(Wagalatia 3:1-14)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com
kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Nilipokuwa mdogo, kulikuwa na programu kwenye
televisheni iliyokuwa inaitwa “Kurogwa.” Katika somo letu juma hili, Paulo
anawaambia Wagalatia kwamba “wamerogwa.” Tunafahamu kwamba Wagalatia
wasingekuwa wanatazama televisheni kupita kiasi! Je, Paulo anazungumzia juu ya
kupagawa pepo? Nimeangalia tafsiri ya “Strong” juu ya neno la Kiyunani na
linamaanisha “kupumbaza (kwa kutumia mbinu za uongo).” Tusingependa kupotoshwa
juu ya injili, hivyo hebu tuzame kwenye somo letu la barua kwa Wagalatia ili
tuubaini ukweli!
I.
Kurogwa
A.
Soma Wagalatia 3:1. Kwa nini ufahamu wa mateso
ya Yesu ni muhimu ili “kutokurogwa?” (Soma Wagalatia 2:21. Tulimalizia somo la
juma lililopita kwa ujumbe huu – ikiwa tunadhani kuwa tunaweza kuokolewa kwa
matendo yetu, tunakidhihaki kifo cha Yesu kwa ajili yetu. Kudhihaki kile
ambacho Yesu ametutendea ni kosa kubwa sana.)
B.
Soma Wagalatia 3:2. Ni muhimu kiasi gani “kumpokea
Roho?” (Kwa namna Paulo anavyoandika jambo hili, ni uthibitisho wa muhimu sana
kwamba maisha yako ya Kikristo yapo kwenye msitari sahihi. Paulo anawakumbusha
kwamba Roho Mtakatifu hakuwaendea kutokana na wao kutii matendo ya sheria.)
1.
Je, umegundua jambo ambalo Paulo analizungumzia?
Makanisa yanayoonekana kujikita kwenye sheria yamekauka kama mifupa. Hawana (wanapungukiwa)
Roho Mtakatifu. Kwa upande mwingine, makanisa yaliyojaa watu wanaofurahia
kukubaliwa kwao kwa imani wanaonekana kujawa Roho. Je, haya ndio maoni yako?
C.
Soma Wagalatia 3:3-4. Wagalatia wametesekea nini
bure? Mateso hayo ni yapi na jambo gani ni bure? (Kubadili imani yako ya dini
kutakufarakanisha na marafiki na wanafamilia. Kwa kuwa kila dini, isipokuwa
Ukristo, imejengwa juu ya matendo kwa namna fulani, Paulo anasema kwamba baada
ya kuteseka kutokana na uamuzi wako wa kubadilika, sasa unarejea kwenye matendo
yako. Hivyo, kubadilika kwako kulikuwa bure.)
D.
Soma Wagalatia 3:5. Paulo anahusianisha nini na
kuwa na Roho Mtakatifu kanisani? (Miujiza.)
1.
Ikiwa hatuna miujiza, na katika eneo la dunia
hii ninakoishi ninadhani kwamba tunapungukiwa/hatuna miujiza ya “hakuna
anayeweza kuwaamulia,” je, hiyo inamaanisha kuwa hatuna Roho Mtakatifu?
(Ninaamini kuwa mjukuu wangu wa kike aliponywa kimiujiza baada ya kuzaliwa. Lakini,
naweza kufikiria jinsi baadhi ya watu wanavyoweza kusema juu ya jambo hili. Ubashiri
wangu ni kwamba wewe pia unao uzoefu wa kufanyiwa/kuona miujiza, lakini miujiza
hiyo si sawa na ile miujiza mbalimbali ya Mathayo 12:22-23 – kila mtu
anashangazwa nayo. Kutokuwepo kwa miujiza ya namna hii katika eneo langu leo
hunitaabisha.)
2.
Je, miujiza inaweza kutokana na kuishika sheria?
(Hapana! Ninachokiona kuwa ni sababu ya kutokuwepo miujiza ni kwamba tunajikita
zaidi kwenye sheria kuliko neema na Roho Mtakatifu. Panaweza kuwepo sababu
nyingine, kwa mfano, kwamba hatuna udhibiti juu ya kazi ya Mungu, lakini hili
ni jambo la kulichukulia kwa umakini.)
II.
Ibrahimu
A.
Soma Wagalatia 3:6. Je, kuhesabiwa haki kwa njia
ya imani ni fundisho la Agano la Kale? (Ndiyo! Fikiria mfumo wa patakatifu. Ulimchinja
mnyama na damu yake ilifanya upatanisho wa dhambi zako. Huo si wokovu kwa njia
ya matendo, huo ni wokovu kwa njia ya kifo cha mnyama. Naam, tunajua kwamba
jambo hilo lilikuwa linazungumzia kifo cha Yesu katika siku zijazo.)
B.
Hebu tusome utangulizi wa kauli ya Paulo juu ya
Ibrahimu. Soma Mwanzo 15:4-6. Ibrahimu anaamini nini? (Kwamba atampata mwana na
uzao mkubwa.)
1.
Kwa nini imani huleta haki? Kwa nini tusisema
kuwa imani huleta “watoto?” (Hii inaonesha kwamba jambo halisi na la msingi ni
kumtumaini Mungu. Je, tunaamini anachokisema Mungu na kile alichokitenda na
atakachotutendea?)
C.
Soma Wagalatia 3:7-9. Kwa nini kusema kwamba
injili ilitangazwa “mapema kabla” kwa Ibrahimu? Je, injili (kuhesabiwa haki kwa
njia ya imani) haikutolewa tangu kipindi hicho? (Hii ilikuwa ni kabla ya
kutolewa kwa Amri Kumi pamoja na sheria nyingine zilizotangazwa na Musa. Dhana iliyopo
ni kwamba kila kilichofuatia, fundisho la msingi lilikuwa ni kuhesabiwa haki
kwa njia ya imani.)
III.
Laana
A.
Soma Wagalatia 3:10. Hivi karibuni, nilikuwa
ninatafakari jinsi ninavyoweza kushiriki injili na mtu aliyekuwa anakaribia
kufariki, na alikuwa anaichukia dini kwa kiasi fulani. Nina uhakika mtu huyu
anadhani kwamba “mimi ni mtu mwema sana, sina hitaji la kitu kingine chochote
kile.” Je, huu ni mtazamo unaoleta laana? (Ndiyo. Mtu anaposema, “mimi ni mwema
na ni mtu bora zaidi kuliko watu wengine wengi tu ninaowafahamu,” mtu huyo
anadhani kuwa wokovu wake unatokana na matendo yake. Tatizo la njia hiyo ni
kwamba haitoshi kuwa bora zaidi ya watu wengine. Unatakiwa kuwa mkamilifu,
unatakiwa “kuendelea kutenda kila jambo lililoandikwa kwenye Kitabu cha Sheria.”)
B.
Soma Wagalatia 3:11-12. Je, unapata wakati mgumu
kutafakari wazo la kwamba mtu anayejtahidi sana kuishika sheria anaweza
kulaaniwa? Huyu ni “mtu mwema.” (Kuyatii mapenzi ya Mungu ni jambo jema. Tatizo
ni kuutegemea utiifu huo kwa ajili ya wokovu wako.)
1.
Watu wangapi wanayategemea matendo yao kwa ajili
ya wokovu na hawajui kuwa wanayategemea? (Utaona kwamba Paulo anawazungumzia
wale wanaoishika sheria: “Mtu atendaye mambo haya ataishi kwa imani.” Hii inatoa
taswira ya mtu mtiifu, na anayeamini kuwa jambo hili huleta stahili ya
kukubaliwa na Mungu.)
C.
Soma Wagalatia 3:13. Je, adhabu, laana ya sheria
ilitundikwa juu ya nani? (Yesu. Alilipa adhabu kwa ajili ya dhambi zetu. Alilaaniwa
ili kutukomboa kutoka kwenye laana.)
1.
Ikiwa tunayategemea matendo yetu kwa ajili ya
wokovu, je, tunaichukua laana? (Ndiyo!)
D.
Siku za hivi karibuni, nimekuwa nikipambana na
dhambi mahsusi. Sina chembe ya shaka mawazoni mwangu kwamba Mungu anatamani
tuwe watiifu, kwa ajili ya manufaa yetu na kwa ajili ya utukufu wake. Tatizo ni
kwamba ninaposhindwa, ninadhani kuwa kitendo hiki kinaathiri kwa kiasi kikubwa
sana uhusiano wangu na Mungu. Wakati huo huo naamini kuwa kitendo hiki
kinakiuka maelekezo ya Paulo kwamba hatupaswi “kutegemea” ushikaji wa sheria. Una
maoni gani?
1.
Je, itakuwa sahihi kuamini kwamba kila (wewe na
mimi) tunapoielekea haki, anguko lolote linaathiri maisha yetu ya hapa duniani,
haliathiri uhusiano wetu na Mungu?
2.
Soma Warumi 7:4-6. Hapa Paulo anatuambia kuwa
tunapaswa kuishi kwa mujibu wa maelekezo ya Roho Mtakatifu. Hii inaashiria
kwamba ikiwa “tunadhibitiwa” na asili ya dhambi, kimsingi tunakuwa na tatizo la
kiuhusiano na Roho Mtakatifu. Unawezaje kuelezea kwa ufupi ukweli juu ya
mapambano dhidi ya dhambi? (Hiki ndicho ninachokifikiria: Roho Mtakatifu akaaye
ndani yetu anasimama mahali pa sheria katika kuyaelekeza matendo yetu. Tunapopambana
na dhambi, ni Roho Mtakatifu ndiye anayetenda kazi pamoja nasi. Tusichoweza kukifanya
ni kumpuuzia Roho Mtakatifu. Katika mapambano haya, bado tunaokolewa kwa neema.
Kazi ya Roho Mtakatifu ni kuyapatanisha zaidi maisha yetu na mapenzi ya Mungu.)
E.
Soma Wagalatia 3:14. “Ahadi aliyopewa Ibrahimu”
ni ipi? Watoto wengi? (Soma tena Wagalatia 3:6. Mbaraka unaozungumziwa hapa ni
kuhesabiwa haki. Fursa hii sasa imeongezwa kwetu sisi tusio Wayahudi.)
1.
Ni jambo gani tunalolipokea kwa imani? (Ahadi ya
Roho Mtakatifu.)
a.
Hii inaongezea msisitizo wa Roho Mtakatifu. Nilidhani
lengo lilikuwa ni kuhesabiwa haki kwa njia ya imani, badala ya karama ya Roho
Mtakatifu. Kwa nini Paulo anabainisha karama ya Roho Mtakatifu kama matokeo ya
imani yetu? Hii inaturejesha kwenye Warumi 7:6. Mbadala wa kuzishika Amri Kumi
sio kuishi kwa namna yoyote ile unayoichagua. Mbadala ni kwamba “tupate
kutumika katika hali mpya ya Roho.”)
F.
Rafiki, ikiwa unaamini (kama nilivyokuwa
ninaamini wakati fulani), kwamba kuzishika Amri Kumi ni muhimu sana kwa ajili
ya wokovu, unaweza kuona jinsi kitendo hicho kinavyoweza kukutumbukiza kwenye
kulaaniwa? Kwa kuwa ni hakika kwamba utashindwa katika juhudi zako za kuishika
sheria yote, utapungukiwa (utaukosa) ukamilifu, na hivyo utaukosa wokovu. Yesu anatupatia
kitu kingine. Anatupatia fursa, kwa njia ya ubatizo, kushiriki kifo chake kwa
ajili ya dhambi zetu, na ufufuo wake kwa ajili ya uzima wa milele. Anatupatia uchaguzi
wa kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu. Je, utakubali, sasa hivi, “ofa”
ya Yesu?
IV. Juma lijalo: Kipaumbele cha Ahadi.
No comments:
Post a Comment