Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Ezekiel 8, Yeremia 29, 37-38)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com
kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani.
Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Katika Yeremia 17:9 anasema kuwa “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa
kufisha; nani awezaye kuujua?” Tunao uwezo mkubwa ajabu wa kuweza kujidanganya
sisi wenyewe. Wale wanaomkataa Mungu wanayo hoja, wana sababu, kutokana na
tabia yao ya kiovu. Yeremia aliwaona watu wakijiingiza kwenye tabia zenye
vioja. Kwa upande mmoja walidai kuwa wanamfuata Mungu, na kwa upande mwingine
walimkataa Mungu. Kwa nini tu wasimkatae Mungu na kuacha kujisingizia
(kujidai)? Je, hili ndilo jambo tunalopaswa kuwa na wasiwasi nalo, kwa kuwa
tunadai kwamba tunamfuata Mungu? Hebu tuchimbue somo letu la Biblia ili
tujifunze zaidi!
I.
Kisingizio
A.
Soma Ezekieli 8:9-11. Kitu gani kipo mbele? (Wazee
wakifanya ibada inayoonekana kumtumikia Mungu.)
1.
Kuna nini nyuma? (Vinyago na vitu vya kuchukiza.)
2.
Ezekieli anapewa maono ya mambo yanayoendelea katika
zama za Yeremia. Unawezaje kuelezea kile alichokiona Ezekieli? (Unafiki. Upande
wa “mbele” unaonekana kuwa sahihi, lakini kinachoendelea nyuma ya pazia ni
mbali sana na mambo sahihi.)
B.
Soma Ezekieli 8:12. Wazee wanatoa sababu gani kutokana
na tabia yao isiyo sahihi? (Sababu mbili. Sababu ya kwanza, ni kwamba kwa namna
fulani Mungu haoni kile wanachokifanya. Sababu ya pili ni kwamba Mungu
amewaacha.)
1.
Ukweli ni upi? (Ni kinyume chake. Mungu anawaona, na
Mungu amefadhaika sana. Badala ya kuwatelekeza, anawaadhibu kwa matumaini ya kurejesha
mambo katika hali ya kawaida.)
2.
Jiweke kwenye nafasi ya mmojawapo wa hawa wazee kwa
kuvaa viatu vyake. Je, mtazamo wako wa mambo unakubaliana na kweli hizi?
(Ndiyo. Ikiwa unadhani kwamba Mungu anapaswa kukutetea bila kujali chochote
kile unachokifanya, basi mtafaruku unaoendelea unaweza kuhusianishwa na kitendo
cha Mungu kukutelekeza.)
3.
Ikiwa wazee wana maelezo yenye mantiki, kwa nini Mungu
hana furaha kiasi hicho? (Kwa sababu wamekataa kumwamini Yeremia. Kuna njia
mbili za kuliangalia jambo hili, na ikiwa utaliangalia kwa kuzingatia maonyo ya
Yeremia, na maelekezo yaliyopo kwenye neno la Mungu kwa njia ya maandishi,
wazee walipaswa kufahamu kuwa mtazamo wao wa mambo haukuwa sahihi.)
4.
Vipi kuhusu wewe? Unapoyachunguza maisha yako, je,
kujihesabia kwako haki kwa sehemu fulani kunatokana na kupuuzia maonyo ya
Biblia?
II.
Kuishi kwa Kisingizio
A.
Soma Yeremia 37:1-2. Je, Mfalme Sedekia na washauri
wake wanasikiliza kile anachokisema Mungu kupitia kwa Yeremia? (Hawatilii
maanani anachokisema Mungu.)
B.
Soma Yeremia 37:3. Kwa nini anaomba kuombewa?
1.
Je, unawafahamu watu wanaofanana na mtu huyu? Hawatilii
maanani kile anachowaambia Mungu, na kisha wanaomba kuombewa wanapojikuta
kwenye matatizo?
a.
Je, kitendo hiki ni kizuri au kibaya? Je, tunapaswa
kujisikia ahueni kwamba hatimaye mfalme anaomba kuombewa?
b.
Au, kuomba kuombewa ni kujidanganya zaidi?
C.
Soma Yeremia 37:5-8. Zedekia alikuwa anategea nini?
(Alidhani Misri itamwokoa. Mpango wake ulionekana kufanya kazi. Misri ilipotoka,
Babeli ilijiondoa mahali ilipokuwa imezingirwa na Yuda.)
D.
Soma Yeremia 37:9-10. Hebu turejee swali linalohusu kumwomba
Mungu wakati ulikuwa ukimpuuzia. Je, Mungu alijibu maombi ya Sedekia? (Ndiyo! Nadhani
mara zote maombi ndilo jibu sahihi. Lakini, utaona kwamba Mungu habadiliki. Bado
ana ujumbe ule ule ambao Sedekia amekua akiukataa.)
III.
Kuugeukia Ubaya Zaidi
A.
Soma Yeremia 38:2-3. Huu ni ujumbe ule ule wa Yeremia –
jisalimisheni na acheni kushindana na Babeli. Endapo ungekuwa kiongozi wa Yuda,
je, ungeupenda ujumbe huu?
B.
Soma Yeremia 38:4. Nahisi nawe ulikuwa unafikiria jambo
hilo hilo. Yeremia hawahamasishi wanajeshi na hatii hamasa morali ya watu. Unadhani
Yeremia alitakiwa awe anafanya nini?
1.
Je, kuna chochote cha kujifunza linapokuja suala la
kuwashauri watu wanaokataa kuuacha uovu? (Ikiwa tuna uhakika kwamba tunao
ujumbe wa Mungu, basi tunatakiwa kuung’ang’ania ukweli. Yeremia alikuwa
hawaambii ujumbe “wenye kuwafurahisha,” alichokuwa anakisema kilikuwa ni
maangamizi katika mipango ya viongozi kumpinga Mungu.)
C.
Soma Yeremia 38:6. Je, ungependa kuzamishwa kwenye
matope shimoni? (Ni jambo la kutisha.)
1.
Je, tutarajie kuwa kwenye “matope” tunapozungumza dhidi
ya uovu? (Ukisoma Yeremia 38:7-13 utaona kwamba Mungu anamhamasisha kiongozi,
Ebedmeleki, kuingilia kati ili kumwokoa Yeremia dhidi ya kufa kwa njaa chini ya
shimo.)
IV.
Nafasi ya Mwisho
A.
Soma Yeremia 38:14-15. Unalichukuliaje ombi la Mfalme
Sedekia? Je, jibu la Yeremia lina mantiki? (Kwa dhahiri Mfalme amekanganyikiwa
kuhusiana na endapo anapaswa kumsikiliza Yeremia.)
B.
Soma Yeremia 38:16. Kwa nini mfalme aliapa kwa “siri”
kiapo hiki kwa Yeremia?
C.
Soma Yeremia 38:17-18. Hii inatufundisha nini kumhusu
Mungu? (Ni mvumilivu. Bado anampa Sedekia njia ya kutokea. Bado ana matumaini.)
V.
Muda Umekwisha
A.
Soma Yeremia 39:1-2 na Yeremia 39:4-7. Wanao wameuawa,
na hicho ndicho kitu cha mwisho kabisa kukiona maishani mwako. Fikiria jinsi
mambo yalivyo kwa Mfalme Sedekia sasa?
B.
Soma Yeremia 39:8-9. Mambo yote yametoweka. Yerusalemu imechomwa
moto na watu wamechukuliwa mateka. Kuzitumainia sanamu na kuitumainia Misri
kumewatendea nini watu wa Yuda?
1.
Je, hii ni kanuni ya jumla inayotumika kwako,
tunapoweka matumaini yetu kwa watu wengine na kwa vitu tulivyovitengeneza?
C.
Soma Yeremia 39:11-12 na Yeremia 39:15-18. Utakumbuka kwamba
Ebedmeleki aliingilia kati ili kumwokoa Yeremia dhidi ya kufa kwa njaa katika
shimo la ghala. Kuna lipi la kujifunza kwa wale wanaosimama kwa ajili ya Mungu
wakati usio na umaarufu? (Mungu anawaangalia watu wanaomtumikia.)
VI.
Kutenda kwa Ubora wa Hali ya Juu
A.
Umepata majanga maishani mwako na lawama zote ni juu
yako kwa kuwa wewe ndio umeyasababisha. Unatakiwa kufanya nini?
1.
Hebu tusome barua ambayo Yeremia aliituma kwa wale
waliochukuliwa mateka Babeli. Soma Yeremia 29:4-6. Yeremia anatoa ushauri gani?
(Jaribu kuishi maisha ya kawaida kwa kadri inavyowezekana. Endapo umeyachezea
maisha, kamwe mambo yanaweza yasiwe kama ilivyotarajiwa yawe, lakini unatakiwa
ujitahidi kuishi maisha ya kawaida.)
B.
Soma Yeremia 29:7-8. Je, unatakiwa kufanya jambo gani
jingine kwa wale waliokupatia maadili mema maishani mwako? (Watu wa Mungu
wanaweza kuwadharau watu wa Babeli na kujaribu kuwaona kuwa ni watu wa hali ya
chini. Lakini, Mungu anasema kuwa watu wake wanatakiwa kufanya kazi pamoja na
watu wa Babeli ili kuyafanya maisha yawe bora zaidi kwa ajili yao wote.)
C.
Soma Yeremia 29:10-11. Hii inamaanisha nini kwa watu
wengi? (Kwamba watakufa wakiwa utumwani.)
1.
Ni kwa jinsi gani ujumbe huu ni wa matumaini? (Watoto
wao watarejea Yuda.)
2.
Unawezaje kutumia somo hili maishani mwako endapo
umefanya mambo yaliyosababisha majanga? (Weka matumaini yako katika kusaidia
kuyafanya maisha ya watoto wako yawe bora zaidi. Jaribu kufanya mambo yawe ya
kawaida kabisa sasa hivi kwa kadri uwezavyo, ili siku zijazo ziwe bora.)
D.
Rafiki, wanadamu wana uwezo mkubwa na wa ajabu wa
kuweza kujidanganya wenyewe. Mwombe Mungu akuoneshe asili ya kweli ya moyo
wako. Ikiwa umechelewa sana, na tayari umeshayaharibu maisha yako, mgeukie
Mungu, jaribu kuyafanya maisha yawe ya kawaida kwa kadri inavyowezekana, na
jitahidi kuwaandalia wanao maisha bora zaidi. Je, utajitoa kwa ajili ya hilo?
VII. Juma lijalo: Agano.
No comments:
Post a Comment