SABATO KATIKA BIBLIA NA HISTORIA

Sehemu ya Tatu: Sabato kama siku ya Ibada katika Kanisa la Yerusalem hadi kufikia mwaka 70AD
Kabla hatuajaanza kuangalia mwanzo wa ibada katika siku ya kwanza ya juma, nimeona hapa nilete ushahidi mwingine kuonyesha kwamba, Wakristo waliokuwa wakiishi Yerusalem, ambako ndipo palikuwa makao makuu ya Kanisa la Kikristo Enzi za Mitume, hadi kufikia katika Mwaka wa 70AD walikuwa wakitunza Sabato kama siku yao ya Ibada.
Katika Kitabu cha Mathayo 24 tunapata unabii wa Yesu juu ya kurudi kwake na dalili za Mwisho wa dunia. Katika aya ya 1-2 Tunapata maelezo haya “Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea, ili kumwonyesha majengo ya hekalu. Naye akajibu akawaambia, hamyaoni haya yote? Amin , nawaambieni. Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa”. Kwa wanafunzi wa Yesu kubomolewa kwa hekalu kungemaanisha mwisho wa dunia, maana kwao kama ilivyokuwa kwa Wayahudi wote, wasingetarajia hekalu hilo kubomolewa. Ndipo wakamuuliza, “tuambie, mambo haya yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? Naye Yesu katika kujibu kwake, akawaleza wanafunzi wake mambo ambayo yangejili kuanzia kuangushwa huko kwa hekalu hadi mwisho wa dunia kama walivyohitaji kujua.
Lengo letu hapa tunataka kutupia macho mstari wa 16-20. Kuhusiana na unabi huu, Yesu anaeleza na kuwatahadharisha wanafunzi wake kuwa, kuna wakati huko mbele Yerusalem ingevamiwa na majeshi maadui, ambao wangeubomoa mji na hekalu, kiasi kwamba halitasalia jiwe juu ya jiwe. Lakini Yesu anawatahadharisha juu ya uvamizi huo, na akiwataka wale ambao wangekuwa waaminifu kiasi cha kutunza neno lake wapate kujisalimisha. Ndipo akasema “Basi wale walioko Uyahudi wakimbilie milimani. Ye yote aliyeko juu ya paa la nyumba asishuke ili kuchukua cho chote kutoka ndani ya nyumba. Yeye aliye shambani na asirudi nyumbani kwenda kuchukua vazi lake. Ole wa wenye mimba na wenye watoto wachanga siku hizo!”
Historia inaonysha kuwa tukio la kuangushwa kwa muji wa Yerusalemu lilitukia katika mwaka wa 70AD. Huu ni wakati ambapo Jemedali Tito wa majeshi ya kirumi alivamia na kuuzingila Yerusaleme toka mwaka 66. Katika Luka 21:20-22 Yesu alikuwa ametoa dalili za tukio hilo ambazo zingesaidia wanafunzi wake kujiepusha. Yesu anaasema, “Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi fahamuni kwamba kuharibiwa kwake kumekaribia. 21Wakati huo, wale walio Uyahudi wakimbilie milimani, walio mjini Yerusalemu watoke humo na wale walioko mashambani wasiingie mjini. 22Kwa sababu huu utakuwa ni wakati wa adhabu ili kutimiza yaliyoandikwa.
Katika wakati huo wa kuharibiwa kwa mji wa Yesusalemu, Yesu alitarajia kwamba wanafunzi wake wangekuwa bado wanatunza Sabato na ndipo anawatahadharisha akisema “Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi au siku ya Sabato.” Mathayo 24:20. Kwanini kukimbia kwao kwa ajili ya kujisalimisha kusiwe siku ya sabato? Kwa sababu katika siku hiyo wangekuwa ibadani nao wangekamatwa kama Wayahudi wengine wasiotii neno lake. Pia kwao ni siku takatifu ya ibada siyo siku ya kukimbia na mizigo ili kujisalimisha. Hivyo twaona kwamba, Yesu hakutarajia kabisha kwamba ingekuja kuzuka siku nyingine ya ibada, tofauti na siku ya Sabato.
USHAHIDI WA KIHISTORIA KUONYESHA KUWA KANISA LA YERUSALEMU LILIENDELEA KUTUNZA SABATO HATA BAADA YA MWAKA 70AD
Wanahistoria, Eusebius(260-340AD) na Epiphanius(315-403) wanatueleza kuwa hadi kufikia wakati wa uvamizi wa Mfalme Hadrian wa Rumi mwaka 135, (Huu ni uvamizi mwingine tofauti na ule wa Tito katika 70AD) Kanisa la Yerusalemu lilikuwa likiongozwa na Wayahudi walioongoka. Kundi moja la kidini la wayahudi hao walijulikana kama Ebionites, hawa walikuwa washika dini wakisisitiza utunzaji wa amri kumi za Mungu, ikiwemo na Sabato. Wengine ni kundi la Wanazarayo (Nazarenes), ambao nao husisitiza juu ya utunzaji wa amri za Mungu na kuabudu katika siku ya Sabato. Eiphanius anasema “Wanazarayo (Nazarenes) wanawakilisha kanisa la Asili kabisa la Yerusalemu (Tazama ecclesiastic History Vol 3. Pg 23)
Jambo lingine linalotuonyesha kwamba Wakristo wa Yerusalemu waliendelea kutunza Sabato ni “Laana kwa Wakristo” Iliyokuwa ikitolewa na Marabi wa Kiyahudi katika mwaka 80-90AD katika maombi yao ya kila siku. Hii ilikuwa imekusudiwa kuwazuia Wakristo kufaya Ibada zao katika Masinagogi. Hivyo yaonyesha kwamba Wakristo wengi bado Walijihesabu kwamba wao nao ni sehemu ya Wayahudi na hivyokushiriki katika Shughuli na Ibada katika hekalu, ikiwa ni pamoja na kuabudu na Wayahudi hao katika Siku ya Sabato. (Tazama, James Parkers, The Conflict of the Church and the Synagogue uk 78)
Biblia iko wazi kabisa kwamba Wakristo wa zama za Kanisa la Mitume waliabudu pamoja katika Masinagogi katika Siku ya Sabato. (Tanzama Mdo 2:46 na Mdo 13:42-45)
Hadi kufikia hapa tumeonyesha kuwa tokea wakati wa Uumbaji hadi Kanisa la Mitume Sabato haikuwahi kusahaulika kwa watu wa Mungu. Historia inashuhudia kwamba ibada katika Siku ya kwanza haikujulikana kwa Wakristo hadi kufikia katika Karne ya Pili.
Katika Sehemu ijayo tutaangalia sasa, ni nini kilitokea hadi ibada katika siku ya kwanza ya jumba ikaanza. Kulikuwa na msukumo gani?
Mungu akubariki sana na Endelea kufuatilia, nia yetu ni kuufanhamu ukweli wote, na kisha tusimame upande wa Kweli ya Mwenyezi Mungu.
NA https://loudcrymediaministries.wordpress.com

No comments:

Post a Comment