SOMO : TORATI KUTIMILIZWA NA NEEMA YA KRISTO

 SIKILIZA: INJILI YA MILELE
Karibuni wote katika mfululizo wa masomo haya ya Injili ya Milele, katika somo la nne tuliona uhusiano uliopo kati ya Neema na Amri za Mungu katika maisha ya wokovu. Kwa wale ambao hawajasoma masomo yaliyotangulia (somo la 1 hadi 4), ni vema wafanye hivyo.

Injili ya MILELE ni ujumbe wa marejeo unaowaongoza walimwengu kumcha Mungu (Ufunuo 14:6-7), na kuwatoa katika ukengeufu wa neno la Mungu, unaotokana na Injili za Kisasa kupitia walimu wasiomtii Mungu kama Yesu na mitume walivyotabiri kupitia maandiko haya - 2Timoyheo 4:2-4, Mathayo 7:15-23.

Katika somo hili tunaangalia jinsi NEEMA ya Kristo ilivyotimiliza TORATI, kama Yesu alivyosema, hakuja KUTANGUA TORATI bali KUTIMILIZA. Kama tulivyojifunza katika masomo yaliyotangulia, kusudi la Mungu kwetu ni kutupatia TABIA yake, yaani tufanane naye, tuishi maisha matakatifu. Na tabia ya Mungu ni UPENDO na neno linasema Mungu ni UPENDO - 1Yohana 4:16 "Nasi tumelifahamu PENDO alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni UPENDO, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake".Na kwamba, ni mapenzi ya Mungu tabia yake iwe ndio tabia yetu, na hilo limetimilika kwa NEEMA yake kupitia mwana wake Yesu Kristo kuja kutufia msalabani.

Yohana anasema "Katika hili pendo la Mungu lilionekana, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate UZIMA kwa yeye.Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma mwanae kuwa kipatanisho kwa Dhambi zetu" 1Yohana 4:9-10. Hili linawezekana tu kwa Imani juu ya Neema hii ya Mungu, ambayo hutupatia Mungu kuwa ndani yetu kwa njia ya Roho mtakatifu. 1Yohana 4:13.

Biblia nzima kutoka kitabu cha Mwanzo hadi Ufunuo, inafunua UPENDO wa Mungu kwa Mwanadamu na Uasi juu ya tabia ya Mungu ya Upendo. Na njia pekee aliyoiweka Mungu ya kudhihirisha kuwa tuna tabia ya Mungu au laa, kwa KUTII AMRI zake au Kutotii (KUASI).Yesu alisema - Mkizishika Amri zangu mtakaa katika pendo langu kama mimi nilivyozishika Amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Yohana 15:10.

TORATI (SHERIA) KUTIMILIZWA KATIKA UPENDO
Pambano kuu kati ya Mungu na Shetani ni juu ya tabia au Amri za Mungu. Ni Yesu pekee anayeweza kuifunua tabia ya Mungu kwetu kuipitia Amri zake, ndiyo maana Mafarisayo walishindwa kumwelewa, hadi wakafikia kusema amekuja kuitangua torati. Naye akathibitisha kuwa hakuja kuitangua Torati au manabii, bali KUTIMILZA. Mathayo 5:17-18 "Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie".

Yesu aliitimiza torati na mafundisho ya manabii Kwa kufanya mambo makuu mawili yafuatayo:

1. ALIFUNUA MAHITAJI HALISI YA SHERIA YA UPENDO
Aliifundisha torati au sheria ya Mungu kwa muktadha wa tabia ya Mungu - Upendo. Mafarisayo waliifundisha kwa njia ya Mwili kama makatazo kwa kuwa walitumia akili zao bila kuruhusu Mungu awaongoze. Mfano: Yesu alifundisha Zinaa kutendeka moyoni kwa njia ya Tamaa, Tendo la KUUA kuwa ni matokeo ya moyo wenye Hasira, Visasi na kutosamehe, Sabato (Pumziko) ya Siku ya Saba ya wiki kuwa Siku ya Ibada, Uponyanyi wa Mwili na Roho, kuwa Siku ya watu kuonyesha Upendo kwa kuhudumia wanaoteseka n.k.

kabla ya NEEMA, mafarisayo waliyafundisha na kuyashika kimwili, wakijitahidi kuitiisha miili yao kwa kuongeza sharia zingine za adhabu, mfano: WAZINIFU, WAVUNJA SABATO, WAUAJI - wote kupigwa mawe hadi kufa, hivyo watu walikuwa sio wacha Mungu, bali waliogopa kufanya UASI kwa hofu ya kupigwa mawe. Ni wazi watu hao hawakuwa na tabia ya Mungu katika mioyo yao, hawakuwa na UPENDO wa dhati. Hivyo walihitaji Neema zaidi ili wabadiishwe nia zao na kuwa na Tabia ya Mungu.

2. KUTIMIZA MPANGO WA UKOMBOZI
Tangia mwanzo Mungu aliweka mpango wa ukombozi kwa mwanadamu aliyeanguka dhambini, kupitia kafara ya Mwanakodoo halisi Yesu Kristo - Ufunuo 13:8. Hata hivyo katika Agano la kale kabla ya Kristo kuja duniani, Mungu alitoa mpango mbadala wa wanadamu kupatanishwa na Mungu, ulikuwa ni wa kutoa Kafara za wanyama, huduma hizo zilikuwa zinaambatana na matoleo ya vyakula na vinywaji. Hayo yalikuwa ni kivuli, yalilenga kifo cha Yesu pale msalabani.

Yesu Kristo alitimiza hitaji la torati juu ya Ukombozi, sheria zote zilizokuwa zikiambatana na huduma za Upatanisho kupitia kafara za wanyama, zilikamilishwa na huduma halisi ya Kristo.... Sheria hizo za kafara zilitimizwa, hazikuondolewa kwa kutohitajika bali sheria zilitimizwa. Kupitia kafara ya Kristo, tunakamilishwa, tunasafishwa dhambi, tunapewa moyo wa nyama, unaoweza kupokea Amri za Mungu kwa moyo wa furaha na Upendo.

Mafarisayo walimtega Yesu wakitaka kumshika uongo, kama kweli anaifundisha Torati au laa, mwanasheria mmoja akamuuliza - "Mwalimu, katika torati ni Amri ipi iliyo kuu?. Akawaambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa Roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo Amri iliyo kuu tena ni ya Kwnaza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika Amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii". Wakanyamaza kimya, ndipo Yesu akaendelea kuwafundisha zaidi juu ya kazi yake aliyotumwa kuifanya.

WITO:
Ujumbe huu ni kwa ajili yetu sote, ili tuweze kukua kiroho, na kufanya matengenezo, kwa kadri tunavyoangaziwa nuru. Kumbuka tunaishi katika kizazi kilichoathiriwa na mapokeo ambayo yamepofusha akili za watu kwa hadithi za kutungwa ili wote wahukumiwe kwa kutotii maagizo ya Mungu.

Wewe ni shahidi, leo kuna Injili nyingi na zenye mafundisho yanayokinzana na Amri za Mungu, kinyume na mafundisho ya Kristo. Lakini pia wegi wako nje ya Neema ya Kristo, wakiukataa wokovu halisi, wakijitahidi kutii kwa nguvu zao, na kujikuta wakiangukia katika utumwa wa Dhambi kila iitwapo leo.

MUNGU AKUBARIKI UNAPOFUNGUA MOYO WAKO NA KURUHUSU ROHO MTAKATIFU AENDELEE KUTAKASA KWA NENO LA MUNGU.

Na. Ev. Eliezer Mwangosi
Simu: 0767210299 - Kwa ajili ya Maswali, ushauri na Maombi.

Wasambazie wengine ujumbe huu wa matengenezo.

No comments:

Post a Comment