NENO LA LEO - HATARI AMBAYO WENGI HAWAIJUI

Mathayo 24:37 "Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adam".

Kati ya mambo yaliyowatatiza wanafunzi wa Yesu, ilikuwa ni kujua siku ya Mwisho wa dunia, hata hivyo Yesu alisema hakuna ajuaye siku wala saa (Mathayo 24:36), badala yake alitoa mfano wa tukio lililotukia katika kizazi cha Nuhu. Yesu alisema Kwa wakati tusiodhani ndipo tutashuhudia mlango wa rehema unafungwa, na Mwana wa Adam anaonekana.

Jambo lingine la hatari ambalo wengi linawapata bila kujiandaa, na hatimae kuishia Jehanamu ya moto ni MAUTI. Tunashuhudia watu wengi wanakutwa na mauti bila taarifa, hivyo sio rahisi kujiandaa na kukutwa na kifo wakiwa na maisha matakatifu. Wengi wanaishi maisha ya kubahatisha, hawana uhakika juu wokovu wao. 

Kumbuka kizazi cha Nuhu kilifutiliwa mbali kwa Gharika baada ya Mungu kuona UASI umezidi, kila kusudi na mawazo ya Mwanadamu yalikuwa yamejaa UOVU tu. Kizazi chetu kinaenda mbio kutelemkia maovuni zaidi ya kizazi cha Nuhu, mbali na upendo wa Kristo kufa kwa ajili yetu, na kukirimiwa uwezo kwa njia ya Roho mtakatifu, ndio kwanza watu wanaziba masikio wasisikie maonyo na kuendelea na maisha ya Dhambi.

Yeyote anayejiita Mkristo, Muislam au mtu wa dini yoyote, huku akiendelea kutenda dhambi za wazi au za siri, anaiongeza hasira ya Mungu na kuharakisha siku ya Mwana wa Adamu. Kuhudhuria ibada makanisani au misikitini, huku miguu imesimama katika matope ya uovu na moyo ukizidi kufurahia maisha hayo ya dhambi bila toba ya kweli, ni kujitia katika Laana na Hasira ya Mungu. 

Huu ni wakati wa wenye hekima kufanya maamuzi ya kusimama mahali salama, sio salama kuishi maisha ya kubahatisha, wokovu ni hakika katika Kristo.

NAWATAKIA MAISHA YA USHINDI NA YENYE KUJAA BARAKA TELE KATIKA KIZAZI HIKI CHA UASI

Na. Ev. Eliezer Mwangosi

No comments:

Post a Comment