(Yakobo
5:13-20)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, umewahi kuwasikia watu wakisema kuwa wanaabudu
kwa namna zao wenyewe? Wamechoshwa na “kanisa” na kwamba kukutanikia jangwani
ni bora zaidi kwa sababu jangwa haliwaambii maneno yasiyo mazuri. Ingawa ni
ukweli kwamba ni muhimu kutenga muda binafsi wa kuwa na Mungu, katika somo letu
juma hili Yakobo anaelezea manufaa ya kushirikiana [kuchangamana] kiibada na
Wakristo wenzetu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!
I.
Ushirika na Mungu
A.
Soma Yakobo 5:13. Maelezo ya fungu hili yanatuhusu watu
wengi. Uwezekano mkubwa ni kwamba aidha tuna matatizo au hatuna furaha. Tunatakiwa
kuitikiaje uzoefu huu wenye tofauti kubwa? (Kwa kumgeukia Mungu. Ama tunatakiwa
kuomba kwa ajili ya kupata msaada au tunatakiwa kumsifu Mungu kwa njia ya
nyimbo.)
1.
Mwitikio wako kimaadili ni upi unapojikuta kwenye
matatizo? (Siku za nyuma, papo hapo nilifanya kile nilichoweza ili kutatua
tatizo. Sasa nimejifunza kwamba hatua ya kwanza lazima iwe ni kumgeukia Mungu.)
2.
Je, huwa unakasirika unapokabiliana na matatizo? (Asili
ya mwanadamu huwa ni kuwalaumu watu wengine, na kisha kukasirika kutokana na
kile walichotutendea. Ikiwa, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, tutamgeukia Mungu
kwanza, itatuepusha kusema au kutenda jambo baya papo hapo kwa sababu ya
hasira. Hii itaepusha kufanya tatizo kuwa gumu zaidi.)
B.
Mtazamo wa namna gani unaakisiwa kwenye ushauri wa
Yakobo kwa ajili yetu kuomba au kusifu? (Mungu ndiye anayeyashikilia maisha
yetu. Yeye ndiye chanzo cha mibaraka yote. Tunamgeukia ili kupata msaada na
tunamshukuru kwa kumpa sifa.)
II.
Ushirika na Waumini
A.
Soma Yakobo 5:14-15. Kuugua ni mfano mahsusi wa tatizo.
Kwa nini usijiombee tu wewe mwenyewe – kama anavyobainisha Yakobo katika mstari
wa 13? Kwa nini kuwahusisha wazee katika jambo hili? (Mungu hahitaji wazee
kumshawishi ili afanye uponyaji, lakini wazo la kushirikiana na waumini wenzako
linaelezewa hapa.)
1.
Kuna nyakati kadhaa nilikuwa sehemu ya kundi la wazee
waliomwombea na kumpaka mafuta mgonjwa. Nchini Marekani, watengenezaji wa dawa
wanaeleza bayana athari za dawa zao wakati ule ule wanapotangaza jinsi dawa zao
zinavyoweza kutibu. Mke wangu alikuwa akiniambia kwamba nilitakiwa kubainisha
jambo hili nilipokuwa sehemu ya wanaofanya maombi na kupaka mafuta katika
kipindi cha nyuma ambapo wagonjwa hawakupona. Mke wangu alikuwa akitania,
lakini hadi siku za hivi karibuni, jambo hilo lilibakia kuwa ukweli mtupu. Je,
Yakobo anatoa ahadi za uongo kuhusu uponyaji?
a.
Je, mimi ndiye niliyekuwa tatizo? Yakobo anapoandika “na
kule kuomba kwa imani,” je, alikuwa akiandika kuhusu imani ya wazee? Kama sivyo,
anaelezea imani ya watu gani, je, ni imani ya mgonjwa?
B.
Soma Marko 2:1-5. Je, hapa Yesu anazungumzia imani ya
nani? (Haiko wazi. Yesu anaonekana kuzungumzia imani yao wote.)
C.
Soma Mathayo 18:19. Vipi kama mgonjwa alikuwa na imani
na mzee mmoja pekee ndiye alikuwa mwenye haki, je, imani hiyo ingetosha kuleta
uponyaji? (Utagundua kwamba Yesu haonyeshi kiwango cha imani au haki inayotakiwa,
anabainisha tu idadi ya waumini waliokubaliana. Wawili wanatosha.)
D.
Hebu tuangalie tena Yakobo 5:15. Je, Yakobo anatoa muda
wa kuinua na kuponya? (Hapana. Nina uhakika kila mtu aliyekuwa kwenye huduma ya
kupaka mafuta ambapo mimi pia nilihusika alikuwa mdhambi – kuanzia mgonjwa hadi
kwa wazee wote. Yakobo hasemi kwamba hatutakiwi kuwa na dhambi, anasema kwamba
tunatakiwa kuwa na imani. Kwa kuongezea, hatoi muda kwa ajili ya uponyaji. Ninaamini
Mungu atawafufua katika uzima wa milele wote waliolala wakimtumaini Yeye.)
E.
Kipindi cha hivi karibuni kabisa ambapo nilikuwa sehemu
ya kundi la wazee waliokwenda kufanya maombi, mgonjwa aliponywa. Mungu anatenda
miujiza maishani mwangu, na kwenye maisha ya wale ninaowaombea, na ninaamini
hili linahusiana zaidi na mapenzi ya Mungu mwenye enzi, badala ya haki yangu. Je,
wewe unadhanije?
III.
Uponyaji, Imani na Dhambi
A.
Angalia tena sehemu ya mwisho ya Yakobo 5:15 na Marko
2:5. Yesu anamwambia mwenye kupooza kwamba dhambi zake zimesamehewa. Yakobo anasema,
dhambi zinaweza kusamehewa. Je, kuna uhusiano gani kati ya uponyaji na dhambi?
B.
Soma Yohana 9:1-3. Kwa nini wanafunzi waliuliza kuhusu
dhambi na upofu? (Uelewa wa kipindi hicho ulikuwa ni kwamba dhambi ilisababisha
magonjwa. Nadhani bado kuna ukweli mwingi kwenye uelewa wao.)
1.
Je, Yesu alisema kuwa sababu ya upofu ni ipi? (Ili
Mungu aweze kutukuzwa. Haikuwa suala la dhambi.)
2.
Dhambi inapoungamwa na kusamehewa, je, Mungu
anatukuzwa? (Ndiyo! Angalao kauli za Yakobo na Yesu kuhusu ugonjwa na dhambi
zina maelezo ya aina mbili. Kwanza, ni uelewa wa watu wa kipindi hicho. Lakini,
jambo la muhimu zaidi ni kwamba, Mungu anataka kutuponya dhambi. Lengo lake kuu
kwetu ni kuwa na maisha yasiyo na dhambi na ugonjwa – na lengo hilo litatimia
mbinguni.)
C.
Siku chache zilizopita nilikuwa mapumzikoni kwa muda wa
siku kadhaa eneo la “Disney World,” ambapo watu wanene wanakusanyika na
kuendesha vijigari. Kiukweli, watu wengi waliokuwepo mahali pale pia walikuwa
wanene. (Katika kuzungumzia suala la unene, niliweza kuongezeka uzito wa
kilogramu 1.8 nilipokuwa likizo!) Wakati huo huo, sikumwona mtu hata mmoja
akivuta sigara. Inaonekana kwamba hatari ya kiafya inayotokana na uvutaji wa
sigara imebadilishwa na hatari ya kiafya inayosababishwa na unene mkubwa kupita
kiasi. Swali gumu ni hili: je, dhambi inaweza kuingiliana na uponyaji?
1.
Kama utasita kumwombea mvuta sigara ili aweze kuponywa,
vipi kuhusu mtu mnene kupita kiasi?
2.
Je, kiasili baadhi ya watu si ni wanene tu? Je, hilo linajalisha?
3.
Nimesoma sana kuhusu ubongo, na ninashawishika kwamba
mazoezi ni tiba ya watu wote kwa magonjwa ya aina yote, yakiwemo masuala ya
kiakili. Je, kushindwa kufanya mazoezi ni dhambi inayotuzuia tusiponywe?
4.
Je, nimemtukana takribani kila mtu? Ninachokimaanisha ni
kwamba tunawaangalia wavuta sigara wanaougua saratani ya mapafu, na wasenge
wanaougua UKIMWI, na hatuwahurumii sana kutokana na matendo yao.
IV.
Kutubu [Kuungama] Dhambi
A.
Soma tena Yakobo 5:15. Muda wa msamaha ni upi? (Baada
ya mtu kuponywa. Hii inaashiria kwamba uponyaji upo kwa ajili ya watu wote.)
B.
Soma Yakobo 5:16. Hebu subiri kidogo! Baada ya mjadala
wetu juu ya dhambi, je, Yakobo anasema kuwa tunatakiwa kutubu dhambi zetu ili
tuweze kuponywa? Au, je, kuombeana sisi kwa sisi ndio kigezo pekee
kinachohusiana na uponyaji?
C.
Angalia tena Yakobo 5:16. Unafikiria nini kuhusu kutubu
dhambi kwa waumini wenzetu?
D.
Soma Zaburu 51:4, Zaburi 32:5 na 1 Yohana 1:9. Je,
mafungu haya yanapendekeza kwamba tutubu dhambi zetu kwa nani? (Tunatenda
dhambi dhidi ya Mungu, na Mungu ndiye ana uwezo wa kusamehe dhambi. Hivyo,
inaleta mantiki kutubu dhambi zetu kwa Mungu.)
E.
Unapotafakari kuhusu jambo hili, je, kuna aina
mbalimbali za kutubu? (Ninadhani hivyo. Kwanza, kuna kutubu na msamaha wa
dhambi, jambo ambalo ni suala kati yako na Mungu. Pili, Mathayo 18:15, Luka
17:4 na Mambo ya Walawi 6:1-5, mafungu yote hayo yanaashiria kwamba kuna dhambi
ambazo tunatakiwa kuombana msamaha sisi kwa sisi. Tatu, ni kile ninachodhani
Yakobo anakizungumzia; mantiki ya jumla kwamba tunatenda kazi na waumini
wenzetu ili kuelekea kwenye haki. Tunaombeana sisi kwa sisi, tunajadiliana
dhambi zetu sisi kwa sisi, tunajadiliana masuala ya kiroho sisi kwa sisi.)
V.
Nguvu ya Maombi
A.
Soma Yakobo 5:17-18 kisha usome sehemu ya mwisho ya
Yakobo 5:16. Tumekuwa tukijadili juu ya dhambi, lakini nadhani Yakobo amejikita
kwenye maombi. Kwa nini Yakobo anamtaja Eliya kama mfano? (Anasema alikuwa “mwanadamu
mwenye tabia moja na sisi.” Sote tuna uwezekano wa kuwa na maombi yenye nguvu
na ufanisi mkubwa.)
1.
Soma 1 Wafalme 19:3-4. Kwenye mjadala wetu hadi
tulipofikia, nimelinganisha [nimehusianisha] masuala ya kiafya na dhambi. Katika
Mathayo 15:16-18 Yesu anapendekeza kwamba mlingayo huu si sahihi. Kwa upande
mwingine, kutokumtumaini Mungu ni dhambi (Ufunuo 21:8). Yakobo anapotuelekeza
kwa Eliya, je, anasema nini? (Imani na udhati katika maombi ndio ufunguo wa
uponyaji, sio kutokuwepo kwa dhambi.)
B.
Soma Yakobo 5:19-20. Haya yanaonekana kama madai ya
mwisho ya “matendo” – ikiwa tutawaongoa upya “waliorudi nyuma” dhambi nyingi
zitasamehewa. Je, muktadha huu unaashiria kuwa uelewa sahihi wa jambo hili ni
upi? (Unazungumzia juu ya uelewa wetu wa dhambi, badala ya asili ya wokovu. Sura
hii ilikuwa inazungumzia juu ya kufanya ushirika [kuchangamana]. Ikiwa mtazamo
wako ni kuwaunga mkono na kuwaokoa washiriki wenzako wa kanisa, basi kitendo
hicho, badala ya kupoteza muda, ndicho kilicho cha muhimu machoni mwa Mungu.)
C.
Rafiki, je, wewe ni sehemu ya watu wanaofanya ushirika
wa mara kwa mara? Kama wewe si sehemu ya kundi hilo, basi unakosa kipengele cha
muhimu sana cha kuwa Mkristo. Kwa nini usitubu juu ya jambo hili na kuungana na
kundi linaloshikilia imani na utii?
VI. Juma lijalo: Injili ya Milele.
No comments:
Post a Comment