Sehemu ya Pili: i/Wakati wa Yesu.
Biblia
Agano Jipya inaelezea matukio yaliyojili katika Ujio wa Masihi, Yesu
Kristo mwana wa Mungu kama Mwokozi wa Ulimwengu, na Uanzishwaji wa
Kanisa kama taasisi inayoundwa na Wafuasi wake. Injili zote Nne zaeleza,
Kazi, matendo makuu na mafundisho aliyofundisha Bwana Yesu akiwa hapa
duniani wakati wa Utu uzima wake. Inasadikika kuwa, Yesu alianza huduma
yake ya hadhara (Public Ministry) akiwa na umri wa miaka kama 27, huduma
ambayo aliifanya kwa muda wa miaka 3½ .
Yapaswa
ieleweke kwamba, ujio huu wa Yesu Kristo haikuwa Mara yake ya kwanza
kujihusisha na Wanadamu moja kwa Moja. Maandiko yanaweka wazi kwamba,
yeye Yesu, ndiye aliyeumba dunia hii, (Yohana 1:1-14, Kol 1:16-17). Ni
Yeye Yesu aliyewatokea manabii wa zamani kwa umbo la kibinadamu, Mfano.
Ibrahimu katika Mwanzo 18-19. Katika kisa hiki cha Ibrahimu, tunaona
watu watatu wakija kwake nay eye akawakarimu kwa chakula. Mmoja kati ya
watu hao watau anatambulikana kama BWANA kwa herufi kubwa. Kisha kisa
kinaendelea kusema “Kisha watu hao wakaondoka huko wakaelekeza nyuso zao
Sodoma, Ibrahimu akaenda pamoja nao awasindikize. BWANA akasema, Je
nimfiche Ibrahim jambo nilifanyalo?” Mwanzo 18:16-17. Katika kisa cha
Yoshua, tunapata tena maelezo ya Jemedali wa Majeshi aliyemtokea Yoshua.
Neno lina sema, “Ikawa hapo Yoshua lipokuwa karibu na Mji wa Yeriko,
akavua macho yake na kuangalia, na tazama mtu mmoja akasimama kumkabili
mbele yake naye alikuwa na upanga wazi mkononi mwake. Yoshua kamwendea
na kumwambia, Je wewe u upande wetu, au upande wa adui zetu? Akasema La,
lakini nimekuja sasa, nili amiri wa Jeshi la BWANA. Yoshua akapomoka ki
usouso hadi chini, naye akasujudu, akamwuuliza, Bwana wangu aniambia
nini mimi mtumishi wake? Huyo amiri wa jeshi la Bwana akamwambia Yoshua,
Vua viatu vyako miguuni mwako; kwakuwa mahali hapo usimamapo ni
patakatifu, Yoshua kafanya hivyo” Yoshua 5:13-15. Maneno ya namna hii
pia aliwahi kuambiwa Mtumishi wa Mungu Musa katika Kutoka 3:5 na
aliyetamka maneno hayo akajitambulisha kuwa jina lake ni MIMI NIKO
AMBAYE NIKO. Yesu mwenyewe akiwa hapa duniani aliwahi kujitambulisha kwa
Wayahudi waliokuwa wanalijua vyema jina hilo katika Yohana 8:58. Yeye
ndiye aliyewaongoza wana wa Israel toka Misri kwenda katika nchi ya
Kanani (2Korintho 10:1-4). Kwa maana hiyo tunaweza kuwa na ujasili wa
kusema, Ni yeye Yesu aliyetoa amri 10 Katika mlima wa Sinai. Ni Yesu
aliyewaokoa Shadrak , Mishak na Abednego katika tanuru la Moto
alipojidhihirisha pamoja nao Katika Tanuru. HAKIKA YESU NI MUNGU PAMOJA
NASI—HALELUYA. Ni Yesu mwenyewe aliyekuja kwa Daniel Katika Daniel sura
ya 10. Hii ni kwa sababu utambulisho wake ni yakini kama vile ulivyokuwa
utambulisho wake katika Ufunuo 1:12-18. Yesu amekuwa akijifunua kwa
watu wake hata baada ya Ufufuo wake kama vile kwa Sauli katika Matendo
Sura ya 9:1-9. Siku zote milele hata milele Yesu amekuwa “kama stadi wa kazi” zote za Mungu Baba. Methali 8:30 na Neno lake analolituma kila wakati Yohana 1:1 , Mungu pamoja nasi Mathayo.1:23
Kwanini
nimeleta utangulizi huu? Ifahamike kuwa kusudi la Yesu kuja hapa
duniani siyo kuja kujipinga yeye mwenyewe kana kwamba ni kigeugeu. Yeye
mwenyewe anasema “Kwa kuwa mimi BWANA sina kigeugeu, ndiyo maana ninyi
hamkuangamizwa…” Malaki 3:6
Mpango
wa wokovu halikuwa jambo la ghafra kwa Mungu, kabla hata ya kuumbwa
mwanadamu, Mungu alikuwa amekwisha kuandaa mpangao wa ukombozi ikiwa
mwanadamu angeasi. Ndiyo maana tunaambiwa Yesu Kristo ni “mwanakondoo
aliyechinjwa tangu kuwekwa kwa misingi ya dunia: Ufunuo 13:8. Kuja kwake
hapa duniani kulikuwa ni kwaajili ya kutimiza mpango huu ulioandaliwa
toka mapema, na ukahubiriwa kwa Israel kwa njia ya vielelezo vya huduma
ya Patakatifu iliyohusu mtu mwenyedhambi kutoa sadaka ya mwana kondoo
asiye na Ila. Damu ya kondoo huyo ilipomwagika ilikuwa ni kwa kusafisha
dhambi.
Yesu
alitabiriwa na manabii kabla ya kuja kwake hapa duniani. Manabii
walitabiri Mahari pa kuzaliwa (Mika 5:2). Jinsi ya kuzaliwa (Isaya
7:14), Huduma yake (Isaya 61) Kusalitiwa kwake (Zaburi41:9) Thamani ya
kusalitiwa kwake (Zab. 11:12) Mateso yake (Isaya 50:6) Matokeo ya kifo
chake (Isaya 53). Karibia mambo zaidi ya 100 yaliyomhusu Yesu
yalitabiriwa kabla ya kuzaliwa kwake.
Yesu
Mwenyewe alipokuja alisema “Dhabihu na toleo hukutaka, lakini mwili
uliniwekea tayari. Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi
hukupendezwa nazo; ndipo niliposema. Tazama, nimekuja, kadika gombo la
chuo nimeandikiwa, Niyafanye mapenzi yako Mungu” Waebrania 10:5-7.
Wanafunzi wake wakishangaa juu ya yale yaliyotokea kuhusu kifo chake,
aliwatokea na kuwaambia “Je haikumpasa Kristo kupata mateso haya na
kuingia katika utukufu wake? Akaanza kutoka Musa na manabii wote,
akawaeleza katika maandiko yote, mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe” Luka
24:26-27 “ Kiasha akawaambia hayo ndiyo maneno yangu iliyowaambia
nilipokuwa nikali pamoja nanyi, yakwamba ni lazima yatimizwe yote
niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii, na Zaburi” Luka
24:44
Hivyo
ni wazi kwamba Kuja kwake hapa duniani hakukuwa ni kwaajili ya kuanzisha
jambo jipya, isipokuwa kuenenda kama ilivyoandikwa, katika Torati ya
Musa na Katika Manabii na Zaburi.
Kuhusu Swala la Ibada Je iliandikwa nini katika Torati ya Musa?
“Mtafanya
kazi siku sita, lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa,
Kusanyiko takatifu,, msifanye kazi ya namna yoyote, ni SABATO KWA BWANA,
katika makao yenu yote.” Lawi 23:3.
Je Yesu Pia litimiza agizo hili, la kukusanyika katika siku ya Sabato kama siku ya Ibada?
“Akaenda zake Nazereti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake” Luka 4:16
Neno
desturi linamaana ya Kawaida, au siku zote au utamaduni wa kila siku.
Biblia haituambii wazi kuhusu, maisha ya awali ya utoto wa Yesu, yaani
kuanzia alipozaliwa hadi umri wa miaka 27. Tunaambia katika Luka 2:21
“hata zilipotimia siku 8 za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama
alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba” pia katika Luka 2:22
tunasoma “Kisha zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati
ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana. Kama
ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana. Kila mtoto mwanamme aliye kifungua
mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana”
Hii
inaonyesha kwamba Yesu katika Maisha yake yote alitii maagizo yote ya
Amri za Mungu kama ilivyoandikwa katika Torati ya Musa. Wala hakuwa na
jambo geni la kuanzisha hapa duniani. Ndiyo mana Mwenyewe anasema
“…kamavile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika Pendo
lake” Yohana 15:10. Hakika Yesu alshika amri za Mungu zote kwani
Maandiko yanamshuhudia “…bali yeye alijaribiwa sawa sawa na sisi katika
mambo yote, bila kufanya dhambi” Waebrania 4:15. Hakuna jaribu
linalompata Mwana damu ambalo halikumpata Yesu. Hakuna ushahidi wowote
wa kimaandiko kuonyesha kwamba Yesu kwa njia yoyote ile aliwafundisha
wanafunzi wake kutotii amri za Mungu. Badala yake tunaona akisisitia
kuwa utunzaji wa amri za Mungu ni kigezo cha kuupata uzima wa milele.
Tunasoma katika Mathayo 19:17 “…lakini ukitaka kuingia katika uzima,
ZISHIKE AMRI.” Baadaye Yesu ananukuru Kutoka 20:1-17. Mitume wake
walimwelewa vyema juu ya hili, kwani nao baadaye baada ya yeye kupaa
mbinguni, nao walifundisha hivyo “Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki
amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake.” 1Yohana 2:4.
Kwa
nini Yesu aliishi maisha haya Matakatifu? “kwa sababu ndiyo mlioitiwa,
maana Kristo naye aliteswa kwa ajili Yenu, akawaachia kielelezo mfuate
nyao zake. Yeye hakutenda dhambi wala hila haikuonekana kinywani mwake.
Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano, alipoteswa hakuogofya, bali
yeye alijikabidhi kwake ahukumuye kwa Haki. Yeye mwenyewe alizichukua
dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tukiwa wafu kwa mambo ya
dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.”
1Petro 2:21-24.
Sote
tunafahamu ni nini maana ya kufuata nyao. Haitakuwa sawa kusema unafuata
nyayo za mtu wakati wewe unatembea kuelekea mashariki na yeye anatembea
kuelekea magharibi. Kufuata nyao ni kukanyaga mahali alipokanyaga
mtangulizi wako. Yesu alishika amri za Mungu ili kutufundisha sisi namna
ya kuzishika. Akiwa ametwaa ubinadamu, aliishi maisha kama ya mwanadamu
asilimia mia moja, huku akimtegemea Roho Mtakatifu kumtia nguvu. Nasi
yatupasa kuishi bila dhambi kwa kutii amri zake tukiwezeshwa na Roho
Mtakatifu. Yohana anasema “Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake,
imempasa kuenenda mwenyewe vilevile kama yeye alivyoenenda” 1Yohana 2:6
YESU NA MAPAMBANO YA MAFARISAYO DHIDI YA SABATO
Katika
vitabu vya Injili, tunaona mara kwa mara Yesu akiingia katika marumbano
na mafasisayo juu ya utunzaji wa sabato. Hii imetafsiriwa na Wakristo
wengi kuwa Yesu hakuitambua Sabato ama haikuwa na umuhimu kwa Yesu. Kama
niliivyoeleza hapo juu ikumbukwe kuwa Yesu mwenyewe ndiye mtoa Amri ya
utunzaji wa sabato kama siku ya kumwabudu Mungu. Katika sehemu ya kwanza
ya mada hii tuliona sababu nyingie ya kutolewa kwa Amri ya utunzaji wa
Sabato ni kukumbuka kuwa mbingu na dunia ziliimbwa kwa siku sita na
katika siku ya saba Bwana akamaliza kazi yake yote ya uumbaji na
kustarehe. Bila shaka Yesu kama muumbaji bado anatamani hata leo wafuasi
wake waendelee kukumbuka uumbaji huo, ili baadaye wasije wakampatia mtu
mwingine utukufu na sifa ya uumbaji. Mapambano ya mara kwa mara na
mafarisayo juu ya utunzaji wa sabato yaonekana yalisababishwa na uelewa
potofu juu ya Sabato hiyo uliosababishwa na mafundisho ya mapokeo ya
Wazee wa Kiyahudi na Mafarisayo hao.
Mafarisayo
walienzi mapokeo ya mababa zao. Mapokeo haya hayakuwa maandiko ya Neno
la Mungu, bali tafsiri ya Neno hilo kama ilivyofundishwa na wazee wa
zamani. Haikuwa ruhusa kwa mafarisayo kuandika mapokeo haya katika
kitabu kwa hofu kwamba nayo yangefanywa kuwa Maandiko matakatifu. Hivyo
maandiko hayo yalipokelewa kizazi baada ya kizazi kwa njia ya
masimulizi. Dini ya Mafarisayo wao walidai kuwa WARITHI WA EZRA
MWANDISHI na baraza lake ambalo lilijulikana kama Baraza Kuu—huu ndiyo
ulikuwa mwanzo wa baraza la SANHEDRIN. Ezra pamoja na baraza lake kuu
waliaminika kuwa wao ndiyo waliohifadhi sheria hizi zilizopokelewa kwa
mdono (Oral Laws) hadi wakati wa Musa. Sheria hizi zilikuwa ni aina ya
tafsiri zilizotolewa juu ya maandiko ya Agano la Kale, na tafsiri hii
ilibidi ipitishwe na kukubarika katika baraza. Soma Kumb. 17:8-12. Hivyo
mawazo ya Marabi yakajengwa juu ya ufafanuzi wao wa Maandiko kufuatia
Tamaduni zilizojengeka kwa muda mrefu na ujanja. Ilifikia muda ambapo
maamuzi ya Marabi yakuwa na uzito kuliko maandiko menyewe. “Maneno ya
Waandishi ni ya kupendeza zaidi kuliko yale ya Maandiko matakatifu”
(Mdrash Rabbah, the song of songs, 1:2:2). Hivyo haishangazi kuona Yesu
akiwakemea Mafarisayo akisema “…mbona nyinyi nanyi huihalifu amri ya
Mungu kwa ajili ya Mapokeo yenu?” Tatizo halikuwa juu ya amri ya Mungu,
Tatizo lilikuwa juu ya Tafsri ya Neno hilo la Amri lililogubikwa na
Mapokeo. Sasa tuyaangalie mapambano ya Yesu na Mafarisayo kwa Muktadha
wa mapokeo yao
- Kuvunja Masuke siku ya Sabato
“Wakati
ule Yesu alipita katika mashamba siku ya Sabato; wanafunzi wake wakaona
njaa, wakaanza kuvunja masuke wakala. Na mafarisayo walipoona,
wakamwambia, Tazama, wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali
kulifanya siku ya Sabato” Mathayo 12:1-2
Katika
Kujibu mashitaka haya, Yesu anarejea kitendo cha Daudi kula Mikate ya
Wonyesho ambayo haikuwa “halali kwake kuila wala kwa wale wenziewe, ila
kwa Makuhani pekee yao”. Kisha akaendelea kusema “Wala hamkusoma katika
Torati, kwamba siku ya Sabato, Makuhani Hekaluni huinaji Sabato wasipate
hatia?” Mathayo 12:3-5. Katika kurejea mifano hi Yesu hakuwa na maana
kwamba Sabato haikuwa na umuhimu kwake. Ingekuwa rahisi kiasi gani
kutamuka wazi, “Wanafunzi wangu hawana haja ya kutunza sabato kwasababu
Sabato ilikuwa kivuli, na sasa mimi nikisha kuja Sabato imefutwa”.
Badala yake Yesu anawakumbusha Mafarisayo kwamba Siku zote kumekuwepo
mambo ambayo ni muhimu kuyatenda katika siku ya Sabato nabado watu
wasihesabiwe hatia. Mfano mzuri ni Makuhani. Katika siku ya Sabato
kulikuwa na mambo mengi ya kutumika kama sehemu ya ibada ambayo
yaliwafanya Makuhani siku hiyo washugulike kweli kweli. Walitakiwa
kufukiza uvumba katika madhabahu, kuhudumu katika utowaji wa sadaka ya
kuteketezwa Asubuhi na Jioni (Hesabu 28:9,10). Hivyo kulikuwa na wanyama
wengi wa kuchinja na kuni kuandaliwa kwa sadaka ya kuteketeza. KWA
KWELI HAKUKUWA NA UTUNZAJI WA SABATO KATIKA HEKALU. Na bado haya yote
haikuwa dhambi. Makuhani walifanya kazi ngumu zaidi katika siku ya
sabato kuliko siku nyingine yeyote ile, lakini kazi yao hii ilikuwa ni
kwa ajili ya kumtumikia Mungu na kwahiyo haikuwa dhambi. Yesu mwisho
anakazia kwa kusema “Lakini nawaambia kwamba, hapa yupo aliye mkuu
kuliko hekalu” Mathayo 12:7. Hivyo Bwana wetu Yuko juu ya Taratibu na
Kanuni za Ibada za Kiyahudi. Taratibu zote za ibada katika hekalu
zilimlenga Yesu kama mwana kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya
ulimwengu. Alikuja duniani kama mwokozi wa ulimwengu, na wanafunzi wake
waliambatana naye katika kazi hiyo ya kuokoa ulimwengu, KAZI HII ILIKUWA
TAKATIFU NA SIYO YA KIDUNIA, NA HIVYO ILIKUWA HALALI WAO KUONDOA NJAA
WAPATE NGUVU YA KUTENDA KAZI HIYO.
Ndipo
katika Marko 2:27 Yesu akaeleza Maana hasa ya Sabato. “Sabato ilifanyika
kwa ajili ya mwanadamu”. Ni siku ya kupumzika katika Uchovu wa kazi za
wiki nzima, ni siku ya Yeye mwanadamu kuitumia kwa ajili ya kutafakari
ukuu wa Mungu na kumwabudu, ni siku ya Kukumbuka kwamba Mbingu na nchi
ziliumbwa kwa siku sita na siku ya Saba Bwana akastrarehe. Mafarisayo
waliifanya Sabato ionekane kama siku ya Kutumikiwa na mwanadamu, badala
ya Sabato kutimiza mahitaji ya mwanadamu.
- Uponyaji katika Siku ya Sabato
“Kisha
akashuka kwenda Kapernaumu, mji wa Galilaya na katika za siku za Sabato
akawa anafundisha. Wakashangazwa sana na mafundisho Yake, maana maneno
Yake yalikuwa na mamlaka.
Ndani
ya sinagogi palikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, akapiga
kelele kwa nguvu akisema, “Tuache! Tuna nini nawe Yesu wa Nazareti? Je,
umekuja kutuangamiza? Ninakujua Wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa
Mungu.” Basi Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akisema, “Nyamaza na
umtoke!’’ Yule pepo mchafu akamwangusha chini yule mtu mbele yao wote,
akatoka pasipo kumdhuru. Watu wote wakashangaa wakaambiana, ‘‘Mafundisho
haya ni ya namna gani? Kwa mamlaka na nguvu, anawaamuru pepo wachafu,
nao wanatoka!” Habari Zake zikaanza kuenea kila mahali katika sehemu
ile.” Luka 4:38-39
Katika
uponyaji huu uliotendeka katika siku ya sabato pamoja na uliotendeka
katika Nyumba ya Petro(Math 8:14,15;Mariko 1:28-29) hatuoni Mafarisayo
wakileta upinzani. Jambo la kushangaza ni pale Yesu alipomponya mtu
aliye pooza mkono katikasiku ya sabato (Math 12:9-14;Mariko 3:1-6, Luka
6:6-11) na alipomponya mama mwenye pepo wa udhaifu Luka 13:10-17.
Kulingana
na Mariko 3:4 Yesu anawauliza Maswali Mafarisayo “Ni halali siku ya
Sabato kundenda mema au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuua?”. Kwa
swali hili Yesu hakuwa anapinga utunzaji wa sabato bali alikuwa
anawakumbusha mafarisayo kwani nao walifahamu wazi kabisa kwamba ni
HAALI KUNDA MEMA KATIKA SIKU YA SABATO. Ndiyo maana hawakutaka kumjibu
Yesu. Maandiko yanasema “wakanyamaza”. Ndipo katika Luka 13:15
akawakemea akisema “Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je, ni yupi kati
yenu hamfungui ng’ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi
aende naye kumnywesha?”
Niwazi
kabisa kwamba Mapambano ya Yesu na Mafarisayo juu ya utunzaji wa Sabato
hayakuwa yanalenga hasa kuonyesha kwamba Yesu alikuwa mvunja Sabato,
lakini kutafuta sababu za uongo na kweli ili wapate kumshitaki Yesu kuwa
anavunja amri za Mungu na hivyo kustahiri kuuawa. Tumeona kuwa
Mafarisayo walikuwa wamewatwika watu mzigo wa mapokeo na mafundisho
yaliyokuwa yametokana na kutafasiri vibaya Maandiko matakatifu. Kamwe
Yesu hakuenda kinyume na Amri za Mungu wala maadiko matakatifu. Hivyo
basi mifano yote ya Mapambano ya Yesu na Mafarisayo kuhusu utunzaji wa
Sabato haiwezi kuchukuliwa kuwa Yesu alikuwa anapinga Sabato, badala
yake alikuwa anaonyesha utunzaji sahihi wa Sabato na kuipatia Sabato
hadhi na heshima yake.
NA https://loudcrymediaministries.wordpress.com
No comments:
Post a Comment