Somo la 12: Kifo na Ufufuo
Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Yohana 11)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Katika 1 Wakorintho 15:26 tunaahidiwa kwamba
katika ujio wa Yesu Mara ya Pili “adui wa mwisho kuangamizwa kitakuwa ni kifo.”
Hizo ni habari njema na ndio mada ya somo letu la Biblia katika juma hili. Je,
unadhani ni muhimu kwamba kifo ndicho adui wa “mwisho” kuangamizwa? Je,
usingependelea kiwe cha kwanza kuangamizwa? Mara ngapi maishani tumemkasirikia
Mungu kwa sababu ya kifo cha rafiki au mwanafamilia? Tunawaambia nini watu
wanaokasirika? Ikiwa unaamini, kama ambavyo mimi ninaamini, kwamba Mungu ndiye
anayeuongoza na kuushikilia ulimwengu, tunayaelezeaje majanga yanayowakabili
wanadamu? Je, tunapaswa hata kujaribu kuyaelezea? Hebu tuzame kwenye somo letu
la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza!
I.
Lazaro
A.
Soma Yohana 11:1-3. Jiweke kwenye nafasi ya Mariamu na
Martha. Kwa nini unatuma ujumbe usemao “yeye umpendaye” hawezi (anaumwa)?
1.
Je, unadhani ni kweli kwamba Yesu ana uhusiano wa pekee
na Lazaro? (Hapa tuaambiwa kuwa Mariamu alimpaka Yesu marhamu na kufuta miguu
yake kwa nywele zake. Mahali pengine tunaambiwa habari za waha ndugu (Mariamu
na Martha) wakimkaribisha Yesu na wanafunzi wake nyumbani kwao (Luka 10:38-39).
Kilichohitajika ilikuwa ni kumwomba Yesu aje ili amponye Lazaro.)
B.
Soma Yohana 11:4. Yesu anauchukuliaje ugonjwa wa
Lazaro? (Anasema kuwa hatma ya ugonjwa wake sio mauti. Badala yake, ugonjwa huo
utaleta utukufu kwa Mungu.)
C.
Soma Yohana 11:5-6. Je, ujumbe ambao Mariamu na Martha
walimtumia Yesu ulikuwa sahihi – kwamba Yesu alimpenda Lazaro? (Ndiyo. Ujumbe huu
unathibitisha kile walichokisema.)
1.
Ikiwa rafiki umpendaye anahitaji msaada, kwa nini
uchelewe kwa siku mbili? (Yesu anafahamu kitakachotokea. Hata hivyo, kama
tutakavyoona, kitendo cha kuchelewa kinawasikitisha sana Mariamu na Martha.)
D.
Soma Yohana 11:7-8. Wanafunzi wanafahamu uhusiano
uliopo kati ya Lazaro, dada zake, na Yesu. Je, wanadhani kuwa wazo la kwenda
kumsaidia Lazaro ni jema? (Hapana. Wanadhani kuwa ni hatari sana kwa Yesu
kwenda.)
E.
Soma Yohana 11:9-10. Je, jibu hili ni la ovyo? Wanafunzi
wanazungumzia hatari iliyopo, na Yesu anazungumzia vigezo vya kufanya
matembezi. Je, hawaelewani katika mazungumzo yao? (Yesu anazungumzia jambo la
muhimu sana juu ya kifo. Unao muda maalum wa kuishi uliotengwa. Ikiwa utatembea
wakati wa mchana katika kipindi cha uhai wako, “hutajikwaa” nawe utakuwa na muda
wa “saa kumi na mbili.” Yesu anawaambia wanafunzi wake kwamba ingawa ni hatari,
hatakufa kabla ya muda wake uliopangwa.)
F.
Soma Yohana 11:11-13. Je, kuna uhusiano gani kati ya
wanafunzi na Lazaro? (Yesu anasema kuwa Lazaro ni rafiki yao wote.)
1.
Angalia jinsi Yesu anavyokizungumzia kifo. Yesu
anaizungumziaje hali ya Lazaro? (Anasema kwamba kifo ni sawa na usingizi. Jambo
hili linathibitisha wazo la kwamba tunapofariki tunakuwa hatuna ufahamu.)
2.
Kwa nini wanafunzi wanaashiria kuwa Lazaro anaendelea
vizuri kiafya? (Bado hawajaridhika kuhusu hatari ya kwenda Uyahudi.)
G.
Soma Yohana 11:14-16. Je, Yesu na wanafunzi wake wana
uelewa wa pamoja – je, wanayaangalia na kuyachukulia mambo kwa namna moja?
(Hapana. Wanafunzi wanalichukulia jambo hili kuwa ni la hatari. Wanajifikiria wao
wenyewe. Yesu anafikiria kwamba yu karibu kuwaonyesha wanafunzi pamoja na
ulimwengu kwamba anao uwezo na mamlaka juu ya kifo.)
1.
Angalia jinsi wanafunzi pamoja na Yesu
wanavyokizungumzia kifo kwa namna tofauti. Hapo awali, katika Yohana 11:4, Yesu
alisema “ugonjwa huu si wa mauti.” Tunazilinganishaje hizi kauli mbili
zinazokinzana wazi kabisa? (Yesu haangalii kifo cha watu watakaofufuliwa kama “kifo”
halisi. Anakichukulia kuwa ni kama usingizi.)
H.
Soma Yohana 11:17-21. Martha anampa Yesu ujumbe gani?
(Kwamba walimtumia ujumbe kuwa walihitaji msaada. Yesu anawapenda, hivyo kwa
hakika angekwenda na kumponya Lazaro. Yesu aliwaponya watu wengi sana ambao
hata hakuwafahamu, kwa nini alishindwa kumponya mtu aliyempenda? Martha amemkasirikia
Yesu.)
1.
Je, unadhani Mariamu, Martha na Lazaro walijadili jambo
hili kabla ya kifo cha Lazaro? (Bila shaka walimfariji Lazaro kwa kumwambia
kuwa Yesu anakuja. Yeye aliyewaponya watu wengi sana, Rafiki aliyempenda, kwa
hakika atakuja na kumwokoa dhidi ya kifo. Lakini, pamoja na yote hayo Lazaro
amefariki.)
2.
Mariamu anampa Yesu ujumbe gani? (Anakataa hata
kumsalimia! Utabiri wangu ni kwamba amekasirika na anataka Yesu atambue hivyo.
Yesu amewaangusha na sasa kaka yake amefariki.)
I.
Soma Yohana 11:22. Martha anasema nini? (Amesikitika
sana kwa kitendo alichokifanya Yesu, lakini bado ana imani naye. Mariamu yeye
amekasirika na kughadhabika.)
1.
Unadhani Martha alikuwa anafikiria nini mawazoni mwake
aliposema kuwa Mungu atampatia Yesu “yoyote utakayomwomba?”
J.
Soma Yohana 11:23-24. Martha ana uelewa gani juu ya
kifo? (Wafu watafufuliwa katika ufufuo wa mwisho.)
K.
Soma Yohana 11:25-27. Hebu tuiangalie kwa kina kauli ya
Yesu. Unadhani anamaanisha nini anaposema kuwa yeye ndiye “ufufuo na uzima?”
(Kwanza Yesu anasema kuwa anao uwezo wa kufufua. Kisha anasema kuwa anao uwezo
wa kuwapa uzima wale anaowafufua.)
1.
Je, unaielewaje kauli ya Yesu kuhusu kutokufa wakati ni
punde tu amezungumzia juu ya kufa kwetu? (Angalia jambo hili katika mfululizo
huu. Tunakufa, Yesu anatufufua. Wale wanaoishi na kumwamini Yesu hawatakufa
tena baada ya hapo. Maisha baada ya ufufuo katika Yesu ndio uzima wa milele. Hii
inaendana na kauli ya Yesu hapo awali kwamba ugonjwa wa Lazaro :si wa mauti.”
Yohana 11:4. Yesu anatufundisha kwamba kiuhalisia, mauti ya kwanza, ni sawa na
usingizi. Marafiki pamoja na wanafamilia hawajafa, bali wamelala. Ikiwa wanamkiri
Yesu kama uzima na ufufuo wao, watafufuliwa katika uzima wa milele.)
L.
Soma Yohana 11:28-29. Je, ukweli kwamba Mariamu aliamka
upesi unaashiria kuwa hajamkasirikia Yesu kwa kumwacha kaka yake hadi
akafariki? (Hisia zinazoambatana na masuala ya kifo mara kwa mara huwa
zinabadilika badilika. Yesu alimuulizia. Hiyo inaonesha kuwa anajali, na huenda
hicho ndicho kilichokuwa kinatakiwa ili kubadili mtazamo wake.)
M.
Soma Yohana 11:32. Je, Mariamu anamtuhumu Yesu? Endapo
ungekuwa Yesu, je, ungesema nini? (Mariamu anamlaumu Yesu. Alimwangukia miguuni
pake. Alikuwa na uwezo. Hakuja wakati alipotaarifiwa kwamba Lazaro alikuwa
akihitaji msaada.)
N.
Soma Yohana 11:33-35. Ikiwa Yesu alifahamu kile
alichokuwa nacho mawazoni mwake, kwa nini alilia? (Yesu anatupenda. Ingawa atakishinda
kifo, anasikitika pale tunaposikitika. Anasikitika pale anapodhani kwamba
ametuangusha.)
O.
Soma Yohana 11:36-37. Baada ya kumwona Yesu analia, kundi
moja linasema kuwa Yesu alimpenda Lazaro. Je, mwitikio wa kundi jingine ukoje?
(Ikiwa Yesu alimpenda Lazaro, kwa nini alimwacha hadi akafariki? Inaonyesha Yesu
hakumpenda Lazaro.)
1.
Je, huu ndio mjadala unaouona kwenye kila msiba wa mtu
ambaye umri wake ni “mdogo sana” kiasi cha kutostahili kufa? (Ndiyo! Na, kisa
hiki kinajibu swali hili. Yesu anaruhusu watu walale hata kama anawapenda.)
P.
Soma Yohana 11:38-39. Martha ndiye aliyependekeza
kwamba Yesu anaweza kutenda jambo lolote. Jambo gani limetokea kwenye imani
yake?
Q.
Soma Yohana 11:40-42. Je, Yesu anataka hili kundi la
watu lifahamu juu ya jambo gani? (Kwamba Mungu ndiye chanzo cha muujiza. Kwamba
Mungu alimtuma Yesu. Kwamba Mungu ndiye anayepewa utukufu.)
R.
Soma Yohana 11:43-44. Sasa jiweke kwenye nafasi ya
Mariamu na Martha. Je, inajalisha kwamba Yesu alichelewa? Je, inajalisha kwamba
hakuitikia wito wao wakati alipohitajika zaidi? (Hapana! Sasa mambo yote yako sawa.
Kila kitu kipo sahihi na jambo hili lilitokea “kwa ajili ya utukufu wa Mungu,
ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo.” Yohana 11:4.)
S.
Soma Yohana 11:45. Mungu anatukuzwaje? (Watu wengi
walimwamini Yesu! Hata leo jambo hili linatupatia imani kwa Mungu na
linatusaidia kuelewa hekima yake katikati ya majanga.)
T.
Soma Yohana 11:46-48 na Yohana 11:53. Je, matokeo
mengine baada ya Yesu kumfufua Lazaro ni yapi? (Yesu alitia mhuri juu ya majaliwa
yake mwenyewe. Hebu weka kweli hizi mbili pamoja unapopitia uzoefu wa kumpoteza
mtu umpendaye. Badala ya kumtuhumu Yesu, badala ya kumkasirikia, chukulia
kwamba kifo na ufufuo wake vinafanya mpendwa wako afufuke kutoka “usingizini.” Alikufa
ili wewe uweze kuishi. Alitupenda sana kiasi cha kufa kwa ajili yetu!)
U.
Rafiki, katika kisa hiki tunaona kwamba tunahitaji
kumtumaini Yesu kwa ajili ya maisha yetu na maisha ya wale tunaowapenda. Upo muda
uliotengwa kwa ajili yetu ikiwa tutatembea nuruni. Baada ya hapo, ikiwa
tutaiweka imani yetu kwa Yesu, tutalala hadi Yesu atakapotuamsha kwa ajili ya
uzima wa milele. Je, utamtumaini Yesu?
II.
Juma lijalo: Kuja kwa Yesu Mara ya Pili.
No comments:
Post a Comment