Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Wagalatia 3:15-20)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Mwanzo 15:6 inasema kuwa “Ibrahamu akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki.” Paulo anatuambia kwamba hii ndio kanuni aiwazayo Mungu kwa ajili yetu. Tunatakiwa kumwamini na kumtumaini Mungu. Tukifanya hivyo, hiyo inatosha kwa sisi kuwa na uhusiano sahihi na Mungu. Hiyo ndio tiketi yetu ya kuingilia mbinguni. Lakini je, hii ni sahihi? Vipi kuhusu ukweli kwamba Mungu aliwapa watu wake Ahadi Kumi kupitia kwa Musa? Vipi kuhusu ukweli kwamba Yesu aliufanya utiifu uwe mgumu zaidi kwa kusema kuwa kitendo cha kuangalia kwa “kutamani” kilikuwa ni sawa na kuzini “moyoni” na mtu kuwa na hasira kunamwingiza kwenye hukumu sawa na mtu aliyeua anavyohukumiwa (Mathayo 5)? Zungumzia juu ya kuweka viwango kuwa vya juu na vyenye ukali! Paulo anajadili athari za sheria katika somo letu la juma hili. Hebu tuzame kwenye Biblia yetu ili tujifunze zaidi!
I. Ahadi
A. Soma Wagalatia 3:15. Unadhani “agano la mwanadamu” ni kitu gani? (Agano ni mkataba, makubaliano kati ya watu wawili (au zaidi).)
1. Fikiria mara ya mwisho uliposaini mkataba. Je, uliahidi kufanya jambo lolote? Je, upande wa pili uliahidi kufanya jambo fulani? (Wanasheria wanaziita ahadi hizi “consideration.” Kila upande katika mkataba unaahidi kutimiza jambo fulani.)
B. Angalia tena Wagalatia 3:15. Paulo anasema kuwa jambo gani haliwezi kutendwa kwenye mkataba uliosainiwa? (Unakubaliana na kuenenda na vigezo na masharti yaliyokubalika. Huwezi kuomba mambo ya ziada, na huwezi kutenda kwa uchache pungufu ya ulivyoahidi.)
1. Je, huo ndio uzoefu wako? (Paulo anazungumzia jambo linaloweza kutekelezwa. Anazungumzia jambo linalofikirika. Ukitoa ahadi yako kwenye mkataba, unapaswa kuitimiza. Ukikubali kwamba mtu mwingine anapaswa kutenda jambo mahsusi, usimtarajie atende zaidi ya makubaliano.)
C. Soma Wagalatia 3:16-17. Unawezaje kuhusianisha Ahadi Kumi na mjadala tuliokuwa nao hivi punde kuhusu ahadi za mkataba? Ikiwa mkataba unasema kwamba Mungu anakuchukulia kuwa u mwenye haki ikiwa unamtumaini, utakuwa na mjibizo (reaction) gani katika kuongezea Ahadi Kumi? (Nitalalamika juu ya uvunjaji wa mkataba. Hata nitalalamika kwa nguvu na sauti kubwa zaidi ikiwa Mungu ataniambia kuwa kanuni hizo zitatafsiriwa kwa namna ya ukali kadri iwezekanavyo! Nitajenga hoja kwamba Mungu ananitaka kutenda mambo mengi zaidi ya yale yaliyomo kwenye mkataba wa awali (halisi).)
1. Paulo anamaanisha nini hapa? (Mungu hatafanya hivyo. Sheria haikutolewa kama sehemu ya mkataba wa awali kati ya Mungu na wanadamu. Ilitolewa kwa malengo mengine. Mkataba wa awali unabaki kama ulivyo.)
II. Mzao
A. Soma tena Wagalatia 3:16 na ujikite kwenye mjadala wa “mzao” na “wazao.” Je, Paulo anasema kwamba mkataba huu haukuwa kati ya Mungu na Ibrahimu (na uzao wake), badala yake ulikuwa kati ya Mungu, Ibrahimu na Yesu?
1. Mungu anawezaje kuingia mkataba baina yake? Mungu Baba aliingia mkataba na Mungu Mwana?
2. Kuna mashaka yoyote kwamba “mzao” ni Yesu? (Paulo anasema kwa umahsusi kabisa kwamba mzao ni Kristo.)
B. Angalia tena mwanzoni mwa Wagalatia 3:17. Je, Paulo anatarajia kwamba tunaweza tusielewe jambo hili? (Anasema, “Nisemalo ni hili….” Sielewi hiki kinachoonekana kuwa ni mkataba na Yesu, hivyo tunatakiwa kuangalia kama Paulo ataliweka bayana hapo baadaye.)
C. Soma Wagalatia 3:18. Sasa Paulo anaingiza msamiati mwingine wa kisheria, “urithi.” Urithi unahusianaje na kile tunachokijadili? (Mtu anaweza kurithi haki za kimkataba. Tuchukulie kwamba baba yako amekubali kumkodisha mtu ardhi kwa miaka kumi kwa $ 10,000 kwa mwaka. Baba yako akifariki, na ukairithi ardhi, utaichukua ardhi hiyo kwa mujibu wa mkataba – ikimaanisha kwamba utaiendeleza ahadi na utaendelea kunufaika kutokana na ahadi iliyowekwa na mtu mwingine. Nadhani Paulo anatuambia kuwa tulirithi matamanio ya Ibrahimu kwenye mkataba kati ya Mungu na Ibrahimu.)
D. Soma Wagalatia 3:19. Hii inabainishaje mkanganyiko wa awali juu ya Mzao? (Badala ya kusema kwamba “Mzao” ni mnufaika wa mkataba, inasema “Mzao” ni kiini cha mkataba. Hiyo inaleta mantiki kamilifu kwangu!)
III. Torati
A. Hebu tuangalie sehemu ya Wagalatia 3:19 inayozungumzia “lengo” la torati. Inaeleza kuwa lengo la torati ni lipi? (Iliingizwa “kwa sababu ya makosa,” na ina ukomo wa matumizi.)
1. Ikiwa Yesu alitii torati kwa niaba yetu, na sisi hatuko chini ya adhabu ya torati, kwa nini pawepo na hitaji la torati kujazilizia ombwe hadi Yesu alipokuja? Kwa nini wahitaji jambo jingine lolote lile? (Fikiria taswira pana. Je, Mungu anataka tutende dhambi? Kwa dhahiri, hapana. Yesu alikuja na kuishika torati kwa sehemu fulani ili kuonesha kuwa Adamu angeweza kuishika torati. Kuishika sheria ni jambo jema. Yesu alipokuja, hakutuonesha tu jinsi ya kuishi (kutuonesha “zaidi ya torati” ilikuwa jambo la kufikirika, kuishika torati pekee ilikuwa ni kuwa na malengo ya chini sana), bali pia alimpeleka Roho Mtakatifu ili atusaidie kuishi maisha yanayoendana na mapenzi ya Mungu. Tulihitaji kiongozi.)
B. Soma Wagalatia 3:19-20. Nimejumuisha kifungu cha 19 kwa sababu nataka kujikita kwenye rejea ya “mjumbe.” Unadhani huyu mjumbe ni nani? Musa? (Soma 1 Timotheo 2:5-6 na Waebrania 9:15. Kwa dhahiri vifungu hivi vinamwita Yesu Mpatanishi wetu – hususani kwa sababu ya kifo chake kwa ajili (niaba) yetu.)
1. Angalia tena Wagalatia 3:19. Je, Yesu aliiweka sheria “katika utekelezaji kwa njia ya malaika?” Ni kwa jinsi gani torati ilikuwa sehemu ya upatanisho? (Soma Warumi 5:10 na 2 Wakorintho 5:17-19. Mungu ni mtakatifu na sisi sio watakatifu. Watu wa Mungu, wakati wakiwa utumwani Misri, kwa hakika walipoteza na kuachana na lengo la Mungu maishani mwao. Katika kuwasaidia waweze kuendana vizuri zaidi na mapenzi ya Mungu, aliwapatia torati. Hivyo, nadhani kwamba Musa ndiye “mpatanishi” wa awali. Hata hivyo, Yesu ndiye Mpatanishi wa kweli alipoishi na kufa na kulipa adhabu kwa ajili ya dhambi zetu.)
2. Paulo anamaanisha nini kwa kuadika kwamba “Mungu ni mmoja?” Hii inahusianaje na Yesu kuwa “Mpatanishi?” (Mpatanishi hawakilishi upande wowote. Katika sheria ya sasa ya Marekani, mpatanishi anajaribu kuzileta pande mbili zinazopingana ili zifikie makubaliano. Yesu ni Mungu kamili na mwanadamu kamili. Yeye ni Mmoja pamoja na Mungu. Hivyo, Yesu, katika namna isiyo ya kawaida kupita zote, ametuleta na kutukutanisha pamoja na Mungu.)
C. Soma tena sentesi ya kwanza ya Wagalatia 3:19 na kisha usome sentesi ya kwanza ya Wagalatia 3:21. Tutajifunza Wagalatia 21 juma lijalo, lakini kwa sasa ninataka uangalie maswali mawili yaliyoulizwa kwenye hivi vifungu viwili. Je, maswali yote mawili yanatuuliza jambo moja? (Ndiyo. Ikiwa tunaweza kuelewa lengo la torati, basi tunaweza kuelezea ikiwa inapingana na mkataba wa awali (asili) kati ya Mungu na Ibrahimu.)
1. Kwa kuangalia lengo la jumla la Mungu kwa ajili yetu, je, torati inakinzana na mkataba?
2. Mungu alimtaka Ibrahimu afanye nini? (Amtumaini yeye!)
3. Kwa nini Mungu awatake wanadamu wamtumaini? (Wataishi (watakaa) kwa amani na Mungu. Tutakuwa na tumaini kwamba njia ya Mungu na mapenzi ya Mungu vilikuwa vitu bora kabisa kwa ajili ya maisha yetu.)
4. Torati inatutendea nini? (Soma Warumi 7:7. Torati inayafunua mapenzi ya Mungu kwa ajili yetu. Je, unataka kufahamu jinsi ya kuishi kwa amani na mapenzi ya Mungu? Soma Amri Kumi.)
5. Vipi kuhusu maoni ya Yesu juu ya tamaa na hasira kuwa matatizo yanayolingana na uzinzi na mauaji? Je, mwelekeo huo ni jambo linalotusaidia kuwa na amani na Mungu? (Soma Yakobo 1:13-15. Wanadamu hawatumbukii kwenye uzinzi na mauaji bila kutarajia. Kitendo huanza na tamaa, mpango unapangiliwa akilini, ili kutenda matendo haya. Nadhani anachokimaanisha Yesu ni kwamba ikiwa hufanyi uzinzi au mauaji kwa sababu tu huna fursa ya kufanya hivyo, maisha yako hayaendani na mapenzi ya Mungu. Ikiwa unapanga kufanya uzinzi au mauaji, basi maisha yako hayaendani na mapenzi ya Mungu.)
D. Tunapaswa kuishije basi? (Tukiyakiri maisha, kifo na ufufuo wa Yesu kwa ajili yetu, tunao uhakika kwamba adhabu ya dhambi haihusiki kwetu. Tumeokolewa. Wakati huo huo, tunapoishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu, tunatambua kwamba yale yote aliyoyafanya Yesu yalilenga kutupatanisha na Mungu. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu, tunachagua kuyaelekeza mawazo yetu na maisha yetu kwa namna inayoendana na amri zilizofunuliwa na Mungu. Tunafanya hivi kwa kuwa tunamtumaini Mungu. Tunajua kwamba hii itayaboresha maisha yetu, na tunafahamu kwamba hii itampa Mungu utukufu!)
E. Rafiki, je, unakubali na kukiri kile alichokitenda Yesu kwa ajili yako? Je, utakubali kumtumaini katika yote uyatendayo?
IV. Juma lijalo: Njia ya Kuiendea Imani.
No comments:
Post a Comment