(Ufunuo
21, Mathayo 24, 1 Wathesalonike 4)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Nilipokuwa kijana nilikuwa na matumaini kwamba
Yesu atachelewesha ujio wake wa Mara ya Pili. Ndugu zangu wote wa karibu
walikuwa wangali hai, na bado nilikuwa sijaoa. Kwa kuwa ilionekana kama Yesu
alisema kuwa hapatakuwepo na ndoa mbinguni, nilidhani kuwa ikiwa atachelewesha
ujio wake, jambo hilo lingekuwa zuri zaidi kwangu. Nahisi baadhi ya wasomaji
wangu wanatamani sana Yesu arudi tena upesi, na wengine hawana shida na
kuchelewa kwake. Ninachokiwaza ni kwamba hatujui mambo yatakuwa makuu kwa
kiwango gani pale Yesu atakapokuja na kutuchukua kwenda naye mbinguni. Kama kweli
tungefahamu, hakuna ambaye angetamani Yesu achelewe kuja. Hebu tuzame kwenye
somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza juu ya ujio wa Yesu
Mara ya Pili!
I.
Malazi/Makao
A.
Soma Yohana 14:1-3. Yesu anatuambia kuwa anayo makao
mengi na makubwa kwa ajili yetu mbinguni (vyumba), na kwamba tusifadhaike. Kwa nini
Yesu anasema kuwa tusifadhaike? (Maisha yana matatizo. Yesu anasema kuwa hatma
ya suluhu ya matatizo maishani ni mbinguni. Ukiangalia muktadha uliopo, katika
sura iliyotangulia Yesu aliwaambia kwamba alikuwa anawaacha.)
1.
Nilipokuwa mdogo, neno hili lililotafsiriwa kama “vyumba”
lilitafsiriwa kama “makao.” (Linganisha tafsiri ya KJV na ile ya NIV). Je,
tumeshushwa hadhi kutoka daraja la kwanza?
2.
Nukuu za Barnes zinaonesha kuwa hapa neno la Kiyunani
linatumika vizuri kwenye mahema, kwa sababu linamaanisha jambo lisilo la kudumu
kama ilivyo kwa nyumba. Je, tumeshushwa zaidi kutoka kwenye makao hadi kwenye
mahema?
B.
Soma Ufunuo 21:1-3. Hii inatuambia nini kuhusu makao
yetu ya mbinguni? (Si ya kudumu. Mungu ataumba nchi mpya na ataishusha
Yerusalemu mpya duniani na kukaa pamoja nasi. Hii inanifanya nifikiri kuwa
dhana ya “si ya kudumu” haizungumzii mahema, badala yake inaelezea ukweli
kwamba makao yetu ya mbinguni ni ya muda (si ya kudumu) hadi Mungu atakapoumba
nchi mpya kwa ajili yetu.)
C.
Soma Ufunuo 21:15-16. Umbo la Yerusalemu Mpya
linafananaje? (Ni mchemraba! Sio mchemraba tu, ni umbo kubwa – maili 1,379
upande mmoja. Kuna umbali wa maili 1,675 kati ya Yerusalemu ya sasa na Moscow. Kuna
umbali wa maili 1,491 kati ya Washington D.C na Denver. Fikiria mamlaka iliyokuwa
na ukuta mmoja ambao urefu wake unatoka Yerusalemu hadi Moscow! Kisha fikiria
kwamba ulikuwa na kimo hicho hicho!)
1.
Ikiwa Yerusalemu Mpya
ndio huu mchemraba mkubwa, je, jambo hili linaashiria nini Yesu anapozungumzia
“chumba” chako? (Hii inaashiria kwamba chochote Yesu alichonacho mawazoni
mbinguni au katika nchi mpya ni kizuri sana na kipo nje ya uwezo wangu wa kufikiri.)
D.
Soma Ufunuo 21:17-21. Je, hii inatuambia nini juu ya
uzuri wa makao yetu mapya? (Ni mazuri ajabu!)
E.
Hivi karibuni, mtu mmoja ninayemheshinu aliniambia kuwa
alikuwa anadhani maelezo haya ni ya kiishara. Kitabu cha Ufunuo kimejaa ishara,
lakini habari za mji zinanifanya nitilie shaka kama mji huo ni wa kiishara. Ikiwa
nimekosea, je, hii itakuwa inaashiria nini? (Ikiwa jambo hili ni la kiishara,
basi inaashiria jambo ambalo linaonekana ni kubwa sana na la pekee kiasi cha
kutokuwa na uwezo wa kulielezea!)
II.
Kupenyeza
A.
Katika Mathayo 24 Yesu anazungumzia ujio wake wa Mara
ya Pili. Soma Mathayo 24:36-42. Je, tutafahamu siku ya kuja kwa Yesu Mara ya
Pili? (Hapana.)
1.
Je, tufanyeje? (Yesu anasema “tukeshe,” tujiandae
nyakati zote.)
B.
Soma Mathayo 24:43-44. Tofauti na wazo la kwamba
hatutafahamu siku Yesu atakayorudi, je, tunaambiwa jambo gani jingine? (Atakuja
siku tusiyomtarajia!)
1.
Kwa sasa kanisa langu mahalia linajifunza kitabu cha
Ufunuo. Je, tunapaswa kujifunza nini kutokana na hili fungu tunapojifunza
kitabu cha Ufunuo? (Usijiamini kupita kiasi kuhusu uelewa wako wa unabii. Mojawapo
ya maonyo ya msingi kwa mujibu wa historia ni kwamba viongozi wa Kiyahudi
kipindi cha Yesu walikuwa wanafunzi wa Biblia. Pamoja na hayo, walikuwa
wakiangalia upande tofauti Yesu alipokuja. Kiburi/majisifu ni jambo la hatari.)
C.
Kwa nini Yesu alitupatia unabii katika kitabu cha
Ufunuo? (Soma Mathayo 24:32-33. Yesu anasema ujio wake Mara ya Pili ni sawa na
ujio wa majira, unaweza kuwa na ufahamu wa jumla kuwa lini majira hayo
yatakuja. Yesu asingetuambia “tukeshe” ikiwa kukesha kusingekuwa na manufaa.)
III.
Ubainifu Chanya
A.
Soma Mathayo 24:23-25. Pamoja na tatizo la tukio
kutokea bila kutarajiwa, je, hapa tunaambiwa juu ya tatizo gani jingine?
(Kupotoshwa.)
1.
Je, tatizo hili ni kubwa kiasi gani? (“Hata wateule
wanaweza kudanganywa. Fungu hili linaashiria kwamba kimsingi jambo hili
haliwezekani, lakini onyo bado linaashiria kuwa huu ni udanganyifu mkubwa.)
B.
Soma Mathayo 24:26-27. Jibu kwa wale wanaosema kuwa
Yesu amesharudi tena ni lipi? (Kama bado hamjamwona, basi bado hajarudi.)
C.
Soma Ufunuo 1:7. Fungu hili linarudia wazo la kwamba
kama wewe mwenyewe hujashuhudia Yesu akija tena, basi huyo si Yesu. Jambo hili
linaibua tatizo halisi, tuchukulie kwamba nimeona tukio hilo, lakini siwezi
kuwa na uhakika kwamba watu waliopo upande mwingine wa dunia wameliona tukio
hilo. Ninawezaje kufahamu kile ambacho watu wengine wamekiona au hawakukiona?
D.
Soma 1 Wathesalonike 4:16-18. Jambo gani jingine
litakuwa likiendelea wakati wa ujio halisi wa Yesu Mara ya Pili? (Hutatilia
shaka juu ya kile ambacho watu wengine wamekiona au hawakukiona. Ikiwa umeokolewa,
utainuliwa na kwenda mbinguni. Utawaona wafu wakifufuliwa na kwenda mbinguni. Hili
si tukio unaloweza kulishuhudia kwa kuliangalia kwa makini sana ili kupata
viashiria! Hutakuwa na mashaka!)
1.
Nakumbuka kipindi fulani nilitembelea kanisa na
nikawasikia wanakikosi waliokuwa wakijifunza Biblia zao kuhusu ujio wa Mara ya
Pili, wakijadili kama miguu ya Yesu itakanyaga ardhini. Ikiwa unaweza kueleza
kuwa miguu yake inagusa ardhini, utakuwa na uwezo wa kueleza kama huyu alikuwa
Yesu halisi au wa bandia. Je, hilo ni jaribio linaloleta mantiki? (Huo ni
upuuzi. Ikiwa unashadadia miguu, angalia kama miguu yako mwenyewe bado inagusa
ardhi!)
IV.
Thawabu
A.
Soma Mathayo 5:19 na Mathayo 16:27. Katika mfululizo wa
masomo haya tumejadili wazo la kwamba tunaokolewa kwa neema pekee, bali uamuzi
wa kumkiri Yesu sio suala la maneno matupu. Matokeo ya imani ya kweli ni
kutembea kuielekea haki. Mathayo 16:27 inaposema kuwa Yesu “atatulipa” “kila
mtu kwa kadiri ya matendo yake,” je, hii inamaanisha kuwa wokovu ni suala la
matendo? (Hivyo sivyo ninavyoelewa jambo hili. Badala yake, Mathayo 5:19
inatuambia kuwa patakuwepo na aina fulani hivi ya madaraja mbinguni. Ni mfumo
wa ustahili.)
B.
Soma 1 Timotheo 6:17-19. Hii inatufundisha nini kuhusu
matendo mema na kushiriki utajiri wako na watu wengine? (Inatuambia kuwa
tumeweka akiba katika benki ya mbinguni.)
1.
Ikiwa, kama Ufunuo 21:21 inavyosema, kwamba mtaa mkubwa
wa Yerusalemu Mpya ni wa “dhahabu safi,” kwa nini mtu atakiwe kuwa na akiba kwenye
benki? Si unaweza tu kuchimba sehemu ndogo ya barabara? (Hatujui sarafu ya
mbinguni ni ipi. Kwa dhahiri, haiwezi kuwa dhahabu. Lakini, sarafu hiyo ni kitu
fulani na Mungu anatuahidi jambo la thamani litakaloakisi matendo yetu mema
hapa duniani.)
C.
Soma Mathayo 6:1. Hii inasema nini kuhusu Mungu na
thawabu? (Kwa dhahiri, Mungu yupo kwenye mchakato wa kutoa thawabu. Ikiwa tunajipatia
thawabu sisi wenyewe hapa, basi tumeshapokea thawabu yetu yote. Lakini, ikiwa
tunatenda matendo mema kwa moyo wa upendo na huruma, basi Mungu anaahidi
thawabu.)
D.
Soma Ufunuo 22:1-3. Je, hapa tunaona thawabu gani?
(Ulaji mzuri na afya njema!)
E.
Soma Ufunuo 21:4. Je, hapa tunaona thawabu gani?
(Hakuna kifo, maombolezo wala maumizu!)
F.
Soma Ufunuo 21:3 na Ufunuo 22:3-5. Je, hapa tunaona
thawabu gani? (Tutakaa pamoja na Mungu. Tutaona sura ya Yesu!)
G.
Rafiki, je, unataka kwenda mbinguni? Je, unataka kuishi
maisha mazuri sana kama ya wale wanaoishi kwa furaha na amani? Je, ungependa
kupewa thawabu mbinguni? Ikiwa jibu lako ni “ndiyo,” basi tubu dhambi zako, kiri
na kuyapokea maisha, kifo na ufufuo wa Yesu kwa ajili yako, na kisha uanze
kuishi maisha yanayokusanya thawabu kwa ajili ya siku zijazo! Kwa nini usijitoe
kufanya hivyo sasa hivi?
V.
Juma lijalo tutaanza kujifunza kitabu cha Yakobo.
No comments:
Post a Comment