NENO LA LEO - VITABU VILIVYOCHANIKA.

Hebu tafakari muundo wa kitabu imara, utakuta kuna "Hard Covers" juu na chini, na zimeungana huwezi ona maungio. Halafu karatasi za ndani zenyewe ni laini, lakini nazo zimeshikiliwa na hizo hard cover kwa kutumia Gundi isiyobanduka. Ikitokea, cover (jarada) moja limechanika, utakuta kitabu kizima kinasambaratika, makaratasi yanaanza kutoka hata kwa upepo.

Mfano huo wa kitabu ni sawa na Ndoa inayounda familia. Baba na Mama ni Majarada (Hard Cover), na watoto ni sawa na Makaratasi ya Ndani ya Kitabu. Mungu anafanya kazi kama GUNDI ambayo ndiyo inaunganisha Majarada na kuyafanya yawe Imara na hatimaye kuyashikiria makaratasi. Mungu anapokosekana kati wa wanandoa, makusudi ya Mungu juu ya Ndoa yanapotea. Yesu alisema maneno Haya.

Marko 10:7-9 "Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.

Mishale mingi yenye sumu za kujeruhi na hata kuua inaelekezwa katika Ndoa na hatimaye familia. Na muasisi wa mashambulizi hayo ni Adui mkuu Shetani, ambaye anapinga mpango wa Mungu aliyeasisi Ndoa pale edeni, na kuifanya sehemu ya kuudhihirisha Upendo wake, ni sehemu yenye usalama, ni sehemu ya furaha na Amani. Kwa bahati mbaya sana Ndoa nyingi zimegeuka kuwa sehemu za kujeruhiwa mioyo.

Ndoa nyingi zimebeba sura za vitabu vilivyochanika, vingine vibaki na jarada moja, na makaratasi ya ndani (watoto), yamechanika na kupeperushwa na kila upepo, kama ilivyo kwa kitabu Gundi ikitoka, ndivyo ilivyo kwa Ndoa Mungu asipokuwa kati yao. Shetani atarusha kila aina ya mishale na kuhakikisha amesambaratisha na kuleta MAJERAHA.

Neno la leo, linamkumbusha kila mmoja anayeanzisha mahusiano, kuunganishwa na Mungu, kama unapenda mahusiano yenu yadumu, omba sana kila mmoja wenu aunganishwe na Mungu, HUU NI WAJIBU WA KILA MMOJA, Kwani mmoja akiachia Kitabu, mahusiano yamesambaratika.

Je kitabu chako kina sura gani? Kama kimeshachanika, usikate tamaa, unganisha moyo wako na Mungu, utakuwa salaama hata kama uko peke yako. Kama majarada au makaratasi ya kitabu yamechakaa, kila mmoja ana wajibu wa kuunganishwa upya na Mungu, ataimarisha mahusiano kama mwanzo.

KUUNA FAMILIA BILA MUNGU NI SAWA NA KITABU KILICHOCHANIKA.

NAWATAKIA SIKU NJEMA YENYE MIANZO MIPYA YA MAFANIKIO.

Na Ev. Eliezer Mwangosi - 0767 210 299
 

No comments:

Post a Comment