(Mithali
6 & 7)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Asubuhi ya leo nilikuwa ninasoma makala
inayohusu utani wa Wakanamungu. Katika utani huo, walikuwa wanamdhihaki Yesu na
kulinganisha vuguvugu la haki za wakanamungu na vuguvugu la haki za wasenge.
Mwandishi wa makala alibainisha kuwa utani na ushindani wa wasenge haudhihaki
ndoa inayohusisha jinsia mbili tofauti, yaani mwanamke na mwanaume. Kwa nini wakanamungu
wanawadhihaki Wakristo? Nimegundua kwamba baadhi ya washiriki wa zamani wa
kanisa langu sio tu kwamba wanaondoka na kuliacha kanisa, bali pia
wanalishambulia kanisa na kulidhihaki. Kwa nini wanafanya hivyo? Nadhani jambo
hili linahusiana na mojawapo ya kile tunachojifunza kwenye somo letu: mafunzo
yetu ya kidini tunayofundishwa tunapokuwa watoto yanakaa ndani yetu. Wale
wanaoacha kuenenda kwenye njia ya kile walichofundishwa wanajisikia hatia, na
hivyo kinachowakabili ni kufanyia dhihaka imani zao za awali ili iweze
kuwasaidia “kuzisahau.” Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone mambo
mapya tunayoweza kuyagundua kuhusu mafundisho ya kidini!
I.
Amri Juu ya Shingo
A.
Soma Mithali 6:20-21 na Mithali 7:3. Unadhani
mafundisho ya wazazi wako yanamaanisha nini yanapokuambia “jivike hayo shingoni
mwako” na “zifunge katika vidole vyako?”
B.
Soma Kumbukumbu la Torati 6:6-9 na Mithali 3:3. Hebu
tufanye tathmini. Tunaambiwa kuyahifadhi mafundisho mazuri katika mioyo yetu,
tujivike kwenye shingo zetu, tuyafunge katika mikono (vidole) vyetu na kwenye
vipaji vya nyuso zetu na kwenye milango na malango yetu. Hayo ni maeneo mengi.
Je, kuna mwelekeo wowote unaouona hapa? (Shingo ndilo njia kuu inayoingia
kwenye mwili, malango na milango ndizo njia za kuingilia nyumbani kwako. Moyo
wako na kipaji cha uso wako ni ishara za kile unachokifikiria na mikono yako ni
ishara ya kile unachokitenda. Nadhani ujumbe tunaopewa ni kwamba kile
tunachokiruhusu kuingia nyumbani kwetu na akilini mwetu, na kile tunachokifikiri
na kukitenda vyote vinapaswa kupitia kwenye chujio la neno la Mungu.)
1.
Kipi cha kujifunza ikiwa wewe ni mzazi unayejaribu
kutafakari jinsi ya kuwalea watoto wako? (Tunatakiwa kuzungumzia kuhusu mapenzi
ya Mungu katika kila fursa inayopatikana tunapokuwa na watoto wetu. Lakini,
tunatakiwa kuwa makini sana kuhusu “njia za kuingilia” katika kujifunza kwao.)
2.
Je, umewahi kulinganisha nyaraka mbili ili
kuzilinganisha kama zinatofautiana? Je, wazo hilo linaweza kuwa linahusika
hapa? (Nadhani hilo ni mojawapo ya jambo la kujifunza hapa. Unalinganisha kile
unachokifikiri na kukitenda, kile unachokiingiza nyumbani kwako na mwilini
mwako, na kile kilichoandikwa kwenye neno la Mungu na kufundishwa na wazazi
wako. Ikiwa huna kawaida ya kuyalinganisha mara kwa mara, ni rahisi sana kutoka
nje ya msitari.)
3.
Fikiria kama ulikuzwa kwa njia hiyo na sasa wewe ni
mkanamungu? (Hayo yatakuwa ni machafuko ya mara kwa mara.)
C.
Soma Mithali 6:22-23. Ni kwa jinsi gani mafunzo ya
wazazi wetu, ikiwa tuko radhi, yanaweza kutusaidia? (Yanatulinda wakati wote
kwa kuangaza njia ya uzima.)
1.
Kauli hiyo inaonekana kuwa ya kimahaba, “kuangaza njia
ya uzima.” Je, kauli hiyo inamaanisha nini kivitendo? (Mara ngapi tunashindwa
kutafakari mambo? Mara ngapi tunakosa kweli za muhimu sana? Maamuzi yetu
yanaashiria ubora wa maisha yetu, na Mithali inatuambia kwamba kile
tulichofundishwa na wazazi wetu kuhusu neno la Mungu kitatusaidia kufanya maamuzi
sahihi.)
II.
Maisha Kama Mkate
A.
Soma Mithali 6:23-24. Sasa tuna kielelezo cha jinsi
mafundisho wakati wa utotoni (pamoja na maonyo) yanavyoweza kutusaidia. Je, “ulimi
utoao sifa za kinafiki (ubembelezi wa mgeni)” unaashiria nini? (Ni rahisi
kumsikiliza mwanamke huyo.)
B.
Soma Mithali 6:25. Tatizo jingine ni lipi? (Uzuri wake,
tamaa yako.)
C.
Soma Mithali 6:26. Mkate ni mzuri! Kuna tatizo gani kwa
kufanywa kuwa mkate? (Tafsiri ya Biblia ya NIV inasema, “malaya hukufanya uwe
kipande cha mkate.” Wewe unakuwa katika hali ya kulika, na unaliwa.)
1.
Unadhani hii inamaanisha nini – unapolinganishwa na
mkate? (Hebu tuangalie uwezekano kadhaa. Kwanza, kutokufa kutakula. Kutachukua mambo
mengi kutoka kwako. Pili, unatumika tu. unatimiza hitaji kwa wakati uliopo,
lakini baada ya “kutumika” mtu mwingine anaendelea na mambo yake.)
D.
Soma Mithali 6:27-28. Je, kuna mtu ambaye anadhani kuwa
anaweza kuwasha moto kwenye mapaja yake bila kuungua? (Watu wenye uhusiano wa
kimapenzi wanadhani kuwa wanaweza kutunza siri ili uhusiano huo usijulikane. Hicho
ni kichekesho tu kwani hiyo ni siri ya muda mfupi tu. Mithali inatuambia kuwa
wazo hilo ni la kipuuzi. Uhusiano huo utajulikana nawe utaunguzwa.)
E.
Soma Mithali 6:30-35. Mafungu haya yanalinganisha wizi
unaofanyika kwa ajili ya kujishibisha na wizi wa “mapenzi.” Watu wanachukuliaje
hizi dhambi mbili tofauti? (Watu wanaelewa sababu ya mtu kuiba kwa ajili ya
kula, lakini hawakubaliani na uzinzi. Ikiwa utaiba chakula, kuna adhabu
iliyowekwa. Ikiwa utamuiba mwenzi wa mtu, unajiingiza kwenye madhara yasiyo na
kikomo.)
F.
Hebu tuchukue muda mfupi kuangalia uhalisia hapa. Linganisha
Kumbukumbu la Torati 17:17 na 1 Wafalme 11:3-4. Je, hiki ndicho kilele cha
unafiki: mtu mwenye wanawake 1,000 wa kulala nao anatuhusia wale tulio na mke
mmoja ambaye macho yetu, akili zetu na mikono yetu imeelekezwa kwake na si kwa
mwingine yeyote yule? (Kwa dhahiri kuna tofauti kubwa kati ya maelekezo ya mwalimu
wetu na utendaji wake. Hata hivyo, kitabu cha Wafalme wa Kwanza kinatuambia kuwa Sulemani alikengeushwa na
wake zake. Sulemani anafahamu kile anachokisema.)
1.
Soma Mathayo 23:2-3 na Mathayo 7:15-18. Unalinganishaje
haya mawazo mawili? (Mara kwa mara nimekuwa nikitania kwamba unafiki
unadunishwa. Kuna watu waovu wanaotenda mambo maovu – unapaswa kuepuka
mafundisho yao. Wakati huo huo, kuna watu ambao maisha yao hayaendani na mafundisho
yao, lakini wanafundisha mambo sahihi. Sulemani anatupatia ushauri sahihi.)
III.
Analojia
A.
Soma Mithali 7:10-14. Kwa nini mwanamke huyu
anabainisha “sadaka za amani?” (Inaashiria upole wa bandia kwenye masuala ya
kidini. Hii ni sawa kwa sababu sisi ni watu wa dini.)
B.
Soma Mithali 7:18-20. Katika sehemu ya utangulizi
tulijadili kuhusu mafunzo ya kidini. Sasa tumenaswa kwenye uzinzi na umalaya
kwenye mafungu mengi. Je, kweli Mfalme wetu Sulemani mwenye wanawake 1,000
anatumia nafasi hii yote kuelezea suala la kutokuwepo kwa uaminifu kwenye ndoa?
1.
Angalia mafungu haya kwa makini, mwanamke huyu anajenga
hoja gani? (Jambo hili litakuwa la kufurahisha na ninaweza kuthibitisha kwamba
kitendo hiki hakitakuwa cha hatari.)
C.
Soma Mithali 7:22-23. Je, kufanya ngono nje ya ndoa
kuaathiri maini? Je, kweli ni sawa na kujiua? (Nadhani Sulemani anazungumzia
taswira pana zaidi. Anatuambia kwamba dhambi na imani potofu vina ushawishi
halisi. Kuna mantiki bandia (ya uongo), hali ya kiroho bandia, na ahadi ya
kupata furaha. Lakini, yote hayo yanajielekeza kwenye kifo kichungu na kibaya.)
D.
Soma Zekaria 5:6-8. Uovu wa wanadamu unalinganishwa na
nini? (Mwanamke.)
E.
Soma Zekaria 5:9-11. Kwa nini unajenga nyumba kwa ajili
ya kikapu (efa)? (Kwa dhahiri hili ni tendo la ishara. Mwanamke anawakilisha
uovu, na Babeli ndiyo itakayokuwa mwenyeji, mahali pakaapo uovu.)
F.
Soma Mithali 7:24-27. Unapotafakari kitabu cha Zekaria,
je, unadhani mafungu haya yanaelezea suala la dhambi ya ngono? (“Jeshi kubwa”
halionekani kuendana na kisa chetu halisi cha kijana aliyejongea kwenda kwenye
nyumba ya mwanamke malaya (Mithali 7:7-8). Badala yake, hii inaonekana kuwa ni
dhambi kwa ujumla wake.)
1.
Mafungu haya yanaanza kwa kusema “nisikilizeni sasa” na
yanamalizia kwa kusema mwisho wa jambo hili ni mauti. Kwa nini unamwomba mtu
awe msikivu kwa jambo litakalomuua?
2.
Kifo kipo karibu sana na dhambi kwa kiasi gani? (Kwa
hakika sio cha haraka sana kiasi cha kusababisha usikivu wa moja kwa moja. Mwanangu
ni daktari, na anasema kwamba anapotoa ushauri wa kitabibu kwa watu wanaougua
saratani huwa wanasikiliza kwa makini sana na kutekeleza kile anachowaagiza
kukifanya. Kwa upande mwingine, wale walio na dalili za mkusanyiko wa magonjwa
(shinikizo la damu, lehemu nyingi mwilini [mafuta mengi kwenye damu], na
kiwango kikubwa cha sukari kinachosababisha ugonjwa wa kisukari), huwa
hawasikilizi kwa makini na kwa nadra sana wanatekeleza kile anachowashauri. Mwisho
wa magonjwa yote mawili ni kifo, na ugonjwa wa kisukari unaweza kusababisha
kifo kichungu. Kwa nini kuna tofauti? (Wale wenye ugonjwa wa saratani wanadhani
kuwa wanakikabili kifo sasa hivi, wale wenye dalili za mkusanyiko wa magonjwa
wanadhani kuwa bado wana muda mrefu wa kuishi.)
3.
Tulianza kwa kuzungumzia mafundisho kwa watoto wetu. Je,
hii ni sehemu ya tatizo – kwamba tunazungumzia jinsi dhambi inavyosababisha
mauti, na wanadhani kuwa “sitakufa katika kipindi cha siku chache zijazo?”
a.
Ikiwa niko sahihi, je, tunapaswa kuwa tunawafundisha
nini watoto wetu? (Bado tunatakiwa kuzungumzia hatima ya dhambi, lakini nadhani
ni bora zaidi kujikita kwenye matokeo ya haraka mabaya ya dhambi.)
4.
Hebu rudi nyuma kidogo. Mojawapo ya malalamiko yangu
enzi za ujana wangu ilikuwa ni kujikita kwenye dhambi badala kujikita kwenye
neema. Je, nimetumbukia (tumetumbukia) kwenye anguko la kizazi kilichotangulia?
(Nadhani ujumbe wote ni sahihi kwa watoto wetu: neema na hukumu kwa wale
wanaoikataa neema.)
G.
Rafiki, je, utavichukulia kwa dhati vishawishi maishani
mwako? Je, utayachukulia kwa dhati mafundisho yako ya kidini uliyofundishwa
utotoni mwako? Haya ni masuala ya kufa na kupona!
IV. Juma lijalo: Hekima ya Mungu.
No comments:
Post a Comment