Somo La 3 | Wafalme Watano wa Mwisho wa Yuda

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Mambo ya Nyakati 34-36, Yeremia 22, 2 Wafalme 24)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Tumejifunza kwamba Yeremia alitumia muda wa miaka aroaini kuionya Yuda kuhusu uangamivu unaokaribia. Katika kipindi hicho cha miaka arobaini, wafalme watano waliitawala Yuda. Je, wote walikuwa wabaya? Kwa nini walipuuzia maonyo ya Mungu? Tunaweza kujifunza nini kutoka kwao? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuvumbue zaidi!

I.                   Yosia
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 34:1-2. “Daudi” anayerejewa hapa ni Mfalme Daudi. Je, yeye ndiye baba yake Yosia? (Soma 2 Wafalme 21:25-26. Baba halisi wa Yosia alikuwa Mfalme Amoni.)
1.                  Soma 2 Wafalme 21:19-24. Amoni alikuwa mfalme mbaya kwa kiwango gani? (Alikuwa mbaya sana kiasi kwamba watumishi wake waliamua kumwua.)
a.                   Je, Yosia alikuwa na babu mcha Mungu? (Hapana. Mafungu haya yanasema kuwa Manase, babu yake, pia alitenda uovu.)
1.                  Kwanini basi tunaambiwa kuwa baba yake Yosia alikuwa Mfalme Daudi? (“Baba” maana yake ni mhenga/babu. Yosia “alienenda katika njia” za babu yake Mfalme Daudi. Inamaanisha alikuwa mtu mwema.)
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 34:3-5. Juma hili nilifahamu kwamba ISIS ilibomoa Hekalu la Bel (Temple Bel) ambalo lina umri wa maelfu ya miaka. Je, hilo ni jambo jema? (Yosia anaangamiza sanamu ambazo zinaabudiwa kwa sasa. Huu sio uangamizaji wa michoro ya kale.)
1.                  Tunaweza kufanya jambo gani leo lenye kufanana na kazi ya Yosia? (Sisi si wafalme, hivyo kuangamiza mali za watu wengine inaweza kuleta tatizo la kimaadili. Lakini, katika familia zetu wenyewe tunapaswa kutenda kazi ya kukomesha ushawishi wa uovu.)
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 34:8. Tunaweza kufanya jambo gani lenye kufanana na kazi ya Yosia ya kufanya ukarabati? (Tunaweza kuhakikisha kuwa jengo la kanisa letu lipo katika hali nzuri. Jambo la muhimu zaidi ni kwamba, tunaweza kuihamasisha familia yetu kumwabudu Mungu.)
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 34:14-15. Wakati wanakarabati hekalu, Kuhani Mkuu Hilkia “alikiona” “Kitabu cha Torati” ambacho “kilitolewa kwa mkono wa Musa.” Je, huu ukweli mpya unahusianaje na kuabudu sanamu? (Kutokusoma Biblia, kusahau neno la Mungu, hutusogeza mbali na kutufanya tusimtegemee Mungu.)
1.                  Fikiria jinsi huu uvumbuzi unavyoweza kubadili maisha ya watu wa Mungu?
1.                  Je, unaweza kufikiria tukio lenye kufanana na hilo maishani mwako? (Kusoma Biblia usiyoweza kuielewa ni sawa na tatizo la “Biblia iliyofichwa.” Tafuta toleo la Biblia unaloweza kulisoma kwa urahisi na kuielewa. Utalifahamu neno la Mungu!)
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 34:29-32. Matokeo ya kazi ya Yosia ni yapi? (Sasa neno la Mungu linajulikana kwa kila mtu katika ufalme wake. Chini ya uongozi wake, watu wanaahidi kumfuata Mungu.)
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 35:20-21. Unayachukuliaje madai ya Farao Neko kwamba Mungu yuko upande wake?
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 35:22. Hii inaashiria nini kuhusu uthabiti wa kile alichokisema Farao Neko?
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 35:23-24. Hili lilikuwa janga baya na mwisho wa utawala wa mtu mkuu wa Mungu. Je, unajifunza nini katika jambo hili? (Tunatakiwa kuwa na uhakika kwamba tunayafuata mapenzi ya Mungu. Baadhi ya watoa maoni wanadhani kuwa Yosia alikuwa anatenda jambo sahihi. Sina uhakika kama tuna uthibitisho wa kutosha kuweza kufikia uamuzi sahihi.)
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 35:25-26. Bila kujali sifa njema ya uamuzi wa hatari wa mwisho wa Yosia, tunaona kwamba anaombolezwa kama mtu aliyejitoa kwa Mungu kikamilifu. Utakumbuka kwamba tulianza kwa kumwangalia Yosia, tukajifunza kuwa alienenda katika njia ya Mfalme Daudi. Je, tumejifunza nini sasa hivi kinachotusaidia kuuelewa huo ukweli? (Daudi hakufanya maamuzi sahihi mara zote. Lakini pamoja na hayo Mungu alifurahia kujitoa kwake kwa Mungu.)
I.                   Yehoahazi na Yehoyakimu
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 36:1-3.  Yehoahazi alitawala kama mfalme kwa muda wa miezi mitatu. Ni kwa vipi matendo ya baba yake, Yosia, ambaye alikuwa mtu mkuu, yaliathiri maisha yake? (Uamuzi wa mwisho wa Yosia ulisababisha mwanaye maarufu aliyechaguliwa kuanguka katika utawala wake.)
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 36:4. Kwa nini Neko alibadili jina la Eliakimu na kumwita Yehoyakimu? (Ili kuonesha mamlaka yake juu ya huyu Mfalme mpya wa Yuda.)
1.                  Unadhani kwa nini Neko alimweka Yehoyakimu madarakani? (Kwa dhahihi alimchukulia kuwa msikivu zaidi kuliko Yehoahazi, chaguo la watu.)
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 36:5-6. Yehoyakimu ni mfalme wa namna gani? (Mwovu.)
1.                  Jambo gani lilimtokea? (Anakamatwa na Nebukadreza.)
1.                  Unadhani Yehoyakimu alimtegemea nani ili kuukomboa ufalme wake? (Soma 2 Wafalme 24:7. Inaonekana kuwa ni Misri! Kuwategemea wanadamu badala ya kumtegemea Mungu, ni wazo la kipumbavu. Angalia pia 2 Wafalme 24:1.)
I.                   Yekonia
A.                Soma 2 Wafalme 24:6 na 2 Wafalme 24:8-9. Mfalme huyu alitawala kwa muda gani? (Miezi mitatu!)
1.                  Yekonia alikuwa mfalme wa namna gani? (Naye alikuwa mtu mbaya – katika kipindi chake cha miezi mitatu!)
1.                  Je, kweli hiki ni kipimo cha haki kwa mtu mwenye umri wa miaka 18?
A.                Soma 2 Wafalme 24:10-12. Jambo gani lilihitimisha utawala wa Yekonia? (Yuda ilivamiwa na Babeli.)
A.                Soma 2 Wafalme 24:13-17. Je, haya ni maafa makubwa kiasi gani kwa Yuda?
1.                  Utakumbuka nilikwambia utafakari endapo kipindi cha miezi mitatu kilitosheleza kusema kwamba Yekonia alikuwa mtu mbaya? Nani aliyechukuliwa Babeli safari hii? (Sura ya kwanza ya kitabu cha Danieli inabainisha kuwa Danieli na marafiki zake ndio waliochukuliwa. Mara moja Danieli na marafiki zake waliamua kuchukua msimamo na kuwa upande wa Mungu.)
A.                Soma Yeremia 22:1-5. Ni jambo gani ambalo hawa wafalme waovu walilitenda kiasi cha kubadili mambo kwa Yuda?
1.                  Hebu tujikite kwenye Yeremia 22:3. Mambo ya jumla ya mfumo wa haki kushindwa kufanya kazi katika Yuda ni yapi? (Kwamba walio wanyonge, wale waliotekwa, wageni, yatima na wajane ndio waathirika wa machafuko na vitendo visivyo vya haki. Sheria inapoparanganyika, watu waliopo katika mazingira hatarishi wanateseka.)
a.                   Je, tunaona tatizo gani jingine katika Yeremia 22:3? (Watu wasio na hatia wanauawa.)
1.                  Hebu tutafakari jambo hili. Mungu anaadhibuje anguko la namna hii ili kutenda haki? (Mungu analeta mataifa yenye nguvu ili kuiteka nyara Yuda. Viongozi wa Yuda wanapitia uzoefu ule ule walioutumia kuwatesa wale waliokuwa wanyonge.)
1.                  Mojawapo ya swali nililouliza kwenye utangulizi ni kwamba kwa nini wafalme hawa hawakubadilika? Wafalme waovu walikuwa na sababu gani kuruhusu mfumo wa utoaji haki uliojaa rushwa? (Bila shaka walinufaika au walidhani wangenufaika kutokana na huo mfumo.)
A.                Soma Yeremia 22:8-9. Hii inahusianaje na kuwadhuru watu wasio na nguvu? (Ni kinyume na agano la Mungu. Kinyume na torati ya Musa. Unapoabudu mungu (miungu) unakuwa umeyafanya mawazo yako yafifie.)
I.                   Sedekia
A.                Soma tena 2 Wafalme 24:16-17 na usome 2 Mambo ya Nyakati 36:11-12. Sedekia ni mfalme wa namna gani? (Kwa mara nyingine, ni mfalme mbaya.)
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 36:13. Endapo utatakiwa kumwelezea Sedekia kwa kutumia neno moja, je, neno hilo litakuwa neno gani? (Mwasi. Hakulikubali neno la Mungu kupitia kwa Yeremia na alimwasi Nebukadreza.)
1.                  Jiweke kwenye nafasi ya Sedekia. Unaweza kuelezea jambo hili? (Nahisi alidhani kwamba Mungu hakuwa wa msaada, Yeremia hakuwa na usawa, na Nebukadreza alikuwa adui. Yeye pamoja na watu wangefanya kile walichokitaka kwa sababu mambo yasingekuwa mabaya sana.)
1.                  Pamoja na kuwa mwasi, jambo gani jingine linaielezea aina hii ya fikra? (Yeye ni mtu mwenye kiburi na kujisifu na haangalii uhalisia. Kulipuuzia neno la Mungu lililotoka kwa Yeremia lilisababisha machungu yote. Nebukadreza alimpondaponda kama mdudu.)
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 36:15-19. Matokeo ya huu uasi wote kwa Mungu ni yapi? (Uangamivu mkuu.)
A.                Soma 2 Mambo ya Nyakati 36:21. Nchi ilipumzika dhidi ya nini? (Uovu.)
A.                Rafiki, chunguza mtazamo wako.  Je, wewe ni mwasi au ni mtu ambaye anataka kumsikiliza Mungu na kuyatenda mapenzi yake? Kwa nini usiamue sasa hivi, kuyatafuta na kuyafuata mapenzi ya Mungu?

I.                   Juma lijalo: Karipio na Adhabu.

No comments:

Post a Comment