Yeremia 28:1-4. Je, huu ni ujumbe wa matumaini? (Naam, hakika!)
A.                Soma Yeremia 28:5-9. Tunapaswa kuwa na mwitikio gani kwa unabii unaotuambia kuwa mambo mazuri yatatokea?
1.                  Je, kuna viwango vya undumakuwili hapa? Kama vipo, kwa nini vipo? (Yeremia anasema kuwa ikiwa unatabiri juu ya amani, basi utajaribiwa ili kujua kama utabiri huo utakuwa wa kweli. Nadhani manabii wote wanajaribiwa kwa ukweli wa kile wanachokitabiri. Kinachoonekana kusemwa na Yeremia ni kwamba ikiwa utatabiri kile usichotaka kitokee, basi jambo hilo lina uzio wa kweli. Ikiwa unatabiri kile unachotaka kitokee, kile ambacho hadhira yako inataka kitokee, kuna uwezekano mkubwa kwamba unabuni na kulazimisha utabiri huo.)
A.                Soma Yeremia 27:1-2 na Yeremia 27:12-15. Hiyo inatuambia nini kuhusu mgongano kati ya ujumbe wa Yeremia na ujumbe wa Hanania? (Ujumbe huo unakinzana moja kwa moja.)
1.                  Mungu amempatia Yeremia zana gani ya kufundishia ili kuupa uzito ujumbe wa Mungu? (Nira halisi. Yeremia amevaa nira.)
1.                  Jiweke kwenye nafasi ya wasikilizaji (hadhira). Ungemchukuliaje mtu ambaye amevaa nira? (Sehemu ya akili yangu ingeniambia kuwa akili za mtu huyo haziko sawa. Sehemu nyingine ingedhani kuwa alikuwa anamaanisha anachokisema kuhusu ujumbe wake, vinginevyo asingejitesa kwa kuvaa nira.)
A.                Soma Yeremia 28:10-11. Sasa Hanania ndiye anayetumia kielelezo halisi. Jambo gani linampa Hanania haki ya kuvunja mali ya Yeremia? Jambo gani linampa haki ya kuingilia ujumbe wa Yeremia?
1.                  Hii inatuambia nini kumhusu Hanania? (Hakubaliani na maongezi matupu! Kwa hakika maongezi matupu yanafanya mambo kuwa magumu mbele ya hadhira. Nani anayesema ukweli kuhusu ujumbe kutoka kwa Mungu?
1.                  Yeremia alifanya nini baada ya Hanania kuvunja nira aliyoitengeneza? (“Yeremia alienda zake.”)
a.                   Je, hicho ndicho ambacho ungekifanya? Mtu huyu anasema uongo kuhusu ujumbe wa Mungu, anasema uongo kuhusu ujumbe ambao Mungu amekupatia, na anahatarisha maisha. (Ningejisikia kumpiga makonde Hanania, au angalao ningemrushia maneno makali. Lakini Mungu anasema tuache kisasi mikononi mwake.)
A.                Soma Yeremia 28:12-16. Mungu anaonesha mwitiko gani juu ya tabia hiyo mbaya inayofanywa na mtu anayekengeusha ujumbe wake? (Soma Yeremia 28:17. Hanania anafariki.)
1.                  Unafikiriaje jambo hili, je, Hanania alikuwa tu anasema uongo na alifahamu kuwa anadanganya? Au, Hanania alikuwa anajidanganya kwamba alikuwa anatekeleza mapenzi ya Mungu? (Soma Yeremia 28:15. Yeremia anakiita kile anachokisema Hanania kuwa ni “uongo.” Hiyo inaashiria kuwa Hanania alifahamu kauli zake ni za uongo, lakini nimewaona watu ambao nilidhani waliuamini uongo wao.)
1.                  Kwa nini Mungu mwenyewe hakumwambia Hanania aache madai yake ya uongo, badala ya kufikisha ujumbe kupitia kwa Yeremia? (Hii inaonesha Hanania hakuwa na uhusiano na Mungu.)
1.                  Je, bado Mungu “anawaondoa kutoka kwenye uso wa dunia” wale wanaohubiri uasi dhidi yake? (Ndiyo, nadhani anafanya hivyo. Namkumbuka mchekeshaji mmoja wa kutisha ambaye mara kwa mara alikuwa akimshambulia Mungu. Alipenda kumdhihaki Mungu. Wakati nilipomsikia akisema maneno haya nilijiuliza Mungu ataendelea kuruhusu jambo hili hadi lini. Miaka michache baadaye, mchekeshaji yule kijana alifariki.)
A.                Ikiwa tutajiweka kwenye nafasi ya hadhira inayowasikiliza Yeremia na Hanania, tunapata wasiwasi kwamba tunaweza kudanganywa. Je, ilikuwa rahisi kwa watu kufahamu nani alikuwa anasema uongo na nani alikuwa anasema ukweli? (Tayari tuna kielelezo kutoka kwa Yeremia kwamba ikiwa nabii anasema kile tunachotaka kukisikia (na kile anachotaka kukisema), basi kitendo hicho kinapaswa kutufanya kuwa makini.)
1.                  Soma 2 Timotheo 4:3-4 na 2 Wathesalonike 2:9-12. Je, kosa ni la nani kutokana na ukweli kwamba watu hawa waliuamini uongo? (Lilikuwa ni kosa lao. Walitaka kuuamini uongo. Ujumbe wa Yeremia haukuwa tu kwamba maangamizi yanakuja, bali yalikuwa yanakuja kwa sababu ya dhambi za watu waliotangulia. Pamoja na mambo mengine, dhambi hizo zilihusisha kuabudu miungu ya uongo. Tayari watu hawa walishaamua kuyapuuzia mapenzi ya Mungu, na Hanania alikuwa amewezesha mwendelezo wa uasi wao dhidi ya mapenzi ya Mungu.)
1.                  Soma 2 Wathesalonike 2:13-15. Utagundua kwamba Paulo anawaambia watu kuwa kihistoria walikuwa kuing’ang’ania kweli na wanapaswa kuendelea kufanya hivyo. Je, Paulo anabainisha vigezo gani vingine muhimu? (“Kazi ya utakaso ya Roho.” Kamwe hatupaswi kuuacha uwezo wa Roho Mtakatifu wa kutufunulia kweli.)
A.                Soma 1 Yohana 4:1. Je, hii inaelezea tatizo lililowasilishwa na Hanania? (Naam, hakika.)
A.                Soma 1 Yohana 4:2-3. Yohana anatupatia kipimo tunachoweza kukitumia kuwabaini manabii wa uongo. Je, kipimo hiki kingefanya kazi kwa Hanania? (Yohana anaandika mahsusi kuhusu kumkiri Yesu. Lakini, nadhani nadharia ya jumla kuhusu kipimo hicho bado inafanya kazi. Ikiwa Hanania alitambua na kuifuata miungu ya uongo sambamba na Mungu wa kweli, basi angefelisha nadharia iliyopo nyuma ya kipimo hiki.)
A.                Soma Warumi 12:2. Paulo anapendekeza kipimo gani kingine? (Ikiwa mawazo yako yamebadilishwa na kufanywa upya na Roho Mtakatifu, basi utakuwa na uwezo wa kuyaelewa mapenzi ya Mungu.)
A.                Rafiki, Mungu anatutaka tuyaelewe mapenzi yake. Sehemu ya upendo wake kwetu ni kwamba yuko upande wetu. Ikiwa tutayatafuta mapenzi yake kwa dhati, basi tutayapata. Kwa nini tusimwombe Roho Mtakatifu sasa hivi atuondolee vikwazo vyovyote vinavyotuzuia tusiyaelewe mapenzi ya Mungu?

I.                   Juma lijalo: Kuangamizwa kwa Yerusalemu.

No comments:

Post a Comment