(Mithali 14-15)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Nilianza kufurahia kompyuta tangu
zilipoanza kutumiwa na watu. Nakumbuka nilinunua kompyuta aina ya Timex
Sinclair iliyokuwa na uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu kiasi cha Kilobite
(KB) 2. Baada ya kuinunua, niliona kwamba kompyuta hiyo ingefaa zaidi
kutumiwa kama chembeo (kabari) ya kuzuia mlango usijifunge na uendelee kuwa
wazi. (Kompyuta hiyo ilikuwa na aina fulani hivi ya umbo la kabari.) Hapo
kabla, nilikuwa na wakati mgumu kuweza “kuona” kile ambacho kumpyuta ilikuwa na
uwezo wa kukifanya ili kurahisisha maisha. Hekima inayotokana na Biblia
inafanana hivyo. Hatutambui ni kwa kiasi gani kufuata njia ya Mungu kunaboresha
maisha yetu. Juma hili somo letu la Mithali linatusaidia kuelewa vizuri zaidi
kile inachomaanisha kuishi maisha bora kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu. Hebu
tuzame kwenye somo letu!
I.
Jinsi ya Kufikia Mwafaka wa Mawazo
A.
Soma Mithali 14:1. Hii inasema nini kuhusu kuwa na
hekima? (Watu wenye hekima hujenga vitu.)
1.
Wapumbavu wanafanya nini? (Wanabomoa vitu.)
2.
Je, hii ndio kanuni ya jumla maishani? Ikiwa huna
uhakika kama wazo lina hekima ya Kibiblia au ni la kipumbavu, je, itakuwa vyema
zaidi kuuliza kama wazo hilo linajenga au linabomoa? (Nadhani hii ni kweli.)
3.
Mimi na binti wangu tulikuwa tunawajadili wakanamungu
na kwa nini wanapigia upatu mambo yasiyo ya imani kwa kuibomoa dini. Binti
wangu aliuliza, “Ikiwa unayakubali mawazo yao, na wao wako sahihi, ni kwa jinsi
gani jambo hilo lina manufaa?” Kwa upande mwingine,ikiwa unaukubali Ukristo,
manufaa ni yapi ikiwa tuko sahihi?
B.
Soma Mithali 14:2. Kuna tofauti gani ya mtazamo kati ya
wanyofu na waovu? (Mmoja anamcha Mungu na mwingine anamdharau Mungu.)
1.
Je, hii ni
kanuni nyingine ya jumla maishani? (Nadhani. Unaweza kumhukumu mtu na
mawazo yake kwa kuangalia mtazamo wake dhidi ya Mungu.)
C.
Soma Mithali 14:3. Je, Biblia ipo kinyume na uhuru wa kuongea? (Hapana. Hii inaashiria
matokeo ya dhahiri ya kuwa na hekima dhidi ya kuwa mpumbavu.)
1.
Je, hii ni kanuni nyingine ya jumla maishani? Ikiwa
unataka kujua kama mtu anakupatia ushauri mzuri, je, unapaswa kuangalia
mwenendo wa maisha ya mtu huyo? (Ndiyo! Huhitaji kufahamu kwa undani zaidi juu ya
ushauri unaohitajika ili kufahamu kama ushauri huo ni mzuri. Angalia tu jinsi
ushauri huo unavyofanya kazi kwa mtu anayetoa ushauri! Sasa tunazo kanuni tatu
za kuuangalia ushauri: a) je, ushauri huo unajenga; b) je, mtu huyo anamtumaini
Mungu; na, c) je, maisha yanamwendea vizuri huyo mtu anayetoa ushauri?)
D.
Soma Mithali 14:6-7. Mithali inaposema “toka mbele ya
uso” wa mpumbavu, je, inamaanisha kuepuka kuchangamana na mtu mpumbavu? (Kwa
kiwango fulani, inamaanisha usifuate ushauri wa mtu mpumbavu.)
1.
Fungu la 6 linaposema kuwa maarifa yanapatikana
kirahisi kutokana na “ufahamu,” je, kitu gani kinafahamika? Kuna tofauti zipi
ambazo mwenye hekima anaweza kuziona ambazo watu wengine hawawezi kuziona? (Kwa
jambo moja, kuwa makini endapo ushauri unatoka kwa mtu mpumbavu au la.)
E.
Soma Mithali 14:8. Je, umewahi kumsikia mtu akisema,
“Usiangalie mambo ya nyuma kwa sababu hakuna unachoweza kukifanya kubadili
mambo yaliyopita?” Je, hiyo ni kweli? (Kwa kiasi fulani. Unaweza kujifunza
kutokana na mambo yaliyopita. Mtu mwenye busara na ufahamu anatafakari jinsi
alivyoishi siku za nyuma, na hii inampatia uelekeo wa siku zijazo.)
F.
Soma Mithali 14:11. Inakuwaje mtu mbaya (mwovu) ana
“nyumba” wakati mtu mnyofu ana “hema” pekee? Je, kinyume chake hakipaswi kuwa
ndio ukweli wa mambo? (Jambo linalozungumziwa hapa ni kwamba mtu mnyofu anaweza
asianze kwa kuwa na vitu vingi. Lakini, Mungu anabariki na kujenga juu ya kile
walichonacho ikiwa wao wana hekima. Hii inaonesha kwamba mtu mwenye hekima ya
Kibiblia anajenga juu ya kile alicho nacho.)
II.
Hekima na Utajiri
A.
Soma Mithali 14:20-21. Je, huwapendi “wahitaji?” Je,
mafungu haya mawili yanasema nini kuhusu mtazamo dhidi ya matajiri na wahitaji?
(Kwa asili moyo huwa na mapenzi kwa tajiri kwa sababu unaweza kupata kitu
fulani kutoka kwa matajiri – huenda hata kutumia vitu walivyo navyo. Lakini,
masikini wanahatarisha vitu vyako. Wanaweza kuwa na uhitaji wa kitu fulani.)
1.
Mithali inatuambia tuwe na mtazamo gani kuhusu jambo
hili? (Tutabarikiwa kwa kuwa wakarimu kwa wahitaji.)
B.
Soma Mithali 14:31. Sababu ya kupokea mibaraka
tunapomsaidia mhitaji ni ipi? (Mungu anajihusisha nao kwa kuwa yeye ndiye
Muumbaji wao.)
C.
Soma Mithali 14:23-24 na Mithali 14:26. Kuwa na utajiri
ni ishara kwamba wewe una (au ulikuwa na) hekima. Kutokuwa na utajiri inaashiria
kwamba umekuwa mtu mpumbavu ambaye anazungumza zaidi badala ya kutenda. Je,
unahusianishaje jambo hili na maelekezo yaliyotolewa kwamba tunapaswa kuwa
wakarimu kwa wahitaji?
1.
“Tiba” ya kuwa mhitaji, kwa mujibu wa somo, ni kumcha
Mungu, kuacha kuwa mpumbavu na kuzungumza sana, na kuanza kufanya kazi.
Tunapaswa kufanya nini ikiwa tunatakiwa kufuata maelekezo ya kuwa wakarimu kwa
wahitaji?
2.
Juma hili nilikuwa nimekaa kwenye gari langu jipya
linalong’aa. Nilipata punguzo kubwa, na ninamshukuru Mungu kwa ukarimu wake
kwangu. Ombaomba mwenye umri wa makamo alikuwa amekaa pembeni mwa barabara,
akiwa ameweka ishara ndogo ambayo nilichukulia kwamba alikuwa anaomba fedha.
Nilifanya uamuzi kwamba nitampatia fedha – kwa sababu tu ya tofauti zetu kubwa
kimaisha. Lakini, kamwe sikufanya hivyo kwa kuwa hakusimama. Je, una maoni
gani? Je, nilikuwa sahihi kufanya uamuzi kwamba ikiwa mtu huyu alikuwa hafanyi
kazi, na hata hakuwa tayari kufanya juhudi ya kusimama, nami simpatii fedha?
a.
Soma Mithali 15:3. Hii inaongezea kigezo gani cha
muhimu kwenye swali langu kuhusu ombaomba? (Sio tu kwamba Mungu ananihukumu,
lakini Mungu pia anafahamu hali ya ombaomba.)
b.
Soma Mithali 15:19. Nani awekaye miiba mwenye njia ya
mvivu? (Kanuni za Mungu maishani. Mimi ninaona kwamba hatupaswi kuondoa “miiba”
inayotokana na uvivu, lakini tunapaswa kuwa wema kwa wahitaji kwa namna inayoendana
na kitabu cha Mithali – kuwafundisha njia bora ya maisha.)
c.
Unawezaje kutumia ushauri huu kwenye hali yangu na
ombaomba? (Jambo bora kabisa tunaloweza kuwatendea ombaomba ni kuwafahamu. Hiyo
itatusaidia kutumia kanuni za Kibiblia maishani mwao. Ikiwa nitampatia tu
ombaomba fedha, siwezi kuwa na uhakika kama ninamdhuru au ninamsaidia.)
D.
Soma Mithali 15:6 na Mithali 15:16-17. Kwa nini utajiri
si jambo zuri mara zote? (Unatakiwa kuwa na uwezo wa kuudhibiti. Huenda, ikiwa
tunamtumaini Mungu, atatuapatia kiasi cha fedha tunachoweza kukidhibiti. Ikiwa
mali inaleta machafuko na chuki, basi ni bora kutokuwa na utajiri.)
III.
Ulimi
A.
Soma Mithali 15:1-2. Je, umejijengea tabia ya kuchunguza
maneno yako kwa makini pale unapokuwa na mazungumzo magumu?
1.
Ni kwa namna gani jinsi tunavyochagua maneno yetu huleta
tofauti kwenye matokeo ya hali iliyopo? (Kuwa muungwana hushusha joto la
hasira. Kuwa mkali hufanya mambo kuwa mabaya zaidi.)
B.
Soma Mithali 15:4. Je, maneno yetu yanaweza kuathiri
afya za watu wengine? (Ndiyo. Tunaweza kuboresha au kuathiri afya ya mtu kwa
jinsi tunavyozungumza nao.)
C.
Soma Mithali 15:7. Je, jambo gani jingine chanya
linaweza kufanywa na maneno yako? (Kueneza maarifa kwa watu wengine!)
D.
Soma Mithali 15:18. Hii inahusianaje na ulimi? (Hii
inahusiana na mjadala wetu uliotangulia kuhusu kutumia muda kidogo kutafakari
maneno yako kwa makini. Mtu “mwenye hasira” anakasirika sana na kuropoka maneno
ambayo atayajutia baadaye. Mtu mvumilivu anatumia muda kuchagua maneno yake kwa
makini.)
E.
Soma Mithali 15:22. Ikiwa tuna hekima, kwa nini
tunahitaji ushauri wa watu wengine? (Huenda hii inahusiana zaidi na majivuno.
Unadhani kwamba uko sahihi na unadhamiria kusonga mbele. Biblia inasema kwamba kwa
kupata mawazo ya watu wengine wenye hekima, husaidia mipango yako maishani
kufanikiwa.)
F.
Soma Mithali 16:7. Hili linatendaje kazi: unampendeza
Mungu naye anawashika maadui wako shingoni na kuwafanya wawe watiifu? (Sidhani
kama fungu hili linarejea suala la Mungu kuingilia kati, ingawa jambo hilo
linawezekana. Badala yake, nadhani tayari Mungu “ameshaingilia kati” kwa
tutupatia hizi mithali. Ikiwa tutazifuata, hususani zile zinazohusu ulimi,
tutaishi kwa amani na maadui wetu.)
G.
Soma Yohana 15:18-19. Unalinganishaje jambo hili na
kuishi maisha ya amani na maadui wetu? (Ulimwengu hautapenda mawazo yetu kwa
sababu maneno yetu yanakemea njia yao ya maisha. Lakini, katika ngazi ya mtu
mmoja mmoja, ikiwa tutafuata ushauri wa kitabu cha Mithali tutaishi kwa amani
na maadui wetu.)
H.
Rafiki, je, ungependa kuwa na migongano michache
maishani mwako? Je, ungependa kuishi maisha yenye furaha zaidi? Kwa hekima
chagua ushauri utakaoufuata, na kisha uufuate. Kwa nini usiamue kubadilika sasa
hivi?
IV. Juma lijalo: Kukabiliana na Ugomvi.
No comments:
Post a Comment