Ayubu
20:12-13, 27. "Ingawa uovu una tamu kinywani mwake, ingawa auficha chini
ya ulimi wake, Ingawa auhurumia, asikubali kuuacha uende zake, lakini
akaushika vivyo kinywani mwake;.......... Mbingu zitafunua wazi uovu
wake, nayo nchi itainuka kinyume chake".
Sitasahau
mkasa uliomtokea dada mmoja aliyekuwa anatembea na mume wa mtu kwa muda
mrefu, siku arobaini zilipofika, saa nane ya usiku wakiwa katikati ya
tendo la kuvunja amri ya Mungu ya Usizini, walivamiwa na majambazi
nyumbani kwa binti, katika purukushani za kujiokoa mwanaume akapigwa
risasi ya kichwa na hatimaye mauti, na binti akavunjwa mguu kwa risasi.
Japo
huyo binti alifanikiwa kuitunza hiyo siri kwa miaka mingi, akidumu
kuihujumu ndoa ya watu, kwa kuuficha utamu wa mapenzi chini ya ulimi
wake, siku ikafika neno la Mungu likatimia, Mbingu zikaufunua uovu
wake, mume wa mtu kauwawa uchi wa mnyama kitandani pake, na yeye
kujikuta hospitali alikopelekwa bila kujitambua akiwa na mguu
uliovunjika unaosubiri kukatwa.
Hata
leo hii, kuna wengi wanaosoma ujumbe huu wakiwa katika mtego huu wa
kuvinjari katika UOVU fulani kwa siri, wengine wamejiegesha kwa waume za
watu, wengine kwa wake za watu, wengine ni wezi wa wachumba za watu,
wengine kazi yao ni kudanganya na kuharibu mabinti na kuwabwaga, na
majimama kuwaharibu vijana wa kiume kwa siri wakitumia mali zao.
Rafiki
hakuna uovu unaotendeka kwa siri utakaomshinda Mungu asiufunue, ukiona
umefanikiwa, ujue Mungu anakuvutia muda ili UTUBU na Kuacha haraka,
kabla hajaruhusu dhoruba itakayokuaibisha milele, iwe ni Ufisadi,
uchonganishi, udokozi, unaruka ukuta kwenda kuzungurusha viuno kweye
muziki wa dansi, unaua vitoto kwa kutoa mimba, ni mla rushwa au mtoa
rushwa, iwe ya pesa au ya ngono nk, ACHA kabla neno la leo halijatimia
au KABLA YA MTEGO KUFYATUKA NA KUKUNASA.
Kumbuka
Mwana wa Mungu alikuja duniani, na hatimaye kufa msalabani, ili
kutukomboa kutoka katika kila mitego (dhambi), na kutuhakikishia uhuru
baada kusamehewa makosa tuliyotenda. Huu ni wakati wa kushinda kwani
hakuna ajuae ya Kesho.
NEEMA YA MUNGU IZIDI KUOGOZA NAFSI ZETU KATIKA USHINDI DAIMA - NAWATAKIA SIKU NJEMA.
Na Ev Eliezer Mwangosi.
Kwa mawasiliano zaidi na ushauri au maswali tumia: 0767210299, eliezer.mwangosi@yahoo.com.
No comments:
Post a Comment