Somo La 2 | Mgogoro (Kutoka Ndani na Nje)


Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Jeremia 2 & 27)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Hebu tupitie historia kidogo. Mungu aliwaongoza watu wake kutoka Misri kwenda katika nchi ya ahadi. Kazi yao ilikuwa ni ipi? Kudai nchi waliyoahidiwa. Kamwe hawakulitimiza jukumu hilo kwa ukamilifu, lakini katika kipindi cha utawala wa Mfalme Daudi na Mfalme Sulemani walidhibiti eneo kubwa la nchi ya ahadi. Baada ya kifo cha Sulemani, kutokana na sera zake zilizoweka kiwango kikubwa cha kodi, watu wa Mungu waligawanyika katika mataifa mawili. Ufalme wa kaskazini (makabila kumi) ulikuwa ni ufalme wa Israeli na ufalme wa kusini (makabila mawili) ulikuwa ni ufalme wa Yuda. Israeli iliendelea kuwepo kwa takribani miaka 200 na kisha ikaangukia kwa Wa-Ashuru. Yuda iliendelea kuwepo kwa takribani miaka 150 hadi ilipoangukia kwa Wababeli. Inakadiriwa kwamba ni katika kipindi cha miaka 40 ya mwisho ya historia ya Yuda ndipo Yeremia aliwaonya watu juu ya uangamivu unaokuja. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

I.                   Kumbukizi ya Mungu
A.                Soma Yeremia 2:1-2. Mungu anakumbuka nyakati gani? (Safari ya Jangwani kutoka Misri.)
1.                  Je, hivi ndivyo unavyowaelezea watu wa Mungu katika kipindi cha safari ya wana wa Israeli kutoka Misri? Walikuwa wenye upendo na wenye kujitoa? (Matumaini yangu ni kwamba Mungu anakumbuka historia yangu kwa uzuri kabisa kiasi hiki! Hivyo sivyo ambavyo nitawaelezea watu katika kipindi cha safari ya Jangwani.)
A.                Soma Yeremia 2:3. Nini kiliwatokea maadui wa watu wa Mungu katika kipindi cha safari ya jangwani na baada ya safari hiyo? (“Walipatwa na maafa.”)
1.                  Je, Bado Mungu anawatendea kwa jinsi hii maadui wa wale wanaompenda?
I.                   Uchambuzi wa Mungu wa Wakati Uliopo
A.                Soma Yeremia 2:4-5. Mungu anawachukuliaje “baba” za watu wa Israeli? (Hawakuwa na “thamani” kwa sababu wanafuata “miungu isiyo na maana.”)
1.                  Angalia kwa makini kile ambacho Mungu anakisema. Je, anamwangalia nani upya mtu ambaye huenda ana makosa? (Mungu anaonekana kujichunguza yeye mwenyewe. “Baba zenu waliona dhuluma gani kwangu?” Kwa dhahiri, Mungu hana makosa. Lakini anaangalia kwa namna gani mfano huu unavyoweza kutufaa. Mambo yanapokuwa hayaendi vizuri, kwanza tunatakiwa kujichunguza sisi wenyewe.)
A.                Soma Yeremia 2:6. Tunapojaribiwa kuzitegemea juhudi zetu wenyewe zitusaidia katika nyakati za shida, je, badala yake tunatakiwa kufanya nini? (Tunatakiwa kupitia upya historia yetu ya kuwa na Mungu. Shinikizo nililo nalo maishani kwa sasa ni ujengaji wa hoja kwa njia ya mazungumzo ninapotakiwa kufanya hivyo hivi karibuni katika Mahakama ya Rufaa ya Marekani. Ninaweza kukumbuka uzoefu wa aina hii mara mbili katika siku za nyuma nilipojenga hoja mbele ya sehemu tofauti za mahakama hii ya juu ambapo kwa mahsusi kabisa Mungu alijidhihirisha kwangu.)
A.                Soma Yeremia 2:7. Mungu analalamikia nini? (Aliwapeleka katika nchi ya ahadi. Lakini, wakainajisi.)
A.                Soma Yeremia 2:8. Nani ambaye, kwa mahsusi kabisa, alimwangusha Mungu? (Viongozi wa dini. Hawakumtafuta Mungu wala hata kumjua. Walizifuata sanamu.)
A.                Soma Yeremia 2:9. Je, watoto ni waaminifu zaidi kwa Mungu kuliko baba zao? (Hapana. Mungu anasema kwamba “kwa mara nyingine” analeta mashtaka dhidi ya watu wake na anatarajia kuendelea kuleta mashtaka dhidi ya uzao wao.)
1.                  Katika mojawapo ya asubuhi juma hili nilitiwa bumbuazi. Nchini Marekani “Mpango za Uzazi” (Planned Parenthood), ni shirika linaloshughulika na utoaji mimba na, kwa mujibu wa mafunuo ya hivi karibuni, limekuwa likiuza sehemu ya miili ya watoto. Takwimu zinaonesha kuwa kwa uwiano wa 2 kwa 1, Wamarekani wanataka serikali iendelee kulisaidia shirika hili kwa kutumia fedha za walipa kodi.  Hoja iliyopo ni kwamba fedha zinatumika kwenye malengo mengine ya muhimu zaidi. Je, Marekani ipo hatarini kushtakiwa na Mungu? (Yeremia anawaelezea watu wanaopaswa kuwa watu wa Mungu, na si wapagani. Wapagani walikuwepo katika nchi na kwa kiasi kikubwa Mungu alikuwa ameshawafukuza. Watu wa Mungu wanapokuwa wapagani, basi Mungu anasema kuwa atachukua hatua.)
A.                Soma Yeremia 2:10-11. Fikra iliyokuwepo kipindi hicho ni kwamba mungu alikuwa na mipaka. Ilikuwa ukiishi katika eneo fulani basi alikuwepo mungu fulani aliyekuwa anatawala eneo hilo. Mungu wetu anasema kuwa watu wanashikilia miungu yao ya bandia, kwa nini watu wake wamwache Mungu wa kweli? Unaweza kutoa jibu gani?
A.                Soma Yeremia 2:12-13. Mungu analeta mashtaka gani mahsusi dhidi ya watu wake? (1. Wamemwacha. 2. Wamejaribu kufanya mambo kwa kufuata njia zao wenyewe.)
1.                  Je, hili ni tatizo kwa kiasi gani maishani mwako?
A.                Soma Yeremia 2:14-15. Je, Israeli ilikuwa mtumwa tangu kuzaliwa? (Hapana! Mungu aliwaokoa kutoka Misri. Baada ya kifo cha Sulemani, walikuwa (Israeli) Ufalme wa Kaskazini. Waliangukia kwa Ashuru.)
1.                  Mungu anamaanisha nini? (Angalia mazingira yanayokuzunguka! Angalia jinsi kugeuka na kumwacha Mungu kunavyoelekea kwenye uangamivu.)
1.                  Je, umeona jambo hili katika maisha ya watu wengine?
A.                Hebu turuke hadi chini na kusoma Yeremia 2:23. Je, watu walikiri kwamba walikuwa wamegeuka na kumwacha Mungu? (Hapana!)
1.                  Je, kuna chochote cha kujifunza kwa ajili yetu?
A.                Soma Yeremia 2:27. Inawezekanaje watu wanaofanya hivi wanaweza kusema kwamba hawajampa Mungu kisogo? (Hii inaonyesha uwezo wetu mkubwa sana wa kujidanganya sisi wenyewe kuhusu uhusiano wetu na Mungu.)
I.                   Kutangaza Hukumu
A.                Soma Yeremia 27:3-4. Je, haya ndio mataifa yanayomfuata Mungu wa kweli? (Hapana! Lakini, wanakutana na Mfalme wa Yuda. Inaonekana wanaungana pamoja ili kujaribu kuishinda Babeli.)
A.                Soma Yeremia 27:5-7. Mungu anajenga wapi msingi wa mamlaka ya kauli yake? (Yeye ni Muumba wetu.)
1.                  Je, mamlaka ya Mungu yanashambuliwa kwa kiwango gani leo?
1.                  Je, mawazo yako kuhusu Uumbaji yanaakisi endapo unaabudu vitu vilivyotengenezwa kwa mikono yako?
1.                  Je, ni nini hatma ya hawa wafalme wa kipagani na Mfalme wa Yuda? (Wote watashindwa na Nebukadreza.)
a.                   Unakumbuka hapo awali tulijadili suala la endapo Marekani inaweza kuwa hatarini kuhukumiwa kwa sababu ya kuusaidia na kuuendeleza uovu? Ikiwa wapagani wanajihusisha na uovu, na wala si Wakristo, je, hilo litatuokoa? (Mungu analeta hukumu kwa haya mataifa ya kipagani.)
A.                Soma Mwanzo 18:32. Pitia sura hiyo kwa haraka haraka ikiwa hukifahamu kisa hiki. Je, hii inaashiria nini kwa wafuasi wa Mungu wanaoishi kwenye mataifa yasiyomfuata Mungu? (Kuna idadi ya wafuasi wanaoweza kuzuia hukumu kwa taifa lote.)
A.                Soma Yeremia 5:1. Idadi gani ya wenye haki inahitajika hapa? (Mtu mmoja tu!)
1.                  Hivi karibuni nilikuwa kwenye mkutano ambapo mhubiri alihubiri kuhusu hukumu. Sijasikia somo linalohusu hukumu kwa muda mrefu sana. Hubiri hilo lilikuwa linavutia sana. Je, tunapaswa kuitikiaje onyo linalohusu hukumu?
A.                Soma Yeremia 27:8. Je, kuna njia yoyote ya kuepuka hukumu ya Mungu? (Soma Yeremia 1:17-18. Kila mtu anatakiwa kuwa mwaminifu kwa Mungu. Hii ndio ahadi ya Mungu kwa Yeremia. Mungu anatutaka tumgeukie. Hapendi kutuadhibu. Hata hivyo, Mungu anatutaka tuutangaze ujumbe wake kwa ulimwengu. Ikiwa kuna idadi kubwa inayotakiwa kuepuka hukumu, tunatakiwa kutenda kazi ili kuileta idadi hiyo kwa Mungu.)
A.                Soma Yeremia 27:9-10. Jambo gani linaifanya (linaitatanisha) hukumu ya Mungu kuwa ngumu zaidi? (Wapo watu wengi wanaoleta mkanganyiko kwenye neno la Mungu. Wanasema kuwa hukumu haitakuwepo.)
A.                Soma Yeremia 5:3. Kuna tatizo gani kwenye asili yetu ya kibinadamu? (Badala ya kukubali kubadilishwa, tunaifanya mioyo yetu kuwa migumu.)
A.                Soma Yeremia 27:11. Ujumbe wa Yeremia una umaarufu kwa kiwango gani? (Fikiria endapo ungekuwa unaishi Marekani na nikatabiri kwamba kwa sababu ya dhambi zetu, China, taifa ambalo halijisingizii kumfuata Mungu, litaivamia Marekani. Endapo unataka kuishi, unatakiwa kujisalimisha katika sheria za China. Vipi kama nitabadilisha na kutumia nchi ya Iran badala ya China?
1.                  Je, ujumbe wa toba na hukumu una umaarufu kiasi gani siku hizi?
A.                Rafiki, je, unamtegemea Mungu au unajitegemea wewe mwenyewe? Je, utaufungua moyo wako na akili yako ili kurekebishwa na Mungu? Kwa nini usimgeukie Mungu leo?

I.                   Juma lijalo: Wafalme Watano wa Mwisho wa Yuda.

No comments:

Post a Comment