NENO LA LEO - WITO WA KUDUMISHA AMANI TANZANIA

Isaya 32:17 "Na kazi ya HAKI itakuwa AMANI; na mazao ya Haki yatakuwa ni UTULIVU na matumaini daima".

��Wapendwa watanzania wenzangu; kama kuna mambo nyeti yanayotakiwa kufanyika kwa uangalifu na ufahamu mkubwa, basi ni jinsi ya kuilinda AMANI ya Tanzania kwenye tukio la Uchaguzi wa viongozi utakaofanyika 25 Octoba. Wengi wameomba na wanaendelea kumuomba Mungu ili uchaguzi uishe vizuri tukiwa bado kwenye kisiwa cha Amani.

��Amani kutoweka, na inchi yetu kuingia katika majanga ya umwagaji damu na wananchi kuishia kuwa wakimbizi ni kitendo cha kufumba na kufumbua. Kila mtanzania mwenye akili timamu anawajibika kuilinda AMANI, hakuna mtu wa nnje atakayekuja kuivunja amani, japo wanaweza kuchochea kwa nguvu zote amani itoweke. Mtanzania mwenzangu, dhamiria kuilinda Amani kwa faida yako na familia yako, Omba Mungu akuonyeshe ni nani kweli anaweza kuleta mabadiliko yenye hofu ya Mungu. Jiandae kupiga kura kwa uhuru, na amani moyoni, acha chuki na hasira, Mungu yupo atatenda.

��Neno la leo limetoka kwa Bwana Mungu wetu, likiwa na jibu kwa wote wanaoitakia Tanzania AMANI, Bwana anasema " Kazi ya HAKI itakuwa AMANI; na mazao ya Haki yatakuwa ni UTULIVU na matumaini daima". Wapendwa; HAKI isipotendeka katika mchakato mzima wa uchaguzi, ni hakika Amani tutakuwa tumeipoteza. Wote wanaohusika, kuanzia mpiga kura, wagombea nafasi za uongozi, wanaohesabu kura,  wasimamizi, serikali ilio madarakani, vyombo vya dola, tume ya uchaguzi ..... MUNGU ANASEMA HAKI ITENDEKE.

��Watanzania kama tunataka mabadiliko ya kweli, yenye tija kwa siku za usoni, basi tunapaswa kuchukuwa hatua kubadili mtindo wa maisha, tukubali kuacha DHAMBI, tuchague kuishi maisha yenye hofu ya Mungu, ndipo Mungu atatupatia kiongozi atakayesimamia amani na hatimae mafanikio ya Maisha. Acheni ufinyu wa mawazo wa kutegemea ahadi zinazotolewa na wanasiasa wanaosaka madaraka majukwaani, kama hawana HOFU YA MUNGU, ni kazi bure na kujilisha upepo na hatimaye kuvuna upepo wa Kimbunga.

��Neno la Bwana linasema "HAPANA AMANI KWA WABAYA, ASEMA BWANA" Isaya 48:22. Bila Mungu kuwa kati yetu, na kukomesha, uovu huu: Udanganyifu, chuki, hasira, visasi, ufisadi, wizi, uonevu, uchawi, rushwa n.k. sio rahisi kufikia mabadiliko yenye manufaa, tunaweza kuishia mabadiliko yenye hasara. Inahitajika hekima kutoka juu, ili kufikia malengo yetu kwa amani. Ni wewe Mtanzania na mimi wenye maamuzi ya kuleta amani kwa kumtumaini Mungu sio Mwanadamu.

��Daudi alisema maneno haya "Bwana, UOKOE, maana mcha Mungu amekoma, maana waaminifu wametoweka katika wanadamu.....Wasio haki hutembea pande zote, UFISADI ukitukuka kati ya Wanadamu" Zaburi 12:1, 8. Chukua hatua mwambie Bwana "OKOA" Tanzania "OKOA" watu wako, naye atatenda sawasawa na ahadi zake.

MUNGU IBARIKI TANZANIA - MUNGU IBARIKI AFRIKA.

NAWATAKIA SIKU NJEMA YENYE AMANI NA BARAKA TELE KATIKA MAANDALIZI YA UCHAGUZI
Na Ev. Eliezer Mwangosi - 07676210299 - Email - eliezer.mwangosi@yahoo.com
��wapelekee wengine ujumbe huu, kwa ajili ya kuitakia amani Tanzania��

No comments:

Post a Comment