(Mithali
1 & 2)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, ungependa kuwa mwerevu? Je, ungependa
kufahamu jambo sahihi la kuzungumza katika nyakati ngumu? Katika masomo
ninayoyafundisha kwenye shule ya Sheria yanayohusiana na ajira, huwa ninajumuisha
“somo dogo” lililojengwa juu ya Biblia kuhusu kutawala hisia. Kutawali hisia si
jambo jingine bali kwa maana nyingine ni hekima. Kuna tafiti kadhaa
zinazodhihirisha kwamba waajiriwa walio na hekima wana mafanikio zaidi. Lifuatalo
ni jambo unaloweza kulifahamu: Kwa ujumla waajiriwa huwa hawafukuzwi kazi kwa
sababu hawawezikufanya kazi vizuri. Mara nyingi huwa ni kutokana na uwezo wao
mdogo wa kutoendna na wenzao. Mafungu ya Biblia ninayoyatumia kufundisha juu ya
hekima yanatoka kwenye kitabu cha Mithali. Habari njema ni kwamba robo hii
tunajifunza kitabu cha Mithali na kuhusu hekima. Hebu tuzame kwenye somo letu
la kwanza!
I.
Yaliyomo
A.
Soma Mithali 1:1-2. Je, umeangalia kielelezo cha kitabu
ili kuona kama utafurahia kukisoma? Kitabu cha Mithali kinaanza kwa kielelezo. Je,
mafungu haya yanaashiria mambo gani tutakayoyaona ndani ya hiki kitabu? (Tunaweza
kujifunza jinsi ya kuwa na hekima/busara na jinsi ya kuwa na utambuzi bora.)
B.
Soma Mithali 1:3. Je, tutajifunza mambo gani mengine
katika kitabu cha Mithali? (Haki. Kuwa na adili.)
C.
Soma Mithali 1:4. Tunazaliwa tukiwa na kiwango fulani cha
akili ambacho inaonekana hakiwezi kuongezwa kwa kiwango kikubwa. Je,
hekima/busara iko hivyo (inafanana na akili) – tunagota kwenye kile
tunachokipata wakati wa kuzaliwa? (Hapana. Hii inatuambia kuwa watu wa “kawaida,”
ikimaanisha wale ambao sio werevu sana, na “vijana,” ikimaanisha wale ambao
hawajakomaa, wanaweza kujifunza kuwa na hekima, wanaweza kuwa na busara.)
D.
Soma Mithali 1:5. Je, Mithali ni kwa ajili ya wale
walio na hitaji la kurekebishwa/kufundishwa kuwa na hekima? (Hapana. Bila kujali
kiwango chako cha hekima, kitabu cha Mithali kinaweza kuboresha hekima na
busara yako.)
II.
Vyanzo vya Hekima
A.
Soma Mithali 1:7. Chanzo cha hekima ya kweli ni kipi?
(Mungu.)
1.
Ni kwa mantiki ipi neno “kumcha” linatumika hapa?
(Inaonekana kuwa ni wito wa kutii mtazamo wa Mungu juu ya mambo.)
2.
Maoni ya mtu mmoja yalibainisha kwamba huku kumcha “hakuhusiani
kivyovyote vile na hofu ya ushirikina na ya kitoto ya hukumu ya Mungu.” Je,
unakubaliana na maoni haya?
B.
Soma Ufunuo 14:9-10. Je, malaika huyu anasambaza hofu
ya kishirikina na ya kitoto? (“Ya kishirikina” inarejea “jambo lisilo la
kawaida” – linalojumuisha kazi ya Mungu. Hofu ya hukumu ya Mungu inaleta
mantiki. Hofu ya “kitoto” pia inaleta mantiki kwa mujibu wa Mathayo 18:2-3. Hapo
Yesu alisema kwamba kuachana na kiburi, na kufanana na watoto, ni mtazamo wa
muhimu sana katika kujifunza.)
C.
Angalia tena sehemu ya mwisho ya Mithali 1:7. Unafikiria
nini kuhusu masuala kadhaa juu ya kumcha na wazo la kumwomba Mungu kutupatia
hekima? (Utabaini kwamba Mithali 1:7 inasema kuwa “wapumbavu” hudharau hekima
ya Mungu. Kwangu binafsi inaonekana ni upumbavu kupuuzia hatma kuu ya wale wanaopotea.
Kumcha Mungu kunaanzia kwenye kutii maoni yake kwa sababu anatupenda na anataka
tuishi maisha bora, kufahamu ubaya wa kutisha wa mauti ya milele. Nadhani mambo
yote haya yanajumuishwa kwenye maneno “kumcha Bwana.”)
1.
Je, sio sahihi, au ni ukiukwaji wa kanuni ya upendo,
kuzungumzia kuhusu uangamivu wa waovu? (Wanangu walipokuwa wadogo, tulikuwa na
wasiwasi kwamba wangeweza kuchezacheza mitaani na kuishia kugongwa na gari. Kuchakuro
(aina ya mnyama) alipouawa barabarani kwa kugongwa, mke wangu aliwapeleka
watoto barabarani na kuwaonyesha jinsi mnyama huyu alivyogongwa. Hilo lilikuwa
somo kubwa sana. Ninaweza kuona hekima “ikianza” kutokana na hili jambo la
msingi.)
2.
Mungu anatupatia hamasa gani katika kitabu cha
Kumbukumbu la Torati 28? Kama tulivyoona kwamba kitabu cha Mithali ni kwa ajili
ya watu wa kawaida na wale ambao tayari wana hekima/busara, vivyo hivyo Mungu
anatufundisha katika ngazi mbalimbali. Kama ilivyo kwa watoto, anaanza kwa
zawadi na adhabu, kisha anatuelekeza kwenye mtazamo mpana zaidi wa uhusiano
wetu.)
D.
Soma Mithali 1:8-10. Vyanzo vingine vya hekima
vilivyopo ni vipi? (Wazazi wetu.)
1.
Je, kuna ukomo katika jambo hili? (Ukiangalia fungu la
10, linatuonya kuhusu kushawishiwa na “wadhambi.” Dhana iliyopo hapa ni kwamba
una wazazi wanaompenda Mungu.)
2.
Kwa nini vilemba na mikufu inatajwa ikilinganishwa na
kukubali ushauri wa wazazi wako? (Hizi ni ishara za heshima.)
3.
Tunapaswa kuchaguaje mahali pa kupata hekima yetu?
(Tunapaswa kuwa na uchaguzi. Fungu la 10 linatuambia kuwa ushauri unaotokana na
Mungu na unaoendana na matakwa ya Mungu ndio tunaouhitaji. Ushauri wa watu
ambao maisha yao hayaendani na ushauri wa Mungu unapaswa kuepukwa.)
E.
Soma Mithali 1:11-14. Lengo la ushauri huu ni lipi? (Kufanya
vurugu ili kupata fedha.)
F.
Soma Mithali 1:15-16. Kwa nini ni muhimu “kutokwenda
njiani pamoja” na watu kama hawa, au “kuweka mguu” katika mapito yao? Kwa nini
usiseme tu kwamba “Usiungane nao katika maovu yao?” (Hili ni jambo la muhimu
sana kwenye sheria ya Marekani. Ikiwa unaendesha gari ukiwa umewabeba marafiki
kadhaa “wabaya,” na mmoja akaruka kutoka kwenye gari na kutenda kosa la jinai,
ikiwa utaendesha na kuwaondoa kutoka kwenye eneo la tukio nawe utakuwa na hatia
kwa ajili ya hilo tukio la jinai! Biblia inasema, “kaa mbali!” Huu ni ushauri
mzuri wa kisheria.)
G.
Soma Mithali 1:17-19. Mithali inamaanisha nini kuhusu
mtego unaoonekana? (Kwa kawaida, unawashika ndege kwa kutumia mtego ambao
hauonekani kirahisi. Mithali inasema kuwa tatizo lililopo kwenye aina ya tabia
mbaya iliyoelezewa hapo juu ni la dhahiri kwa mtu yeyote mwenye busara. Badala ya
tabia mbaya kuingizia fedha, inayaharibu maisha ya mtenda maovu.)
III.
Wito wa Hekima
A.
Soma Mithali 1:20-21. Wito wa kumcha Mungu unatolewa
wapi? (Sio kanisani peke yake, bali hadharani! Wito upo kila mahali.)
B.
Soma Mithali 1:22-23. Hii inatofauanaje na mtazamo wa
ulimwengu kuhusu kumfuata Mungu? (Ulimwengu unadai kwamba Wakristo ni wapumbavu
na hawajaelimika. Mithali inasema kuwa kinyume chake ndio ukweli. Wale wanaomkataa
Mungu ni watu wa kawaida (sio werevu sana), wadhihaki na wapumbavu.)
1.
Tunawezaje kuonyesha upendo kwa wapagani, na wakati huo
huo kusema kwamba wao ndio wajinga halisi?
2.
Kumdhihaki mpinzani wako ni silaha kuu inayojadiliwa. Mungu
anapowaita wapagani kuwa ni “wadhihaki” je, anamaanisha kwamba aina hii ya
mjadala ipo nje ya mipaka kwa Wakristo? (Utabaini kwamba dhihaka inaonekana kutofautishwa
na maarifa ya Mungu. Inaonekana kwamba hoja zinazojengwa juu juu ya dhihaka
badala ya kujengwa juu ya maarifa zinapaswa kuwa nje ya mipaka.)
3.
Ikiwa tutatubu, Mungu atafanya nini? (Atatujaza hekima.
Atatufundisha njia zake.)
C.
Soma Mithali 1:25-26. Sasa tunaona kwamba Mungu
anawadhihaki wale wanaoukataa ushauri wake. Sasa je, tunaweza kuwadhihaki
wapagani?
1.
Utagundua kwamba dhihaka inatokana na maafa na majanga.
Je, hilo linaathirije mawazo yako? (Hili ni gumu. Taswira ninayoiona ni kwamba
Mungu anawadhihaki wale waliomdhihaki. Maafa kwa watu wa dhati ni fursa wa
kushiriki nao injili kwa upendo.)
IV.
Kuishikilia Hekima
A.
Soma Mithali 2:1-4. Juhudi gani zinahitajika katika
kuifukuzia hekima ya Mungu? (Tunatakiwa kuitafuta kwa dhati – kama vile
tunavyotafuta hazina iliyositirika (iliyozikwa)!)
B.
Soma Mithali 2:5-6. Kama tulivyobainisha hapo awali,
akili ya kawaida inabainishwa wakati wa kuzaliwa. Vipi kuhusu hekima, je, mtu
yeyote anaweza kuwa nayo? (Wale tu wanaoitafuta kwa dhati ndio wanaoweza kuipata.
Habari njema ni kwamba kila mtu ana fursa ya kuwa na hekima. Habari mbaya ni
kwamba jambo hili ni la kufanyia kazi – tunatakiwa kuifanyia kazi.)
C.
Soma Mithali 3:1-2. Mara tunapopata hekima, je, inakuwa
sehemu ya kudumu maishani mwetu? (Tunaweza kusahau kanuni za Mungu. Lengo ni
kuwa nazo mawazoni mwetu. Kuzifanya ziwe sehemu ya jinsi tunavyotafakari na
jinsi tunavyoishi.)
V.
Matokeo ya Hekima
A.
Soma Mithali 1:32-33. Je, maamuzi yetu juu ya Mungu
yana athari?
B.
Soma Mithali 2:6-8. Kipengele kipi cha kujali kwa Mungu
kinarudiwarudiwa hapa? (Ulinzi wa Mungu. Mungu ni “ngao,” “mlinzi” na “mhifadhi.”)
1.
Je, unadhani kwamba Mungu anaingilia kati ili kuwalinda
wale wanaofuata ushauri wake? (Kwa hakika inawezekana kabisa Mungu kuingilia
kati, lakini ninadhani kwa ujumla jambo hili linarejea matokeo ya asili ya
matendo fulani. Kufuata ushauri wa Mungu (kuonyesha hekima) kunakulinda dhidi
ya mambo mengi mabaya maishani.)
C.
Rafiki, je, uko radhi kutia juhudu ili kupata hekima ya
Mungu? Kwa nini usijitoe kwa ajili ya jambo hilo leo, ili kwamba maisha yako yawe
kwenye njia ya kuboresheka!
VI. Juma lijalo: Kutoka Masikioni Hadi Kwenye Miguu.
No comments:
Post a Comment