Somo La 2 | Kutoka Masikioni Hadi Miguuni [Lesson]


(Mithali 4 - 6)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Jambo moja ambalo huwa ninawaambia wachungaji vijana ni kwamba mahubiri yanapaswa kuhusisha visa. Jambo hili linaweza kuonekana kutokuwa na mantiki. Ikiwa una dakika 20-30 za kuhubiri, unatakiwa kujazijazia “nyama” nyingi kwa kadri inavyowezekana, na kuepuka kufanya makosa, sawa? Sio sahihi! Ninamkumbuka mhubiri mmoja aliyekuwa akifungua fungu la Biblia baada ya jingine akijaribu kuelezea alichokuwa akikifundisha. Hapakuwepo na gramu hata moja ya “mafuta.” Lakini, saa moja baadaye, hakuna mtu hata mmoja aliyeweza kukumbuka kile alichokisema. Ikiwa hubiri lake lilisikika, basi halikuweza kuingia na kunasa akilini mwa watu. Visa vinawafanya watu wasikilize kwa makini na kufanya kile unachokisema kuwakaa akilini mwao. Kukumbuka kile kilichosemwa kinakusaidia kufanya maamuzi. Yesu alidhihirisha jambo hili kutokana na mifano aliyoitoa. Usikivu ndio mwanzo wa safari yetu katika somo la juma hili kuhusu kufanya maamuzi sahihi, hivyo, hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia!
I.                   Kuwa Makini na Afya
A.                Soma Mithali 4:20. Jambo gani ni la muhimu sana kuhusu kuzungumza? (Kuwa na mtu “anayesikiliza.”)
1.                  Je, unadhani jambo hili ni rahisi zaidi leo kuliko ilivyokuwa ulipokuwa kijana mdogo? (Siku hizi video/sinema na simu za kisasa ni washindani halisi kwenye suala zima la usikivu.)
B.                 Soma Mithali 4:21. Jambo linalofuata kwa umuhimu kuhusu kuzungumza ni lipi? (Maneno yako kukumbukwa. Kuyatekeleza maneno yako kivitendo.)
C.                 Nakumbuka utafiti uliobainisha kwamba muda wa usikivu na umakini wa wazee wa baraza ni dakika saba. Hebu tafakari jambo hilo! Katika hali ya kushangaza, kwenye chumba cha mahakama, wakati maisha au mali inapogeuka dhidi ya uamuzi wako, na kiwango chako cha usikivu ni dakika saba tu! Fikiria jinsi hali ilivyo kanisani. Nimeelezea habari za visa, je, unaweza kufanya jambo gani jingine ili kuboresha usikivu wa maneno yako? (Kwenye madarasa yangu, katika darasa la kujifunza Biblia na katika madarasa ya shule ya sheria, huwa ninatembea na kuzunguka sana ninapokuwa ninafundisha. Ninauliza maswali mengi, ninafanya darasa liwe shirikishi, nafanya uchekeshaji, na mifano inayoonekana – vyote hivi ni sehemu ya mkakati wangu wa kuifanya hadhira ijikite kwenye malengo yaliyopo mbele yao. Unaweza kuwa umegundua kwamba sehemu kubwa ya Biblia inajumuisha visa.)
D.                Soma Mithali 4:22. Kwa jinsi ilivyo, kauli hii si ya kawaida. Unataka watu wajifunze kutoka kwako, lakini matokeo yake yanahusiana na uhai na afya. Je, unafundisha masuala ya lishe? (Utakumbuka kwamba somo linahusu hekima ya Mungu. Kuufuata mpango wa Mungu kwa ajili ya maisha yako huongeza urefu wa maisha yako (angalia Mithali 3:1-2) na afya bora (angalia Mithali 3:7-8).)
1.                  Mithali 4:22 inapoahidi “afya ya mwili wao wote,” je, unadhani hii inahusisha afya ya akili?

E.                 Soma Mithali 1:1, Mhubiri 9:5 na Mhubiri 9:9. Mithali inatuambia kuwa Sulemani ndiye mwandishi/mhariri wa kitabu cha Mithali. Je, mafungu haya kutoka kwenye kitabu cha Mhubiri yanaonekana kuandikwa na mtu aliyekuwa na afya ya akili iliyo sahihi? (Usomaji wangu wa maandiko ya Sulemani unanifanya nidhani kwamba alikuwa na msongo wa mawazo. Mara kwa mara Mhubiri 9:5 huwa inanukuliwa kuhusu hali ya wafu, lakini hilo halileti mantiki kwangu kwa sababu maneno yanayofuata yanasema kwamba wafu “hawana ijara tena.” Hakuna Mkristo anayeamini katika mbingu anadhani kwamba waliokufa katika Yesu “hawana ijara tena.” Hii ni kauli ya mtu aliyejaa msongo wa mawazo.)
1.                  Ikiwa niko sahihi kwamba Mfalme Sulemani alikuwa na msongo wa mawazo, je, hali hii inaashiria nini kuhusu kauli ya Sulemani kwamba hekima huzaa “afya ya mwili wa mtu?” (Hii inayafanya maneno yake yaaminike zaidi. Mtu anayeteseka na msongo wa mawazo anaelewa faida za kuifuata hekima ya Mungu. Tunafahamu si mara zote Sulemani alifuata ushauri wake mwenyewe. Kwa hiyo, alielewa jinsi kuifuata njia ya Mungu kunavyotusaidia kukabiliana na masuala ya afya.)
F.                  Soma Mithali 4:23-25. Unaposikia maneno ya hekima na kujaribu kuyaweka kivitendo, je, unapaswa kuwa unafanya nini wakati huo huo? (Unatakiwa kuchukua hatua madhubuti. Unatakiwa kuchunga kile kinachoingia akilini mwako (moyoni mwako). Hii inahusiana na kile unachokiona, malengo uliyo nayo, na kile unachokisema.)
II.                Uaminifu na Usitawi (Mafanikio)
A.                Soma Mithali 5:1-4. Kwa nini watu wanafanya ngono nje ya ndoa? (Tunapenda asali. Mafunu haya yanaashiria mvuto.)
1.                  Kwa nini “maneno malaini” ni sehemu ya vitendo hivyo? Nina mashaka watu wengi walio na mahusiano ya aina hiyo wanafanya hivyo kutokana na uwezo wao mkubwa wa kuzungumza mbele za watu! (Nadhani watu wengi wana mahusiano ya aina hiyo kwa sababu ya majisifu na ubinafsi. Wanaona sifa kwamba mtu mwingine tofauti na mwenzi wako amevutiwa naye. Hapa ndipo penye umuhimu wa “maneno laini.”)
2.                  Kilichopo mwishoni mwa asali na majififu/ubinafsi ni kipi? (Machungu.)
3.                  Unadhani nini maana ya upanga wa makali kuwili? (Yule ambaye una uhusiano naye anakuumiza.)
B.                 Soma Mithali 5:7-8. Ushauri wa kuepuka uhusiano wa kimapenzi ni upi? (Usiukaribie, kaa nao mbali.)
1.                  Je, hivyo ndivyo wafanyavyo watu wengi? (Unapenda asali, unapenda sifa, kwa hiyo kwa asili moyo unasogea karibu kwa kadri inavyowezekana huku ukifikiria kwamba hatari inaweza kuepukika.)
C.                 Soma Mithali 5:9-10. Je, hatima hii inaingilianaje na wazo la majisifu? (Kinyume chake ndicho kinachotokea. Unapoteza heshima yako, hadhi yako, na mali zako.)

1.                  Je, Sulemani anatunga tu jambo hili, au jambo hili linaendana na jinsi unavyouchukulia uhalisia?
D.                Soma Mithali 5:15-18. Hii ni taswira ya maneno yenye kufurahisha sana. Je, maji hutupatia nini? (Uzima. Ngono hutupatia uzima. Wazo lililopo hapa ni kwamba ngono ni jambo la pekee kati ya mume na mke.)
1.                  Mke wangu (ndoa yangu ina zaidi ya miaka arobaini), mara kwa mara huwa anawabainisha wanawake ambao wameachwa na waume wao wakati wake hao wakiwa kwenye umri wa miaka kati ya hamsini na kuendelea. Wanaume hawa hawakufurahia wake wa ujana wao. Kwa nini hawakufurahia? (Kwa ujumla, wanakuwa wamempata mke kijana zaidi. Hiki ni kipengele cha “asali.” Biblia inasema kwamba inabadilika na kuwa nyongo. Huenda nyongo inatokea pale mke mpya anapotambua kwamba ameolewa na mzee! Wanandoa ambao wameoana kwa muda mrefu wanatambua furaha ya kudumu katika uhusiano – angalao hilo ndilo lengo.)
III.             Busara na Fedha
A.                Soma Mithali 6:1-2. Tatizo ni lipi? (Umeweka ahadi ya kutenda jambo kwa ajili ya rafiki wako au jirani yako. Mfano wa kawaida ni kushirikiana kusaini mkopo kwa ajili ya rafiki yako.)
B.                 Soma Mithali 6:3-5. Suluhisho la tatizo la aina hii ni lipi? (Kwanza kabisa usikubali kujitumbukiza kwenye ahadi kama hiyo!)
1.                  Vipi kama tayari umeshafanya hivyo? Fungu la 3 linatuambia nini pale linaposema “usimpumzishe jirani yako?” (Unatakiwa kumsisitiza mtu uliyekubali kumsaidia ili kuhakikisha kwamba anatimiza wajibu wake. Rafiki anatakiwa kusisitiziwa ili alipe mkopo.)
2.                  Je, fungu hili linatupatia suluhisho gani jingine? (Kufanya haraka. Tatua tatizo hili mara moja.)
C.                 Soma Mithali 6:6-7. Nani anayeshauriwa kumfikiria chungu? (Mtu mvivu.)
1.                  Kwa nini fungu linabainisha kwamba chungu hana akida? (Chungu “anajiongoza mwenyewe.” Hahitaji mtu wa kumsisitiza kufanya kazi.)
a.                   Je, unadhani mafungu haya yanasema chochote kuhusu mfumo wa serikali anaoupendelea Mungu? (Yanatueleza kwamba mafanikio kazini hayategemei serikali kuingilia kati.)
D.                Soma Mithali 6:8. Kwa nini ni muhimu kwa chungu kukusanya na kuweka akiba wakati wa jua na mavuno? (Kazi ya kufanya inapokuwepo, chakula kinapokuwepo, chungu anafanya kile kinachotakiwa (anatenda jambo sahihi).)
1.                  Je, tunajifunza nini? (Usiwe na mazoea ya kuahirisha ahirisha mambo.)
E.                 Soma Mithali 6:9-11. Hivi karibuni nimesoma utafiti uliobainisha kwamba Wamarekani hawalali vya kutosha. Je, wale walio Marekani wanaosoma fungu hili wanapaswa kujipigapiga mgongoni?


1.                  Kwa nini usingizi unafananishwa na mnyang’anyi? (Uvivu utakukosesha vitu – kama ilivyo kwa mnyang’anyi. Pamoja na takwimu zinazohusu usingizi, hili ni onyo linalohusu kutokufanya kazi. Ikiwa utaiingiza akili yako kwenye mtazamo kama huo, basi suala la umasikini liko mlangoni.)
2.                  Siku chache tu zilizopita tumemaliza kujifunza habari za Yakobo, ambapo Yakobo ana mambo yasiyo ya kawaida kuhusu matajiri. Ingawa Wamarekani wanaweza wasiwe wanapata usingizi wa kutosha, utafiti uliofanyika mwaka 2013 unaonesha kuwa asilimia 58.6 pekee ndio wanaofanya kazi. Je, hii inaashiria nini kuhusu chanzo cha umasikini? (Watu wanatakiwa kumwangalia chungu na kufanya kazi pale wanapoweza.)
F.                  Rafiki, tumejifunza mambo mengi! Kwa kutumia sentesi moja, je, somo letu linahusu nini? Msikilize Mungu, yatekeleze maneno yake, nawe utafurahia kuwa na afya njema, utakuwa na ndoa bora, na utakuwa na fedha nyingi. Je, utaifuata njia hii ya mafanikio?

IV.             Juma lijalo: Kufa na Kupona.

No comments:

Post a Comment