Tarehe
17 Oktoba 2015, imetengwa na Kanisa la Waadventista wa Sabato
ulimwenguni, kuwa siku ya kutambua mchango wa wachungaji wake wanaofanya
kazi katika mazingira magumu na ya kujinyima. Huu ni wakati maalumu
katika mwaka, wa kuonesha utambuzi na shukrani za mitaa, makanisa, na
mshiriki mmoja mmoja kwa wachungaji wao ambao hutumia muda mwingi
kuwahudumia waumini hao kiasi cha hata wengine kushindwa kuzihudumia
familia zao inavyostahili. Wachungaji wetu licha ya kutoa mahubiri kila
wakati, wamekuwa pia wakitembelea washiriki, makundi na makanisa,
wakiwaombea, wakitoa ushauri wa kiroho na kifamilia, na huduma zingine
mbalimbali za kijamii.
Kanisa
mahalia au mtaa uandae mhubiri atakayechambua namna mchungaji
anavyojitoa mhanga katika kuwatumikia watu wa Mungu na jinsi waumini
wanavyopasa kumtia moyo na kushirikiana naye. Miongoni mwa mafungu
anayoweza kuyatumia ni kama; “Lakini, ndugu, tunataka mwatambue wale
wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana, na
kuwaonyeni; mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao. Iweni
na amani ninyi kwa ninyi. (1 Thess. 5:12, 13), na “Wakumbukeni wale
waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa
kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao.” (Waeb.
13:7). Kwa kadri itakavyowezekana nyimbo za tukio hili ziendane na
kutambua huduma inayotolewa na mchungaji.
Hii
ni siku ya kutambua jinsi mchungaji alivyotumia vipawa, muda, nguvu na
mali zake katika kusaidia kusukuma maendeleo ya watu anaowasimamia
kufikia hapo walipo sasa. Kwa wengine itakuwa siku ya kumtambua
mchungaji aliyekubatiza, aliyefunga ndoa yako, aliyekuhubiria ukweli
uliokuweka huru, au aliyefanya jambo maalumu la kukusaidia kimaisha.
Hata kama ni mchungaji anayehudumu mbali na ulipo huu ndiyo wakati wa
kuwasiliana naye na kumjulisha kuwa unathamini huduma aliyokutendea na
unamuombea. Ni siku pia ya kutoa ushuhuda mbele ya familia ya mchungaji
juu ya namna unavyoguswa na huduma yake, kwa wengine watakaokosa nafasi
hiyo watatumia njia zingine za mawasiliano kufikisha ujumbe huo, kama
mazungumzo ya simu, ujumbe mfupi wa maneno, kadi, barua, na mitandao ya
facebook, au Whatsap.
Katika
siku hiyo chakula cha pamoja chaweza kuandaliwa na zawadi kadhaa
zikatolewa kwa mchungaji na familia yake kama ishara ya kutambua mchango
wake. Zawadi si lazima ziwe kubwa bali zilenge kurahisisha kazi zake
mfano chombo cha usafiri au ukarabati mdogo wa chombo chake cha usafiri,
uboreshaji wa ofisi ya mchungaji, au uboreshaji wa mazingira anapoishi,
zinafaa sana katika juma hili. Licha ya kutoa zawadi ya vitu
watakaojisikia kuwapatia familia ya mchungaji au mchungaji mwenyewe
fursa fulani maalumu ambayo wamekuwa wakiikosa pia wanaweza kufanya
hivyo. Fursa hizo ni kama ya kutembelea maeneo maalumu ya kiutalii,
maeneo ya kihistoria ya Biblia (Israel n.k.), ama fursa ya kwenda kusoma
nk. Waumini wanaweza kuandaa cheti au ngao ya kutambua mchango wa
mchungaji wao ambapo yaweza kuandikwa hivi.
CHETI CHA UTAMBUZI
Tunatambua
mchango wa kujikana nafsi uliotolewa na [Jina la Mchungaji] na [Mke wa
Mchungaji] na Familia yao, katika kusaidia kulijenga kanisa/mtaa
___________
Leo tarehe 17, Oktoba, 2015
Kwa
kutambua kuwa mchungaji anazungukwa na majaribu mengi na ya kuwa yeye
naye ni binadamu mwenye madhaifu mbalimbali, itakuwa jambo la muhimu
siku hiyo au siku kadhaa kabla ya siku hiyo kuwa na maombi maalumu kwa
ajili yake na familia yake. Pia kikundi maalumu cha viongozi wa kanisa
waweza kupanga ziara nyumbani kwa mchungaji katikati ya juma ili
kuisalimu familia, kuiombea na kuipa maneno ya faraja. Katika juma la
kuelekea Sabato ya utambuzi wa huduma ya mchungaji somo maalumu linaweza
kuendeshwa likisimamiwa na wazee wa kanisa kwa mashauriano na mchungaji
wa mtaa na mkurugenzi wa wachungaji wa konferensi husika. Hebu kila
mmoja shiriki kikamilifu kuifanya siku ya kutambua huduma ya Mchungaji
kuwa yenye mafanikiko. Kila la heri na Mungu awabariki.
IMETOLEWA NA KATIBU WA WACHUNGAJI - STU
No comments:
Post a Comment