(Yakobo
1:22-27)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, unapata ushauri mara nyingi kiasi gani?
Inaonekana huwa ninapata ushauri kutoka kwa watu wengine nyakati zote. Huwa
ninapewa ushauri mwingine bila ya mimi kuuomba. Ushauri mwingine huwa ninauomba
na huwa ninauhitaji kweli. Ninapata ushauri mwingi kuhusu mambo mbalimbali maishani.
Siku chache zilizopita, nilikuwa ninajaribu kuunganisha mwanasesere wa gari kwa
ajili ya mjukuu wangu wa kike, gari lililokuwa kubwa kiasi cha yeye kuweza
kuingia ndani na kulikalia. Mtengenezaji alinishauri jinsi ya kuliunganisha,
lakini niliona kwamba baadhi ya ushauri haukuwa mzuri, na ilitokea kwamba
nilikuwa sahihi. Kwa upande mwingine, GPS
ya simu yangu inaponishauri kuhusu uelekeo ninaotakiwa kwenda niendeshapo gari,
huwa ninauchukulia ushauri huo kwa dhati kabisa. Jinsi tunavyoitikia ushauri
huakisi vile tunavyokichukulia chanzo cha ushauri. Hicho ndicho kinachozungumziwa
katika somo letu la Biblia la juma hili. Hebu tuzame mara moja kwenye somo
letu!
I.
Udanganyifu
A.
Soma Yakobo 1:22. Mara kwa mara huwa ninasikia au
kusoma ushauri ambao huwa ninadhani kuwa haufai hata kidogo. Kwa nini Yakobo
anasema kuwa suala la kusikiliza tu ni aina fulani hivi ya udanganyifu?
1.
Kwa kuwa huwa ninajitahidi nisidanganywe, huwa sikubali
ushauri usio na maana. Ujumbe wa Yakobo kwa wasikilizaji ni upi? (Ushauri wake
ni kwamba si kweli kuwa ushauri hauna maana. Yakobo analirejea “neno,” ambalo
linairejea Biblia. Wasikilizaji hawaamini kuwa ushauri hauna maana. Hata hivyo,
wanaenenda kana kwamba ushauri hauna maana kwa sababu hawaufuati.)
a.
Je, kuna udanganyifu gani katika jambo hilo? (Kwa
hakika, wasikilizaji hawa wanajidanganya wenyewe. Wanadai kwamba Biblia
inawapatia ushauri mzuri, lakini wanashindwa kuufuata ushauri huo. Ikiwa
wanashindwa kuufuata ushauri, wanadanganyika wanapodhani kuwa wao ni Wakristo
wazuri.)
(1)
Je, unawafahamu watu kama hao?
B.
Angalia tena Yakobo 1:22. Je, tiba ya udanganyifu huu
ni ipi? (Yakobo anatuambia kutenda kile ambacho Biblia inatuambia tukifanye.)
II.
Kioo
A.
Soma Yakobo 1:23-24. Kwa nini unauangalia uso wako
kwenye kioo? (Ninataka kuhakikisha kuwa mambo yote yako vizuri.)
1.
Unajuaje kama mambo hayako vizuri? (Unafahamu jinsi
unavyotakiwa kuonekana.)
2.
Kwa nini “unaiangalia” sheria? Sheria ndio “jinsi
ambavyo mambo yanatakiwa kuwa” maishani mwako.” Ikiwa utagundua kuwa maisha
yako sivyo jinsi ambavyo yanatakiwa kuwa, unapaswa kubadili mambo fulani –
vinginevyo unajidanganya mwenyewe.)
B.
Tafakari tena Yakobo 1:23-24. Ikiwa mtu atakuambia kuwa
anajiangalia kwenye kioo na papo hapo anasahau jinsi anavyoonekana, je,
utafikiria nini? (Kuna jambo lisilo la kawaida kwa mtu huyo. Kwa ujumla sio tu
kwamba tunapaswa kufahamu jinsi tunavyoonekana (unawezaje kusahau?), lakini pia
tunahitaji kuangalia kama mambo yote yako sawa. Kwa kuwa tunaangalia jambo
lisilo sahihi, tunawezaje kusahau?)
1.
Unaweza kufikiria maelezo mengine kwa mtu anayesahau –
tofauti na kuwepo kwa tatizo fulani la akili/ubongo wa mtu huyo? (Ikiwa
unasahau papo hapo, inaweza kuwa ni kwa sababu hujali kama kuna jambo lisilo
sahihi. Ikiwa hujali jinsi mwonekano wako ulivyo, kwa nini kumbukumbu iwe jambo
la muhimu?)
2.
Je, Yakobo anajaribu kufikisha ujumbe gani? (Ikiwa
tunaiangalia sheria na kuona kuwa maisha yetu sivyo jinsi ambavyo sheria
inapendekeza yawe, lakini hufanyi jambo lolote kuhusu tatizo hilo, hiyo
inaashiria kuwa ama kuna tatizo kwenye ubongo wetu au hatujali.)
a.
Je, kuna maelezo mengine unayoweza kuyatoa? (Hatudhani
kama ushauri ni mzuri. Ikiwa tunadhani Biblia ina ujumbe usiofaa, tunawezaje
kudai kuwa sisi ni Wakristo? Hii inaturejesha kwenye ujumbe halisi wa Yakobo. Ikiwa
tunadhani kuwa Biblia ina ushauri mzuri na hatuufuati, basi tunajidanganya juu
ya sisi kuwa Wakristo.)
b.
Vipi kama tunadhani kuwa Biblia ina ushauri mzuri
baadhi ya nyakati? Kwenye utangulizi, niliandika kuhusu maelekezo ya
kuunganisha mwanasesere wa gari. Nilifuata maelekezo mengi, lakini nilifahamu
kuwa baadhi ya ushauri haukuwa sahihi. Je, mtazamo huo unakubalika kwenye
Biblia? (Mtazamo wangu kuhusu maelekezo ya kuunganisha gari ulikuwa ni kwamba
ninaweza kukubali au kukataa baadhi ya maelekezo. Ikiwa tutauchukulia mtazamo
huo kwenye Biblia, basi sisi ni miungu yetu wenyewe. Tunaabudu mawazo yetu
wenyewe, na tuna kiburi kudhani kwamba tuna ufahamu zaidi ya Muumbaji wetu.)
III.
Uhuru
A.
Soma Yakobo 1:25. Unapata uhuru gani kwa kujiangalia
kwenye kioo? (Nikijiangalia kwenye kioo, na kuona kuwa hakuna kasoro yoyote,
ninapata uhuru unaotokana na kuwa na ujasiri wa jinsi ninavyoonekana. Sina haja
ya kuwa na wasiwasi kwamba kuna kitu kimenasa kwenye meno yangu, au kwamba
sijafunga zipu ya suruali yangu, au kuna uchafu kwenye ukosi (collar) wa shati
langu.)
1.
Yakobo anaandika kuwa sheria inatupatia uhuru, badala
ya kioo kutupatia uhuru. Je, anamaanisha nini kwa kauli hiyo? (Tulipojifunza
mfululizo wa masomo juu ya sheria tuliona kuwa Mungu Muumbaji wetu anatupenda na
anafahamu kilicho bora kwa ajili yetu. Sababu ya sheria yake ni kutuambia jinsi
ya kuishi ili kuepuka kujidhuru sisi wenyewe. Sheria inaakisi upendo wa Mungu
kwetu. Sheria inaakisi uelewa wa Mungu wa jinsi ya kuepuka madhara. Huo ndio
uhuru!)
B.
Angalia tena Yakobo 1:25. Utabaini Yakobo anasema kuwa
mtu anaendelea kuangalia kwenye kioo cha sheria, hasahau kile anachokiona, na
anaenenda na kutenda kwa kile anachokiona. Matokeo yake ni nini? (Maisha yenye
mbaraka.)
1.
Soma Yakobo 1:17. Kwa nini matokeo ya utii wa sheria ni
kuwa na maisha yenye mbaraka? (Mungu anatupatia karama/zawadi njema. Sheria ni
mojawapo ya hizo zawadi njema ambayo inayaboresha maisha yetu.)
2.
Vipi kuhusu watu ambao Yakobo anawaandikia? Je, hawa si
watu ambao walilazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na mateso? (Soma Yakobo
1:12. Yakobo anasema kuwa ikiwa hakuna jambo jingine, mbaraka utafuatiwa na
uzima wa milele. Yakobo 1:15 inaelezea kuwa matokeo mbadala ni mauti.)
IV.
Ndimi na Yatima
A.
Soma Yakobo 1:26. Je, uandishi wa Yakobo ni sawa na ulimi
wa chura, ambao mara zote hujongea kwenye uelekeo mpya? Je, uzungumzaji
unajihusishaje na vioo vya kujitazama? (Soma Mithali 27:19 na Mathayo 12:34-37.
Mithali 27 inatuambia kuwa kama ambavyo kioo (katika muktadha huu maji ndio
yaliyotumika) kinavyotuonesha jinsi uso wetu unavyoonekana, kadhalika mioyo
yetu huakisi jinsi tulivyo. Yesu anaongezea katika Mathayo 12:37 kwamba kwa
usahihi kabisa maneno yetu yanaakisi mioyo yetu kiasi kwamba maneno yetu ndio
msingi wa hukumu yetu. Kwa hiyo, maneno yetu ni kioo cha mioyo yetu.)
1.
Jambo hili linaibua swali la dhati kabisa la Yesu. Suluhisho
la Yakobo (Yakobo 1:26) ni “kuuzuia ulimi wako kwa hatamu.” Je, jambo hilo
litawezekana? Je, hiyo si sawa na kujaribu kurekebisha kioo chako ili uonekane
vizuri zaidi?
2.
Je, Yakobo anasema kuwa hali ya mtu ambaye ulimi wake
unaakisi moyo mwovu ikoje? (Mtu huyo amedanganyika na dini yake haina maana. Hili
wazo la mtu kujidanganya ni mada ya kawaida kwa Yakobo. Hii inanifanya
nitafakari kuwa inawezekana Yakobo anasema kwamba ulimi wako unapaswa kuwa wito
kwamba kuna jambo lisilo jema sahihi kwenye ulimi wako. Natumai haashirii
kwamba kuutunza ulimi wako tu kutabadili moyo wako.)
3.
Soma tena Yakobo 1:19. Je, hapa Yakobo anapendekeza
nini kuhusu ulimi? (Fikiri kabla hujazungumza. Kuwa makini na mazungumzo yetu
ni mwanzo mzuri wa kutuepusha na matatizo na ni kipimo cha tabia yetu.)
B.
Soma Yakobo 1:27. Dini ambayo Mungu anaikubali ni
kutenda mambo mema kwa watu wenye dhiki na kujilinda na dunia pasipo mawaa. Wokovu kwa njia ya matendo! Unadhani Yakobo
anaweza kuwa anamaanisha nini zaidi ya kwamba tunaokolewa kwa matendo yetu
mema? (Chukulia kwamba bado Yakobo yupo kwenye mada yake ya vioo. Sheria ni
kioo ambacho tunaitumia kuyalinganisha maisha yetu. Maneno yetu ni kioo
kinachoakisi mioyo yetu. Hiyo inamaanisha kuwasaidia wale wasioweza kutusaidia
(wajane na yatima) ni kioo cha uzoefu wetu wa kidini. Kuepuka kuenenda na mambo
ya dunia pia ni kioo cha uzoefu wetu wa kidini.)
C.
Rafiki, ikiwa unaikubali na kuikiri Biblia kama mwongozo
wenye mamlaka wa maisha yako, je, unaonekanaje kwenye kipimo cha kioo? Ikiwa huu
ndio wito wako, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu sasa hivi, ili akuanzishie
mchakato wa kubadili moyo wako?
V. Juma lijalo: Upendo na Sheria
No comments:
Post a Comment