(Mithali
8 & 9)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata
kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, ukweli unatofautiana kutegemeana na mtu na
mtu? Hivi karibuni kuna mtu aliniandikia na kuniambia kwamba “kuna njia nyingi
maishani,” ambapo nilimjibu kuwa, “lakini ni njia moja pekee ndio inayoelekea
kwenye uelekeo sahihi.” Huu ndio uelewa wa wanasheria. “Utawala wa sheria”
maana yake ni kwamba kuna sheria moja pekee. Watawala hawawezi kutenda chochote
wanachotaka. Vivyo hivyo kwa watawaliwa. Badala yake, tunakubaliana nini kiwe
utawala wa sheria katika nchi. Mnaweza msikubaliane jinsi ya kuutekeleza huo
utawala wa sheria, lakini panaweza kuwepo na sheria moja pekee ikiwa tunataka
kuwa na utaratibu mmoja. Somo letu la Mithali juma hili linahusu hekima. Mungu anatenda
kazi kwa mujibu wa utawala wa sheria, na hekima ndio kanuni ya jinsi ya kuishi.
Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!
I.
Wito wa Kuwa na Hekima
A.
Soma Mithali 8:1-3. Je, hapa hekima inalinganishwa na
nini? (Angalao mambo mawili: uelewa na mtu anayetafuta kusikilizwa.)
1.
Hekima kutoka “mahali palipoinuka,” “penye njia panda,”
na “karibu na malango” na “mahali pa kuingia” mjini. Tunapaswa kuelewaje haya
maeneo tofauti yanayoelezewa? (Haya yote ni maeneo ambayo hekima itawapata
wasikilizaji. Haya ni maeneo ambapo watu wanakutana.)
a.
Hekima imeajiri timu nzuri ya watu wanaohusika na
kitengo cha uhusiano kazini! Kuna ujumbe gani wa kiteolojia? (Wanadamu hawana
kisingizio kwa kukosa ujumbe wa Biblia kuhusu hekima.)
B.
Soma Mithali 8:4-5. Kisingizio gani kingine cha
kutousikia wito wa hekima kinaondoshwa hapa? (Hoja inayotolewa kwamba baadhi ya
watu ni wajinga sana au wapumbavu sana kiasi cha kutoweza kuielewa hekima. Kwa hakika
hekima ipo kwa ajili ya watu wote.)
II.
Ujumbe wa Hekima
A.
Soma Mithali 8:6-8. Je, hekima inatoa ujumbe gani?
(Ujumbe wa kweli na wa haki. Kamwe hauna uovu wala haujapotoka.)
1.
Je, hii inaruhusu tafsiri kadhaa za hekima, ambapo
baadhi zinakinzana?
B.
Soma Mithali 8:9. Je, hii inaashiria kuwa sababu ya
baadhi ya watu kutumia njia nyingine maishani zisizo za busara ni ipi? (Mtu asiye
na utambuzi au uelewa anaweza kuukataa ujumbe.)
1.
Nilidhani tumekubaliana kwamba hata wajinga na
wapumbavu wanaweza kujaribu kuwa na hekima? (Sehemu ya muhimu ni “kujaribu kuwa
na.” Unatakiwa kuwa na tamaa ya kuelewa hekima ya Mungu. Ikiwa utafanya hivyo,
basi hekima hiyo ipo kwa ajili yetu sote.)
III.
Faida ya Hekima
A.
Soma Mithali 8:10-11. Kwa nini watu wengi wanataka
fedha, dhahabu au marijani? (Vinawakilisha usalama, heshima (hadhi), na
furaha.)
1.
Je, hii inatufundisha nini kuhusu hekima? (Inatufundisha
kwamba hekima ndio inayoleta mambo haya (usalama, hadhi na furaha) na mengine
mengi zaidi!)
B.
Soma Mithali 8:18-21. Unauelezeaje umasikini wa Yesu na
wanafunzi wake? (Endapo Yesu angekuja kama mfalme wa kidunia, tunaweza kujenga
hoja kwamba hakujaribiwa kwa njia zote tunazojaribiwa. Angalia Waebrania 4:15. Yesu
alikuwa na vizuizi vingi. Nadhani fundisho la jumla la Biblia ni kwamba utii
kwa Mungu huleta usitawi.)
C.
Soma Mithali 8:12. Biblia inaonekana kusema kwamba
hekima ni mkusanyiko wa maadili unaojumuisha busara, maarifa na
uelekevu/uangalifu. Mpumbavu hana busara na maarifa. Je, ni haki kusema kwamba
mpumbavu anaweza kuwa na hekima ya Mungu? (Nadhani hili ni pendekezo jingine
kwamba hekima ya Mungu inatubadilisha. Hekima ya Mungu inaondosha upumbavu
wetu. Inajumuisha “maarifa na busara” na ni mshirika wa karibu wa uangalifu,
yaani, “prudence.”)
1.
Je, unamfahamu mtu mwenye hekima: maarifa, busara, na
uangalifu? Je, maisha ya mtu huyo yakoje?
D.
Hebu turukie kwenye sura inayofuata kwanza. Soma Mithali
9:10-12. Kuna uhusiano gani kati ya hekima na kusoma Biblia?
1.
Hekima inatunufaishaje kwa namna nyingine? (Sio tu
kwamba tutakuwa na usalama, heshima (hadhi) na furaha, bali pia tutaishi kwa
muda mrefu! Hekima ina thawabu.)
IV.
Chanzo cha Hekima
A.
Soma Mithali 8:13. Hebu tuwe waaminifu kidogo. Je,
huvutiwi na uovu (dhambi)? Kwa nini Yakobo anatuambia “Mpingeni Shetani”
(Yakobo 4:7) na Waebrania inarejea “kujifurahisha katika dhambi” (Waebrania
11:25) ikiwa dhambi haifurahishi?
1.
Ikiwa unavutiwa kutenda baadhi ya dhambi, ni kwa jinsi
gani basi Sulemani anazungumzia “kuuchukia uovu?”
2.
Nani ambaye ni “Mimi” katika “Mimi ninachukia kiburi na
majivuno?” (Ukiangalia Mithali 8:12 tunaona kwamba “Mimi” ni hekima. Tunapojiendeleza
katika njia ya hekima tutaishia kuichukia dhambi. Kwa nini? Kwa sababu
tutaelewa matokeo yake vizuri zaidi.)
3.
Utagundua kwamba hekima huchukia kiburi, majivuno,
tabia ovu na kauli potofu. Kiburi na majivuno vinafanana kwa kiasi gani?
B.
Angalia tena mwanzoni mwa Mithali 8:13 na Mithali 9:10.
Chanzo cha hekima ya kweli ni kipi? (Mungu. Tunatakiwa kwenda kwenye chanzo
sahihi.)
C.
Soma Mithali 8:22-23. Hekima ina nasaba ya aina gani?
(Ilikuwa kazi ya kwanza ya Mungu! Ilikuwepo kabla Mungu hajaumba ulimwengu.)
1.
Hiyo inaashiria nini kuhusu umuhimu wa kuwa na hekima?
D.
Soma Mithali 8:24-29. Jambo gani linaelezewa hapa?
(Uumbaji wa Mungu.)
1.
Suala la uumbaji linahusikaje na hekima? (Hii inafunua
mgongano/makinzano ya mitazamo ya dunia. Ama unaamini kwamba dunia na viumbe
wote vilitokea kuwepo kwa bahati na nguvu nyingi (kwa asili) au unaamini kwamba
Mungu mahiri, mwenye kanuni kwa ajili ya kila jambo, ndiye aliyetuumba. Chaguo lako
kati ya madai ya pande hizi mbili zinazokinzana yanaathiri jinsi
unavyouchukulia ulimwengu.)
E.
Soma Mithali 8:30-31. Nani aliyemsaidia Mungu wakati wa
uumbaji? (Hekima! Tafakari jambo hili. Unaweza kuwa na kipimo cha hekima ya
Mungu – aina ya fikra iliyokuwa ikiongoza wakati wa uumbaji wa ulimwengu!)
V.
Njia ya Hekima
A.
Soma Mithali 9:1-6. Hii inatoa taswira ya hekima
inayoishi kwenye nyumba kubwa, na sio kujinyima chakula na kuwa na msaada
kwenye mambo ya ndani ya nyumba. Kwa nini? (Kuishi kwa hekima ni kuishi vizuri.
Hii inatuambia kuwa hekima ni njia ya uzima. Sio tu kwamba ni ushauri
uliotengwa, ni jinsi tunavyoishi maisha mazuri.)
B.
Soma Mithali 9:7-8. Utagundua kwamba sasa tunahamia
kwenye ushauri mahsusi wa jinsi ya kutumia hekima. Mwenye kudharau ni nani?
(Yule anayemdharau Mungu au anayeidharau njia ya Mungu.)
1.
Tafakari jambo hili kidogo. Je, hatuitwi kuwapelekea
injili wadhambi? Jambo hili linatuambia nini? (Nadhani tunatakiwa kumwomba Roho
Mtakatifu atupatie utambuzi wa kutumia jambo hili. Kumkemea au kumsahihisha mtu
anayetaka kujifunza ni jambo moja. Kumkemea au kumsahihisha mtu mwenye uhasama
ni sawa na safari ya kuzurura – atakuchukia tu zaidi. Tunapaswa kuwa werevu, na
sio kupoteza nguvu zetu kwa watu ambao wamedhamiria kutupinga.)
C.
Soma Mithali 9:9. Nani yuko tayari kujifunza hekima
zaidi? (Wenye hekima na wenye haki.)
D.
Fikiria mafungu yetu machache ya mwisho. Je, hili
linaashiria nini kuhusu jinsi ambavyo tunapaswa kupeleka injili? (Tunatakiwa
kujikita kwa wale ambao wanataka kumwendea Mungu, ambao wana udadisi wa
kujifunza. Nadhani makanisa yanapaswa kujikita kwa watu wanaowatembelea. Ikiwa mtu
anayeishi maeneo ya jirani anawatembelea, kanisa linapaswa kuwa na mpango wa
kuandika jina la mtu huyo na namba zake za mawasiliano, na kisha kumfuatilia. Vipi
kuhusu kuweka njia ya kufanya ufuatiliaji kwa watu ambao wanatembelea tovuti ya
kanisa lako?
VI.
Kujipatia Hekima
A.
Soma Mithali 8:32-34. Hapo awali tulikubaliana kwamba
Mungu ndiye chanzo cha hekima ya kweli, na tunaiona hekima yake kwenye Biblia. Tunatakiwa
kutumia juhudi gani ili kupata hekima? (Juhudi za kila siku zenye mwelekeo
maalumu.)
B.
Soma Mithali 8:35-36. Tumejadili jinsi hekima
inavyotupatia faida za kupata vitu. Hatma ya manufaa inayotokana na juhudu za
kuipata hekima ni ipi? (Unafurahia upendeleo wa Mungu. Unapata uzima, na
kuepuka madhara na kifo.)
C.
Rafiki, je, ungependa kuboresha maisha yako? Hekima ya
Mungu ndio ufunguo. Je, utaamua kuweka lengo la kujifunza Biblia kila siku ili
kuwa na hekima zaidi katika njia za Mungu? Kwa nini usijitoe kufanya hivyo sasa
hivi?
VII. Juma lijalo: Baraka za Wenye Haki.
No comments:
Post a Comment