(Mithali 10, 11-13)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, unamfahamu mtu ambaye maisha
yake hayana udhibiti? Ikiwa moyo wako unakushuhudia kwa dhati kabisa, je,
maisha yako yanaonekana kuwa kwenye hatari ya kupoteza uelekeo mara kadhaa? Sote
tunaweza kuhitaji msaada kidogo. Kwa kawaida, huwa tunamwomba Mungu atusaidie
kutatua matatizo yetu. Lakini, je, umewahi kutafakari kwamba tayari Mungu
ameshatusaidia? Katika kitabu cha Mithali Mungu anatupatia ushauri wa jinsi ya
kuishi maisha bora. Unawafikiriaje watu ambao ni wavivu sana kiasi cha
kushindwa kusoma maelekezo, na badala yake wanataka waambiwe nini cha kufanya? Hebu
tuzame kwenye somo letu linalohusu maelekezo ya Mungu ya jinsi ya kuishi maisha
bora!
I.
Watoto na Wazazi
A.
Soma Mithali 10:1. Kwa nini
Sulemani anamtaja mama mwenye mwana mpumbavu na baba mwenye mwana mwenye
hekima? (Baba anajivunia kuwa na mwana mwenye mafanikio. Mama ndiye ambaye
anateseka pale mwanaye anapofanya maamuzi mabaya.)
B.
Soma Mithali 10:2-6. Tunayo mifululizo
ya misemo inayohusu uhusiano uliopo kati ya fedha na haki. Je, tunaona maadili
gani yanayoendana na kuwa na utajiri? (Uhusiano na Mungu, uadilifu, na kufanya
kazi pale fursa inapojitokeza.)
1.
Kipi kinachoonekana kuwa cha
muhimu zaidi, ikiwa utaangalia muktadha? (“Haki,” ambayo ni kipengele cha
kidini, imetajwa mara nyingi zaidi kuliko maadili ya aina nyingine.)
C.
Angalia Mithali 10:2-6 tena. Athari
gani za kitabia zinaendana na umasikini? (Wizi, tamaa, uvivu, kulala wakati
unaotakiwa kufanya kazi, na vurugu.)
1.
Jambo gani linaonekana kuwa na
athari kubwa kitabia, ikiwa tu utauangalia huo muktadha? (Linabainisha kuhusu
kuwa “mwovu” mara mbili, lakini pia linaonyesha aina ya uvivu mara mbili na
tabia mbaya mara mbili. Hata kama kuwa mwovu kunabainishwa, kwa ujumla
kunaelezewa kama kushindwa mahsusi kwenye matendo ya mtu. Kwa hiyo, inaonekana
kwamba vigezo vya msingi kabisa vinavyosababisha umasikini ni matendo mahsusi
(au kutokuwepo kwa matendo/kuchukua hatua).)
D.
Je, hii inatufundisha nini sisi
kama wazazi? Ikiwa sisi (akina baba) tunataka kujivunia watoto wetu na sisi
(akina mama) tunataka kuepuka kuwahuzunikia watoto wetu, je, tunapaswa
kuwafundisha nini? (Tunatakiwa kuwafundisha kuhusu upendo wa Mungu, na
tunatakiwa kuwafundisha wawe na bidii na uaminifu.)
II.
Wapumbavu Wenye Maneno Mengi
A.
Soma Mithali 10:8-10. Je, mtu
amewahi kukwambia kwamba una maneno mengi/unaongea sana? Je, mtu huyo alisema
hivyo kwa sababu alikutaka unyamaze ili yeye aweze kuzungumza zaidi?
1.
Mafungu yetu yamerejea “wapumbavu
wenye maneno mengi” mara mbili. Kuna tatizo gani kuhusu uzungumzaji katika haya
mafungu? (Katika fungu la nane tatizo ni kwamba mpumbavu anazungumza wakati
ambapo anatakiwa kusikiliza maelekezo. Katika fungu la 10, mpumbavu anazungumza
wakati ambapo anatakiwa kuwa makini na mtu anayetoa ishara kwamba anadhamiria
kusababisha madhara.)
B.
Hebu turukie chini hadi Mithali
10:19. Je, kitendo cha kuzungumza sana ni tatizo? Kwa nini Biblia inaashiria kuwa
wingi wa maneno ni ishara ya tatizo kitabia? (Ikiwa mara zote unataka kupata
usikivu kutoka kwa watu, hiyo ni ishara ya dosari kitabia – majivuno/majisifu.)
C.
Soma Mithali 10:11-14. Tunazo kauli
kadhaa zinazohusu matumizi ya midomo yetu, yaani matumizi mazuri na mabaya. Kwa
nini kinywa cha mwenye haki “ni chemchemi ya uzima?” (Je, umewahi kubarikiwa na
maneno ya mtu mwingine? Ikiwa umewahi, basi unaelewa jinsi maneno yanavyoweza
kutoa uzima.)
1.
Je, maneno yanatoa uzima kwa msikilizaji pekee? (Utagundua kwamba
kuzungumza maneno yenye upendo “husitiri” makosa. Hii inatuambia kuwa wale
wanaozungumza maneno mazuri pia wananufaika na maneno hayo.)
2.
Nini humtokea “mpumbavu mwenye
maneno mengi” anayeongea mambo maovu? (Wanateseka kwa kupata machafuko na
maangamivu, wanasababisha mfarakano na wanaadhibiwa kwayo.)
D.
Soma Mithali 10:21. Je, maneno mazuri ni sawa na chakula? (Lazima
yawe hivyo. Dhana iliyopo ni kwamba maneno chanya, ushauri chanya, ni chanzo
cha maisha bora kwa wale wanaosikiliza. Hii ni sawa na kauli ya awali iliyosema
kwamba maneno sahihi ni “chemchemi ya uzima.” “Wapumbavu” hawasikilizi (hawana
usikivu), na wanakufa kutokana na kutokuwa wasikivu.)
E.
Soma Mithali 11:12. Vipi kuhusu
kumdhihaki jirani yako au kumkandamiza? (Huwezi kufanya vitendo hivyo ikiwa wewe
ni mtu mwenye mawazo na uelewa mzuri.)
F.
Soma Mithali 11:22. Uzuri una
manufaa makubwa maishani. Jambo gani
linaweza kuuharibu uzuri? (Kutokuwa na busara kwenye maneno yako. Kunaharibu
uzuri wako kwa sababu kile watu watakachokiona zaidi kwako ni ile sehemu ya “nguruwe”
iliyomo ndani mwako.)
III.
Uadilifu
A.
Soma Mithali 11:1-4. Utagundua
kwamba kati ya kauli nne, kauli tatu zinahusiana na uadilifu. Je, Mithali 11:2
iko nje ya msitari? Au, je, kauli hiyo pia inahusika kwa namna fulani na suala
la uadilifu? (Kwa ujumla kiburi ni njia mbaya ya kujiangalia. Ikiwa kila mtu
anafahamu kila kitu kuhusiana na wewe, huenda ungekuwa na kiburi kidogo na
mnyenyekevu zaidi.)
B.
Soma Mithali 11:6-7. Kuna matatizo
gani mawili kwenye utajiri unaotokana na udhalimu? (Matamanio yako maovu
yanaishia kukunasa. Kibaya zaidi, kifo kinahitimisha matumaini na raha yote ya
waovu. Kwa waovu, mambo hayaishii kuwa kama walivyoyapanga.)
C.
Soma Mithali 11:13. Je, hii
inamaanisha kuwa siri ni njema? Kwamba watu wenye uadilifu wanatunza siri? (Kwa
dhahiri, kuna nyakati ambazo kutunza mambo fulani yawe ya siri ndilo jambo
sahihi kulitenda.)
D.
Soma Mithali 11:16-17. Aina gani
nyingine ya uadilifu tuwezayo kuionesha kwa maneno yetu? (Kuwa wema kwa watu
wengine katika kile tukisemacho. Matokeo ya kuwa wapole ni kwa sisi kupata
mibaraka. Tunarudishiwa wema wetu kwa kupata heshima zaidi. Kwa upande
mwingine, kuwa wakatili pasipokuwa na huruma hutuletea matatizo, na hata kama
ni utajiri, basi utakuwa ni wa kitambo kifupi tu.)
E.
Soma Mithali 12:20-22. Je,unawafahamu
watu wasemao uongo ili kusababisha matatizo? Matokeo ya tabia ya aina hii ni
yapi?
1.
Je, unapaswa kufanya nini katika
aina ya tabia hii ya kiovu? (Tunapaswa kuisimamia amani.)
IV.
Ukarimu
A.
Soma Mithali 11:24-25. Mtazamo wa
ulimwengu wa utoaji ni kwamba unapotoa kitu, basi unakuwa umekipoteza. Biblia inasema
nini kuhusu sisi kuwa wakarimu kwa muda na fedha zetu? (Kwamba tutazidishiwa
zaidi!)
1.
Je, umewahi kujaribu jambo hili? (Hivi karibuni, palitokea hali isiyo ya
kawaida, hivyo mimi na mke wangu tulitoa fedha ili kusaidia. Muda mfupi
baadaye, nilipokea fedha takribani kiasi kama kile nilichokitoa. Nakumbuka nilitafakari,
“pengine ni vyema nikatunza fedha hizi, nitoe hizi fedha nyingine nilizopata, kisha
nione jinsi mambo yatakavyokwenda.” Lakini, nasikitika ubinafsi uliingilia
kati.)
B.
Soma Mithali 11:27. Je, umewahi
kumsikia mtu akisema, “Hakuna aliye mkarimu katika lile kanisa?” “Kila mtu ni
mbaya kwangu?” Kwa mujibu wa hili fungu, chanzo cha tatizo ni kipi? (Ikiwa wewe
ni mkarimu, watu watakuwa wakarimu kwako. Ikiwa unatafuta hali ya kutokuwa na
ukarimu, utapata kitu hicho hicho. Huwa ninajaribu kutekeleza jambo hili (kuwa
mkarimu) mara zote ninaposafiri, na ninagundua kwamba kitendo hiki kinanibariki
kivitendo.)
C.
Soma Mithali 11:31. Je, wenye haki
watapata thawabu yao lini? (Tunatarajia kuipata mbinguni, lakini fungu hili
linafundisha kwamba wenye haki wanapata thawabu yao hapa duniani.)
1.
Je, watu wasiofuata mambo ya Mungu
na wadhambi watapata kile wanachostahili? (Ndiyo. Watakipata katika maisha
haya.)
D.
Soma Mithali 12:23. Je, hii
inamaanisha kwamba tunapaswa kuwa wachoyo wa maarifa yetu? Ikiwa tunaweza
kuwasaidia watu wengine, kwa nini liwe jambo la busara kuhifadhi maarifa yetu?
1.
Soma Mithali 12:15-16 na Mithali
13:3. Je, mafungu haya yanatoa mwanga kwenye wazo la kuyatunza maarifa ndani
mwetu? (Sidhani kama Mungu anaashiria kwamba tuache kuwasaidia watu wengine kwa
maarifa yetu tuliyonayo. Katika miktadha mingine anaashiria tuwe wakarimu. Nadhani
ushauri ni kwamba tuwe kinyume na majisifu juu ya kile tunachokifahamu badala
yake tuwe wasikivu. Ni ushauri dhidi ya kuzungumza kabla ya kutafakari. Mara nyingine
kile tunachokifahamu kitawadhuru watu wengine.)
E.
Rafiki, je, umegundua jinsi
ushauri wa kuishi maisha bora tuliojifunza juma hili unavyohusiana na kile
tunachokisema? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu auweke akilini mwako huu
ushauri unaopatikana kwenye kitabu cha Mithali kwa wakati muafaka?
No comments:
Post a Comment