Somo La 1 | Yakobo, Nduguye Bwana | Lesson @Babatsda


(Luka 2, Marko 3, Matendo 1, Yakobo 1)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Je, unapendelea nini: kujifunza mada moja au kujifunza/kusoma kitabu kimoja cha Biblia? Mimi ninapendelea kufundisha juu ya vitabu, badala ya kufundisha mada moja moja. Kwa nini? Kwa sababu Mungu anaweka mpangilio wa mambo ya kujifunza. Robo hii tutajifunza kitabu kimoja! Lakini, kati ya vitabu vyote vinavyoweza kufundishwa, nisingevutiwa sana kufundisha kitabu cha Yakobo. Yakobo anasisitiza juu ya matendo, sio neema. Anaonekana kutokuwapenda watu wenye fedha, hata kama anasema kwamba kuwa na upendeleo ni dhambi. Baadhi ya kauli zake zinaonekana kukinzana na kauli nyingine zilizomo kwenye Biblia. Ikiwa unapendelea changamoto, basi tayari tumeshaipata! Tutapewa changamoto ya kuingia kwa undani zaidi katika kitabu cha Yakobo na kujaribu kuelewa kile ambacho Yakobo, kwa njia ya uvuvio wa Roho Mtakatifu, anatufundisha! Hebu tuanze juma hili kwa kujifunza juu ya historia fupi ya Yakobo.
I.                   Familia
A.                Soma Mathayo 1:20-21. Unadhani babaye Yesu alielewa nini kuhusu utume wa Yesu?
B.                 Soma Luka 1:30-34. Sehemu gani ya ujumbe wa malaika ambayo Mariamu hakudhani kuwa ni ya muhimu? (Sehemu inayohusu yeye kuzaa mtoto ingawa alikuwa bikira.)
1.                  Je, wazazi wa Yesu walipaswa kuelewa utume wake? (Malaika waliwapa wazazi wa Yesu ujumbe wa kushangaza. Inaonekana ujumbe ulikuwa mkubwa sana, na walikuwa wamejikita sana kwenye uhalisia wa maisha, kiasi kwamba hawakuelewa vizuri.)
C.                 Soma Luka 2:41-43. Kwa nini mtoto wa miaka kumi na miwili anabaki Yerusalemu? (Soma Luka 2:45-47. Alikuwa na wakati mzuri na walimu wa Kiyahudi. Alipenda kujifunza.)
D.                Soma Luka 2:48. Wazazi wa Yesu walilichukuliaje jambo hili? (Walidhani kwamba Yesu hakuwatendea haki. Walikuwa wanaangalia mambo yao wenyewe, badala ya kuangalia kazi (utume) yake.)
E.                 Soma Luka 2:49-50. Kuna tatizo gani hapa? (Wazazi wa Yesu hawakuelewa utume wake.)
F.                  Soma Marko 3:13-15. Kwa nini Yesu aliwachagua wanafunzi ili wawe pamoja naye? (Watamsaidia katika utume wake.)
G.                Soma Marko 3:20-21. Utakumbuka kwamba Yesu alizaliwa kwenye familia ya daraja la watu wanaofanya kazi. Unadhani walifikiriaje juu ya kitendo cha Yesu kuwachagua wanafunzi na kuwavutia makutano? (Walidhani kwamba Yesu alikuwa amerukwa akili. Alihitaji kuwa na mtu wa “kumwangalia.”)


1.                  Je, wazazi wa Yesu walipaswa kuelewa kinachoendelea? (Walipaswa kuelewa, lakini kwa hakika hawakuelewa.)
H.                Soma Marko 3:22. Viongozi wa dini walifikiria nini kuhusu kazi ya Yesu? (Walisema kuwa alikuwa na pepo.)
1.                  Kama ungekuwa Yesu, je, ungejisikiaje? (Familia yako inadhani kuwa umechanganyikiwa na hivyo unatakiwa kuwa chini ya uangalizi, na viongozi wa dini wanadhani kuwa una pepo.)
I.                   Soma Yohana 7:1-5. Hapa ni baadaye sana katika utume wa Yesu. Je, Yesu anapewa ushauri gani na nduguze? (Ajidhihirishe kwa ulimwengu. Atende miujiza ili watu wengi waweze kuiona na kuamini.)
1.                  Kwa nini walimpa Yesu huu ushauri? (Kwa sababu hata ndugu zake hawakushawishika kwamba alikuwa “mtu maarufu” sahihi.)
J.                   Soma Marko 6:1-3. Je, Yesu ni shujaa katika mji wake aliozaliwa? (Hapana! Walichukizwa kutokana na sababu kwamba Yesu alikuwa akidai kuwa yeye ni mtu wa pekee (maalumu).)
1.                  Angalia majina na kaka wa kambo wa Yesu. Inaonekana kwamba kaka wa kambo mkubwa wa Yesu anaitwa Yakobo. Baadaye katika somo hili, natumaini utahitimisha kwamba mwandishi wa kitabu cha Yakobo ni kaka wa kambo mkubwa wa Yesu. Kutokana na kile tulichojifunza kuhusu mtazamo wa wazazi wa Yesu, familia ya Yesu, na watu waliopo katika mji alikozaliwa Yesu, unadhani Yakobo atakuwa na mtazamo wa aina gani kuhusu Yesu?
II.                Mabadiliko
A.                Soma Matendo 1:10-11. Hapa ni wakati gani katika utume wa Yesu? (Yesu aliuawa, akafufuka, na kuwatokea wafuasi wake, na sasa anarejea mbinguni.)
B.                 Soma Matendo 1:12-14. Jambo gani limetokea katika familia ya Yesu? (Wameshawishika. Sasa wanaamini kuwa Yesu ni Masihi, na kwamba hajarukwa akili.)
C.                 Soma 1 Wakorintho 15:3-7. Je, huyu Yakobo ni nani? (Marko 3:16-18 inatuambia kuwa wanafuzi wawili wa Yesu wanaitwa Yakobo. Hata hivyo, kwa kuwa 1 Wakorintho15:7 inamtenga huyu Yakobo na wale “Kumi na Wawili,” hii inaonekana kumzungumzia ndugu wa kambo mkubwa wa Yesu.)
D.                Soma Wagalatia 1:15-19. Paulo anajenga hoja kwamba alipokea ujumbe wake kutoka kwa Yesu, na si kutoka kwa mwanadamu yeyote. Je, fungu hili linaashiria nini kuhusu Yakobo, kaka wa kambo wa Yesu? (Kwamba alikuwa mtu wa muhimu katika kanisa la mwanzo.)
E.                 Soma Wagalatia 2:9. Yakobo ni wa muhimu kwa kiwango gani? (Yeye ni “nguzo” ya kanisa la mwanzo!)

F.                  Soma Matendo 15:12-14 na Matendo 15:19-21. Hapa tunajifunza nini kutoka kwa Yakobo? (Yeye ndio mkuu/kiongozi wa kanisa la mwanzo. Anatangaza hukumu yake (Kwa hakika kwa niaba ya kanisa la mwanzo) kwa kile kinachopaswa kutendwa na waongofu wa Mataifa.)
G.                Kama tunavyoona taarifa hii kwa mtazamo wa Yakobo, na umuhimu wake katika kuibuka kwa kanisa la mwanzo, je, jambo hili linaleta mantiki kwako? (Ndiyo. Yakobo ana taarifa makini na za ndani za maisha ya Yesu hapa duniani tangu mwanzo kabisa. Anashawishika kwamba Yesu ni Masihi. Bila shaka wazazi wa Yakobo walimpa habari juu ya kile walichoambiwa na malaika. Pili, inaonekana ni kawaida kwamba kanisa la mwanzo lilivutiwa na kushikamana na kaka wa Yesu. Mama yao alikuwa mmoja. Huenda walikuwa wakifanana. Huenda sauti zao zilikuwa zinafanana. Yesu alirejea mbinguni, lakini ndugu yake bado alikuwepo hapa.)
H.                Kwa muktadha wa mwanasheria mwenye kuangalia masuala ya ushahidi, ninatambua kuwa bado sijathibitisha “kikamilifu” kwamba Yakobo, kaka wa kambo wa Yesu, ndiye aliyeandika kitabu tunachojifunza. Lakini, huo ndio mtazamo wa watu wengi na jambo hilo linaonekana kuwa sahihi tu kwangu.)
III.             Kitabu
A.                Soma Yakobo 1:1. Kutokana na kile tulichojifunza, je, unauchukulia utangulizi kuwa sahihi? (Bila shaka anachokisema Yakobo ni sahihi, kile asichokisema ndicho kinachonisumbua.)
1.                  Kwa nini Yakobo anaondoa “mtumwa wa Mungu, na wa Bwana Yesu Kristo?” (Yeye ni mtu asiyejivuna kuliko wengi wetu!)
2.                  Je, kutokujivuna huku hakupo mahali pake? (Kanisa la Mwanzo lilidhani Yakobo ni mtu maalum (wa pekee), bila shaka angalao kwa sehemu fulani ni kwa sababu ya uhusiano wake na Yesu. Nadhani uhusiano unampa nafasi ya pekee ambao alipaswa kuusema. Huenda Yakobo alidhani “tayari watu wanafahamu, sina haja ya kulisema.”)
3.                  Unaona kuna umuhimu gani kwenye ukweli kwamba Yakobo alilenga barua yake iwafikie waongofu wa Kiyahudi badala ya waongofu wa Mataifa? (Hii inaweza kusaidia kuelezea msisitizo wake wa baadaye kuhusu utendaji kazi (utume).)
B.                 Angalia tena Yakobo 1:1. Tunafahamu nini kuhusu Wayahudi “kutapakaa/kutawanyika miongoni mwa mataifa?” (Soma Matendo 11:19-21. Kifo cha Stefano kilisababisha “mateso makuu” miongoni mwa waumini wa mwanzo na matokeo yake ni kwamba “walitawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria.” Matendo 8:1.)
C.                 Soma Yakobo 1:2. Wangapi kati yenu wanataka furaha maishani mwao? Wangapi wanataka majaribu? (Bila shaka sote tunataka furaha na sote tungependa kuepuka majaribu. Kumbuka, wasikilizaji wa Yakobo ni wale waliokimbia makazi yao ili kuepuka mateso.)
1.                  Yakobo anasema kuwa kuna uhusiano kati ya furaha na majaribu? (Anasema kuwa tunapaswa kutafuta furaha katika majaribu.)
D.                Soma Yakobo 1:3. Kutafuta furaha katika majaribu linaonekana kuwa ni jambo la kihisia. Kwa nini ni jambo la mantiki kuitafuta furaha? (Majaribu hujaribu imani yetu na kitendo hicho hukuza ustahimilivu.)

1.                  Binafsi ninaona kwamba furaha na ustahimilivu havikai kwenye kasha (boksi) moja! Ustahimilivu huleta akilini tatizo linaloendelea kuwepo. Unalitazamaje jambo hili?
E.                 Soma Yakobo 1:4. Jambo hili linaielezeaje furaha? (Yakobo anatuambia kuwa majaribu yanatufundisha kuwa na saburi, na saburi hutupatia zana zote tunazozihitaji. Kutambua jambo hilo ni chanzo cha furaha.)
F.                  Rafiki, je, unakubaliana na somo hili? Je, wewe ni mmoja wa wale waliodhani kuwa mafundisho ya Yesu yalikuwa ya kijinga, lakini baadaye, kama ilivyokuwa kwa Yakobo, umekuja kuwa muumini wa kweli? Huenda wewe ndiye ambaye familia yako ilidhani kuwa umechanganyikiwa kwa sababu ya imani yako. Jambo moja nililojifunza maishani ni kwamba kama “nimeongoka” kutoka kwenye mtazamo mmoja hadi mwingine, ninaushikilia mtazamo wangu mpya kwa nguvu zaidi. Bila shaka ndio maana Yakobo alikuwa muumini madhubuti. Je, utaungana nami kutafakari kile alichonacho Yakobo kwa ajili yetu katika masomo yanayofuata?

IV.             Juma lijalo: Kuikamilisha Imani Yetu.

No comments:

Post a Comment