Somo La 7 | Yesu : Bwana wa Utume

(Mathayo 10 & 28, Marko 16)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Yesu anatufundisha nini kuhusu kupeleka injili kwa watu wengine? Anatupatia dondoo gani za “kimisionari?” Dondoo mojawapo ya kufurahisha inahusu nuru na utume. Dondoo nyingine inatusaidia kuuelewa “Ufalme wa Mungu” vizuri zaidi. Hebu tuchimbue somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!
I.                   Nuru
A.                Soma Isaya 7:14 na Isaya 42:6-7. Huu ni unabii kuhusu ujio wa Yesu. Kazi gani za kimisionari za Yesu zinatabiriwa? (Angalia kipengele cha nuru. Atakuwa “nuru” ya Mataifa. “Atayafunua macho.”  Atawatoa “walioketi gizani” katika nyumba ya kufungwa.)
1.                  Je, hii inaashiria kuwa kazi ya mmisionari ni ipi?
B.                 Soma Luka 2:8-11. Huyu malaika mpweke aliambatana na nini? “Utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote.” Kwa mara nyingine tena, hii ni rejea ya nuru kuu.)
C.                 Soma Luka 2:25-32. Simeoni anasema kuwa kazi ya Yesu ni ipi? (Yesu ni “nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa.” Yeye ni “utukufu wa watu wako Israeli.”)
1.                  Tuchukulie kwamba kuna kitu unakitafuta na unapata wakati mgumu sana kukipata. Unapoongeza mwanga zaidi, je, unabadili kile unachokitafuta? (Hapana. Mwanga unakuruhusu tu kukiona na kukielewa vizuri zaidi. Hata unaweza usijue kuna kitu kipo mahali pale ikiwa hutakuwa na mwanga wa kutosha.)
D.                Tunapoendelea kutafakari fursa tulizonazo za kushirikiana na watu wengine, je, wazo la kupeleka “nuru” kwa watu wengine linaashiria nini? (Hatuhitajiki kuwapa watu habari mpya kwa kiasi kikubwa zaidi ya kuwasaidia kuelewa zaidi taarifa ambayo tayari wanayo.)
II.                Nuru na Ufalme wa Mbinguni
A.                Soma Mathayo 10:5-6. Hapo awali tulijifunza unabii uliosema kwamba Yesu alikuwa nuru kwa Mataifa. Unaelezeaje msisitizo huu? (Je, umegundua kwamba unahitajika kujikita kwenye mwanga ili kuufanya uangaze zaidi? Katika Osisi (Foundation)  ninayofanyia kazi, miaka kadhaa iliyopita taasisi hii iliamua kuwa na lengo dogo. Kwa kuelekeza nguvu zetu kwenye jambo mahsusi, tunaweza kuleta mabadiliko. Yesu hawatengi watu wa Mataifa, badala yake anajikita kwenye utume wa wanafunzi wake katika kipindi hiki.)
B.                 Soma Mathayo 10:7. Yesu anawapa wanafunzi wake ujumbe mfupi sana: “Ufalme wa mbinguni umekaribia.” Je, hiyo inamanisha nini?

C.                 Soma Mathayo 3:1-3. Yohana Mbatizaji alihubiri ujumbe gani? (Alihubiri ujumbe ule ule: “Ufalme wa mbinguni umekaribia.”)
1.                  Yohana alimaanisha nini kwa ujumbe huu? (Kwamba Yesu alikuwa anakuja!)
D.                Soma Danieli 7:13-14. Danieli aliona nini katika njozi? (Jambo lile lile! Kwamba ufalme wa Yesu ulikuwa unakuja!)
E.                 Yesu alikuwepo wakati anawaambia wanafunzi kuhubiri kwamba ufalme wa mbingu umekaribia. Kwa nini asiseme kwamba ufalme huo upo hapa?
F.                  Soma Warumi 14:17-18. Nini kinaufanya ufalme wa mbingu? (“Haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu.” Yohana na Yesu walipozungumzia “ufalme wa mbinguni,” hawakumaanisha tu kwamba Yesu alikuwepo, walimaanisha kuwa watu watamkubali na kumpokea kama Mwokozi na Bwana. Watamfuata Yesu na kitendo hicho kingeleta “haki, amani na furaha.”)
1.                  Je, ufalme wa mbinguni upo ndani yako?
G.                Soma Matendo 1:6. Uelewa wa wanafunzi kuhusu ufalme wa mbinguni ulikuwaje? (Walikuwa wanauhubiri, lakini hawakuuelewa kikamilifu. Ufalme wa mbinguni umo ndani yetu. Unakuja kwako na kwangu sasa hivi.)
1.                  Kwa kuwa Yesu alikuwa anaondoka kipindi kile ili kurejea mbinguni, wanafunzi walielewaje jambo hili akilini mwao? (Soma Matendo 1:4-5. Ilikuwa ni umwagaji wa Roho Mtakatifu kwa uwezo mkubwa uliowasaidia kuelewa jambo hili kwa usahihi.)
H.                Hebu tuendelee na maelekezo ya kimisionari ya Yesu kwa wanafunzi wake. Soma Mathayo 10:8. Wanafunzi wamepokea nini? (Hii ni sehemu ya nguvu ya ufalme wa mbinguni – Roho Mtakatifu. Ikiwa tumepokea uwezo wa kuponya, tunapaswa kushirikiana na wengine uwezo huo. Kati ya fungu hili na sura mbili za kwanza za kitabu cha Matendo, tunaona jinsi Roho Mtakatifu alivyo wa muhimu sana katika kazi zetu za kimisionari.)
I.                   Soma Mathayo 10:9-10. Kila tukio la kimisionari nililohusika, hapakuwepo na kiingilio. Je, unathamini kitu ambacho umepewa tu?
1.                  Je, tunapaswa kubadili njia hii na kuweka gharama ya kiingilio kwa wale wanaokuja kwenye mikutano yetu ya kimisionari? (Yesu hakuwatoza watu fedha ili wamsikilize, lakini hapa anasema tuwabebeshe gharama wasikilizaji.)
J.                   Soma Mathayo 10:11-13. Yesu anaposema “amani yenu iifikilie [nyumba ya mtu mtakayeingia kwake], je, hii ni sehemu ya ufalme wa mbinguni? (Ndiyo!)
K.                Soma Mathayo 10:14-15. Hii inaashiria nini kuhusu majaribio kadhaa ya kumwongoa mtu? (Wakristo katika maeneo ya kazi wanaingia kwenye matatizo kwa sababu “wanawabughudhi” (hili si neno ninalopenda kulitumia) waajiriwa wenzao ili kuwa waumini. Fungu hili linatuambia kwamba tunatakiwa kufanya majaribio kadhaa ili kumwongoa mtu ambaye hana shauku ya kujifunza.)
L.                 Soma Mathayo 10:16. Unayaelewaje maelekezo haya? (Tumia akili yako! Tumia busara kwa namna ya dhati katika kupeleka injili kwa watu wengine.)
M.               Soma Mathayo 10:17-20. Tulizungumzia kuhusu lengo la awali la ujumbe wa injili. Ni nani ambaye sasa hivi amejumuishwa kwenye hadhira iliyokusudiwa? (Maliwali, wafalme na Mataifa.)
1.                  Endapo tu ungekuwa unakwenda nyumba kwa nyumba, je, ungekuwa na uwezo wa kumshuhudia mfalme au liwali? (Sio rahisi.)
a.                   Kitu gani kinafanya jambo hili liwezekane? (Mazingira magumu. Wanafunzi watashitakiwa kwa makosa ya jinai.)
2.                  Ninapokuwa ninajenga hoja mahakamani, huwa ninaandaa kwa makini kile nitakachokisema. Ninapohubiri, huwa ninalirudia rudia hubiri angalao mara saba kabla sijalihubiri kanisani. Kwa nini niwe na juhudi kidogo kwenye utetezi wangu mwenyewe ikiwa nitakamatwa na kushitakiwa? (Tutapewa maneno ya Mungu ili kuyasema. Maneno ya Mungu yana hadhi kubwa kuliko maneno yangu mwenyewe.)
a.                   Mungu si Mungu asiye na mpangilio. Kwa nini asubiri hadi dakika ya mwisho ili aniambie maneno yake? (Nadhani jambo la msingi ni kwamba hatupaswi kuwa na wasiwasi.)
III.             Imani
A.                Soma Mathayo 28:16-17 na Marko 16:14. Tutaingia kwenye “Utume Mkuu” katika mafungu yanayofuata kila fungu kati ya haya tuliyoyasoma. Unaelezeaje huku kutokuwa na imani kuhusu ufufuo wa Yesu?
1.                  Wakosoaji wa Biblia wanasema kuwa visa vya ufufuo ni vya uongo. Endapo ungekuwa unatunga kisa cha kufufuka kwa Yesu, je, ungeingiza maoni kama haya? (Hapana! Ungesema kwamba “kila mtu anafahamu kuwa Yesu alifufuka.”)
2.                  Je, una vigezo vya kupeleka injili?
B.                 Soma Marko 16:15-16. “Habari njema” ni ipi? (Habari njema ni kwamba Ufalme wa Mbinguni umekaribia, Yesu aliishi maisha makamilifu, akafa kwa ajili yetu, na alifufuka katika uzima wa milele – hivyo kutuhakikishia uzima wa milele ikiwa tutaamini na kubatizwa. Hii inatupatia “haki, amani na furaha katika Roho Mtakatifu.” Warumi 14:17-18.)
C.                 Soma Marko 16:17-18. Je, tunapaswa kujumuisha ushikaji wa nyoka kwenye huduma zetu za ibada? Ikiwa umesema, “Hapana!” je, unaelezeaje jambo hili?
1.                  Angalia kwa makini kila jambo ambalo Yesu analibainisha kwa umahsusi. Endapo ungetakiwa kuongoza timu ya safari ya kimisionari katika nchi ya kigeni, je, ungehitaji “zana” gani? (Ungetakiwa kuwasiliana na watu, ungetakiwa kukingwa dhidi ya mashambulio ya wanyama au kunywa au kula kitu kitakachokufanya uugue. Ungetakiwa kuepuka pepo. Kutenda miujiza huleta hadhira ya watu kusikiliza ujumbe wako. Hivi si “viburudisho,” hizi ni zana za kimisionari.)
D.                Soma Mathayo 28:18-20. Yesu anatupatia jukumu na ahadi gani? (Kuwafanya watu kuwa wanafunzi, kubatiza, na kuwafundisha kuhusu mapenzi ya Mungu. Mungu anaahidi kuwa pamoja nasi (kwa njia ya Roho wake Mtakatifu) hadi mwisho.)

E.                 Rafiki, je, unakubali jukumu alilokupatia Yesu? Je, utafuata dondoo zake na kutumia zana zake ili kushiriki na watu wengine kwamba Ufalme wa Mbinguni umekaribia?

IV.             Juma lijalo: Utume Katika Tamaduni Mbalimbali.

No comments:

Post a Comment