(Luka 19, 20 & 22)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na
http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Luka 19:28 inaanza kwa kusema “Na alipokwisha
kusema hayo.” Ni jambo gani hilo alilolisema Yesu? Majuma mawili yaliyopita
tulijifunza juu ya watumwa, kisa cha watumwa na fedha walizopewa na bwana wao
na utekelezaji kwa kuchukua hatua (uangamizaji)! Utakumbuka Yesu aliwazawadia
wale waliokuwa waaminifu, na hata alimpatia mtu aliyekuwa na utajiri mkubwa fedha
za yule mtumwa mvivu! Kisha maadui wa mfalme waliuawa. Hakikuwa kisa halisi cha
Yesu, lakini ni mwongozo wa somo letu kuhusu juma la mwisho linaloelezea maisha
ya Yesu hapa duniani. Je, kuna uhusiano wowote? Hebu tuchimbue somo letu la
Biblia ili tujifunze zaidi!
I.
Yesu Anaingia Kama Mfalme
A.
Soma Luka 19:29-31. Ungejisikiaje kama ungekuwa
unamuiba punda na kisingizio chako ni kwamba “Bwana anamhitaji?” (Ningekuwa na
ujasiri kutokana na ukweli kwamba Yesu aliyafahamu mambo yote kumhusu huyu
punda (mwana-punda) na hivyo anamfahamu mtu yeyote ambaye angeweza kuniletea
vikwazo.)
B.
Soma Luka 19:32-36. Ombi hili lisilo la kawaida
linatendeka kikamilifu! Lakini jambo jingine la kushangaza linaanza kutokea:
watu wanatandaza nguo zao njiani ili Yesu apite juu yake. Kwa nini wanafanya
hivyo?
C.
Soma 2 Wafalme 9:12-13. Makutano (kundi la watu)
wanafikiria nini? (Sio tu kwamba wamiliki wa mwana-punda wanamtambua Yesu kuwa
ni Bwana, bali pia tunaona watu, kwa kutandaza nguo zao njiani, wanatambua
kwamba Yesu ni Mfalme!)
D.
Soma Zekaria 9:9-10. Je, kisa hiki kinahusianaje na
kile cha watumwa na fedha walizopewa na bwana wao?” (Sehemu ya kisa kile ulikuwa
ni upinzani kwa mfalme ajaye, na ushindi wake unaotokana na kuwaua wale
waliompinga. Huu ni unabii kuhusu Mfalme ajaye.)
E.
Soma Luka 19:37-39. Kwa nini Yesu awakanye wanafunzi
wake? (Soma Mathayo 21:9. Hizi kumbukumbu mbili zinathibitisha kuwa wanafunzi
wa Yesu wanatangaza kwamba Yesu ni Masihi na Bwana na Mfalme wao aliyeahidiwa! Haya
hayakuwa makufuru tu, ingeonekana kama ni upinzani dhidi ya Warumi!)
F.
Soma Luka 19:40. Yesu anashughulikiaje tatizo hili?
(Anaidhinisha kile ambacho makutano wanakifanya. Anasema kwamba vitu vingine
vya asili vitaendeleza sifa ikiwa wanafunzi wangenyamazishwa.)
1.
Unadhani wanafunzi walilichukuliaje jambo hili? (Hebu
fikiria jinsi walivyofurahi! Hatimaye kile walichokitarajia (kwamba Yesu atakuwa
Mfalme) sasa kinatokea!)
G.
Soma Luka 19:41-44. Soma jambo hili sehemu ya nyuma
kidogo katika Luka 19:27. Mtazamo wa Mfalme juu ya uangamivu wa maadui zake ni
upi? (Yesu analia! Hii inasahihisha dhana yetu kuhusu hatma ya kisa cha watumwa
na fedha walizopewa na bwana wao!)
1.
Yesu anasema kuwa mambo yangewezaje kuwa tofauti?
(Endapo wangemtambua Yesu kama Masihi wao, wangeweza kuitambua amani na si
maangamizi.)
a.
Je, huu ndio ujumbe kwa ajili yetu leo?
II.
Wabadili Fedha
A.
Soma Luka 19:45 na Mathayo 21:12. Luka anatuambia
kwamba Yesu alikuwa “akiwatoa” wale waliokuwa wakiuza, na Mathayo anatuambia kuwa
alikuwa akipindua meza na viti. Jambo hili linaonekana kuwa la fujo, je
unakubaliana nami?
B.
Soma Luka 19:46. Je, hii inaashiria kuwa “wauzaji”
walikuwa wanafanya nini? (Wakiwanyang’anya watu. Bila kuingia kwa undani zaidi,
palikuwepo na sarafu maalumu ya hekalu iliyohitajika na wageni na kafara
(sadaka) zingeweza kununuliwa. “Wauzaji” hawa walikuwa wakitoa huduma, lakini
hawakuwa waaminifu katika kushughulika kwao na wale waliokuja kumwabudu Mungu.)
1.
Unajisikiaje pale unapokuwa umefanyiwa kitendo cha
udanganyifu? Je, unaweza kuona jinsi ambavyo wageni hekaluni walivyoweza
kujikita kwenye suala la kulaghaiwa badala ya kujikita kwenye maombi?
C.
Soma Luka 19:47-48. Kwa nini viongozi wa dini
hawafurahishwi na mabadiliko yaliyofanywa na Yesu? (Kutokana na ukweli kwamba
walitaka kumuua Yesu, inaonesha jinsi walivyojihusisha kwenye vitendo visivyo
vya uaminifu. Ikiwa watu walichukia kuibiwa, na kwamba kutokuwepo kwa uaminifu
kulitia doa uzoefu wao wa kidini, uwajibikaji katika jambo hili ulikuwa katika
viwango vya juu sana.)
D.
Soma Luka 20:1-2. Unadhani makuhani wakuu walidhani
kwamba mamlaka sahihi yalikuwa ni yapi? (Wao!)
1.
Kwa nini wanajishusha na kuuliza maswali? Kwa nini wasionyeshe
mamlaka yao? (Hii inaturejesha nyuma kwenye Luka 19:48 – Yesu alikuwa maarufu
sana kwa watu.)
2.
Je, ni “mambo” gani ambayo Yesu anahitaji mamlaka nayo?
(Kupindua meza na viti vya wauzaji kwa nguvu.)
a.
Jiweke kwenye nafasi ya kiongozi wa dini. Je, unataka
kutetea wizi? Unadhani watu wa kawaida wanafikiria nini kuhusu vitendo vya wauzaji
visivyo vya uaminifu? (Kwa ghafula, tunao mtazamo bora zaidi kuhusu sababu ya
viongozi ya dini kujishusha hadi kuuliza maswali. Yesu amewabana na kuwaweka
mahali pabaya. Mauaji ndilo jibu lao bora kabisa.)
E.
Soma Luka 20:3-8. Kungekuwa na ubaya gani kusema kwamba
Yohana Mbatizaji alikuwa nabii? (Soma Yohana 1:29. Yohana alisema kwamba Yesu
ni Masihi! Suala la viongozi wa dini kutomwamini Yohana lilikuwa na uhusiano na
kile alichokisema Yohana kuhusu mamlaka ya Yesu.)
1.
Kwa nini Yesu hakutaka kusema moja kwa moja chanzo cha
mamlaka yake? (Kitendo hicho kingeibua tena suala la kukufuru.)
F.
Fikiria mafungu machache yaliyopita kuhusu kupindua
meza na mjadala unaohusu mamlaka. Kwa nini Yesu alikuwa anatumia saa zake za
mwisho za thamani kabisa kwenye kazi kama hii? (Kwanza kabisa fikiria juu ya
taswira pana ya kiishara. Yesu anakaribia kuwa, kama alivyotabiri Yohana katika
Yohana 1:29, mwana-kondoo wa kafara aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Hii inaakisi
Siku ya Upatanisho, hekalu liliposafishwa dhambi. Kwa hivyo, Yesu anaondoa
dhambi hekaluni kabla ya kifo chake – taswira ambayo watu watakuwa na uhakika
wa kuikumbuka. Katika taswira ya kawaida, watu wanaweza kujikita kwenye
fundisho la Yesu badala ya biashara na udanganyifu ambayo hapo kabla iliwawekea
watu vikwazo.)
III.
Shamba la Mzabibu
A.
Soma Luka 20:9-15. Kisa hiki kinalinganishwaje na kisa
cha watumwa na fedha walizopewa na bwana wao katika Luka 19:12-27? (Taswira ya
Yesu katika kisa cha watumwa na fedha za bwana wao inapata ushindi. Taswira ya
Yesu katika kisa cha shamba la mzabibu inakufa.)
1.
Kwa nini Yesu anaelezea hiki kisa cha pili kuhusu
shamba la mzabibu? (Atakufa kabla hajapata ushindi.)
B.
Soma Luka 20:16. Utagundua kwamba Yesu anajijibu swali
lake mwenyewe: mmiliki wa shamba la mzabibu atawaangamiza wale waliomuua
mwanaye. Watu walipojibu, “Hasha! Yasitukie haya!,” je, wanazungumzia jambo
gani? (Nadhani wanazungumzia mauaji ya mwana.)
C.
Soma Luka 20:17-19. Sasa tunafahamu kuwa kwa muda mrefu
viongozi wa Kiyahudi walikuwa wakitafuta namna ya kumuua Yesu. Je, anawapa onyo
gani? (Sasa ameelezea visa viwili (kisa cha watumwa na fedha walizopewa na
bwana wao na kisa cha shamba la mzabibu) ambapo wale waliompinga mfalme
walikufa. Sasa katika Luka 20:18 Yesu anasema kuwa maadui wake watasagwasagwa.)
1.
Unadhani kwa nini viongozi wa Kiyahudi waliendelea
kutafuta jinsi ya kumuua Yesu?
2.
Angalia jambo fulani hapa. Viongozi wa Kiyahudi
walikuwa wanawaogopa watu. Walipaswa kukumbuka jambo gani? (Katika Luka 12:4-5
Yesu aliwaambia wamwogope Mungu badala ya kuwaogopa wanadamu. Wanachoweza kufanya
watu ni kukuua tu. Mungu “ana uwezo wa kukutupa jehanum.”)
IV.
Pasaka
A.
Soma Luka 22:14-21. Wanafunzi waliposikia juu ya kuja
kwa Ufalme wa Mungu, unadhani walidhani Yesu alimaanisha nini? (Soma Luka
22:24. Wanataka Yesu awe Mfalme na wao watakuwa watawala wake. Hata hivyo, Yesu
amesema mambo ya kutatiza kuhusu siku zijazo.)
1.
Unadhani wanafunzi walihitimisha nini kuhusu msaliti
kuwepo pale mezani? (Jambo hili linatatiza zaidi.)
2.
Unadhani msaliti alifikiria nini? (Yumkini alikuwa
anampa Yesu upendeleo. Atamlazimisha Yesu kuwa Mfalme – na kisha atapata sifa
kwa kulazimisha jambo hilo kutokea.)
B.
Soma Luka 22:31-33. Hii inaonesha nini kuhusu fikra ya
wanafunzi? (Wao (au angalao Simoni Petro) walipata ujumbe kwamba Yesu alikuwa
kwenye wakati mgumu sana – licha ya kuingia mjini kama Mfalme na Masihi.)
C.
Rafiki, je, u radhi kupokea maonyo ya Mungu? Mara zote
huwa kuna ujumbe tunaotaka kuusikia, na ujumbe ambao tusingependa kuufikiria. Mwombe
Yesu leo ayabainishe wazi mapenzi yake kwako na aufungue moyo wako uwe tayari
kusikiliza ili uendane na Ufalme wa Mungu.
V. Juma lijalo: Kusulubiwa na Kufufuka.
No comments:
Post a Comment