(Yakobo
3:13 – 4:10)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, umewahi kusema kuwa, “Mtu yule anahitaji
kurekebisha mtazamo wake?” Je, umewahi kutafakari kwamba mtazamo wako unahitaji
kurekebishwa? Katika somo letu juma hili, Yakobo anatoa mawazo yanayoweza
kutekelezwa kivitendo kuhusu hekima pamoja na mtazamo wetu. Kwa mara nyingine,
anapendekeza baadhi ya mambo yanayoonekana kutoendana na mafungu mengine ya
Biblia. Tutajaribu kufumbua hiyo migongano ya dhahiri. Hebu tuzame kwenye somo
letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu mitazamo na hekima!
I.
Hekima na Ufahamu
A.
Soma Yakobo 3:13. Angalia swali hilo. Unadhani Yakobo
alitarajia nini? Je, watu watanyoosha mikono yao na kusema, “Naam,
anayezungumziwa ni mimi. Mimi nina hekima na uelewa (ufahamu).” (Ninawafahamu watu ambao ninadhani wanaweza
kunyoosha mikono yao. Lakini, ninachokiwaza ni kwamba Yakobo anauliza swali ili
kutufanya tuanze kutafakari: “Ninawezaje kuwa na hekima na ufahamu?” Je, inamaanisha
nini kuwa na hekima na ufahamu?)
B.
Angalia tena Yakobo 3:13, lakini safari hii angalia
jibu la Yakobo juu ya swali hilo. Je, hiki ni kile kile kitarajiwacho kutoka
kwa Yakobo: matendo yetu yanathibitisha imani yetu? (Ndiyo, ni jambo lile lile,
lakini pia linafungua mjadala wa kile kinachomaanishwa kuwa na hekima na
ufahamu.)
C.
Soma Yakobo 3:14-15. Je, wivu na tamaa ya makuu (malengo)
ni mambo mazuri ikiwa hayana “uchungu” na “ubinafsi?” (Wivu na tamaa (malengo)
vinatuhamasisha kuinuka na kutenda jambo fulani. Lakini, unaweza kuvuka
msitari. Uchungu unaoonekana kufanana na mgongano, na kwa Kiyunani tafsiri ya neno
“tamaa” ina chembechembe ya ugomvi ndani yake.)
1.
Kwa nini mtu ajivunie wivu wenye uchungu na tamaa yenye
ubinafsi? (Tunayaona mambo haya nyakati zote. Kimsingi mtu huyu anasema “Nitapambana
hadi kufikia kiwango cha juu kabisa.”)
a.
Yakobo pia anabainisha “kuukana ukweli.” Je, “ukweli”
upi unakanwa? (Ukweli ambao kimsingi ni kwamba tunang’ang’ania wivu wenye
uchungu na ubinafsi kimalengo.)
2.
Hebu subiri kidogo! Yakobo anauita “wivu wenye uchungu
na ubinafsi kimalengo” kuwa ni mambo ya “hekima.” Swali halisi la Yakobo
lilikuwa lipi? (“N’nani aliye na hekina na ufahamu?”)
D.
Soma tena Yakobo 3:13-15. Je, Yakobo analinganisha
mitazamo miwili ya hekima? (Ndiyo. Hekima ya Mungu huzaa maisha bora na matendo
yanayotendwa kwa mtazamo wa unyenyekevu. Hekima ya Shetani huzaa mtazamo wa
wivu wenye uchungu na tamaa yenye ubinafsi ndani yake.)
1.
Kwa nini Yakobo anailinganisha hii mitazamo ya aina
mbili? (Anataka tuchague hekima sahihi, hekima itokayo kwa Mungu.)
E.
Soma Yakobo 3:16. Je, hekima ya Shetani huzaa maisha ya
namna gani? (“Machafuko na kila tendo baya.” Hii inatuhamasisha kuitafuta
hekima ya Mungu.)
F.
Soma Yakobo 3:17. Tuna tatizo la “nini hutokea kwanza?”
Je, mitazamo hii ni matokeo ya hekima itokayo juu (kama ambavyo machafuko na
matendo mabaya yatokanavyo na hekima ya Shetani), au Yakobo anaelezea aina ya
mitazamo tunayotakiwa kuikuza (kuiendeleza) ili kupata hekima itokayo juu
(mbinguni)? (Vipi kuhusu jibu la tatu: Nadhani hili ni jaribio. Unawezaje kuielezea
hekima itokayo juu? Inaonekama kama hivi: Safi, yenye amani, ya dhati, tayari
kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema, ina matunda (matendo) mema, ina
mtazamo wa unyenyekevu na wenye kuwajali wengine.)
G.
Soma Yakobo 3:18. Unadhani kwa nini Yakobo
anawabainisha “wafanyao amani?” “Amani” ni mojawapo tu ya mitazamo inayotokana
na hekima ya Mungu, kwa nini anaitaja? (Nadhani unakubaliana na Yakobo: kuwa na
mtu maishani mwako anayetangaza na kuendeleza amani, badala ya kuendeleza
matatizo, ni jambo la muhimu sana. Amani huzaa mavuno ya haki.)
II.
Wasababishao Matatizo
A.
Soma Yakobo 4:1–2. Angalia swali la Yakobo, “Mapigano
yatoka wapi?” Una maoni gani juu ya jibu lake kwa swali hilo? (Linaonekana kuwa
sahihi. Tunaingia kwenye mapigano kwa sababu tunadhani tunapaswa kuwa na kitu
ambacho hatuna.)
1.
Hebu tuangalie jambo hili kwa kuiangalia hekima ya
Shetani. Jambo gani huwaelekeza watu kwenye hekima ya Shetani? (Mtazamo wa
kwamba wamenyimwa jambo fulani. Hii hutokana na wivu wenye uchungu na tamaa
yenye ubinafsi. Matokeo yake ni tamaa (uchu), ugomvi, mapigano, na mauaji.)
2.
Suluhisho la hili tatizo kubwa ni lipi? (Kumwomba Mungu
vile vitu tunavyovitamani.)
B.
Soma Yakobo 4:3. Hivi punde tu Yakobo amependekeza kwamba
tumwombe Mungu tunapojisikia kwamba tumenyimwa kitu fulani. Sasa anaweka ukomo
kwenye uwezo wetu wa kuomba. Je, unafikiria nini kuhusu ukomo anaouweka Yakobo?
1.
Mambo mangapi kati ya umwombayo Mungu yanahusisha tamaa
yako mwenyewe?
2.
Soma Mathayo 7:9-11. Je, unawapa wanao vipawa (zawadi)
vyema ambavyo vinawafurahisha?
a.
Je, ungependa kumpa mwanao zawadi ambayo haimfurahishi?
(1)
Ikiwa umesema, “Hapana, ninataka mwanangu afurahie
zawadi yangu,” je, Yakobo anazungumzia jambo gani? (Nahisi jambo hili
linahusisha kile kinachomaanishwa na vipawa “vyema” na aina ya furaha
inayomaanishwa na Yakobo.)
C.
Soma Yakobo 4:4-5. Je, Yakobo amerukia mada nyingine?
1.
Ikiwa umesema kuwa, “hapana,” je, hii inajihusishaje na
hekima ya Mungu – hekima inayojikita kwenye mambo yaliyo sahihi? (Sidhani kama
Yakobo amebadili mada. Badala yake, anasema kuwa kinachotupatia raha (furaha)
kinatokana na wale tulio nao kama marafiki. Ikiwa tuna mtazamo wa kidunia, mara
zote tutatamani sana (kuwa na husuda [wivu mkubwa]), tamaa inayosababisha
kutokuwa na furaha, ugomvi na mapigano maishani mwetu. Tusitarajie Mungu azibe
tundu (shimo) lililosababishwa na huu wivu. Endapo Mungu atafanya hivyo, basi
atakuwa anahimiza na kutekeleza lengo lisilo sahihi.)
III.
Tiba
A.
Soma Yakobo 4:6. Tiba ya hekima ya Shetani ni ipi,
hekima ambayo matokeo yake ni wivu na matatizo? (Neema. Mungu anajitolea kumtoa
Roho wake Mtakatifu ili kuibadilisha mioyo yetu. Tunatakiwa kuachana na majivuno
yetu, na kutambua hitaji letu la neema.)
B.
Soma Yakobo 4:7-8. Je. Ungependa kuwa na maisha yenye
amani tele? Je, Yakobo anatoa tiba gani ambayo inapaswa kuchukuliwa hatua
kivitendo? (Mtazamo wa kujitoa kwa Mungu, kumpinga Shetani.)
1.
Yakobo anapotuambia “tuitakase” mikono yetu na “kuisafisha”
mioyo yetu, je, anasisitiza mazingira mazuri ya usafi? (Mikono yetu
inawakilisha kile tunachokitenda, na mioyo yetu inawakilisha kile
tunachokiwaza.)
a.
Je, Yakobo anasisitiza matendo? (Utagundua kwamba
Yakobo anatoa utangulizi wa jambo hili kwa kusema “mkaribieni Mungu” naye Mungu
“atawakaribia ninyi.” Ninalielewa na kulichukulia jambo hilo kuwa ni neema.)
C.
Soma Yakobo 4:9. Je, hii ndio hekima ya Mungu:
kuhuzunika, kuomboleza, kulia kwa huzuni na kusononeka? Mitazamo na matendo hayo
inapaswa kuufanya Ukristo uwe wa kuvutia!
1.
Soma Yohana 15:9-11 na Wagalatia 5:22. Yesu anatuambia
kuwa utii huleta furaha. Paulo anatuambia kuwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu
huleta furaha. Je, Yakobo yuko nje ya mada na amebadili mawazo ghafla? Swali hili
ni la dhati sana kwa sababu nimewasikia watu wanaojiita Wakristo wakitetea
mtazamo wa huzuni na maombolezo. (Angalia muktadha. Yakobo anawashauri wale
wanaotoka gizani. Hawa ni watu wanaohitaji kubadilika kimtazamo na kubadilika
kimatendo. Hivyo, nadhani Yakobo anazungumzia suala la kuwa dhati juu ya dhambi
zetu. Kuhuzunikia na kuomboleza maisha yetu ya dhambi. Mara tunapopeleka hii
dhambi kwa Mungu kwa ajili ya msamaha, basi furaha ni mojawapo ya karama za
Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu.)
D.
Soma Yakobo 4:10. Yakobo anasisitiza juu ya unyenyekevu
wa aina gani? (Angalia huo muktadha tena. Unyenyekevu ni kujitoa kwa ajili ya
mapenzi ya Mungu maishani mwako. Ikiwa tuna huo mtazamo, Mungu “atakuinua
(atakukuza).”)
1.
Je, huu unaonekana kuwa ushauri kuhusu majonzi na
furaha? (Huu ni mfanano halisi. Kuhuzunikia dhambi zako huleta furaha kwa ajili
ya siku zijazo. Kunyenyekeza mapenzi yako mbele za Mungu huleta utukufu katika
siku zijazo.)
E.
Tuchukulie kwamba unawashauri vijana wadogo. Unawezaje kuweka
mbele yao njia zote mbili na kuwahamasisha waifuate njia ya hekima ya Mungu? (Waulize
aina ya maisha wanayotaka kuwa nayo. Je, mara zote watataka kuwa na wivu na
uchungu kwenye mafanikio ya watu wanaowazunguka? Je, wanataka kuwa na
machafuko, ugomvi na mapigano kama sehemu ya kawaida ya maisha? Ikiwa wanapendelea
amani, kuridhika na heshima, basi wanatakiwa kufanya uamuzi wa kuichagua njia
ya Mungu na mitazamo ya Mungu.)
F.
Rafiki, vipi kuhusu wewe? Maisha yako yakoje? Mtazamo wako
ukoje? Angalia tena Yakobo 3:17 na uone kama hekima maishani mwako inafanana na
hii. Kama haifanani, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu abadilishe mitazamo yako
ili akupatie hekima ya Mungu?
IV. Juma lijalo: Mtoa Sheria na Hakimu Mmoja.
No comments:
Post a Comment