Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Wagalatia 2:15-21, Warumi 7)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Juma hili tunaanza mjadala juu ya kiini cha injili – ni kwa jinsi gani Mkristo anaokolewa kutoka kwenye dhambi zake. Ni muhimu sana kuelewa jambo hili kwa usahihi. Unakumbuka kwamba katika Wagalatia 1:8 Paulo anasema kuwa wale wanaofundisha injili ya uongo wanapaswa “kulaaniwa milele.” Nitajaribu kuelezea jambo hili kwa usahihi! Jambo la muhimu zaidi ya kile ninachokiandika, angalia kwa makini kile anachokiandika Paulo ili uweze kuyaelewa mapenzi ya Mungu kwa usahihi kabisa. Hebu tuzame kwenye somo hili la muhimu kabisa!
I. Wayahudi Dhidi ya Mataifa
A. Soma Wagalatia 2:15-16. Utakumbuka kwamba tulipohitimisha mjadala wetu wa somo lililopita, Paulo alihoji kuwa Petro alikuwa anaenenda kama mnafiki katika kujitenga na Mataifa. Nilibainisha kwamba Paulo anapaswa (na anatakiwa) kujenga hoja inayojengwa juu ya Biblia. Je, hiyo ndio hoja uliyoahidiwa? Hoja iliyojengwa juu ya Biblia? (Hapana, sio kwa kiasi hicho. Badala yake, Paulo anawaambia Wayahudi kutafakari uelewa wao juu ya tofauti zilizopo kati ya Wayahudi na Mataifa.)
1. Tofauti hiyo ni ipi? (Soma Warumi 2:17-18. Wayahudi walikuwa na uhusiano wa pekee na Mungu. Aliwapa sheria nyingi ili kuyafanya maisha yao kuwa bora zaidi kuliko watu wa Mataifa waliokuwa wakiwazunguka. Wahayudi walikuwa “nuru” miongoni mwa giza la Mataifa.)
2. Licha ya huu uelewa kwamba Wayahudi walipendelewa na sheria na kuwa na uhusiano wa pekee na Mungu, je, Wayahudi walioongoka na kuingia kwenye Ukristo pia wanaonesha nini? (Kwamba hawahesabiwi haki kwa sheria. Badala yake, wanahesabiwa haki kwa njia ya imani katika Yesu.)
a. Je, tunapaswa kuamini jambo hili kwa kuwa tu waongofu wa mwanzo wa Kiyahudi waliamini hivyo?
B. Soma Warumi 2:21-24. Hivi punde tumesoma sehemu ya kwanza ya hoja ya Paulo hapa – kwamba Wayahudi wanapendelewa kwa kupewa sheria na kuwa na uhusiano wa pekee na Mungu. Matokeo ya kuwa na huu uhusiano wa pekee ni yapi? Je, waliishika sheria iliyokuwa mbaraka wa pekee kwao? (Hapana. Badala ya kuwa nuru, hawakumtii Mungu na walimkufuru kwa matendo yao ya dhambi.)
1. Ni jambo gani hilo basi ambalo waongofu wa Kiyahudi walilijua linalopaswa kutufanya tukiri kwamba sheria haituokoi? (Walifahamu kwamba wasingeweza kuishika sheria.)
2. Hebu tusiache jambo hili katika mawazo ya watu tusiowafahamu. Je, unafahamu kwamba mara kwa mara huwa unaivunja sheria? (Kama utajibu kwa uaminifu, basi utasema kuwa (kama ilivyokuwa kwa waongofu wa Kiyahudi wa mwanzo) “ndiyo, ninaivunja sheria mara kwa mara.”)
3. Hebu tupitie tena Wagalatia 2:16. Ukitenda dhambi, je, unaweza “kuhesabiwa haki kwa kuishika sheria?” (Kwa dhahiri, hapana. Paulo haanzi kwa hoja ya kiteolojia, anaanza na uzoefu wa kila mwana na binti wa Adamu na Hawa. “Kwa kuishika sheria hakuna atakayehesabiwa haki.”)
II. Kuhesabiwa Haki Kwa Njia ya Imani
A. Wagalatia 2:15-16 inatumia neno “kuhesabiwa haki” mara kadhaa. Unadhani hiyo inamaanisha nini? (Katika mtazamo wa sheria ya Marekani, inamaanisha kuwa unavunja sheria lakini hauchukuliwi kwamba una hatia. Kwa mfano, mtu anavunja mlango na kuingia nyumbani kwako usiku, na unahofia kwamba mtu huyo atakudhuru. Ukimpiga risasi na kumwua mtu huyo anapokuwa anakukaribia, hicho ndicho sheria inachokiita, “mauaji ya haki.” Kumwua mtu kwa makusudi ni kosa la jinai la kutisha. Lakini, katika mazingira haya mauaji ni ya “haki.”)
1. Umewahi kuusikia msemo “Umeokolewa kutoka dhambini na si katika dhambi zako?” Ikiwa tunahesabiwa haki hata pale tunapotenda dhambi, je, huu msemo ni wa kweli?
B. Soma Wagalatia 2:17. Fikiria muktadha wa sheria ya Marekani niliouelezea hivi punde. Je, sheria hii inakuza na kuhamasisha mauaji? Je, inahafifisha sheria dhidi ya mauaji? (Inayaacha mamlaka ya sheria mahali pake. Inasema tu kwamba katika mazingira fulani, utawala wa sheria unakuzwa kwa kumruhusu mtu kujitetea.)
C. Soma Wagalatia 2:18. Kitu gani “kilibomolewa?” (Tukitumia jambo hili katika mazingira ya Petro, alipogeukia njia zake za kale kwa kujitenga na Mataifa, alifufua sheria (ushikiliaji mno wa sheria) na, matokeo yake, alijihukumu mwenyewe. Ingawa baadhi ya watu wanadhani kuwa sheria imeangamizwa, nadhani ni sahihi zaidi kuhitimisha kwamba adhabu ya sheria “imeangamizwa” tunapookolewa kwa imani.)
D. Soma Wagalatia 2:19. Hii inasema kuwa “naliifia sheria.” Haisemi kuwa sheria “iliangamizwa.” Mkristo “anaifiaje sheria?” (Soma Warumi 6:3-7. Tunapobatizwa, tunakufa pamoja na Yesu, na kufufuka pamoja na Yesu. Tunafahamu kwamba Yesu alikufa kwa sababu ya dhambi zetu. Kwa hiyo, sisi (kwa njia ya Yesu) tumelipa adhabu kwa ajili ya dhambi zetu. Tayari tumeshalipa gharama ambayo sheria inatutaka kufanya hivyo kwa ajili ya dhambi. Sheria “haiangamizwi,” bali si tishio tena kwetu kwa sababu tumeshalipa adhabu kamili ya dhambi kupitia kwa Yesu.)
E. Soma Warumi 7:1-4. Paulo anasema kuwa sisi ni sawa na mke aliyefiwa mume, na hivyo mwanamke huyo yuko huru dhidi ya sheria ya uzinzi. (Soma Warumi 6:1-2 na Warumi 6:5-7. Vifungu hivi vinatuambia kuwa hatutakiwi kuendelea kutenda dhambi. Vinatuambia kuwa “utu wetu wa kale” ulikufa. Namna bora ya kuelewa jambo hili ni kusema kuwa tuliifia adhabu kwa ajili ya uzinzi – pamoja na adhabu kwa ajili ya kutenda dhambi nyingine yoyote ile. Lakini, hatukufa kutokana na uelewa wa kwamba sheria ipo ili kuyafanya maisha yetu kuwa bora. Hatukufa kutokana na uelewa wa kwamba kuishi kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu humpa yeye utukufu.)
F. Soma Wagalatia 2:19-20. Je, mtu anayezini “anaishi kwa ajili ya Mungu?” (Kwa dhahiri kabisa, hapana.)
1. Kristo anaishije ndani yetu? (Hii inarejea suala la Roho Mtakatifu kukaa ndani yetu.)
2. Hebu tutumie mfano. Chukulia kwamba nimesema kuwa ulizifia sheria zote za usalama barabarani. Je, hiyo itakufanya kuwa dereva bora? (Ikiwa ulikuwa umekufa, usingezijua sheria za usalama barabarani. Hivyo, tukichukulia kwamba ungeweza kuendesha ilhali umekufa, basi utakuwa dereva mbaya sana.)
a. Sasa chukulia kwamba mtunzi wa sheria zote za usalama barabarani “anakaa ndani yako.” Je, utakuwa dereva wa namna gani? (Endapo ningekuwa nimejawa na mtu aliyetunga sheria zote za usalama barabarani, basi ningekuwa ninazifahamu kwa ukamilifu. Nisingezitii kwa sababu ninaweza kuandikiwa makosa na kupewa adhabu na polisi. Ningezitii kwa sababu nilifahamu kwamba ziliweka mazingira salama ya uendeshaji. Nadhani hicho ndicho anachokimaanisha Paulo.)
G. Soma Wagalatia 2:21. Mtu anawezaje “kuitenga” neema? (Kwa kudhani kuwa anatakiwa kuishika sheria ili aweze kuokolewa. Kamwe sheria haitatuokoa. Hivyo, ni makosa kuishika sheria kwa kuwa tunadhani ina athari kwenye wokovu wetu. Sio tu kwamba hatuwezi kuishika sheria kikamilifu kutokana na asili yetu ya dhambi, bali kuishika sheria ili tuweze kuokolewa ni kumkashifu Yesu kwa sababu inamaanisha kuwa alikufa bure.)
III. Sheria
A. Tumekuwa tukizungumzia sheria. Nilipokuwa mdogo, nilifundishwa na baadhi ya watu kwamba Paulo anarejea “sheria ya mapokeo,” ikimaanisha sheria zilizoandikwa na Musa zikihusiana na huduma za patakatifu. Ninaposoma “commentaries” za zamani za Biblia, inaonekana kuwa baadhi ya watu walioandika maoni hayo wanaamini kwamba Paulo anamaanisha sheria ya mapokeo. Hivyo, nadhani huu ndio uliokuwa (nadhani hata sasa) uelewa miongoni mwa baadhi ya Wakristo. Utakumbuka jambo mahsusi linaloleta mtafaruku (mkanganyikio) ni tohara. Je, hiyo ni sehemu ya sheria ya mapokeo? (Hapana. Muda mrefu kabla ya huduma ya patakatifu, Mungu alimpa Ibrahamu hii sheria. Mwanzo 17:9-11.)
B. Ikiwa Paulo hazungumzii sheria ya mapokeo peke yake, je, anajumuisha Amri Kumi? (Soma Warumi 7:7-8. Paulo anazungumzia “amri,” na tunaitambua kama Amri ya Kumi. Kutoka 20:17. Paulo anapoandika kuhusu uzinzi na tamaa kwenye mjadala wake wa “sheria,” tunajifunza kwamba anaamini tulizifia Amri Kumi.)
C. Soma Warumi 7:4-5. Tunaweza kudhani kwamba kuiwekea ukomo tafsiri ya Paulo ya “sheria” katika sheria ya mapokeo hutusaidia kuwa na tabia njema. Paulo anazungumzia nini juu ya athari ya sheria kwa tabia njema? (Sheria inaamsha tamaa zetu za dhambi. Unalielewa jambo hili. Mwambie mtu kwamba hatakiwi kutenda jambo fulani, na atataka kulitenda. Hivyo, kuitafsiri sheria kwa mapana (na kisha kusema kwamba tunaifia sheria yote) hutusaidia kuishi maisha bora. Kupitia kwa Yesu, tulilipa adhabu ya kukiuka kila aina ya sheria ya kiroho.)
D. Soma Warumi 7:6. Sasa tunamtumikiaje Mungu? (Kwa kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu!)
E. Rafiki, je, umezipata habari njema hapa? Ulipobatizwa, ulishiriki katika maisha makamilifu ya Yesu na kifo chake kwa ajili ya dhambi zako. Adhabu ya dhambi zako imekwishalipwa. Je, sasa utaishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu? Kwa nini usiombe, sasa hivi, kwa ajili ya msamaha wa dhambi na ujazwe Roho Mtakatifu? Kwa nini usichague kuishi maisha yanayoongozwa na Roho?
IV. Juma lijalo: Imani Katika Agano la Kale.
No comments:
Post a Comment