(Mithali 20 - 22)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: “Hekima anuwai” ndivyo ambavyo mchambuzi wa
Biblia anavyorejea sehemu ya somo letu juma hili. Kauli hiyo imenipa tabasamu
usoni mwangu, kwa sababu usomaji wetu katika kitabu cha Mithali juma hili
unaonekana kuvurugika na wa kujirudiarudia. Jambo la kujirudiarudia ni jema –
walau kwangu binafsi. Huwa ninapenda mambo yajirudierudie ili yaweze kukaa
akilini mwangu. Katika madarasa ninayofundisha kwenye shule ya sheria, huwa
ninafundisha baadhi ya Mithali ambazo tutajifunza leo. Ingawa ninafundisha
Mithali hizo, huwa ninahitaji kujikumbusha – kitendo ambacho ni faida ya hekima
anuwai inayojirudiarudia! Juma lililopita nilitofautiana kimawazo na mmojawapo
wa mabosi. Nilidhani kwamba alikuwa amekosea, lakini Mithali inayohusu kuepuka ghadhabu
ya mfalme ilinijia akilini. Hebu tuzame kwenye Biblia na tusome kuhusu ghadhabu
ya mfalme na maelekezo mengine kwa lengo la kuwa na maisha yenye mafanikio
zaidi!
I.
Ghadhabu ya Mfalme
A.
Soma Mithali 20:2 na Mithali 19:12. Je, nani
ambaye ni “mfalme” maishani mwako? (Watu walio na mamlaka juu yetu.)
1.
Je, ungependa kusimama karibu na simba
aungurumaye? (Kitendo hicho hakifurahishi, kutosema chochote kuhusu
kuogopeshwa.)
2.
Unapotafakari kuhusu “umande juu ya majani”
hisia gani zinakujia akilini? (Hisia za kufurahisha. Hisia tulivu.)
3.
Je, umegundua kwamba hizi mithali zote mbili
zinaanza na maneno yanayofanana, lakini zinaishia na maonyo tofauti? Mithali moja
inaelezea upande chanya unaotokana na kuwa na uhusiano mzuri na mfalme, na
upande mwingine unaonya juu ya nini? (Kifo.)
B.
Soma Mithali 20:3. Tafakari migongano iliyopo
dhidi ya walio na mamlaka juu yako. Je, sababu gani inaweza kukufanya utake kujibizana
nao? (Majivuno ya mawazo ndio sababu kubwa. Kiburi chako kinapokusababishia
ujibizane na kiongozi (bosi) wako, basi “kifo” cha kazi yako kinaweza
kufuatia.)
1.
Je, kuna nyakati ambapo kujibizana na bosi wako
ni jambo sahihi? (Sina uhakika kama kujibizana kuna manufaa yoyote, ingawa bosi
mnyenyekevu atakuwa wazi kupokea mawazo mapya. Lakini, kuna nyakati ambazo
vigezo vya uaminifu, uadilifu na haki vinatutaka tupaze sauti zetu. Tunatakiwa tu
kufahamu kwamba kitendo hicho kinaweza kugharimu kazi zetu (yaani, kufukuzwa
kazi).)
C.
Soma Mithali 21:1. Je, njia bora ya
kushughulikia kutokubaliana na bosi wako ni ipi? (Hatupaswi kugombana, badala
yake tunapaswa kumwomba Mungu. Bosi ndiye msimamizi wetu wa kazi, lakini Mungu
ndiye msimamizi wa bosi (mfalme). Mungu anaweza kuuelekeza moyo wa mfalme
kwenye njia aichaguayo Mungu.)
D.
Soma Mithali 21:2. Tumejadili kwamba kiburi
chetu kinaweza kuwa chanzo cha kutokubaliana kwetu na “mfalme.” Je, kuna tatizo
gani la kukabiliana na majivuno yetu wenyewe? (Kuna uwezekano mkubwa wa
kushindwa kuona kiburi chetu wenyewe. Tunaweza kudai kwamba mjadala unahusu
uaminifu, uadilifu au haki, lakini huenda tunajidanganya tu wenyewe.)
E.
Soma Mithali 21:4. Je, kiburi chetu kinahusikaje
na jinsi tunavyoangalia mambo? (Hii ni sababu nyingine kwa nini hatuwezi
kuamini mawazo yetu wenyewe suala la majivuno linapohusika. Kiburi chetu ni “taa.”
Tunaona mambo kupitia kwenye majivuno yetu – na matokeo yake ni upotoshaji na
dhambi.)
1.
Je, tunapaswa kufanya nini ikiwa hatuwezi
kujiamini sisi wenyewe (kutokana na majivuno) katika kukabiliana na walio na
mamlaka juu yetu? (Soma Mithali 20:18. Tunatakiwa kuzungumza na watu wengine
ambao tunaamini hekima yao.)
F.
Soma Mithali 20:8. “Kupepeta/kupembua” ni neno
linalotumika katika kutenganisha ngano na majani makavu. Mfalme anawezaje “kupepeta”
kwa kutumia “macho” yake? (Mfalme makini anafahamu kinachoendelea. Kwa hiyo,
ikiwa mamlaka zilizopo maishani mwako ziko makini, zitatambua utakapopendekeza
jambo sahihi linalotakiwa kutekelezwa, na zitatambua pale ambapo ni majivuno
yako tu ndiyo kiini cha mazungumzo yako.)
1.
Je, unapaswa kufanya nini ikiwa mamlaka iliyopo
maishani mwako ni ya kiovu? (Nitabadili kazi fursa inapojitokeza.)
II.
Wavivu/Magoigoi
A.
Soma Mithali 20:4. Anguko la mtu mvivu hapa ni
lipi? Je, hafanyi kazi kabisa? (Hapana. Inaonekana kwamba hafanyi kazi kwa
umakini. Analima kwa wakati usio sahihi.)
1.
Kwa nini anatafuta mazao wakati alilima katika
kipindi kibaya? (Anatafuta kwa sababu anatarajia kupata.)
2.
Hapo kabla tulisoma kuhusu wavivu ambao ni
wazembe na wenye kupenda usingizi. Lakini, hiki kinaonekana kuwa kipengele
tofauti na kuwa mvivu. Tatizo la huyu “mvivu” ni lipi? (Mtu huyu mvivu hajajifunza
biashara yake. Hasomi maelekezo, hayuko makini (sio msikivu), wala hajitahidi
kutenda mambo yake vizuri zaidi.)
B.
Soma Mithali 22:13. Anguko la mvivu ni lipi
hapa? (Anaogopa kila kitu! Anafikiria matatizo ili kutafuta visingizio vya
kutokufanya kazi.)
C.
Soma Mithali 20:5. Je, umewahi kumwita mtu “mzembe”
(mvivu) isivyo sahihi?
1.
Je, tahadhari gani inatolewa hapa? (Watu wana
tabia nyingi, changamani (ni wagumu kufahamika). Tunatakiwa kuwaelewa kabla
hatujafikia hitimisho sahihi kuwahusu.)
D.
Soma Mithali 20:6 na Mithali 20:9. Je, sisi sote
ni wavivu linapokuja suala la dhambi?
E.
Soma Mithali 20:7. Kwa dhahiri, si kila mtu ni
mvivu linapokuja suala la dhambi! Soma Isaya 64:6. Je, unayalinganishaje mafungu
haya mawili? (Isaya 64:6 inaendana na Mithali 20:6 na Mithali 20:9. Nadhani lengo
letu ni Mithali 20:7. Manufaa yake ni kwamba tutawabariki watoto wetu kutokana
na tabia yetu sahihi.)
F.
Soma Mithali 20:16. Umasikini unaweza kutokana na
uvivu, lakini pia unaweza kutokana na upumbavu wa mtu. Je, tatizo la kwanza
linaloelezewa hapa ni lipi? (Mtu huyu anakubali kumwajibikia mgeni. Mithali inasema
kwamba ikiwa wewe ni mpumbavu sana kiasi cha kufanya hivyo, basi ni sahihi
kuchukua mali yako ili iwe fundisho kwako.)
1.
Angalia nusu ya pili ya Mithali 20:16. Je, “mwanamke
asiye mtiifu” anaendanaje na hili somo la upumbavu? (Unapaswa pia kuchukua mali
ya mtu ambaye ni mpumbavu sana kiasi cha kukubali kuwajibika kwa mwanamke
ambaye mtu mpumbavu ana uhusiano naye wa kimahaba/kimapenzi.)
2.
Rafiki wangu wa zamani, ambaye hatujaonana kwa
miaka mingi, hivi karibuni alianza kutumikia kifungo gerezani. Sababu moja
iliyomfanya aende jela ni kwamba malaya mmoja alitishia kwenda kwa mkewe isipokuwa
tu kama rafiki wangu angempa fedha malaya huyo. Rafiki wangu aliwataarifu
polisi ambao walimtishia yule malaya – na kwa dhahiri hiyo ndio sababu moja
kubwa iliyomfanya aende jela. Ikiwa hoja zangu ziko sahihi, inaonekana hakuna aliye
na “mikono safi” katika hali kama hii. Unadhani Mithali 20:16 inapendekeza jambo
gani la kujifunza? (Dhambi za ngono zinaishia kukugharimu zaidi ya hadhi yako. Zinasababishia
madhara kwa namna nyingine nyingi.)
G.
Soma Mithali 21:17. Je, ni kwa njia gani
nyingine tuwezayo kuwa wavivu? (Kutumia muda mwingi sana kwenye sratehe (anasa).)
1.
Je, kupumzika si jambo jema? (Hapana. Mungu asingeamuru
pumziko (Marko 2:27) endapo lisingekuwa jambo jema. Tatizo lililopo ni “kupenda”
starehe – kuendekeza starehe kupita kiasi.)
H.
Soma Mithali 22:1. Rafiki wangu amepoteza jina
lake jema, na kuwa mvivu ndio njia inayojielekeza kwenye jina baya. Kwa nini
jina jema ni bora kuliko mali nyingi? (Lengo la utajiri ni lipi? Kwa nini watu
wanataka kuwa matajiri? Kwa sehemu fulani ni ili watu wawaheshimu. Watu wawasifie.
Jina jema linakupatia heshima na sifa)
III.
Matokeo Sahihi
A.
Soma Mithali 22:5. Je, inamaanisha nini “kuitunza
nafsi yako?” (Kuwa makini na mawazo yako na kile kinachoshawishi mawazo yako. Dhambi
inaanzia akilini. Ikiwa unataka kuepuka “miiba na mitego,” angalia sana mawazo
yako.)
B.
Soma Mithali 22:6. Wazazi wana wajibu gani
kwenye mafanikio ya watoto wao? (Mfundishe mwanao kumpenda Mungu na hekima ya
Mungu, mafunzo hayo yatakuwa na manufaa baadaye.)
C.
Soma Mithali 22:10. Mwanzoni kabisa katika kazi
yangu kanisani, nilijaribu kuwatuliza washiriki waliokuwa wakilikosoa kanisa. Je,
hiyo ilikuwa njia sahihi? (Kama ambavyo fungu hili linavyopendekeza, baadaye
nilijifunza kuendanana na wenye kudhihihaki. Wanatakiwa kuwa kwenye kanisa
tofauti.)
D.
Soma Mithali 22:29. Matokeo ya jitihada kuzidi
wengine ni yapi? (Mafanikio!)
E.
Rafiki, ikiwa uko makini kwenye makabiliano yako
na watu walio kwenye mamlaka, ikiwa wewe ni muadilifu kwenye kazi yako, ikiwa
utatafuta ubora na uko makini kwenye mawazo yako, maisha yako yatakuwa bora! Kwa
nini usijitoe kufanya hivyo leo?
IV. Juma lijalo: Maneno ya Kweli.
No comments:
Post a Comment