Somo La 5 | Majonzi Zaidi Kwa Nabii

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Yeremia 18-19, 20 & 21)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: “Hakuna jambo jema lisiloadhibiwa” ni msemo wa zamani sana. Katika somo letu juma hili, inaonekana msemo huu ulitumika katika kipindi cha Yeremia! Je, ni mara ngapi kiongozi wa dini amepata mateso ikiwa ni matokeo ya kuyatenda mapenzi ya Mungu? Watu wanaohusika na uovu hawataki kukemewa au kukumbushwa juu ya mapenzi ya Mungu. Bila shaka ndio maana mara nyingine ukubwa wa tatizo unaongezeka kwa sababu ya upungufu wa hekima na busara, lakini tatizo kubwa ni ukinzani dhidi ya nuru kwa wale wanaopenda giza (angalia Yohana 3:19-21). Hebu tuzame kwenye somo letu la Yeremia ili tujifunze zaidi!

I.                   Masikio Yawakayo (Yawashayo)
A.                Soma Yeremia 19:1-3. Ikiwa mtu anakuambia kuwa kile anachotaka kukuambia “kitayawasha” masikio yako, je, utaendelea kusubiria kuyasikiliza maneno hayo?
A.                Soma Yeremia 19:7. Je, una mipango kwa ajili ya maisha yako? Je, jambo gani litatokea kwenye mipango ya wale wanaoishi katika nchi ya Yuda? (Wataangamizwa.)
1.                  Binafsi ninabashiri kwamba hakuna mtu hata mmoja ambaye angependa aliwe na mnyama pale atakapofariki. Kuna jambo gani kubwa hapa linalojalisha? (Hakuna mtu hata mmoja ambaye anakujali ambaye yuko hai kwa ajili ya kukuzika!)
A.                Soma Yeremia 19:8-9. Mambo yatakuwa mabaya kwa kiwango gani kule Yerusalemu? (Watu watakuwa wala nyama - watawala watoto wao wenyewe.)
A.                Soma Yeremia 19:10-12. Mungu anamfanya Yeremia atumie mfano wa kifaa kinachoonekana, gudulia la mfinyanzi, kufikisha ujumbe wa Mungu kwa watu. Kwa nini? (Watu tofauti tofauti hujifunza kwa njia tofauti tofauti, lakini mfano wa kitu kinachoonekana unawasaidia watu kuuelewa na kuukumbuka ujumbe.)
1.                  Tunazo rejea kadhaa kwenye mafungu haya zinazourejea mji wa Tofethi. Soma Isaya 30:33 na 2 Wafalme 23:10 kisha uniambie maeneo haya yanaonekana kuwa ni mahali gani? (Hii ni jehanamu ya duniani. Walitengeneza moto mkubwa kisha wakawachoma watoto wao kama sadaka kwa Baali na Moleki.)
1.                  Je, masikio yako yanawasha? Yeremia anasema kuwa Yerusalemu itakuwa kama jehanamu hapa duniani. Je, mwitikio wako ungekuwaje endapo Yeremia angekuwa anazungumza nawe kwa namna hii?
I.                   Mwitikio wa Viongozi
A.                Soma Yeremia 20:1-2. Masikio ya viongozi wa dini yanawaka moto sana kiasi kwamba wanampiga Yeremia na kumtia katika mkatale. Nilipokuwa Williamsburg, Virginia, nilijaribu kuvaa mikatale ya mbao waliyonayo katika kijiji cha kikoloni. Endapo una uzoefu wa jinsi mtu anavyojisikia akiwa amevaa mkatale, hebu niambie ni matatizo gani ya ziada unayoweza kuyafikiria kwa mtu kupigwa kwanza kabla ya kuvaa mikatale? (Soma Kumbukumbu la Torati 25:2-3. Mikatale inatia karaha sana, na endapo muda mfupi tu nitakuwa nimetoka kuchapwa viboko, mambo yatakuwa mabaya zaidi!)
1.                  Unakielezea kitendo ambacho viongozi wa dini walimtendea Yeremia? (Machafuko ndio majibu ya watu ambao hawawezi kujenga hoja ya kujibu mada iliyoibuliwa.)
A.                Soma Yeremia 20:3-6. Je, Yeremia amepata fundisho lolote? (Anamwambia Pashuri, mtu ambaye alimwingiza kwenye mkatale, kwamba atatiwa hofu (jina lake jipya linamaanisha “hofu kila mahali”), atakamatwa na kufia Babeli.)
1.                  Tunapata ishara (kidokezo) gani kuhusu matamanio mahsusi ya Pashuri katika kile anachokitabiri Yeremia? (Msitari wa mwisho unatuambia kwamba Pashuru ni nabii wa uongo ambaye amekuwa akisema uongo kuhusu hatma ya Yuda. Sasa tunaona kwa wazi zaidi sababu ya Pashuri kutaka kumdhuru Yeremia.)
I.                   Mwitikio wa Yeremia
A.                Soma Yeremia 20:7-8. Unajisikiaje watu wanapokufanya kuwa kituko kwao? Wanapokufedhehesha? Fikiria kwamba watu hawakukuheshimu, badala yake kila siku wanakufanyia mzaha. Je, utakuwa na mtazamo gani wa maisha, hususani pale ambapo dhihaka inaendelea kuwa ile ile?
1.                  Soma Yeremia 1:6-8. Unayakumbuka mazungumzo haya kati ya Mungu na Yeremia mwanzoni kabisa? Yeremia anamaanisha nini anaposema kwamba Mungu “amemhadaa?” (Mungu alimwambia Yeremia asiogope, na kwamba Mungu atamwokoa.)
a.                   Je, Mungu amemhadaa Yeremia?
a.                   Endapo umesema kuwa, “ndiyo,” (au “huenda”), je, hii inaashiria nini kuhusu uhakika wa Yeremia katika ujumbe wake mkuu anaoupeleka Yuda?
A.                Soma Yeremia 20:9. Kwa dhahiri Yeremia alijaribu kufumba mdomo wake ili kuepuka dhihaka zaidi. Kwa nini hilo ni tatizo? (Kuyatenda mapenzi ya Mungu ni sawa na moto ndani yake. Hawezi kuuhimili moto wa Mungu ndani yake.)
1.                  Je, umewahi kupitia uzoefu huo? Kuyatenda mapenzi ya Mungu inaonekana ni jambo la kawaida sana kiasi kwamba huwezi kuacha kuyatenda?
A.                Soma Yeremia 20:10. Je, ni maadui wa Yeremia pekee ndio wanaomdhihaki na kumpinga? (Yeremia anaandika kuwa “rafiki zangu wote” wanamvizia atende kosa.)
1.                  Utagundua kwamba marafiki wana matumaini kuwa Yeremia “atahadaika.” Je, hivi punde tu Yeremia hajasema (Yeremia 20:7) kwamba alihadaiwa?
a.                   Je, hii inamaanisha Yeremia anaamini kuwa “marafiki” zake (ambao kiuhalisia ni maadui wake) watashinda?
A.                Soma Yeremia 20:11. Unaelezeaje kauli hii ya kijasiri kwa kuzingatia Yeremia 20:7? (Yeremia ni mwanadamu. Alipigwa. Amedhihakiwa na kuaibishwa. Imani yake ilitetereka mambo mabaya yalipotokea ambayo alidhani Mungu angeyazuia. Lakini sasa imani yake inaimarika.)
1.                  Aibu anayoipata Yeremia inatofautianaje na aibu watakayoipata maadui zake? (Aibu yake ni ya muda [si ya kudumu]. Aibu yao “haitasahauliwa kamwe.”)
a.                   Tunajifunza nini katika jambo hili? (Mara zote tunapaswa kuwa na “mtazamo mpana” maishani. Mambo yanaweza yasituendee vizuri kwa kipindi fulani, lakini hatimaye Mungu ameahidi kutenda mambo yote kwa usahihi.)
A.                Soma Yeremia 20:12. Je, tutajisikia vizuri kufahamu kwamba hatma ya wale waliotutesa haitakuwa nzuri? (Soma Luka 23:34 na Marko 11:25. Yeremia anaweza kujisikia vizuri kuomba kuona kisasi, lakini huu sio mtazamo ambao Mungu anatutaka tuwe nao.)
A.                Soma Yeremia 20:14-15 na Yeremia 20:18. Je, Yeremia anarejea kwenye msongo baada ya kauli yake kuu ya imani katika Yeremia 20:11? (Ndiyo, sasa anasema kuwa anatamani kamwe asingezaliwa.)
1.                  Soma Yeremia 1:4-5. Mungu anasema kuwa alimjua Yeremia “akiwa tumboni” na yeremia anasema kuwa anatamani angefia tumboni, kuliko kuishi maisha ya nabii. Tunajifunza nini? (Yeremia anaonekana kama vile yupo kwenye msongo mkubwa wa mawazo. Watumishi wa Mungu wanaweza kupitia nyakati ambazo wanakuwa na msongo wa mawazo. Ukitafakari jambo hili, unaweza kukumbuka kwamba Sulemani alikuwa na msongo wa mawazo (Mhubiri 6 & 9), Eliya alipata hofu na alikuwa na msongo wa mawazo (1 Wafalme 19), na Daudi aliogopa (1 Samweli 21:12-13). Mungu anatufunulia mambo haya ili tusidhani kuwa sisi pekee ndio tunaopitia uzoefu wa aina hii.)
A.                Soma Yeremia 21:1-2. Hebu subiri kidogo! Ni nani sasa ambaye anaomba ushauri? (Mfalme Sedekia! Sasa Yeremia anaombwa na afisa wa ngazi za juu wa nchi yake amuulize Mungu.)
1.                  Unapohisi kukata tamaa na kuogopa, unajisikiaje pale mtu wa muhimu kabisa anapoomba msaada wako?
I.                   Uchaguzi wetu
A.                Soma Yeremia 18:1-5. Mungu anamwambiaje Yeremia kuhusu kupeleka ujumbe mwingine kwa mfinyanzi? (Kwa mara nyingine, huu ni msaada wa kitu kinachoonekana ili kusaidia kuelewa ujumbe wa Mungu.)
A.                Soma Yeremia 18:6-10. Tunajifunza nini kuhusu uelewa wetu wa unabii? (Tunao wajibu wa kutimiza katika siku zetu zijazo. Kwa kuwa Mungu anazifahamu siku zijazo, nina uhakika kwamba baadhi ya unabii unaakisi maarifa ya Mungu juu ya wakati ujao na hauna vigezo. Kwa upande mwingine, Mungu anamwambia Yeremia kuwa wanadamu wanaweza kubadili kile anachokisema Mungu kutokana na tabia zao. Angalao baadhi ya unabii una vigezo.)
A.                Rafiki, je, mara nyingine huwa unajisikia kukata tamaa? Endapo mambo hayakuendei vizuri kutokana na chaguzi zako mbaya, Mungu anatuambia kwamba mustakabali wetu unaweza kuboresheka ikiwa tutayafuata mapenzi yake. Endapo mambo yanakuendea kombo kwa sababu umekuwa ukiyafuata mapenzi ya Mungu, na watu waovu wanakudhuru, Mungu anasema kuwa atalishughulikia tatizo na kulitekeleza kikamilifu katika siku za usoni. Jambo la msingi ni kuyafuata mapenzi ya Mungu. Je, utafanya uamuzi, sasa hivi, kufanya hivyo?

I.                   Juma lijalo: Matendo ya Ishara.

No comments:

Post a Comment