Somo La 11 | Kujiandaa kwa Ajili ya Mavuno [Lesson]


(Yakobo 5:7-12)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Katika somo letu juma lililopita Yakobo aliwaambia matajiri kuwa kipindi kigumu kinawajia. Mojawapo ya sababu ni kwamba hawakutenda haki kwa watendakazi (watumishi) wao. Juma hili anaielezea hadhira tofauti, washiriki wa kanisa. Hata hivyo, ujumbe wa juma lililopita na ujumbe wa juma hili unaonekana kufanana. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza!
I.                   Uvumilivu
A.                Soma Yakobo 5:7. Anasema, “Kwa hiyo ndugu, vumilieni.” Ikiwa Yakobo anaendeleza mada ya juma lililopita, je, wanatakiwa kuvumilia jambo gani? (Juma lililopita Yakobo aliwaambia matajiri, “……mashaka yenu yanayowajia.” (Yakobo 5:1). Kwa dhahiri washiriki wa kanisa ndio wafanyakazi waliopunjwa (walionyanyaswa). Wanatakiwa kuvumilia kwa sababu uthibitisho unakaribia. Mungu atakabiliana na matajiri.)
1.                  Jambo gani litawathibitisha washiriki wa kanisa? (Ujio wa Bwana – ambao upo karibu.)
2.                  Hili ni tatizo, si ndio? Ikiwa Yakobo aliandika kwamba wanapaswa kujiandaa kwa ujio wa Mara ya Pili, huo ulikuwa ujumbe mzuri. Lakini, anasema kuwa matajiri watapata haki yao na uthibitisho wa waathirika wao ikiwa wataonyesha uvumilivu. Tatizo ni kwamba wote walifariki kabla Yesu hajarejea. Je, Yakobo ni nabii wa uongo? (Ningedhani kwamba Mungu angenitendea haki mapema.)
3.                  Soma Yakobo 4:14. Yakobo anasema kuwa maisha ni kama mvuke ambao huonekana na kutoweka haraka. Tunapofariki, matatizo ya aina hii hufikia hatima yake. Je, hicho ndicho alichokimaanisha Yakobo?
B.                 Soma tena Yakobo 5:7 kisha uongezee kwa kusoma Yakobo 5:8. Je, hii inaonekana kana kwamba Yakobo anazungumzia mauti? (Hapana! Wakulima wanaona mvua za kwanza na za mwisho. Mvua hizo hutokea mara moja kwa mwaka. Yakobo pia anasema kuwa “kuja kwake Bwana kunakaribia.”)
1.                  Ikiwa muda wa uthibitisho ni tukio linalotokea mara moja kwa mwaka, na Yakobo anasema kuwa muda “umekaribia,” je, unaelezeaje inapoonekana kwamba sasa ni miaka 2,000 iliyopita?
2.                  Inaonekana wanafunzi wote walidhani kuwa ujio wa Yesu ulikuwa umekaribia. Ili kuelezea jambo hili nimewasikia watu wakisema jambo kama hili: “Basi, ikiwa wanafunzi walidhani kuwa ujio wa Yesu Mara ya Pili ulikuwa ni miaka 2,000 ijayo, wasingehamasika kushiriki injili na watu.” Je, unayachukuliaje maelezo hayo?

a.                   Watu wangapi wanadanganya ili kukuhamasisha kununua kitu fulani, kwa sababu ukweli hautakuwa ukihamasisha sana?
C.                 Soma Matendo 1:6-8. Je, ni jambo gani la mwisho alilolisema Bwana wetu kabla hajarejea mbinguni? (Aliwaambia wanafunzi kuwa Mungu ametenga nyakati kwa ajili ya matukio yajayo na sio kazi yetu kuzifahamu nyakati hizo.)
1.                  Je, jambo hili linamweka Yakobo mahali pabaya zaidi? Anasema kuwa ujio wa Mara ya Pili umekaribia wakati hafahamu chochote – na ameambiwa na Yesu kwamba Mungu pekee ndiye anayefahamu muda wa ujio wa Mara ya Pili?
2.                  Haya ni maswali magumu, maswali unayoweza kuyatarajia kutoka kwa mwanasheria anapouliza ili kufanya uchunguzi. Lakini, maswali haya ni ya haki kabisa. Hebu tufanye uchunguzi zaidi, uchunguzi ambao hauhusishi kauli kwamba Yesu hakuwa akieleza ukweli.
II.                Kuvuka
A.                Soma Yohana 5:24-25. Yakobo na Yesu wanazungumzia tukio moja – ujio wa Yesu Mara ya Pili. Utabaini kwamba Yesu anasema kuwa kipindi cha ujio wa Mara ya Pili “kimekuja na sasa kipo.” Yesu anawezaje kusema kuwa ujio wa Mara ya Pili “sasa upo” wakati ilikuwa maelfu ya miaka ijayo?
1.                  Sehemu ya muhimu kabisa ya ujio wa Mara ya Pili ni ipi? (Kifo kimeshindwa. Tunapewa uzima wa milele. Kutokana na namna ambayo Yesu aliweka jambo hili, nadhani anazungumzia umuhimu wa tukio (ambalo ni kukishinda kifo) badala ya kujikita kwenye muda wa ujio wa Mara ya Pili.)
2.                  Ikiwa unadhani kuwa ninaweza kuwa sahihi kwenye jambo hili, je, kuna ushahidi gani kwamba kifo kilishindwa wakati Yesu bado akiwapo hapa mara ya kwanza? (Angalia tena Yohana 5:24. Yesu aliwaambia wale waliokuwa wakimsikiliza kuwa sasa hivi wanaweza kupita kutoka mautini kuingia uzimani.)
3.                  Je, unadhani kuwa unaweza kuingia kwenye uzima wa milele sasa hivi? (Soma Yohana 5:26. Yesu anao uwezo wa kutupatia uzima wa milele. Sehemu ya msingi ya ujio wa Mara ya Pili – kukishinda kifo – inaweza kutokea sasa hivi.)
B.                 Soma Yakobo 5:8-9. Yakobo anaweza kuwa anazungumzia jambo gani hapa ambalo ni la kweli? (Mwamuzi wetu “anasimama mbele ya mlango” mara zote. Yu radhi kufungua mlango wa uzima wa milele sasa hivi. Tunapoyatoa maisha yetu kwa Yesu, anafungua mlango unaoturuhusu kuvuka kupita kutoka mautini kuingia kwenye uzima wa milele. Umuhimu wa ujio wa Mara ya Pili unapatikana kwetu sasa hivi. Tukilitambua hilo, itatusaidia kuwa wavumilivu na huku kusubiri kwa kitambo kirefu.)
III.             Mifano ya Uvumilivu

A.                Soma Yakobo 5:10-11. Kwa nini manabii ni mfano mzuri wa watu ambao Yakobo anaandika kuwahusu? (Manabii walihitaji uvumilivu kwa sababu waliteseka sana kutokana na mateso ya wananchi wenzao. Wale waliodai kumjua Mungu ndio waliokuwa tatizo kubwa. Utakumbuka kwamba Yakobo anawaandikia waumini waliokimbia mateso kutoka kwa Wayahudi wenzao. Kwa muktadha huo wao ni kama manabii.)
1.                  Kwa nini Ayubu ni mfano mzuri sana kwa watu hawa? (Ayubu sio tu kwamba alipewa wakati mgumu na marafiki zake, bali pia alipoteza utajiri wake wa hapa duniani. Yumkini hiyo ndio hali waliyo nayo wale ambao Yakobo anawaandikia.)
B.                 Angalia tena Yakobo 5:11. Yakobo anasema hatimaye angalia kile ambacho Mungu alimtendea Ayubu. Kile ambacho Mungu alimtendea Ayubu kilitokea wakati wa uhai wake. Je, wale ambao Yakobo alikuwa akiwaandikia walitakiwa kuelewaje huu ushauri wa “iweni wavumilivu?”
1.                  Je, huwa huchukii unapoona watu wanatafakari kinadharia zaidi kiasi cha kuonekana kutotumia akili ya kawaida tu? Tulianza mjadala wetu (Yakobo 5:7) kwa Yakobo kuwaambia watu walionyanyaswa na matajiri wawe wavumilivu “hata kuja kwake Bwana.” Kisha nilielezea kipengele cha kiroho cha kuja kwa Bwana, kupita kutoka mautini kuingia uzimani. Vipi kuhusu suala la adhabu dhidi ya matajiri? Ikiwa tutaangalia mtazamo wa akili ya kawaida, je, Yakobo anawapotosha watu anaowaandikia?
2.                  Soma Mathayo 24:1-3, kisha pitia kwa haraka haraka sura nzima ya Mathayo 24. Je, Yesu anaelezea jambo gani ambalo ni jibu kwa swali la wanafunzi? (anaelezea anguko la Yerusalemu na ujio wake wa Mara ya Pili.)
a.                   Kwa nini ni vizuri kwa Yesu kuchanganya hayo mambo mawili? (Angalia tena swali walilouliza wanafunzi. Waliuliza kuhusu matukio yote mawili. Wao walichukulia kwamba matukio hayo mawili lilikuwa ni tukio moja.)
b.                  Je, mjadala huu unatusaidia kwenye kipengele cha adhabu ya kivitendo ambayo Yakobo aliiandika? (Ndiyo. Anguko la Yerusalemu lilikuwa limekaribia sana. Matajiri waliokuwa wamewanyanyasa masikini walikuwa wanakaribia kupata mateso makubwa kutokana na adhabu (malipo) kali. Kitendo cha kuwapunja masikini ili kupata fedha nyingi zaidi sasa hakitawasaidia.)
C.                 Hebu tuangalie maswali magumu ya uchunguzi niliyoyauliza. Je, Yakobo anawapotosha watu anaowaandikia? (Walikuwa wanakaribia kabisa kuamini kwamba ujio wa Mara ya Pili ulikuwa unakaribia. Lakini, umuhimu wa ujumbe, kuingia kwenye uzima wa milele na adhabu (malipo) inayotokana na kudanganywa, kwa hakika hayo yalikuwa yamekaribia.)
IV.             Kuapa
A.                Soma Yakobo 5:12. Je, Yakobo ameingia kwenye mada nyingine kabisa isiyohusiana na ile ya awali? (Soma Mathayo 5:34-35. Utagundua kwamba kuapa kwa jina la Yerusalemu ilikuwa ni mojawapo ya msingi wa kudai kuwa ulikuwa ukisema ukweli.)

1.                  Mtu alikua anaaminika kwa kiasi gani kwa kuapa kwa jina la Yerusalemu? (Nadhani ushauri huu unahusiana na mjadala wetu wa awali. Yakobo anawaambia wasomaji wake wasitegemee fedha, wamtegemee Mungu kwa sababu atafanya mambo yote kuwa vizuri. Sasa anasema kuwa linapokuja suala la kutenda jambo sahihi, usishauri kutegemea kitu chochote kile ambacho Mungu amekiumba (amekifanya), badala yake wewe fanya tu kilicho sahihi ukiwa kama mwana (mtoto) wa Mungu. Kuapa kwa jina la Yerusalemu kutathibitika kuwa wazo baya muda mfupi tu ujao.)
B.                 Rafiki, je, ungependa kupita kutoka mautini kuingia uzimani sasa hivi? Yakobo anashauri kuwa hili ni suluhisho la matatizo mengi maishani. Kwa nini usitubu, usikiri na kudai ahadi ya Yesu ya kuingia kwenye uzima wa milele leo?

V.                Juma lijalo: Maombi, Uponyaji na Urejeshaji.

No comments:

Post a Comment