Somo La 4 | Karipio Na Adhabu

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Yeremia 11, 12 & 17)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Unajilinganishaje na watu ambao Yeremia alikuwa anawaonya? Unapotafakari kile ambacho Mungu anakuambia kwa njia ya Biblia na maneno ya uvuvio ya watu wengine, je, unayachukulia “maonyo” hayo kwa dhati, au unafanya tu kile unachokitaka? Je, unayaamini maamuzi yako? Je, unaweza kujitegemea (kujitumainia) mwenyewe kufanya maamuzi mazuri linapokuja suala la kufanya mabadiliko unayopaswa kuyafanya? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza kitakachotuweka wazi zaidi na kutuelekeza katika uongozi wa Roho Mtakatifu! 


I.                   Suala la Kutegemea (Kutumaini)
A.                Soma Yeremia 17:5. Fungu linaposema kuwa ni laana kumtegemea mwanadamu, je, hiyo inamaanisha kujitegemea wewe mwenyewe?
1.                  Angalia neno “na,” kwenye maneno “na moyoni mwake amemwacha Bwana.” Je, lazima tuendane na vigezo vyote viwili; kuwategemea wanadamu na kumwacha Mungu?
a.                   Je, tunaweza kuwategemea wote wawili? (Soma Mithali 3:5. Kama kweli tunaifahamu nafasi ya Mungu maishani mwetu, basi tunatambua kwamba ufahamu wetu ni mdogo sana.)
A.                Soma Yeremia 17:6. Kwa nini huu ni ukweli? Je, ni kwa sababu Mungu anayafanya mambo kuwa magumu pale mwanadamu anapojitegemea? Au, ni kwa sababu kujitegemea wewe mwenyewe ni mkakati mbaya tu?
A.                Soma Yeremia 17:7-8. Angalia maneno matatu yanayofanana “kutegemea” (“ambaye Bwana ni tumaini lake”), “hofu” (“hautaona hofu wakati wa hari ujapo”) na “wasiwasi” (“hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua”). Kuna ujumbe upi unaohusu wasiwasi? (Ikiwa unajitegemea wewe mwenyewe, utakuwa na wasiwasi. Ikiwa unamtegemea Mungu, unaweza kuachana na wasiwasi.)
1.                  Hebu tujadili jambo hili kidogo. Je, hii inamaanisha kuwa mara zote mambo yatakuendea vyema kwa jinsi unavyotaka? (Inamaanisha kwamba tunatakiwa kumtegemea Mungu bila kujali matokeo ya aina yoyote. Ikiwa tunaamini kwamba Mungu anatupenda, na kwamba ana mambo mazuri moyoni mwake kwa ajili yetu, basi tunapaswa kumtegemea.)
1.                  Soma Kumbukumbu la Torati 3:23-26. Hii ni taarifa ya Musa kuhusu uamuzi wa Mungu kwamba hataingia katika nchi ya ahadi. Unadhani Musa alifikiria Mungu ana nia njema mawazoni mwake pale Mungu alipomwambia anyamaze kuhusu maombi yake ya kuingia katika nchi ya ahadi? (Ikiwa Musa alifanya hivyo, imani yake ina nuru na ni kubwa sana kuliko imani yangu. Hata hivyo, utakumbuka kwamba Yuda 9 inabainisha kuwa badala yake Mungu alimchukua na kumpeleka Musa katika nchi ya ahadi ya mbinguni. Mungu alimpatia zawadi kubwa zaidi. Mungu alikuwa na nia njema mawazoni mwake kwa ajili ya Musa.)
A.                Soma Yeremia 17:9. Tunaweza kuwa na ujasiri wa namna gani katika uchunguzi wetu kwamba tunamtegemea Mungu na kwamba hatujitegemei sisi wenyewe? (Tunatakiwa kuwa na mashaka na nafsi zetu.)
A.                Soma Yeremia 17:10. Ikiwa hatuwezi kuyaamini maamuzi yetu wenyewe, je, kuna namna yoyote tunayoweza kueleza kama tunamtegemea Mungu? (Angalia jinsi maisha yako yalivyo. Mungu anatupatia thawabu kwa uaminifu wetu. Hata hivyo, tunatakiwa tu kukiangalia kisa cha Ayubu na waebrania 11:35-39 ili kufahamu kwamba “jinsi mambo yanavyoendelea na kutokea” sio mwongozo mkamilifu tunaoweza kuutegemea.)
A.                Soma Yohana 3:19-21. Je, ni kizingiti gani kingine tunachokabiliana nacho katika kulifuata neno la Mungu? (Tunapenda uovu. Sio tu kwamba uamuzi wetu si wa kutegemewa, bali pia unashawishiwa na ukweli kwamba tunapenda kutenda uovu na hatupendi “matendo yetu… yaanikwe hadharani.”)
1.                  Tiba ya jambo hili ni ipi? (Kuishi kwa kuufuata ukweli kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Hiyo inamaanisha kuishi maisha ya “nuru.”)
A.                Soma Yeremia 17:11. Je, mara zote watu wanaojitegemea (wanaojitumainia) na wale wanaotenda uovu watagundua kwamba “hawataona yatakapotokea mema (Yeremia 17:6)”? (Hii inatuambia kuwa mtu mwovu anaweza kuendelea vyema kwa kitambo kifupi. Hata hivyo, hatimaye mambo yatakwenda kombo.)
I.                   Onyo
A.                Soma Yeremia 17:1. Kwa nini unaandika jina lako juu ya kitu fulani? (Kuwaonyesha watu wengine kwamba unakimiliki.)
1.                  Unadhani inamaanisha nini kwa dhambi zako kutiwa alama? (Yumkini ni sababu ile ile, inaonyesha kwamba ni mali yako. Unaimiliki. Au, uwezekano mkubwa zaidi ni kwamba dhambi hiyo imeuteka moyo wako.)
A.                Soma 2 Wakorintho 3:3. Lengo lako linapaswa kuwa lipi? (Kuwa na “barua” ya Mungu iliyoandikwa mioyoni mwetu kwa ajili ya ulimwengu. Hiyo sio tu kwamba inaonesha kuwa sisi ni waja wake, bali pia inaakisiwa katika jinsi tunavyoenenda.)
A.                Soma Yeremia 17:2. Kuna ujumbe gani hapa – kwamba watoto wana kumbukumbu nzuri? (Maoni ya watu mbalimbali hayakubaliani na kile kinachomaanishwa hapa. Hata hivyo, kutokana na jinsi tafsiri ya Kiingereza ya Biblia ya NIV inavyotafsiri jambo hili, inaonekana kuwa watu wa Mungu waliwafundisha watoto wao kuziabudu sanamu badala ya kumwabudu Mungu wa kweli. Mafundisho haya ya kiovu yaliwaingia watoto.)
A.                Soma Yeremia 17:3-4. Matokeo ya kumwacha Mungu na kuwafundisha watoto wako kumwacha Mungu ni yapi? (Unaupoteza urithi ambao Mungu angekupatia. Unakuwa mtumwa wa watu wengine.)
I.                   Tahadhari ya Nabii
A.                Soma Yeremia 11:18-19. Upinzani dhidi ya Yeremia ni mkubwa kwa kiwango gani? (Walipanga kumwua.)
1.                  Mara kwa mara huwa ninasikia wenzi wanaowaua (au wanajarobu kuwaua) wenzi wao. Swali la dhahiri ni, “kwa nini, badala yake, wasiamue kumpa talaka?” Katika sakata la Yeremia, kwa nini tu wasiamue kumpuuzia, badala ya kujaribu kumwua?
A.                Soma Yeremia 11:20. Una maoni gani kuhusu ombi la Yeremia?
1.                  Soma Luka 11:2-4. Nafahamu bado Yesu alikuwa hajatoa ombi lake la mfano wakati Yeremia alipopeleka hili ombi, lakini angalia tofauti iliyopo. Je, ni sahihi kusema, “Ninawasamehe,” na “Mungu lipiza kisasi kwa maadui zangu?”
A.                Soma Yeremia 11:21-23. Hatuna haja tena ya kubashiri mtazamo wa Mungu kuhusu jambo hili. Mungu anasema kuwa atafanya nini? (Atalipiza kisasi (“Nitawaadhibu.” “Nitaleta mabaya [juu yao].”)
1.                  Unalinganishaje jambo hili na ombi la mfano lililotolewa na Yesu? (Soma Warumi 12:19-21. Kisasi ni cha Mungu pekee.)
A.                Angalia tena Yeremia 11:23. Watu wanaopanga kumuua Yeremia wanaishi wapi? (Anathothi.)
1.                  Soma Yeremia 1:1. Utagundua kwamba nyumbani kwao Yeremia ni Anathothi. Je, hii inaongezea nini katika mawazo yako kuhusu hali hii? (Soma Luka 4:24. Nina uhakika njama hii ilimuuma sana Yeremia alipokwa akiitafakari. Watu anaowafahamu wanapanga kumwua.)
I.                   Mtazamo wa Yeremia
A.                Soma Yeremia 12:1. Yeremia amewasilisha “mashtaka mbele ya” Mungu – mashtaka juu ya njama za kuuawa kwake. Mungu alimwambia Yeremia kuwa atawaadhibu. Je, unadhani Yereemia bado anazungumzia mashtaka yale yale, hali ile ile?
1.                  Yeremia anauchukuliaje utoaji haki wa Mungu? (Kwamba waovu wanasitawi, wanaishi vyema.)
1.                  Soma tena Yeremia 17:10. Unakumbuka nilidhani kwamba hii inaonesha namna ya kudhihirisha hukumu ya Mungu juu ya maisha yako? Je, sisi, kama ilivyo kwa Yeremia, tunatakiwa kumkumbusha Mungu kwamba wale wanaomfuata wanapaswa kuenenda na kutendewa vyema, na wale wasiomfuata hawapaswi kutendewa vyema?
A.                Soma Yeremia 12:2. Je, watu hawa wanamshuhudia Mungu? Je, wanamzungumzia Mungu? (Ndiyo! Lakini, Yeremia anasema kuwa yale wanayoyasema hayaakisi mtazamo wao wa kweli.)
A.                Soma Yeremia 12:3. Niambie jinsi unavyoutafakari moyo wa Yeremia?
1.                  Je, Mungu alifanya uchaguzi wa busara pale alipomchagua Yeremia kuwaonya watu kuhusu hukumu inayokuja?
A.                Soma Yeremia 12:4. Je, Yeremia ni mtu anayependa kutoa hukumu, anayethubutu kumfundisha Mungu juu ya masuala ya haki? (Msitari wa mwisho unadhihirisha kwamba Yeremia anaonekana kujali jinsi jambo hili linavyoonekana kwa watu wengine. Watu wengine wanadhani kuwa Mungu hajali, si mwangalifu na haangalii mambo yanayoendelea.)
A.                Hebu turuke mafungu kadhaa na tusome Yeremia 12:14-17 ili tuone majibu ya Mungu. Mtazamo wa Mungu unatofautianaje na mtazamo wa Yeremia? (Tunaona huruma katika jibu la Mungu. Anamwambia Yeremia kuwa atatekeleza hukumu, lakini Mungu anasema kuwa anatazamia na kuangalia muda ambao anaweza kuonesha huruma kwa watu wake.)
A.                Rafiki, je, umeyachunguza maisha yako? Je, unamtegemea Mungu? Je, uhusiano wako na Mungu ni wa maneno tu pasipo matendo? Je, huna huruma kwa watu wanaotenda uovu? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu sasa hivi akusaidie ili mtazamo wako uwe wa kumtegemea Mungu zaidi na kuwa na huruma zaidi?

I.                   Juma lijalo: Majonzi zaidi kwa Nabii.

No comments:

Post a Comment