LESONI - SHERIA YA MUNGU _-_[Somo La 10] @BabatiSda

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

(Mathayo 5, Yakobo 1, Marko 7, Warumi 3 & 6)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Ikiwa unafuatilia somo hili basi utagundua kwamba ninafundisha kuhusu wokovu unaopatikana kwa njia ya neema pekee. Somo letu juma hili linabainisha kwamba sheria, ikiwa itashikwa vizuri, inahitaji kiwango cha tabia cha hali ya juu. Kiwango hiki cha hali ya juu kinawafanya watu wengine waamini kwamba sheria ya Mungu sio ya muhimu sana kwa kuzingatia neema iliyopo. Ikiwa hatuwezi kuishika sheria, na kuishika sio kigezo cha kuingia mbinguni, kwa nini basi tujaribu kuishika? Kwa upande mwingine kila mtu anayeutafakari ulimwengu anafahamu umuhimu wa sheria. Sheria, kama ilivyo kwa nguvu za uvutano, zinatawala kila jambo. Ulimwengu wetu hauongozwi kwa sheria pekee, bali pia kuna sheria za asili zinazoongoza mustakabali wa maisha yetu. Tunaweza kuona kundi la mataifa pamoja na watu wanaotuzunguka wanaoamini kwamba wako nje ya sheria. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!
I.                   Yesu na Sheria
A.                Soma Mathayo 5:17. Tunajuaje kwamba sheria inaendelea kuwa ya muhimu sana? (Wanaohoji juu ya neema wanasema kuwa Yesu aliitangua torati. Hapa Yesu anasema kwamba hakuja kuitangua torati.)
1.                  Yesu anamaanisha nini anaposema kuwa alikuja “kutimiliza” torati na manabii? (Alikuja kutimiliza unabii uliokuwa umemtabiri. Alikuja kutimiliza mfumo wa kafara uliotabiriwa kwa ajili yake. Alikuja kuitunza sheria kikamilifu kwa niaba yetu.)
B.                 Soma Mathayo 5:18. Hapa tuna kauli mbili zinazosema “hadi.” Kauli ya kwanza inasema “mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka” na ya pili inasema “hata yote yatimie.” Je, hizo ni nyakati mbili tofauti?
1.                  Ikiwa umejibu kuwa nyakati hizo zilikuwa sawa, na kipindi hicho ni Ujio wa Yesu Mara ya Pili, je, hiyo inamaanisha kuwa mbinguni hapatakuwepo sheria?
C.                 Soma Waebrania 8:10-12. Je, hii inaashiria nini juu ya mustakabali wa sheria? (Kwamba wakati fulani sheria itaungana sana na tabia yetu kiasi kwamba hakuna atakayehitaji kuifundisha. Hiyo inaashiria kwamba sheria inaendelea kuwepo kwa namna moja au nyingine – hadi mbinguni.)
D.                Soma Mathayo 5:19. Walimu wanapaswa kufundisha nini kuhusu sheria? (Walimu hawapaswi tu kuwa mfano katika utunzaji wa sheria, bali pia wanapaswa kufundisha juu ya umuhimu wa kushika sheria.)
1.                  Angalia kauli ile ile ya kupendeza kuhusu mbingu. Je, walimu wanaosema kuwa sheria haitufungi wanakwenda mbinguni?
II.                Nafasi ya Sheria


A.                Soma Mathayo 5:21-22. Tunaitambua “Usiue” kama amri ya sita (Kutoka 20:13). Je, Yesu anasema kuwa kukasirika, au kumwambia mtu kwamba ni “mpumbavu,” ni sawa na mauaji?
1.                  “Kufyolea (kusonya)” maana yake ni nini na kwa nini kitendo hicho ni kosa kwa mujibu wa sheriai? (Inamaanisha kuwa mtu “hana akili.”)
2.                  Soma Mathayo 23:16-17. Hebu subiri kidogo! Yesu anawaambia walimu mwamba ni “wapumbavu.” Je, Yesu amekiuka kanuni yake mwenyewe?
B.                 Soma Mathayo 5:27-28. Tunaitambua “Usizini” kama amri ya saba (Kutoka 20:14). Je, Yesu anasema kuwa kutazama na kutenda vinalingana?
1.                  Je, kuzini “moyoni” maana yake ni nini? Je, kuzini huko kunakatazwa na amri ya saba?
C.                 Soma Mathayo 5:29-30. Tumesoma kwamba kukasirika ni sawa na kufanya mauaji na kutazama kwa kuatamani ni aina fulani ya uzinzi. Je, kung’oa jicho au kukata mkono vitaondoa hasira au matamanio? (Hapana. Hakuna hata jambo moja lionekanalo kuleta mantiki. Kukasirika sio sawa na kukatisha uhai wa mtu (kuua) na kutazama sio sawa na kufanya uzinzi. Kuondoa viungo vya mwili wetu hakubadili fikra zetu.)
1.                  Kwa nini Yesu anasema hivi? Je, alifahamu kuwa jambo hili halitakuwa na mantiki kwetu? (Kumbuka kwamba, sisi ni viumbe walioumbwa hivyo tunatakiwa kulikubali neno la Muumbaji wetu! Lakini, ikiwa jambo analolisema Yesu halileti mantiki yoyote, huenda hatujaelewa kile anachokifundisha Yesu.)
2.                  Ikiwa kung’oa au kukata viungo vya mwili sio suluhisho la dhambi, unadhani Yesu anamaanisha nini kwa kauli hizo? (Anamaanisha kuwa mara nyingine hatua kali na za msingi zinahitaji kuchukuliwa ili kuepuka kuikiuka sheria. Sidhani kama anatetea hatua hizi mahsusi.)
3.                  Je, hili wazo la “hatua kali na za msingi” linatusaidia kuelewa kauli za hasira na kutazama? (Hilo ni jambo la kulifikiria! Ikiwa tutasema kuwa tutakuwa waangalifu hata kwenye suala la kutazama na kisha kufadhaishwa, basi hiyo ni hatua kali.)
D.                Soma Yakobo 1:13-15. Yakobo anatufundisha nini kuhusu jinsi ambavyo tunaingia dhambini? Tamaa ya dhambi inaibuka mawazoni mwetu, na hii inajielekeza kwenye dhambi halisi, ambayo hatimaye huzaa mauti.)
1.                  Hii inatufundisha nini kuhusu kauli za Yesu juu ya hasira na tamaa? (Angalao dhambi mahsusi ni kufikiria kuua na kufanya uzinzi. Ikiwa umekasirika sana kiasi cha kuweza kumwua mtu kama utaweza kufanya hivyo, ikiwa utafanya ngono nje ya ndoa kama utaweza kufanya hivyo, basi Yesu anafundisha kwamba tayari dhambi imeshatendeka. Hiyo inaleta mantiki kwangu. Kwa nini dhambi igeuke na kuwa fursa?)
a.                   Je, Yesu anatufundisha jambo jingine zaidi ya hilo? (Yakobo anatufundisha kwamba dhambi ni endelevu. Inazaliwa mawazoni mwetu. Kwa hiyo, inaleta mantiki kuhitimisha kwamba Yesu anatuambia kuwa makini na mitazamo yetu.)


E.                 Soma Kutoka 20:17. Je, fungu hili linazungumzia nini kuhusu kumtamani mke (au mume) wa jirani yako? (Kauli hii inakamilisha taswira kamili kwangu. Kwa umahsusi amri ya kumi inaelezea mawazo yaliyomo akilini. Kama asemavyo Yakobo, dhambi huanza kwa kuwaza.)
F.                  Soma Marko 7:14-17. Je, kauli hii ilileta mantiki kwa wanafunzi wa Yesu? (Hapana. Walitaka kufahamu alichokimaanisha Yesu. Tunajishughulisha na mfululizo wa kauli zilizosemwa na Yesu zinazohitaji kuangaliwa kwa makini!)
G.                Soma Marko 7:18-19.Je, kile ulacho ni kitendo au mtazamo? (Ni kitendo. Kimsingi, unatakiwa kuamua kipi cha kula. Lakini, kinachomaanishwa hapa ni kwamba kile ulacho kinaenda tumboni, hakiingii moyoni mwako (akilini mwako).)
H.                Soma Marko 7:20-23. Hebu tupitie tena mjadala wetu juu ya hasira, mauaji, tamaa na uzinzi. Hapo awali niliandika kwamba kuwa na hasira si sawa na kuua, na kutazama si sawa na kuzini. Je, nilichokiandika si sahihi? Yesu analinganishaje mawazo na matendo? (Mawazo (akili) ndio chanzo cha uovu wote. Mauaji na uzinzi ni utekelezaji kivitendo wa kile kinachoendelea mawazoni. Ikiwa kwa namna fulani, hatuwezi kufanya kitendo halisi, basi hatupati alama au kujigamba kwa kufikiria jinsi ambavyo tungependa jambo hilo litendeke.)
III.             Mwitikio Wetu
A.                Soma Warumi 3:19-20. Je, sasa unaweza kuelewa kwamba wigo wa sheria hutufanya tusiwe na cha kuongea? Je, inaonekana ni sahihi kwamba sheria inatufanya tuitambue dhambi, lakini haitufanyi kuwa wenye haki? (Kwa hakika kwangu mimi jambo hilo linaonekana kuwa ni sahihi kutokana na kiwango cha juu tulichokiona.)
B.                 Soma Warumi 3:21-24. Tunakuwaje wenye haki? (Kwa njia ya imani katika Yesu. Tunahesabiwa haki kwa neema yake.)
C.                 Soma Warumi 6:1-4. Je, neema inahitaji mtazamo gani wa kiakili? (Kwamba tuliifia dhambi. Hatutaki kuishi dhambini tena.)
D.                Soma Warumi 6:15-18. Je, inamaanisha nini “kujitoa nafsi” kwa ajili ya dhambi? Hususan kwa muktadha wa mjadala wetu juu ya dhambi kuanzia mawazoni? (Mawazo ndio uwanja wa mapambano. Tunajitoa nafsi zetu dhambini kwa kuamua kuingia dhambini.)
1.                  Je, “tunajitoaje” kwa Mungu, na kuwa watiifu? (Soma Warumi 8:5-6. Lengo ni kuyaweka mawazo yetu kwa kile ambacho “Roho anakitamani.”)
E.                 Rafiki, je, utafanya uamuzi leo wa kujitoa kwa Mungu? Je, utapanga kwamba kila asubuhi utakuwa ukisema, “Je, nifikiri na kutenda jambo gani ambalo linaendana na kile ambacho Roho Mtakatifu anatamani nikifanye leo? Roho wa Mungu, nakuomba uyaongoze mawazo yangu pamoja na mikono yangu.”

IV.             Juma lijalo: Sabato

No comments:

Post a Comment