(Mithali 17 & 18)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Kuna sababu nyingi zinazothibitisha kwamba
mtandao wa intaneti ni wa muhimu na wa pekee. Sababu mojawapo ni kwamba mtandao
unarahisisha kuwasiliana na marafiki wengi na jamaa. Hata hivyo, mawasiliano
hayo makubwa yanaendana na tatizo kubwa la kutokuwepo kwa uungwana. Watu
wanajisikia kuwa huru kusema mambo mabaya kwa njia ya mtandao kuliko wanavyoweza
kukuambia uso kwa uso. Wengi wetu tuna “chujio” tunalolitumia kujizuia kusema
mambo tunayoyafikiria – mambo yanayoweza kuwa na athari hasi kwa watu wengine.
Je, umewahi kukutana na watu wanaoonekana kutokuwa na chujio? Watu wanaoonekana
kung’ang’ania ugomvi na mfululizo wa matukio hususani uso kwa uso? Wengi wetu
tunapenda kuboresha “chujio” letu, hivyo hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia
ili tupate hekima ya kufanya hivyo!
I.
Ugomvi
A.
Soma Mithali 17:14. Je, umewahi kuona picha za bwawa
linalovunjika? Je, mchakato huo unaonekana kama wenye kudhibitika? (Hapana!
Mambo yanaonekana kutodhibitika (na kimsingi hayadhibitiki).)
1.
Kwa nini kuanzisha ugomvi kunafanana hivyo? (Ni vigumu
sana kudhibiti ukubwa wa tatizo na athari zinazotokana na ugomvi.)
2.
Tofauti na kuharibika kwa bwawa, je, matatizo gani
mengine yanaibuka kutokana na kuharibika kwa bwawa? (Watu na mali zilizo upande
wa chini wa bwawa (ambapo maji yanaelekea) vinaathirika.)
a.
Je, ugomvi unafanana hivyo? (Ndiyo, watu wengine
wanaingia kwenye ugomvi. Wakati mwingine watu walio nje ya huo ugomvi
wanaathirika nao.)
3.
Biblia inatupatia ushauri gani kuhusu kuepuka ugomvi?
(Kuuacha mara moja.)
B.
Soma Mithali 18:19. Mara baada ya kujitumbukiza kwenye
ugomvi na kusababisha uvunjaji wa sheria, je, ni vigumu kiasi gani kurekebisha
athari ulizozisababisha? (Watu waliochukizwa wanajenga kuta kubwa kati yenu
wawili. Itakuwa vigumu sana kuzivunja kuta hizo. Kwa hiyo, jambo la busara ni
kuepuka kabisa kusababisha makosa.)
C.
Soma Mithali 17:19. Je, unamfahamu mtu anayependa
ugomvi? Biblia inaupa jina gani mtazamo wa aina hiyo? (Dhambi.)
1.
Mara ya kwanza niliposoma nusu ya mwisho ya fungu hili,
mara moja nilidhani kuwa rejea hii inawahusu watu wanaojitenga. Watu wanaojenga
ukuta kati yao na wengine “wanaokaribisha” maangamizi. Je, unadhani hicho
ndicho kinachomaanishwa hapa?
2.
Kwa nini kila mtu “anapenda” ugomvi? (Tofauti na
kutokuwa na haiba, inaonekana kwamba ni mtu anayependa mjadala. Ni sawa na mtu
mwenye nguvu anayependa kupigana na watu wengine ili aweze kudhihirisha nguvu
zake. Mtu anayependa ugomvi anadhani kwamba yeye ni mwerevu na mjanja.)
a.
Je, mtu kama huyo anaweza “kukaribisha” maangamizi?
(Kujiwekea mazingira kwamba wewe ni mtu bora kunakufanya uwe mlengwa, “mlengwa
mkuu.”)
D.
Soma Mithali 17:1. Amani na utulivu vina thamani gani?
Kuna umuhimu gani wa kuepuka magomvi? (Ni bora zaidi kuliko kuwa na karamu!)
1.
Uelewa wangu unaniambia kwamba ndoa nyingi zinavunjika
kutokana na kutokuwepo na uelewano kwenye masuala ya fedha. Je, hiyo inaashiria
kwamba nyumba nyingi zina “mego kavu” na ugomvi? (Kimsingi, kitendo hicho ni
kibaya. Hata hivyo, nadhani fundisho la Biblia ni kwamba kuishi maisha ya
amani, hata kama huna vitu vingi, ni jambo la furaha.)
E.
Soma Mithali 17:9. Je, njia gani moja iwezayo kutumika
kuendeleza Amani kazini na nyumbani? (Hatuhitajiki kusonda kila kosa
linalofanywa na watu wanaotuzunguka. Kutatua tatizo kwa utulivu kutamfanya mtu
aliyetenda kosa akupende Zaidi.)
1.
Soma Mithali 17:10. Je, kutatua tatizo kwa utulivu
hakuendani na wazo la ukemeaji? (Hapana. Unaweza kukemea mtu mwenye ufahamu, na
kutatua tatizo.)
a.
Vipi ikiwa unakabiliana na mpumbavu? (Kwa kuwa mpumbavu
hatajifunza kwa urahisi, inaonekana ni upotezaji wa muda kutatua tatizo kwa
utulivu kwa mtu mpumbavu.)
F.
Soma Mithali 17:13. Hivi punde tu tumejadili juu ya mtu
anayejaribu kutatua matatizo. Vipi kuhusu mtu anayejaribu kusababisha matatizo?
Mtu wa aina hiyo atarajie maisha ya namna gani? (Kamwe mabaya hayataondoka
nyumbani mwake.)
G.
Soma Mithali 17:17. Tunapaswa kufanya nini tunapomwona
mtu yupo kweye matatizo? (Tukionesha upendo, tukijaribu kutoa msaada, basi sisi
ni “marafiki” na “ndugu.”)
H.
Soma Mithali 17:22. Tunaweza kuchukua hatua gani kujikinga
dhidi ya matatizo? (Kuwa mchangamfu kutawafanya watu wanaokuzunguka
wachangamke. Kutokuwa na furaha kuna athari hasi kwako na kwa watu
wanaokuzunguka.)
I.
Soma Mithali 18:21. Ikiwa unakubaliana na jambo hili,
elezea kwa nini unadhani ulimi una uwezo dhidi ya uzima na mauti?
1.
Angalia kauli “wale wanaopenda.” Wanaopenda nini?
(Nadhani inamaanisha “wale wanaopenda uwezo wa ulimi.”)
2.
Inamaanisha nini “kupenda” uwezo wa ulimi? (Muda mfupi
uliopita tumepitia mfullizo wa Mithali zilizotufundisha kuepuka kujiingiza
kwenye ugomvi. Ikiwa “tunapenda” kile kinachoweza kufanywa na ulimi, basi sisi
ni wanafunzi wa huo uwezo wake. Hiyo inamaanisha kwamba tunajifunza hizo
Mithali, na kutumia ndimi zetu kuepuka magomvi na kufanya makosa. Badala yake,
tunatumia ulimi kuleta upendo na amani.)
II.
Maji ya Vilindi
A.
Soma Mithali 18:4. Unapoyafikiria “maji ya vilindi”
jambo gani linakujia akilini? (Hatari. Mwujiza.)
1.
Soma Mithali 20:5 na Zaburi 69:2. Mafungu haya
yanapendekeza kwamba maana ya “maji ya vilindi” ni ipi? (Ngumu. Inatishia
uhai.)
2.
Ni kwa jinsi gani basi, maneno ya mtu yanafanana na
“maji ya vilindi?” (Mara zote hatuna uhakika kwamba yanamaanisha nini. Wakati
mwingine maneno ya mtu huwa ni magumu sana kuliko inavyoweza kuonekana kwenye
kile yanachomaanisha.)
3.
Kuna jambo gani chanya kuhusu kijito kinachotiririsha
maji baridi? (Sio kirefu, hakina ugumu, badala yake kinaburudisha na
kuchangamsha.)
a.
Jambo hili linaashiria nini kuhusu uelewa wa hekima ya
Mithali? (Mambo yanayofafanuliwa hapa sio magumu kiasi hicho. Watu wanaweza
kuwa wagumu kueleweka, lakini maelekezo ya Mungu sio magumu.)
B.
Soma Mithali 18:8. Jambo gani jingine “linazama chini?”
(Umbeya/uchongezi.)
1.
Inamaanisha nini kusema kwamba “vitoweo” vya Mchongezi
hushuka “pande za ndani za tumbo” (Mambo mawili. Unavikumbuka. Bila kujali kama
wewe ndio mtu unayesikia uchochezi/usengenyaji, au unayeathirika na uchongezi,
athari zinadumu muda mrefu.)
C.
Soma Mithali 18:2 na Mithali 18:6-7. Je, unaweza
kushughulikia upumbavu wako? (Kama isingekuwa inawezekana, nadhani tusingeonywa
kuhusu upumbavu. Hatua ya kwanza kwa mpumbavu inapaswa kuwa ni kusikiliza zaidi
katika jitihada za kuwa na ufahamu/uelewa, na kupunguza kuzungumza. Ikiwa
utafanya hivyo, unaweza kuepuka matatizo ya aina zote.)
III.
Uwazi Kwenye Masuala ya Fedha
A.
Soma Mithali 18:9. Uvivu ni tatizo kwa kiwango gani?
Je, jamii inapaswa kuuvumilia uvivu ukiachilia mbali kuutunuku? (Ikiwa kuwa
mvivu kunafananishwa na kuharibu mali, basi uvivu unapaswa kuadhibiwa, na si
kutunukiwa.)
1.
Hapo kabla tumezungumza kuhusu kuwa wakarimu. Je, njia
ya upole ya kutibu uvivu ni ipi?
B.
Soma Mithali 18:10-11. Je, kuwa na fedha ni sawa na
kuishi ndani ya mji uliozingirwa na ukuta? (Ndiyo. Fedha zinakukinga dhidi ya
matatizo ya aina yote.)
1.
Je, fedha ni sawa na ukuta usio na vipimo? (Hapana. Ulinzi
sio kamili.)
2.
Je, ukuta usio na vipimo ni upi? (Kumtumaini Mungu.
Yeye ni mnara imara ambao tunaweza kuukimbilia na kuwa salama.)
3.
Je, watu weye mali (matajiri) wana uwezekano mkubwa wa
kuwa watu wa Mungu? Mithali kadhaa zinafundisha kwamba hekima hutupatia fedha.
Lakini, fungu hili linatoa onyo. Kwa udanganyifu matajiri wanadhani kwamba
fedha zao zitawalinda, bali Mungu pekee ndiye mlinzi wa uhakika. Usigeuke na
kumwacha Mungu kwa kuzitumainia fedha.)
C.
Soma Mithali 18:16. Je, Biblia inaidhinisha/inaunga
mkono rushwa?
1.
Je, kuna cha kujifunza juu ya uinjilisti hapa? (Badala
ya kumwambia jirani wako jinsi anavyotakiwa kumtii Mungu vizuri zaidi, kwanza
unapaswa kumwonesha ukarimu. Kumsaidia mtu ni njia bora zaidi ya kukubalika na
moyo wa mtu huyo.)
D.
Soma Mithali 18:22. Je, ni aina gani nyingine ya
utajiri tuwezayo kuifurahia? (Mwenzi mwema!)
E.
Rafiki, kwa kuwa ulimi una uwezo mkubwa sana, kwa nini usidhamirie
leo kuwa mwanafunzi wa matumizi bora ya ulimi?
IV. Juma lijalo: Maneno ya Hekima.
No comments:
Post a Comment