Somo La 13 | Msulubiwa na Mfufuka [Mwongozo]

(Luka 22 - 24)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Lengo la maandiko ya Luka linatufikisha kwenye jambo hili, somo letu la mwisho: kutufikisha kwenye hitimisho kwamba Yesu ni Mungu. Mungu alikuja duniani na kuishi kama mwanadamu ili kufunua tabia ya Mungu, na kisha Mungu akafa badala yetu ili kutuokoa. Yesu alifufuka kutoka kaburini na kuingia kwenye uzima wa milele huku akitupatia uchaguzi wa uzima wa milele. Ni kisa che pekee kilichobadili historia ya kuwapa wanadamu matumaini makubwa! Hebu tuzame kwenye somo letu la mwisho la Luka ili tujifunze zaidi!
I.                   Bustani
A.                Soma Luka 22:39-40. Utakumbuka kuwa tulipojadili Luka 11:4 (“na usitutie majaribuni”) tulipingana na wazo kwamba Mungu anatuingiza majaribuni. Yesu anapowaambia wanafunzi “waombe” ili “wasiingie majaribuni” je, anatafakari na kujihusisha sana na suala la wao kuingizwa majaribuni? (Anaomba ili wasishindwe na majaribu. Anafahamu kuwa watajaribiwa. Linganisha Luka 22:31-32.)
B.                 Soma Luka 22:41-42. Ni kwa kiasi gani Yesu anataka kuepuka kuchubuliwa na kuteswa hadi kufa?
1.                  Je, Yesu angependa njia ya kuepa jambo hili? (Ndiyo. Katika Luka 4:5-8 Shetani alitaka kumpa Yesu njia ya kuuchukua upya ulimwengu na kuepuka mateso ya kutisha. Hata hivyo, suluhisho jepesi la Shetani lingemaanisha ushindi.)
2.                  Yesu anasema nini kuhusu mtazamo wake dhidi ya mapenzi ya Mungu Baba? (Anayastahi.)
C.                 Soma Luka 22:43-44. Mungu anafanya nini ili kumsaidia Yesu katika kipindi hiki chenye shinikizo la kutisha? (Anamtuma malaika kumtia Yesu nguvu.)
1.                  Je, umewahi kuwa kwenye msongo mkubwa sana wa mawazo, ukamwomba Mungu akusaidie, na kisha ukajisikia hatia kwa sababu bado ulikuwa na wasiwasi? Je, ni vibaya kuendelea kuwa na wasiwasi?
2.                  Soma Ufunuo 21:8. Je, umeshtushwa kuona kwamba tabia ya kwanza iliyobainishwa kwa watu waliopotea ni walio waoga? Je, hivi hata hilo pia ni dhambi? (Jambo pekee linalofanya kitendo hiki kiwe na mantiki kwangu ni endapo linawarejea wale wasiomtumaini Mungu. Kwa hiyo, huwa ninachukia pale ninapomwomba Mungu anisaidie na bado ninaendelea kuwa na wasiwasi.)
3.                  Angalia tena Luka 22:44. Je, bado Yesu ana maumivu makali (uchungu) baada ya kuomba na baada ya malaika kuja na kumfariji? (Ndiyo. Mashinikizo maishani mwangu kamwe hayataweza kukaribia shinikizo alilokabiliana nalo Yesu katika wakati kama huu. Lakini, ninajisikia faraja kufahamu kwamba bado Yesu anatokwa jasho la damu baada ya kumwomba Mungu msaada.)

a.                   Yesu alipata shinikizo, lakini je, alichukua hatua gani? (Hakurudi nyuma. Hakuwa mwoga. Alimtumaini Baba yake.)
D.                Soma Luka 22:45-46. Je, wanafunzi wamemwangusha Yesu? Je, watu wengine watakuangusha wakati unapokabiliana na matatizo?
1.                  Kuna tatizo gani mahsusi lililowafanya wanafunzi kukulala usingizi? (Kwa mara nyingine, Yesu anaonesha kujali kwake juu ya kuanguka kwao majaribuni.)
II.                Busu
A.                Soma Luka 22:47-48. Je, kwa kawaida busu huwa linawakilisha jambo gani? (Utu wema, upendo, huba.)
1.                  Unadhani Yuda alijibuje swali la Yesu? (Nadhani Yuda alidhani kuwa alikuwa akimlazimisha Yesu kuwashinda Warumi. Kiburi na majivuno ndivyo vilivyoruhusu mawazo hayo: mimi ni mwerevu zaidi ya Yesu linapokuja sualala kushughulika na mambo yajayo.)
a.                   Kipi kibaya zaidi: kiburi na majivuno, au kumsaliti Yesu? (Je, hali ya mtu kujitegemea mwenyewe sio usaliti kwa upendo na uwezo wa Mungu?)
B.                 Soma Luka 22:49. Je, swali hili lina mantiki? (Hapo kabla tuliruka jambo hili: soma Luka 22:36-38. Hapo awali Yesu aliwaambia wanafunzi wake wajivike silaha, hata akawaambia kuwa upanga ni wa muhimu zaidi kuliko joho. Kwa kufuata ushauri wa Yesu wanafunzi wanajivika silaha, na sasa wanauliza endapo huu ndio muda muafaka wa kupambana.)
1.                  Je, wanafunzi ni waoga? (Sio katika hatua hii.)
C.                 Soma Luka 22:50-51. Mwanafunzi huyu hakutaka kusubiri maelekezo ya Yesu. Nani aliyejeruhi kabla ya kuruhusiwa? (Soma Yohana 18:10-11. Petro! Utagundua kwamba hapo kabla Petro (Luka 22:32-33) alisema kuwa yu radhi kufa kwa ajili ya Yesu. Alikuwa anasema ukweli.)
D.                Soma Luka 22:51. Kundi lile la watu lingepaswa kukichukuliaje kitendo hiki? (Waliona muujiza!)
E.                 Soma Luka 22:52-54. Unadhani Yuda na Petro wanawazia mambo gani akilini mwao? (Mambo yanaenda kinyume kabisa na yameharibika. Yesu aliwaambia wanafunzi wawe na upanga. Kundi kinzani limejivika silaha. Petro alitumia upanga wake. Lakini, Yesu anamkaripia na anajitoa ili akamatwe. Hatumii nguvu kuwashinda maadui zake.)
III.             Mateso
A.                Soma Luka 23:33-34. Yesu anaonyesha uwezo gani? (Uwezo wa kupenda na kusamehe! Sio nguvu za kimwili.)
B.                 Soma Luka 23:35-39. Ungejibuje kama wewe ndio ungekuwa Yesu, Mtawala wa Ulimwengu? (Ni jambo moja kudhihakiwa tunapokuwa hatuna uwezo. Ni jambo jingine kabisa kuteseka kwa dhihaka wakati ambapo tungeweza kuwashinda maadui zetu kwa urahisi.)
1.                  Je, kuzipuuzia fedheha ni sehemu ya tabia yako?
C.                 Soma Luka 23:40-43. Badala ya kufikiria adhabu, je, Yesu anafikiria jambo gani? (Kumwokoa mhalifu. Katikati ya maumivu makali ya mwili na maumivu makali moyoni, bado Yesu anatafuta kilichopotea!)
1.                  Angalia ujumbe huu wa neema. Mhalifu huyu anakiri kwamba anauawa kwa haki kutokana na uhalifu wake. Pamoja na hayo, tunafahamu anaokolewa na Yesu.
D.                Soma Luka 23:44-46. Hebu niambie, unadhani kuna kipi cha muhimu katika maneno ya mwisho ya Yesu? (Anamtumaini Baba yake hadi mwisho.)
E.                 Soma tena Luka 23:45. Kwa nini pazia la hekalu lilipasuka katikati vipande viwili? (Katika Kutoka 26:33-34 tunaona kwamba ndani ya hekalu pazia lilitenganisha Mahali Patakatifu na Mahali Patakatifu Sana. Sanduku lilikuwa Mahali Patakatifu Sana na liliashiria uwepo wa Mungu kama sehemu ya huduma hekaluni. Yesu alipokufa kama “Mwana-kondoo wa Mungu” (Yohana 1:29), alitimiza kile kilichoashiriwa na mfumo wa kafara hekaluni.)
IV.             Ufufuo
A.                Soma Luka 24:1-5. Hii inamaanisha nini? (Yesu yu hai!)
B.                 Soma Luka 24:6-8. Kwa nini kuwakumbusha wanawake kile alichokisema Yesu hapo awali? (Hii inasaidia kuthibitisha muujiza na kukifanya kiaminike. Yesu aliwaambia hapo kabla kwamba jambo hili litatokea!)
1.                  Unadhani kwa nini ufufuo wa Yesu ulitaarifiwa kwa wanawake kwanza? (Soma Luka 23:49; Marko 14:48-50; na Yohana 18:15. Inaonekana kwamba wanaume wengi walimwacha Yesu, lakini wanawake wengi walikaa na Yesu.)
C.                 Soma Luka 24:36-43. Yesu anafanya nini? (Anawapa ushuhuda madhubuti kwamba amefufuka kutoka katika wafu.)
D.                Soma Luka 24:44-47. Hapa lengo la Yesu ni lipi? (Anaunga mkono ushuhuda wa kimwili na ule wa mafungu ya Biblia yaliyotabiri kifo chake na ufufuo wake. Walidhani kifo cha Yesu kilikuwa ni tukio la kutisha kilichotokea kinyume na matarajio, lakini anawaonesha kwamba hicho ndicho haswaa kilichotabiriwa na Biblia na kwa hakika ndicho alichowaambia kuwa kitaokea.)
E.                 Soma Luka 24:48-49. Yesu aliwapa wanafunzi wake jukumu gani? (Kuwa mashuhuda wa kifo chake na ufufuo wake!)
1.                  Yesu aliahidi msaada gani katika jukumu hili? (Roho Mtakatifu! Je, unaye Roho Mtakatifu akuongozaye kuuendeleza Ufalme wa Mungu?)
F.                  Soma Luka 24:50-53. Kisa cha Yesu kinaishiaje? (Yesu anarudi mbinguni, na wanadamu wanamwabudu na kumsifu Mungu aliyeishi, akafa na kufufuka ili kuwaokoa.)
G.                Rafiki, ikiwa bado haujaukubali ukweli uliomo kwenye ujumbe huu, je, utaukubali na kuupokea sasa hivi? Ikiwa bado hujamwomba Roho Mtakatifu akujie maishani mwako ili akusaidie kupeleka injili kwa watu wengine, je, utafanya hivyo sasa hivi? Huyu ni Mungu mkuu, mwenye upendo, mwenye kujitoa na mshindi wa namna gani tumtumikiaye. Sifa kwake!

V.                Juma lijalo: Tutaanza somo jipya juu ya Wamisionari wa Kibiblia.

No comments:

Post a Comment