(Esta 1-8)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Yumkini maisha yako hayakujengwa juu ya tukio
moja kubwa ambalo unaweza kulitumia kuzuia maangamizi makubwa. Yumkini zaidi ni
kwamba, maisha yako ni mkusanyiko wa maamuzi madogo-madogo kuhusu mambo sahihi
na yasiyo sahihi. Je, jinsi unavyofanya maamuzi katika mambo madogo madogo
maishani ni kielelezo cha jinsi utakavyofanya maamuzi makubwa maishani? Ikiwa
utashindwa kufanya maamuzi katika mambo madogo, je, kitendo hiki
kitakulazimisha kufanya maamuzi makubwa na magumu zaidi? Hebu tuchimbue kisa
cha Esta kinachofahamika sana na tukiangalie kwa namna tofauti!
I.
Utangulizi
A.
Soma Esta 1:1-5. Ufalme wa Ahasuero una ukubwa gani?
(“Kushi” ni sehemu ya kaskazini ya Misri, kwa hiyo alitawala kuanzia India hadi
Misri!)
1.
Je, Ahasuero ni mtu anayependa karamu? Au, je, unadhani
karamu hii ina malengo mengine? (Hii ni karamu kubwa, lakini nadhani Ahasuero
alifanya karamu hii kwa sehemu fulani ili kuimarisha utawala wake kwa kuonana
ana kwa ana na viongozi ambao alikuwa haonani nao mara kwa mara. Anathibitisha
tena kwamba yeye ni mtawala.)
B.
Soma Esta 1:6-8. Kundi hili lina utulivu wa kiasi gani?
(Unaweza kunywa kwa kadri uwezavyo-vinywaji vilitolewa bure!)
II.
Vashti
A.
Soma Esta 1:9. Fungu hili linazungumzia nini kuhusu
wajibu wa wanawake katika Ufalme wa Ahasuero?
B.
Soma Esta 1:10-12. Hali ya utulivu wa Mfalme ikoje?
(“Amefurahiwa moyo.” Utabiri wangu ni kwamba wanaume wote walikuwa wamekunywa
divai nyingi.)
1.
Malkia anapaswa kuvaa nini? (Taji yake ya kifalme.
Utakumbuka kwamba Ahasuero alikuwa akionesha vitu vyake, sasa anataka kuonesha
taji ya mke wake pamoja na mkewe.)
2.
Amevaa kitu gani kingine? (Maoni ya Adam Clarke
yanabainisha kwamba tofauti na taji yake, alitakiwa kuwa uchi. Maoni ya watu
wengine hayakubaliani na jambo hilo. Fungu linasema kuwa Mfalme alitaka
“kuonesha uzuri wake.” Malkia Vashti anatambua kwamba kutokutii ni jambo baya,
lakini anakaidi. Maoni ya watu wengi yanaashiria kwamba hakutaka kuoneshwa
mbele ya kundi la wanaume. Utagundua kwamba hadi kufikia hatua hii kundi hili
la watu lilijumuisha watu wa kawaida. Walevi wa kawaida ndio wanaoweza kuwa
tatizo. Bila kujali hali halisi iliyokuwepo, inaonekana Vashti alifikiria
kwamba atanyanyasika kwa namna fulani.)
C.
Soma Esta 1:13-15. Tatizo halisi la Ahasuero ni lipi?
(Kwa sehemu kubwa anaandaa karamu ili kudhihirisha uwezo na mamlaka yake. Sasa,
mkewe hawi mtiifu kwake!)
D.
Soma Esta 1:19-22. Hii inasema nini kuwahusu wanaume?
(Mtu yeyote, hata wanaume, wanadhani kwamba “[sasa] wanawake wote watawaheshimu
waume zao?” (Utabiri wangu ni kwamba ikiwa Ahasuero alitaka Vashti atokee mbele
za watu akiwa amevaa taji yake pekee, kwa sasa yeye ndiye shujaa wa wanawake
wote, na heshima kwa wanaume imeshuka, na si kuongezeka.)
III.
Esta
A.
Soma Esta 2:2-7. Ni kwa jinsi gani Mordekai
anafananishwa na Danieli na rafiki zake? (Wao ni mateka kutoka Yerusalemu.)
1.
Esta ameishi maisha ya namna gani hadi kufikia hapa?
(Wazazi wake wote wamefariki. Yeye ni binti wa watu walio uhamishoni.
Hayaonekani kuwa maisha mazuri.)
B.
Soma Esta 2:8-10. Utagundua kwamba yeye (Esta), kama
ilivyokuwa kwa Danieli, alipewa “chakula maalumu.” Je, Esta na Mordekai hawana
viwango vya juu kama vya Danieli?
1.
Kwa nini Mordekai amemzuia Esta asidhihirishe kwamba
yeye ni Myahudi?
2.
Ikiwa Esta, kama ilivyokuwa kwa Danieli, angekuwa na
msimamo wa kukataa chakula, je, kitendo hicho kingedhihirisha kwamba alikuwa
Myahudi?
3.
Je, ni vyema kwa Esta kukubali ushauri wa Mordekai?
C.
Soma Esta 2:12 na Esta 2:15-17. Je, Esta anatenda
dhambi kwa kulala na Mfalme? (Esta hakuanzisha mfumo. Alipolala na Mfalme
alifanyika kuwa mkewe (au angalao suria/hawara yake). Endapo mambo yangetendeka
kama ilivyokuwa kwa wengine wengi, kamwe asingemwona Mfalme tena na yatima huyu
angekabiliana na maisha ya kuishi katika nyumba ya harimu ya Mfalme.)
1.
Badala ya kuwa suria/hawara, jambo gani linamtokea
Esta? (Anavikwa taji na kuwa Malkia!)
D.
Soma Esta 2:20. Kwa nini kisa hiki kinaendelea
kubainisha jambo hili? Je, Esta anaishi maisha ya udanganyifu? (Ahasuero
hakumwoa kutokana na historia ya familia yake. inaonekana jambo hilo
halikujitokeza, na hana haja nalo. Esta anaheshimu ushauri wa mtu (mwanaume)
aliyemuasili kuwa kama binti yake.)
IV.
Njama
A.
Soma Esta 2:21-23. Esta anampa sifa njema Mordekai. Je,
ingekuwa na manufaa kwake endapo angejipatia sifa yeye mwenyewe?
B.
Soma Esta 3:1-2. Kwa nini Mordekai alikataa? (Soma Esta
3:3-4. Jibu la Mordekai ni kwamba yeye ni Myahudi – kwa hiyo alikuwa na sababu
za kidini kwa kutoinama na kumsujudia Hamani.)
1.
Soma Kutoka 20:4-5. Je, kanuni hii ndio inayotumika?
2.
Unakumbuka majuma matatu yaliyopita tulipojifunza
habari za Naamani? Soma 2 Wafalme 5:18-19. Kwa nini jambo hili ni sahihi kwa
Naamani, lakini sio sahihi kwa Mordekai?
3.
Soma Warumi 14:22-23. Endapo una muda wa kutosha, soma
sura yote ya 14 ya kitabu cha Warumi. Tunapokuwa na mambo “yenye mashaka (yenye
kuzua mjadala)” (Warumi 14:1), Biblia inatuambia kuwa dhamiri zetu ndio
mwongozo wetu.)
a.
Je, hii ndio sababu Danieli anapingana na chakula
chake, lakini Esta hafanyi hivyo?
b.
Je, kumwinamia na Kumsujudia Hamani ni “jambo lenye
mashaka?” (Hamani si mungu. Tunaye Namani anayemwinamia mtu ambaye kwa dhahiri
ni mungu, kwa hiyo katika suala la Mordekai linaonekana kuwa ni jambo lenye
mashaka.)
C.
Soma Esta 3:5-6. Hamani ni mtu wa namna gani?
D.
Soma Esta 3:8-11. Majivuno ya Hamani yanamgharimu
talanta 10,000 za fedha. Kwa nini mfalme anamwambia atunze fedha zake?
(Ahasuero anamwamini Hamani. Anadhani kuwa anatenda jambo sahihi.)
1.
Endapo Esta asingekaa kimya kuwa yeye kuwa Myahudi, je,
mgogoro huu ungeibuka?
a.
Endapo angesimama imara katika suala la chakula, je,
angeepusha huu mtafaruku mkubwa?
E.
Soma Esta 3:12-14. Je, Hamani atapata matatizo kuwaua
Wayahudi katika siku iliyokubalika? (Mali yao yote itachukuliwa! Huu ni
urasimishaji wa utawala huria (kutokuwepo kwa serikali)! Siku ya mauaji ya
wezi! Sasa tunafahamu sababu ya Hamani kuweza kutunza fedha zake.)
F.
Soma Esta 4:1-3. Nani anawajibika kwa maangamizi
yanayotazamiwa ya Wayahudi?
1.
Tumejadili maelekezo ya Mordekai kwa Esta kuficha
kwamba alikuwa Myahudi. Endapo uamuzi wake wa kukataa kuinama na kumsujudu
Hamani ni wa “mashaka,” je, Mordeki amewaua watu wake pasipo na sababu ya
msingi?
V.
Wokovu
A.
Soma Esta 4:5-11. Jambo gani linamsikitisha Esta?
B.
Soma Esta 4:12-14. Mordekai anajenga hoja gani, na
unazichukuliaje hoja hizo? (Hoja yake ya kwanza ni kwamba pamoja na yote naye
atakufa. Hoja yake ya pili ni kwamba mgogoro huu ndio sababu ya Mungu kumfanya
yeye kuwa Malkia. Ninaipenda hoja ya pili zaidi.)
1.
Kwa kuwa Mordekai alimwambia afanye siri suala la
kabila lake, je, hoja ya kwanza ni tishio halali?
C.
Soma Esta 4:15-16. Sasa tumefikia mahali ambapo Esta
anampa Mordekai maelekezo, na si vinginevyo. Je, jibu lake ni lipi katika
mgogoro huu? (Maombi na kufunga.)
D.
Soma Esta 5:1-8. Niambie kile unachodhani kinaendelea
mawazoni mwa Ahasuero? Malkia wake mpya anahatarisha maisha yake kumwomba ale
naye chakula cha jioni, na kasha hamwambii kile anachokitaka.
E.
Soma Esta 5:9-14. Je, tunapaswa mara zote kufuata
ushauri wa wake zetu?
F.
Katika Esta 6:1-5 Ahasuero anakumbushwa kwamba Modekai
aliyaokoa maisha yake na kamwe hakupewa tuzo. Hebu tuendelee kwa kusoma Esta
6:6-12. Asubuhi ile haikuwa kama ilivyotarajiwa! Je, umewahi kuwa na siku kama
hizo?
G.
Soma Esta 6:12-14. Zereshi pamoja na washauri
wanafahamu kwamba Mordekai ni Myahudi. Je, unaweza kuielezeaje hofu hii? (Roho
Mtakatifu anazungumza nao.)
H.
Soma Esta 7:3-9, Esta 8:3-4 na Esta 8:7-8 na Esta 8:11.
Je, hivi ndivyo ambavyo ulimwengu unapaswa kutenda kazi? Tumefikiaje hatua hii?
(Esta alionesha ujasiri, aliomba, na Mungu alimpatia mpango mkuu.)
I.
Soma Esta 8:16-17. Je, hii ni jitihada ya kimisionari?
1.
Unaichukuliaje nia ya uongofu?
J.
Rafiki, kwangu mimi ninaona kwamba endapo Esta
angeenenda kama Danieli, mgogoro mkubwa ungeweza kuzuiwa. Habari njema ni hii:
Esta alifanya uamuzi sahihi wakati maisha ya maelfu ya watu yalipokuwa
hatarini. Mungu aliheshimu kitendo hicho na kuwalinda watu wake. Je,
utadhamiria leo kufuata mapenzi ya Mungu, hata kama yumkini umekuwa humheshimu
Mungu katika siku za nyuma?
VI. Juma lijalo: Yesu: Bwana wa Utume.
No comments:
Post a Comment