Somo la 7: Kuutawala Ulimi | @BababaSda


(Yakobo 3:1 - 12)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Hapo kabla Yakobo alituasa tuwe wepesi wa kusikia bali si wepesi wa kusema (Yakobo 1:19), kuuzuia ulimi wetu kwa hatamu (1:26) na kwamba maneno yetu yatatumika katika hukumu (Yakobo 2:12). Hii inaakisi kauli ya Yesu katika Mathayo 12:37 kwamba kwa maneno yetu tutahesabiwa haki au kuhukumiwa. Kwa dhahiri, ulimi wetu ni sehemu ya muhimu sana katika kuishi maisha kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi kuhusu kile inachotufundisha juu ya maneno yetu!
I.                   Walimu
A.                Soma Yakobo 3:1. Je, sababu gani ya kawaida sana unayoisikia kuhusu baadhi ya watu kuacha kabisa kwenda kanisani? (Kudhihakiwa na mtu. Mtu fulani aliamua “kuwafundisha” jinsi ya namna ya kuishi.)
1.                  Yakobo anawapa walimu onyo gani? (Watapata hukumu kubwa zaidi.)
2.                  Mafundisho yanahusikaje na ulimi (Walimu wanatumia sana ulimi!)
3.                  Yakobo anamaanisha nini anaposema, “msiwe waalimu wengi.” Unadhani anamaanisha nini asemapo kuwa “msiwe?” (Usifundishe kwa kujitakia mwenyewe. Hakikisha kuwa umeitwa (wito) kufundisha. Kufundisha ni karama ya roho. Warumi 12:6-7.)
B.                 Angalia tena Yakobo 3:1 na kauli ya Yakobo kuhusu kupata hukumu “kubwa zaidi.” Ikiwa tunaokolewa kwa njia ya neema, na sio kwa kuishika sheria, je, Yakobo anazungumzia jambo gani? Je, anamaanisha kuwa walimu wasiookolewa wanapata hukumu kubwa zaidi?
1.                  Je, inawezekana kwamba anazungumzia kuhusu kuhukumiwa na wanadamu badala ya kuhukumiwa na Mungu? (Kwangu mimi hiyo inaleta mantiki. Mke wangu alikuwa akikosa furaha pale mtu alipokosoa tena kwa ubaya kabisa, mojawapo ya mahubiri yangu. Nilikuwa nikijitolea muda wangu kuhubiri, alifahamu jinsi nilivyotia bidii kuandaa hubiri, na alidhani kwamba ukosoaji haukuwa jambo la haki. Nilichokuwa nikikiwaza ni kwamba ikiwa nilikuwa ninawasilisha mawazo yangu mbele ya watu wengine, basi watu hao walikuwa na haki ya kuyahukumu mawazo hayo.)
C.                 Soma 1 Wakorintho 3:10. Paulo anamaanisha nini anapojiita “mkuu wa wajenzi?” (Anarejea fundisho lake.)
D.                Soma 1 Wakorintho 3:11-13. Ni watu gani hawa wajengao kwa kutumia dhahabu, majani au chochote kile? (Waalimu. Msingi wa mafundisho yote ya Kikristo ni Yesu. Hata hivyo, walimu wanatofautiana sana katika ubora wa mafundisho yao. Ubora wa mafundisho utajaribiwa kwa moto.)

E.                 Soma 1 Wakorintho 3:14-15. Hebu tuangalie hii rejea ya “moto.” Je, inamaanisha nini kwa kazi ya mwalimu kulambwa na “moto?” Je, hii ndio hukumu ya mwisho ambayo Yakobo anaizungumzia? (Kwa hakika hiyo ni hukumu, lakini nadhani ni hukumu juu ya fundisho kama lilivyotumiwa katika maisha ya wanafunzi. Matatizo yanapokuja, bila kujali kama mwalimu anajenga kwa kutumia dhahabu au majani italeta tofauti kubwa katika maisha ya mwanafunzi.)
1.                  Nini kinatokea kwa mwalimu “anayejenga kwa kutumia majani?” (Anatoroka! Wanafunzi wake wanaweza wasiweze kutoroka, lakini mwalimu anatoroka.)
a.                   Je, hilo linaendanaje na kauli ya Yakobo kuhusu “kupata hukumu kubwa zaidi?” (Kwa dhahiri inaonyesha kuwa ubora wa ufundishaji una athari kubwa kwa wanafunzi, kwa hiyo hukumu ni “kubwa zaidi” kwa maana kwamba ina athari kubwa. Hata hivyo, Paulo anatuambia kuwa mwalimu mbaya (mwalimu wa ovyo) anaweza kustahimili wakati wanafunzi wake hawawezi.)
(1)               Wanafunzi wanajifunza nini katika jambo hili? (Kumjaribu mwalimu!)
F.                  Soma Yakobo 3:2. Je, Yakobo anatuambia kuwa walimu ni wakamilifu? (Hapana. Anasema (akiwemo na yeye pia) kuwa “sisi sote tunajikwaa.” Tunapowajaribu walimu wetu, tunatakiwa kulizingatia jambo hili. Tusitarajie kwamba walimu watakuwa wakamilifu.)
1.                  Kuna ujumbe gani kuhusu kufundisha, kujikwaa na kuhukumu? (Waalimu watajikwaa “kwa namna nyingi.” Tunapojikwaa, tunaweza kutarajia “kupata hukumu kubwa zaidi.” Sote tunafahamu kuwa jambo hili ni kweli.)
II.                Ulimi
A.                Soma Yakobo 3:3-4. Yakobo anazungumza jambo gumu kulielewa: ulimi wako ni sawa na “lijamu” au “usukani.” Je, ni kwa jinsi gani ulimi wako unafanana na usukani au lijamu? (Hitimisho lenye mantiki ni kwamba kile tunachokisema kinaathiri jinsi tunavyofikiri. Ulimi wetu unaamsha mwili wetu.)
1.                  Soma Yakobo 1:15. Tulijadili jambo hili kwa kina hapo kabla. Yakobo anasema kuwa matendo maovu yanatokana na fikra ovu, sio mazungumzo maovu. Je, Yakobo amejichanganya? (Yakobo yuko sahihi kusema kwamba dhambi inaanzia kwenye mawazo. Lakini, inaonekana kwamba mawazo yetu yanayasikiliza maneno yetu, na yanaathiriwa na kile tunachokisema. Ni jambo lenye pande mbili - tunachokifikiria kina ushawishi kwenye kile tunachokisema, na kile tunachokisema kina athari kwenye kile tunachokifikiri.)
2.                  Je, umewahi kumsikia mtu akisema kwamba ikiwa unataka kuwa na siku njema, basi kuwa mwema kwa watu wengine, ongea mambo mazuri kwa watu wengine? (Ninaamini kwamba maneno yetu yana athari kwenye fikra zetu, kama vile ambavyo fikra zetu zilivyo na athari kwenye maneno yetu. Inawezekana kwamba tunapotumia maneno kwenye jambo fulani tunayafanya mawazo yetu juu ya jambo hilo yawe thabiti.)
B.                 Soma Yakobo 3:5. Hii inaonekana kutofautiana na kauli ya Yakobo kuhusu lijamu na usukani. Unadhani hii inamaanisha nini kuuhusu ulimi? (Maneno yanaweza kusababisha matatizo makubwa. “Cheche” ya neno “huyaunguza” maisha yako.)
1.                  Je, umewahi kupitia uzoefu huu?
C.                 Soma Yakobo 3:6. Yakobo anarudia baadhi ya yale aliyoyasema: ulimi unaathiri mwili mzima, na ulimi unaathiri uhusiano. Je, Yakobo anaongezea dhana gani nyingine? (Nadhani anaongezea kwamba athari ya ulimi kwa mtu sio ya muda mfupi tu, badala yake inaweza kusababisha mustakabali wa maisha ya mtu “ukawaka moto.”)
D.                Soma Yakobo 3:7-8. Je, lengo la kutuonya kuhusu ulimi ni lipi, ikiwa hakuna tunachoweza kukifanya kuuhusu? (Kwa kuwa Yakobo ametuonya juu ya hatari ya kutisha ya ndimi zetu, nadhani wazo lake hapa ni kupendekeza kwamba kila mara tutathmini kile tunachokisema.)
III.             Ulimi Wenye Chumvi.
A.                Soma Yakobo 3:9-10. Muda mfupi tu uliopita Yakobo ametuambia kuwa ulimi wetu hauwezi kufugwa, na huu ni uthibitisho wake, je, ni sawa?
1.                  Wangapi kati yenu (hakuna haja ya kunyoosha mikono) wanaenenda kwa mujibu wa mafungu haya? (Mara kwa mara huwa “siwalaani” watu (huwa ninasikitishwa sana na madereva wenzangu), lakini ninafahamu si kila ninachokisema ni jambo ambalo ningependa kulirudia katika darasa langu la kujifunza Biblia.)
B.                 Soma Yakobo 3:11-12. Ikiwa wewe, kama ilivyo kwangu, unakiri kwamba si mara zote ndimi zetu hutoa maji matamu, je, tumeangamia kwa hukumu? (Katika Yakobo 3:8 anasema kwamba kutoa maji matamu (kuufuga ulimi) si jambo linalowezekana kwa mwanadamu. Huenda kuna mwanya wa kisheria hapa. Yakobo anasema “chemchemi ya chumvi” haiwezi kutoa maji matamu, hasemi kwamba chemchemi ya maji matamu haiwezi kutoa chumvi kila mara.)
1.                  Tuhitimisheje? Tufanyeje, hususan pale ambapo huutaki mwanya wangu wa kisheria? (Mambo mawili. Kwanza, kisichowezekana kwa wanadamu kinawezekana kwa Mungu. Tunatakiwa kumwomba Roho Mtakatifu kuyaongoza maneno yetu. Pili, nadhani Yakobo anajaribu kututia moyo kuwa makini na maneno yetu na kutambua kwamba yanaakisi asili yetu.)
C.                 Soma Yohana 15:5. Ninahudhuria kwenye kikundi kidogo cha kujifunza Biblia kila juma ambapo mimi sio mratibu wa kikundi hicho. Tulikuwa tunajadili baadhi ya kauli ngumu zaidi za Yakobo, kama vile Yakobo 2:24, “mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake, si kwa imani peke yake.” Mmojawapo wa washiriki wa kikundi hicho alielezea maelezo ya mzabibu na matawi katika Yohana 15:5-8 na akasema kwamba ufunuo huu ulimsaidia kuelewa uhusiano uliopo kati ya imani na matendo. Ikiwa “tumefungamanishwa” na Yesu kwa imani, kwa kawaida (kwa asili) tutazaa matendo. Hatutajivunia matendo, bali matendo yatakuwa kielelezo cha “mafungamano.” Una maoni gani kuhusu maelezo haya?

1.                  Angalia tena Yakobo 3:12. Je, hii ni kauli nyingine ya Yakobo kuhusu “mafungamano?” (Nadhani.  Yakobo anakiri kuwa sisi sio wakamilifu na ndimi zetu ni matatizo magumu. Anasema kuwa maneno yetu yanaakisi mafungamano yetu. Ama tunacho chanzo cha maji ya chumvi, au tuna chanzo cha maji matamu. Ama tunafungamanishwa kama matawi kwenye mzabibu au hatufungamanishwi. Tunachokizalisha kinaakisi uhusiano wa maisha yetu.)
D.                Rafiki, je, maneno yako yana ujumbe gani kukuhusu? Ikiwa hupendi matokeo ya hii tathmini yako binafsi, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu sasa hivi aingie maishani mwako na kurekebisha uhusiano wako na Yesu?
IV.             Juma lijalo: Unyenyekevu wa Hekima ya Mbunguni.

No comments:

Post a Comment