Somo La 10 | Lieni, Mkapige Yowe! [Lesson]

Somo la 10: Lieni, Mkapige Yowe!
(Yakobo 5:1-6)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Kitabu bora kimauzo kilichoorodheshwa kwenye New York Times na kijulikanacho kwa jina la “Drive” kinaelezea jambo linalowafanya wafanyakazi (waajiriwa) waridhike na kazi yao. Kitabu hicho kinabainisha kwamba kuwalipa tu waajiriwa fedha nyingi zaidi sio njia ya kumfanya mtu aridhike na kazi yake ya ajira. Kimsingi, fedha ni za muhimu, lakini umuhimu wake unafikia kwenye ukomo fulani. Pale mwajiriwa anapoweza kuishi kwa raha mustarehe, basi jambo la muhimu zaidi ni uwezo wa kuwa wabunifu, kuamini kwamba unafanya jambo linalostahili, na kuwa na uhuru wa kufanya maamuzi kazini. Je, jambo hili pia ni la kweli kwa viumbe wote? Fedha sio chemchemi ya furaha? Yakobo anaonekana kuwabagua matajiri. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza kutoka kwa Yakobo kuhusu utajiri na furaha!
I.                   Utajiri Usio na Maana
A.                Je, ungependa kuwa tajiri au masikini? Nadhani takribani kila mtu atajibu kwamba anapenda kuwa “tajiri.” Hebu tusome Yakobo 5:1. Je, Yakobo angejibuje swali nililouliza? (Inaonekana kwamba angekubaliana nawe – utajiri ni kitu bora. Yakobo anasema kuwa taabu inawajia matajiri, na sio kwamba wanayo taabu hivi sasa. Hii inanikumbusha kauli ya Yakobo aliyoisema hapo awali (Yakobo 1:10-11) anapowaambia matajiri kuwa, “mtakufa [mtanyauka] hivi karibuni.” Wote wanachukulia kwamba matajiri wanaendelea vizuri kwa sasa, lakini Yakobo anasema kuwa mambo mabaya yanakuja.)
B.                 Soma Yakobo 5:2-3. Je, taabu [mateso] itakayowakabili matajiri ni ipi hiyo? (Kwa mshangao mkubwa, Yakobo anasema kuwa taabu watakayoipata matajiri ni kwamba wataupoteza utajiri wao! Utajiri wa matajiri utaharibiwa [utaoza]. Yakobo anaonekana kukubaliana na ukweli kwamba kuwa na mali [utajiri] ni jambo la baraka, kwa sababu unaponyang’anywa utajiri kinachofuata ni taabu.)
1.                  Kitabu kingine bora kabisa kimauzo cha New York Times kinachoitwa, “Nudge,” kinazungumzia jinsi ya kupangilia chaguzi. Kitabu hicho kinatoa mfano mzuri sana kuhusu uchaguzi. Chukulia kwamba mwajiri wako amekwambia kuwa mwaka ujao (2015) unaweza kuchagua kuwa na siku 30 za ziada kwenye likizo yako, au kulipwa Dola 10,000 zaidi kwenye mshahara wako. Unaamua kuchukua Dola 10,000, ingawa ungependelea pia kuchukua siku 30 za ziada. Ikiwa mwaka unaofuatia (2016) mwajiri wako ataamua kubadilisha, na badala yake kukupatia siku 30 za ziada, najua sasa hutafurahia jambo hilo – hata kama hukuwa na upendeleo mkubwa zaidi kati ya hizi chaguzi mbili. Kitabu hicho kinataarifu kuwa watu wanajisikia kupoteza kitu wanachokimiliki kwa sasa mara mbili zaidi kuliko kile ambacho hawajawahi kuwa nacho. Je, hilo linatufundisha nini kuhusu utabiri wa Yakobo kwamba matajiri watapoteza fedha zao? (Kwa hakika itasababisha kulia na kupiga yowe.)

C.                 Angalia tena Yakobo 5:3. Kwa nini “kutu” ya dhahabu na fedha za matajiri “itawashuhudia” dhidi yao? (Tuhuma inaonekana kuwa ni kwamba hawakutumia fedha zao kwa malengo mazuri. “Kutu” inaashiria kutokuwa na matumizi.)
1.                  Yakobo anazungumzia nini anaposema kuwa wamehodhi utajiri katika “siku za mwisho?” Hadhira yake haikuuona ujio wa Yesu Mara ya Pili. Unadhani Yakobo alikuwa anamaanisha nini? (Maoni ya watu kadhaa niliyoyapitia hawakubaliani. Inaweza kuwa ni kauli ya kiunabii kuwahusu matajiri kabla tu ya ujio wa Yesu Mara ya Pili, au yawezekana ilikuwa ni kauli inayohusu uangamivu wa taifa la Kiyahudi katika kipindi kifupi kijacho. Kura yangu inaangukia kwenye tafsiri ya pili.)
2.                  Tuchukulie kwamba niko sahihi, kwa nini utajiri “ushuhudie” dhidi ya matajiri na “kula miili yao kama moto” kwa sababu ya uangamivu wa Yerusalemu uliofanywa na Warumi? (Matajiri walikusanya fedha ili kujipatia ulinzi, pamoja na hayo fedha hazikuweza kuwalinda dhidi ya Warumi. Kwa hiyo, ilishuhudia kwamba waliweka matumaini yao kwenye kitu kisicho sahihi.)
3.                  Je, unaweza kuanza kuona sababu ya Yakobo kutabiri kwa usahihi taabu inayowajia matajiri? Kauli zake hazitokani na ubaguzi wake binafsi.
4.                  Unadhani matajiri walipaswa kuzitumiaje fedha zao?
II.                Uaminifu
A.                Soma Yakobo 5:4. Kwa wale wanaofuatilia masomo yangu wanafahamu kuhusu Kumbukumbu la Torati 28 inayosema kuwa kumfuata Mungu hutupatia utajiri, na kutokumtii Mungu hutupatia umaskini. Mara nyingine huwa tunaongezea Waebrania 11 kwenye suala hii kwa sababu inasema kuwa maisha ya hapa duniani hayatabiriki kwa walio waaminifu, wengine wanafurahia mafanikio na wengine wanateseka. Kwa hiyo, mada ya Yakobo inayosema kwamba kuwa na utajiri inamaanisha kuwa tabia yako ina kasoro inapaswa kulinganishwa na Kumbukumbu la Torati 28 na Waebrania 11. Sababu ya Yakobo kuutuhumu utajiri hapa ni ipi? (Tajiri mmiliki wa shamba hakuwalipa watumishi wake ujira wao.)
1.                  Je, rejea ya “vilio vyao vimeingia masikioni mwa Bwana” inamaanisha nini? (Watumishi hawa wanamwamini Mungu na wamemwomba Mungu awatendee haki. Hii inatuambia kuwa matajiri wanaoelezewa hapa wamewadhulumu waajiriwa wao.)
B.                 Angalia tena Yakobo 5:4, unadhani tuhuma ya Yakobo inajumuisha kulipa ujira mdogo, na sio tu kutokulipa ujira kabisa?
1.                  Ikiwa umejibu kuwa, “ndiyo,” je, dhambi ina udogo gani?

2.                  AFL-CIO (a collection of American labor unions) ina suala linaloitwa “Executive Pay Watch.” Inaorodhesha kipato cha mameneja wa makampuni makubwa. Kwa kuwa AFL-CIO haiwawakilishi mameneja hawa, haijisifu juu ya kile ilichowafanyia. Badala yake, inavutia tamaa ya wafanyakazi inaowawakilisha. Nakumbuka mshiriki wa kanisa aliyekuwa akilalamika kuhusu tofauti ya kipato kati ya mumewe (ambaye alikuwa mhandisi mahiri) na meneja mkuu wa kampuni yake. Je, hicho ndicho anachokilalamikia Yakobo – kwamba wamiliki na mameneja wananufaika zaidi kuliko wafanyakazi?
3.                  Hebu tumwangalie Henry Ford. Henry Ford alikuwa mvumbuzi wa kwanza wa magari. Alitengeneza magari ambayo watu wa kawaida walimudu kuyanunua. Je, mtu aliyekuwa akifanya kazi ya kuunganisha magari alistahili ujira gani? Tuchukulie kwamba kila gari lililouzwa lilizalisha faida ya Dola 50, na kwamba watu 50 walihusika kutengeneza kila gari, na kwamba watu hamsini walitengeneza magari hamsini kwa mwaka. Hiyo maana yake ni kwamba kiwango cha juu alichostahili kulipwa kila mtu kati ya wale hamsini kilikuwa ni Dola 50 kwa mwaka, je, ni sawa?
a.                   Je, itakuwa haki kulipa faida yote kwa wafanyakazi, na isilipwe faida yoyote kwa Henry Ford?
b.                  Je, thamani ya mtu aliyegundua gari, aliyegundua njia za uzalishaji, na kujenga kiwanda ni ipi? (Tuchukulie mgawanyo wa asilimia 50 ya faida kati ya Henry na wafanyakazi ni kitendo cha haki. Sasa mfanyakazi mmoja analipwa Dola 25 kwa mwaka. Ikiwa unakubaliana kwamba mgawanyo wa asilimia 50 ni haki kwa mtu aliyegundua gari, kujenga kiwanda na kuzalisha ajira, unaweza kuona kwamba Henry atakuwa anaingiza kipato kikubwa zaidi kuliko mfanyakazi mmoja mmoja.)
(1)               Vipi ikiwa tutamweka kando Henry na tuseme kwamba wewe ndiye uliyegundua kitu fulani, ukagundua njia bora ya kukitengeneza, na ukamiliki kiwanda na mashine za kutengeneza kitu hicho: je, utakubali kugawanya asilimia 50 ya faida na mtu aliyefanya kazi ya uunganishaji ili kutengeneza kitu hicho?
(2)               Je, kuwalipa wafanyakazi ujira mdogo kuliko mmiliki ndilo tatizo la dhambi lililobainishwa na Yakobo? (Mjadala huu unaashiria kwamba kitendo hicho sio dhambi.)
C.                 Soma Yakobo 5:5. “Mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo.” Kauli hii inafurahisha sana. Je, kauli hiyo inamaanisha nini kwa ng’ombe? (Tunataka ng’ombe anenepe siku ya machinjo.)
1.                  Ikiwa hilo ni sahihi, je, kauli hiyo inamaanisha nini kwa wanadamu? (Kwamba kwa kuwa kwao matajiri kumewafanya kuwa walengwa taifa lao lilipoangamizwa. Taswira iliyopo ni kwamba hawa matajiri wamefanya chaguzi mbaya. Wamewadanganya na kuwatenga wafanyakazi wao, wametumia fedha za watu wengine kufanya mambo yao wenyewe. Hii iliwafanya wawe walengwa taifa linapoanza kuporomoka.)

2.                  Mataifa ya Magharibi yanayoongoza kwa ustawi yana mzigo mkubwa sana wa madeni. Hii inafanya uwezekano wa anguko la kiuchumi kutokea uwe mkubwa. Ninawafahamu watu wanaohifadhi chakula endapo maafa yatatokea. Hata hivyo, pia wanatunza bunduki kwa ajili ya kulinda vyakula vyao dhidi ya watu watakaokuwa na njaa kwa sababu hawakujiandaa na maafa. Unalichukuliaje jambo hili? Je, hii ni sawa na tajiri aliyehodhi utajiri na taifa la Kiyahudi likaanguka?
D.                Soma Yakobo 5:6. Je, ni sahihi kuwahukumu na kuwaua watu wasio na hatia wanaokupinga? (Hapana. Yakobo anatuambia kuwa hivi ni vitendo vya kikatili. Kwa dhahiri si sahihi kuwahukumu na kuwaua watu wasio na hatia. Lakini, ikiwa unawaua watu wasio na hatia ambao hata hawakupingi, je, unaweza kuwa na kisingizio gani? Hakuna kisingizio chochote. Matajiri hawa waliwaua watu wasio na hatia kwa kuwa walikuwa na uwezo wa kufanya hivyo.)
E.                 Rafiki, je, ujumbe wa Yakobo kuhusu utajiri na furaha ni upi? Yakobo anatuambia kuwa utajiri ni mzuri mno. Kibaya ni kwamba, matumizi mabaya ya utajiri na mamlaka matokeo yake yataonekana wakati wa hukumu. Je, Yakobo anakuelezea wewe? Kama hivvyo ndivyo, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu aongoze matumizi yako katika utajiri na mamlaka yako?

III.             Juma lijalo: Kujiandaa kwa Ajili ya Mavuno.

No comments:

Post a Comment