Somo La 11 | Ufalme Wa Mungu [#Mwongozo]

(Luka 11, 17 & 21)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Mara kwa mara huwa ninaandika kuhusu Ufalme wa Mungu na huwa ninautaja ninapozungumza na watu wengine. Je, Ufalme wa Mungu ni kitu gani hasa? Matumaini yako ni kwamba ninafahamu ninachokizungumzia, sawa? Wakati ni kweli kwamba ninafahamu ninachokiongelea, somo letu juma hili limenionesha kwamba kuna mambo mengi ya kujifunza ili kuelewa vizuri anachokiwazia Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze pamoja!
I.                   Ndani ya Ufalme wa Mungu
A.                Soma Luka 17:20. Unalielewaje jibu la Mungu kwenye swali la “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” (Yesu anasema kwamba si jambo tunaloweza kuliona kwa kuwa makini na kulifanyia uchunguzi.)
B.                 Soma Luka 17:21. Kwa nini hatuwezi kuuona Ufalme wa Mungu mara utakapokuja? (Kwa sababu umo ndani yetu.)
1.                  Ufalme wa Mungu unawezaje kuwa ndani yetu?
2.                  Soma Warumi 14:17. Paulo anatupatia mifano madhubuti wa mambo yaliyo ya nje na mambo yaliyo ya ndani. Hii inatusaidiaje kuelewa namna ambavyo Ufalme wa Mungu umo ndani yetu? (Ni mtazamo unaoletwa na Roho Mtakatifu: furaha, amani, na kuhesabiwa haki.)
C.                 Soma Luka 11:14-16. Mashtaka gani yanatolewa dhidi ya Yesu? (Kwamba uwezo wake unatoka kwa Shetani.)
D.                Soma Luka 11:17-19. Hoja ya Yesu yenye mantiki dhidi ya hili shtaka la kushindana na Shetani ni ipi? (Kwa nini Shetani amwondoe pepo? Kitendo hiki kitalishinda lengo la Shetani.)
E.                 Soma Luka 11:20. Angalia rejea ya Yesu kwenye Ufalme wa Mungu. Je, hii inatufundisha nini kuhusu Ufalme wa Mungu? (Ufalme wa Mungu umekuja ikiwa tunatumia uwezo wa Mungu kuondoa pepo.)
F.                  Soma Mathayo 12:24, Mathayo 12:28 na Mathayo 12:31-32. Katika kitabu cha Mathayo tunaona shtaka lile lile dhidi ya Yesu: Anatenda kazi kwa uwezo wa Shetani kuondoa pepo. Pia tunaona kauli ya Yesu kuhusu Ufalme wa Mungu. Je, Yesu anamaanisha nini kuhusu dhambi isiyosamehewa? (Yesu anatuonesha kwamba uwezo wake wa kuponya unatoka kwa Roho Mtakatifu, si kwa Shetani. Ikiwa unaiita kazi ya Roho Mtakatifu kuwa ni ya kishetani, basi unakuwa umeingia kwenye mazingira ya hatari sana!)
G.                Angalia hii miktadha miwili inayohusu kisa kile kile kuhusu Yesu kuondoa pepo na kusema kwamba Ufalme wa Mungu upo. Je, hiyo inatufundisha nini kuhusu jinsi Ufalme wa Mungu ulivyo ndani yetu? (Ufalme wa Mungu kuwa ndani yetu si jambo jingine tofauti na Roho Mtakatifu kukaa ndani yetu!)

1.                  Je, kuna sababu yoyote kuamini kwamba Roho Mtakatifu anakaa ndani yako? Kama sivyo, kwa nini?
2.                  Tunapoangalia vipaumbele vyetu vyote vya kiroho, je, Ufalme wa Mungu kuja ndani yetu haupaswi kuwa kipaumbele chetu kikuu? (Linganisha Luka 11:2.)
3.                  Unadhani kwa nini Yesu anamlinganisha (Luka 11:20) Roho Mtakatifu na “kidole cha Mungu?”
II.                Nje ya Ufalme wa Mungu
A.                Soma Luka 17:22. Ikiwa Ufalme wa Mungu umo ndani, kwa nini wanafunzi watamani kuona siku za Yesu? (Yesu anasema mtaangalia siku za nyuma mkitamani siku nilipokuwa pamoja nanyi kimwili.)
1.                  Je, una mwanafamilia au rafiki aliyefariki, na ungependa kuishi naye tena kwa siku moja?
B.                 Soma Luka 17:23-25. Ni punde tu Yesu ametuambia kwamba Ufalme wa Mungu umo ndani yetu. Je, kuna lolote zaidi ya hilo? (Wanafunzi, watakaomkosa Yesu katika siku za usoni, wanaweza kutarajia ujio wa Ufalme wa Mungu. Ujio huo utalimulika anga “kutoka upande mmoja hadi mwingine.”)
1.                  Je, Yesu anajikanganya? (Yesu anaonekana kujibu maswali kadhaa yanayohusiana na Ufalme wa Mungu. Swali la msingi ni, “Je, Ufalme wa Mungu utakuja sasa hivi?” Jibu ni, “ndiyo,” Ufalme wa Mungu umo ndani yenu, lakini “hapana,” hamuwezi kuupata sasa hivi kwa kuutafuta kwa makini. Katika siku zijazo Ufalme wa Mungu utakuja kwa namna ambayo utakuwa nje yetu, lakini “uchunguzi makinifu” hautahitajika ili kuuona.)
C.                 Soma Luka 17:26-30. Hebu tuyaangalie mafungu haya na tusitafakari chochote tunachokifahamu kuhusu utangulizi. Je, mambo haya (kama vile kula na kunywa) yanaonekana kuwa mema? (Ndiyo, yanapendeza. Haya ni kielelezo cha maisha yenye furaha na biashara yenye mafanikio.)
1.                  Je, ni “habari gani ya nje” tuliyonayo kuhusu siku za Nuhu na Lutu? (Soma Mwanzo 6:11-13 na Mwanzo 18:20-23. Watu walikuwa wabaya sana.)
2.                  Kwa nini Yesu anazungumzia mambo mazuri maishani wakati watu hawa walikuwa wakitenda mambo mengi sana mabaya? (Walikuwa hawamsikilizi Mungu. Hawakuwa na Ufalme wa Mungu ndani yao.)
D.                Angalia tena Luka 17:27-29. Matokeo ya kufanana kwa watu waliokuwepo nyakati za Nuhu na Sodoma ni yapi? (Waliangamizwa.)
1.                  Waliangamizwa wakati gani? (“Watu wema” walipoondoka. “Nuhu aliingia kwenye safina.” “Lutu aliondoka Sodoma.”)
III.             Kuuandaa Ufalme Ndani
A.                Soma tena Luka 17:30. Kwa kuzingatia utangulizi tuliokwishauona, je, unalielewaje jambo hili? (Ufalme wa Mungu umo ndani ya wenye haki. Wanapoondoka, waovu wataangamizwa.)

1.                  Je, unakumbuka Yesu alisema katika Luka 17:20 kwamba Ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza? Ikiwa Ufalme wa Mungu umo ndani ya wenye haki, na Mungu atawapeleka mbinguni katika ujio wa Mara ya Pili, mara zote Ufalme u pamoja nao! Kwa nini basi mtu yeyote ahitaji kuuchunguza?
B.                 Soma Luka 17:31. Tunaye mtu mmoja nyumbani na mwingine shambani. Kwa nini tunaambiwa tusijaribu kurudi nyuma kuchukua vitu vyetu? (Ikiwa Ufalme wa Mungu umo ndani yako, kwa nini uhitaji kitu kingine chochote kile?)
C.                 Soma Luka 17:32-35. Watu wawili wanafanya kazi, watu wawili wamelala. Jambo gani linaleta tofauti bila kujali kama wanaishi au wanakufa? Jambo gani linaleta tofauti kwa mke wa Lutu? (Tunayo taswira ya watu kujihusisha kwenye kazi za kawaida. Hii ni sawa na rejea ya awali kuhusu kula, kunywa na kufurahia. Swali ni endapo kipaumbele chako cha msingi kipo kwenye Ufalme wa Mungu au kwenye mambo yako na shughuli zako maishani.)
1.                  Luka 17:33 inamaanisha nini inaposema kwamba tukijaribu kuiponya nafsi yetu tutaiangamiza? (Mfano mahsusi (Luka 17:31) ni kurudi nyuma ili kuchukua vitu vyetu. Lakini, mfano mkubwa ni kujikita kwenye maisha yetu ya sasa. Shughuli zote za kawaida maishani zinaendelea, swali ni endapo Ufalme wa Mungu umo ndani yako na ni kipaumbele chako.)
D.                Soma Luka 21:34-36. Utagundua tunaambiwa kwamba “tujiangalie!” Hebu tujipe mashaka na tuseme kwamba jambo baya kabisa maishani mwetu ni “kuangushwa” na “madukuduku maishani.” Kila mtu ana wasiwasi wa namna fulani. Tiba yake ni ipi? (Tukiyageuzia matatizo haya kwa Mungu, tukijikita ndani ya Ufalme, mioyo yetu haitaangushwa.)
E.                 Hili wazo la Ufalme wa Mungu kuwa ndani yetu, na kuwa msisitizo wetu, linaweza kuwa wazo jipya kwako. Kwa nini Yesu anatumia mambo mazuri, kama vile kula, kunywa, kununua, kuuza na kuoa na kuolewa kuelezea mambo ya kutisha yanayoendelea Sodoma na nyakati za Nuhu? Kwa nini asitaje dhambi tu? (Mambo mbalimbali maishani yanaelekea kuondoa msisitizo/matazamio yetu kutoka kwenye matazamio aliyonayo Roho Mtakatifu kwa ajili yetu. Ikiwa tutajikita kwenye Ufalme wa Mungu ndani yetu, hatutatangatanga kwenye dhambi za kutisha za Sodoma na nyakati za Nuhu.)
F.                  Soma Ufunuo 21:1-3. Tangazo gani linatolewa kutoka katika kiti cha enzi cha Mungu? (Mungu atakaa pamoja na wanadamu!)
1.                  Jambo gani halijabadilika? (Ikiwa Roho Mtakatifu anakaa ndani yetu, yaani ikiwa Ufalme wa Mungu, “kidole cha Mungu,” kipo ndani yako sasa hivi, basi Mungu anakaa pamoja nawe sasa! Tofauti iliyopo ni kwamba mambo ya nje yamebadilika. Waovu wametoweka, na tunayo mbingu mpya na nchi mpya.)
G.                Rafiki, je, ungependa kujiunga na Ufalme wa Mungu sasa hivi? Je, ungependa kukaa na Mungu sasa hivi? Kama ndivyo, omba msamaha wa dhambi zako, na mwombe Mungu amtume Roho Mtakatifu akae ndani yako. Kuanzia leo na kuendelea, jikite kwenye Ufalme wa Mungu kuishi ndani yako!

IV.             Juma lijalo: Yesu Ndani ya Yerusalemu.

No comments:

Post a Comment