Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Mara kadhaa katika matukio ya kanisa, ninakumbuka
baadhi ya mazungumzo yaliyonishangaza. Nakumbuka mara kadhaa nilikuwa
nikizungumza na washiriki wa kanisa ambao sikuwa nikiwafahamu vizuri, na
walinishukuru kwa kuzungumza nao. Nilijiuliza, “kwa nini wananishukuru?” Kwa
sababu walihisi kuna utofauti ya madaraja (hadhi) kati yetu. Kuna wakati fulani
rafiki wangu aliniambia kuwa alishangaa kwa kitendo cha mimi kuwa rafiki wake
kutokana na tofauti ya kazi zetu. Kuna kipindi daktari (tabibu) tuliyekuwa
tunasali naye kanisani kwetu alibaini kuwa sote (yaani mimi na yeye) tulikuwa
tumevaa suti, na akasema kuwa wale ambao hawakuvaa suti walikuwa watu wa daraja
la chini. Nilimwambia kuwa huwa tunavaa suti tuendapo kazini, na hiyo inaweza
kuwa ndio sababu ya msingi kwa kile tukivaacho tuendapo kanisani. Halikuwa
suala la hadhi. Kuna mifano mingine ninayoweza kuikumbuka. Kila mara mtu
anaposema kuwa elimu yangu au kazi yangu inanifanya nionekane mtu wa hadhi ya
juu kuliko watu wengine, huwa ninashangaa au kujisikia vibaya. Yakobo
anazungumzia jambo hili katika somo letu la leo, lakini kile anachokisema
kinanifanya nijisikie vibaya pia. Hebu tuzame kwenye Biblia ili kwa uaminifu
kabisa tujadili masuala ya “madaraja/hadhi za watu!”
I.
Upendeleo
A.
Soma Yakobo 2:1-4. Unafikiriaje, je, wote wanaokuja
kanisani wanastahili kupata mahali pazuri pa kukaa? (Ndiyo, kwa hakika kabisa.)
1.
Je, unaweza kufikiria sababu yoyote ya kuwabagua, kwa
misingi ya utajiri, wageni wanaokuja kanisani kwenu? (Ikiwa ningeweza
kumshawishi mtu tajiri sana kuwa mshiriki wa kanisa, huo unaweza kuwa mbaraka
mkubwa sana kwa kanisa. Mtu masikini sana anaweza asijishughulishe na michango
ya kifedha kanisani.)
2.
Yakobo analiita jambo hili kuwa ni “ubaguzi” na “mawazo
mabovu.” Je, wakati gani ubaguzi una mantiki na wakati gani ubaguzi ni jambo ovu?
(Kuwatendea vibaya maskini ni kitendo kiovu. Kutambua faida ambayo mtu anaweza
kuileta kanisani kwenu ni jambo linaloleta mantiki.)
3.
Hebu tuachane kidogo na huu mjadala wa suala la fedha.
Je, utatia bidii kumshauri mwimbaji mashuhuri au mwalimu mzuri wa Shule ya
Sabato kujiunga na kanisa lako kuliko mtu atakayekalia benchi tu bila kufanya
kazi yoyote? (Hii inaakisi dhana ya kutumia mantiki katika jambo hili.)
B.
Soma Yakobo 2:5. Ikiwa kitendo cha ubaguzi kwa kutumia
kigezo cha utajiri ni kitendo kiovu, je, si kitendo cha ubaguzi Mungu
anapowapendelea maskini dhidi ya matajiri?
1.
Utagundua kwamba Yakobo anauliza swali. Nadhani swali
la Yakobo halihitaji majibu, lakini hebu tulichukulie kama swali halisi
linalohitaji majibu. Je, utalijibuje? (Jibu langu ni “hapana,” Mungu
hakuwachagua maskini kuwa matajiri wa imani. Waangalie mashujaa kadhaa wa Agano
la Kale: Musa, Ibrahimu, Ayubu, Mfalme Daudi, Danieli – hakuna hata mmojawao
aliyekuwa maskini.)
2.
Soma Waebrania 11:32-39. Je, hii inaashiria nini kuhusu
mafanikio, utajiri na imani? (Watu wote hawa walikuwa na imani – ingawa maisha
yao yalibadilika na kuwa tofauti kabisa. Ujumbe uliopo hapa ni kwamba fedha na
mafanikio hapa duniani havihusiani na imani.)
3.
Pitia kwa haraka haraka Kumbukumbu la Torati 28. Kuna
ujumbe gani hapa kuhusu utii na utajiri? (Hii ni sura ya kitabu cha Biblia
ambayo huwa ninairejea mara kwa mara. Inasema kuwa mtii Mungu ili ustawi.
Usimtii Mungu na maisha yako yataharibika kiasi cha kutisha. Kimsingi, inasema
kuwa kutokuwa na utii huleta umaskini.)
4.
Hiyo inamaanisha kuwa tuna ujumbe wa aina tatu
unaotofautiana: Yakobo anasema kuwa
Mungu anawapendelea maskini walio na imani, Waebrania inasema kuwa imani haina
uhusiano na mafanikio ya hapa duniani, na Kumbukumbu la Torati inasema kuwa
utii (imani) huleta utajiri. Je, unalinganishaje huu ujumbe wa aina tatu kutoka
kwenye Biblia?
C.
Soma Mithali 10:15 na Mithali 4:6. Je, mafungu haya
yanasema nini kuhusu utajiri na hekima? (Vinamlinda mtu anayevimiliki.)
1.
Kitabu maarufu kinachojulikana kwa jina la the Bell Curve, kinahusianisha
akili nyingi na elimu kubwa, na elimu kubwa na kipato kikubwa. Ninatambua kuwa
hekima na kuwa na akili nyingi haviko sawa, lakini ninaamini haya mafungu
mawili ya Biblia pamoja na hiki kitabu vinalenga kuthibitisha jambo kuhusu
utajiri – wanalindwa na fedha zao pamoja na akili zao. Unawezaje kuhusianisha
wazo hili na Yakobo 2:5? (Wale wasio na fedha au akili nyingi za kuweza
kuwalinda, wana uwezekano mkubwa wa kumgeukia Mungu ili awalinde. Wale
wanaoweza kuzitegemea fedha na akili ili kutatua matatizo, wana uwezekano mdogo
wa kumgeukia Mungu ili kutatua matatizo.)
D.
Angalia tena Yakobo 2:5. Ikiwa Yakobo anatakiwa
kueleweka kwa namna inayoendana na Waebrania na Kumbukumbu la Torati, je,
itakuwa haki kusema kuwa “wateule” inamaanisha kuwa maskini wana uwezekano
mkubwa wa kumgeukia Mungu kwa imani ili kutatua matatizo?
E.
Soma Yakobo 2:6. Hebu turejee kwenye tatizo halisi –
kumfanya maskini akae sakafuni na kumpa tajiri kiti kizuri. Ikiwa ungetakiwa kufanya
ubaguzi wenye mantiki kwa kutumia kigezo cha kipato, je, ungehitimishaje kuhusu
watu maskini? (Wanao uwezekano mkubwa wa kujawa imani – na hivyo kuwa watu
ambao ungependa kuwa nao kanisani kwako.)
1.
Soma Mathayo 28:19-20 na Ufunuo 3:15-17. Endapo umeikubali
Mathayo 28 kama dhamana maishani mwako, je, unapaswa kumpa tajiri kiti cha aina
gani kanisani? (Viti vizuri, vilivyo karibu, kwa kuwa wanatakiwa kuongolewa na
kuitegemea imani.)
II.
Mpambano wa Madaraja
A.
Soma Yakobo 2:6-7. Ikiwa mtu atakuuliza maswali matatu
ya Yakobo, je, utasema kuwa mtu huyo ameonesha upendeleo kwa maskini? Je, mtu
huyu haonekani kuwabagua matajiri?
1.
Utagundua kwamba maswali ya Yakobo yamejengwa juu ya
madai ya kweli – matajiri wanakunyonya. Endapo jambo hili lisingekuwa la kweli,
je, Yakobo angekuwa na hoja yenye ushawishi mkubwa? (Inawezekana kabisa kuwa
Yakobo alikuwa akiwaandikia watu ambao sasa walikuwa maskini, hivyo yumkini
alikuwa anazungumzia ubaguzi, lakini endapo kile alichokisema kilitokana na
wazo la ubaguzi pekee, sidhani kama angeaminika. Lazima jambo hili linaakisi
muktadha wa kipindi hicho.)
2.
Vipi kuhusu muktadha wako, je, matajiri wanawanyonya
maskini au maskini wanawanyonya matajiri? (Ninaishi katika nchi yenye
demokrasia. Kwa sababu tunao watu maskini wengi kuliko matajiri, matajiri
wanashindwa kwenye kura. Mungu alipokuwa kiongozi wa Israeli, alianzisha kodi ya
asilimia 10 (zaka) kwenye kipato, bila kujali kiwango cha kipato. Mambo ya
Walawi 27:30. Katika eneo ninaloishi, matajiri wanalipa zaidi kwa kuwa wana
kipato kikubwa zaidi, lakini pia wanalipa asilimia kubwa ya kipato chao. Kuna kipindi
matajiri walitozwa kodi iliyofikia kiwango cha asilimia 90 ya kipato. (Hata
hivyo sheria hiyo imeshatanguliwa.) Je, hii inaashiria nini kuhusu unyonyaji
katika utamaduni wa eneo langu?
3.
Ni matumaini yangu kwamba, ngumi hazijazuka
tunapoendelea na huu mjadala wa Biblia! Hebu turejee kwenye wazo halisi la
Yakobo kuhusu ubaguzi. Je, mitazamo yetu kuhusu utajiri inapaswa kutufanya
tuwatendee watu vibaya wanapokuja kanisani? Ikiwa unadhani matajiri wanafanya
mambo yao kwa kutumia mgongo wako au kama unadhani maskini wanafanya mambo kwa
kutumia mgongo wako, je, unapaswa kuwatendeaje wale unaodhani kuwa wanafanya
mambo kwa mgongo wako? (Hatupaswi kumtukana mtu yeyote kwa kumtendea vibaya.)
B.
Angalia tena Yakobo 2:7. Je, jambo hili ni kweli katika
utamaduni wa eneo lako, kwamba maskini wanalikashifu jina la Yesu? (Ikiwa kuna
kinyume cha uhusiano kati ya fedha na kumtegemea Mungu, basi kuna uwezekano
mkubwa kuwa jambo hili ni la kweli.)
1.
Je, tungependa kuwakalisha wapi watu wanaomkashifu
Yesu? (Ikiwa wako dhati kabisa kuja kanisani, kwa hakika tungependa kuwapatia
viti vizuri ili waweze kusikiliza ujumbe wa injili.)
a.
Unadhani Yakobo anaweza asikubaliane na kile
nilichokipendekeza? (Sidhani! Yakobo analaani kitendo cha kuwatukana maskini. Nakubaliana
na jambo hili. Yakobo hasemi jambo lolote kuhusu jinsi tunavyopaswa kuwakalisha
wenye hitaji kubwa la kuongolewa mioyo yao.)
III.
Wavunja Sheria Wanaotawala
A.
Soma Yakobo 2:8. Hebu subiri kidogo! Je, Yakobo anasema
kuwa kanuni inayotawala ni ipi? (Kuwapenda watu wengine kama tunavyojipenda
wenyewe.)
1.
Unawezaje kutumia kanuni hii kwenye mjadala wetu wa
mpambano wa madaraja? (Ubaguzi hauruhusiwi hata kidogo. Ubaguzi hautakiwi dhidi
ya maskini. Ubaguzi hautakiwi dhidi ya matajiri. Ubaguzi hautakiwi kwa watu wa
daraja la kati. Tunamtendea kila mtu kama ambavyo tungependa kutendewa.)
B.
Soma Yakobo 2:9-11. Je, Yakobo anatuambia kuwa kuwapendelea
matajiri ni sawa na kuwaua maskini na kuwapendelea maskini ni sawa na kuwaua
matajiri?
1.
Je, unatoa shukrani kwa kuwa na neema sasa hivi? (Soma
Warumi 3:19-24. Yakobo anasema jambo la muhimu sana, ikiwa utakiuka sehemu
yoyote ile ya sheria basi unakiuka sheria yote. Sheria imeweka mbele yetu lengo
la kuachana na ubaguzi, na kuwatendea watu wengine kwa upendo. Lakini,
tumshukuru Mungu, tunaokolewa kwa neema katika Yesu.)
C.
Soma Yakobo 2:12-13. Je, utahukumiwa kwa sheria? (Si
kwa mujibu wa mafungu tuliyoyasoma katika Warumi, ikiwa utaitegemea haki ya
Yesu.)
1.
Je, ujumbe wa Yakobo ni upi basi? (Wale ambao
hawaokolewi kwa neema watahukumiwa kwa sheria ya Mungu. Je, haileti mantiki
kuishi kwa mujibu wa sheria ya Mungu? Sheria ya Mungu ipo kwa faida yetu, hivyo
inatupatia uhuru kwa wale waliookolewa kwa neema.)
D.
Rafiki, somo hili linahusu kuonesha upendeleo. Je, hili
ni tatizo maishani mwako? Ikiwa umesema kuwa “hapana,” ninatilia shaka neno
lako. Kwa nini usiwe mwaminifu sasa hivi, na kumwomba Roho Mtakatifu akusaidie
kuonesha upendo sawa kwa wale wanaokuzunguka?
IV.
Juma lijalo: Imani Itendayo Kazi.
No comments:
Post a Comment