Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Wagalatia 2)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com
kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Paulo anawasilisha umoja wa namna gani? Hadi kufikia
hapa, anaonekana kupendelea zaidi kusema kwamba injili yake inatoka kwa Mungu
moja kwa moja, na si kwa viongozi wa kanisa. Hiyo inaonekana kuwa njia ya ajabu
katika kuufikia umoja! Yumkini sisi sio wajuzi kama Paulo. Huenda Paulo alijua
kwamba alipaswa aendelee katika njia yake mwenyewe kuwafundisha Mataifa kama
alivyoelekezwa na Mungu. Ni baada tu ya kuanzisha kazi yake ndipo aweze kwenda
kwa viongozi wa kanisa kwa ajili ya wao kuidhinisha kazi yake. Hebu tusome kile
anachokiandika Paulo ili tuone kama hiyo ndio njia aliyoitumia!
I.
Miaka Mingi Baadaye
A.
Soma Wagalatia 2:1. Linganisha na Wagalatia
1:18-19. Paulo anataarifu kwamba miaka mitatu baada ya kuongoka kwake
anatembelea Yerusalemu na ana mawasiliano machache sana na uongozi wa kanisa. Kisha
miaka kumi na minne baadaye, anajitokeza ili kukutana na uongozi wa kanisa
tena. Ikiwa ulikuwa unamshauri Paulo awe na umoja na uongozi wa kanisa, je,
ungependekeza hii njia iliyotumika? (Nisingeshauri hivyo. Hii inaonekana kuwa
kinyume na kile kinachopaswa kufanyika ili kuleta umoja.)
B.
Soma Wagalatia 2:2. Kwa nini Paulo alijitokeza
miaka kumi na minne badaye? (“Katika kuitikia ufunuo.” Mungu alimwambia
awatembelee viongozi. Hiyo inaashiria kwamba hapo awali Mungu hakumwambia arudi
Yerusalemu ili kuonana na kushauriana na uongozi.)
1.
Unadhani Paulo angesafiri kwenda Yerusalemu
endapo Mungu angekuwa hajamwelekeza kuwatembelea viongozi? (Sidhani. Ikiwa ulikuwa
umepotea kwa miaka kumi na minne, na hudhani kwamba unahitaji kushauriana na
uongozi, kwa nini basi ushauriane nao?)
2.
Unadhani kwa nini Mungu alimsubirisha Paulo kwa
muda mrefu?
II.
Mwendelezo Ule Ule?
A.
Soma 1 Wakorintho 1:10-12. Paulo anawezaje
kuaminika anapojenga hoja ya umoja miongoni mwa uongozi, wakati yeye binafsi
anafanya mambo yake mwenyewe miongoni mwa Mataifa angalao kwa muda wa miaka
kumi na minne?
B.
Soma tena Wagalatia 2:2. Kwa nini Paulo anasema
kuwa aliamua kukutana na uongozi wa kanisa kwa faragha? (Aliogopa kwamba
alichokuwa anakifanya kilikuwa ni sawa na kazi bure.)
1.
Unadhani hiyo inamaanisha nini?
2.
Soma Wagalatia 1:6-8. Paulo hana mashaka na
namna anavyowasilisha injili, hivyo basi yawezekana Paulo alikuwa anazungumzia
jambo gani anaposema kuwa alihofia kwamba kutanga kwake kote kulikuwa ni kazi
bure?
C.
Haya ni maswali magumu. Paulo anawezaje kuwa
anatangaza umoja kwa kukaa mbali, na ni kwa jinsi gani Paulo anaweza kudhani
kuwa yumkini alikuwa akitanga bure? Je, inawezekana kwamba tunaliangalia jambo
hili kwa njia isiyo sahihi?
D.
Soma 1 Wakorintho 1:18-19. Je, mara zote Mungu
anatenda kazi kwa namna inayoleta mantiki kwetu?
1.
Ikiwa Paulo yuko sahihi kwamba anahubiri injili
ya kweli, hilo fundisho sahihi linaweza kuonekanaje kwa wale walioikataa neema?
(“Upumbavu.”)
2.
Tafakari jambo hili kidogo. Kituo cha usaidizi
wa sheria ya Musa kilikuwa Yerusalemu. Endapo Paulo angewasilisha mara moja
injili yake ya neema kwa watu wa Yerusalemu, kitendo hicho kingepokelewaje?
(Soma Matendo 9:23-25 na Matendo 22:17-21. Baada ya uongofu wake, Paulo alidhani
kwamba anastahili sana kuwasilisha injili kwa Wayahudi waliofanya naye kazi. Tunaona
sio tu kwamba Mungu hakukubaliani naye na kumpeleka kwa Mataifa, bali pia
Wayahudi walijaribu kumwua. Jambo la mwisho ambalo Paulo alipaswa kulifanya ili
kuutangaza “umoja” ilikuwa ni kuwasilisha injili yake kwa Wayahudi kule Yerusalemu.)
a.
Mara baada ya Paulo kukataliwa na washiriki wa
kanisa Yerusalemu, tayari hilo liliathirije kwa kiasi kikubwa kazi yake?
(Endapo Paulo asingekuwa amefanya kazi peke yake kwa miaka yote hiyo,
angewasilisha hoja yake (inaonekana hivyo) kwa makundi ya watu Yerusalemu,
angekataliwa (au kuuawa) na hiyo ingehitimisha kazi yake bado ikiwa changa.)
E.
Soma Wagalatia 2:3-5. Jambo gani linaleta
mtafaruku? (Tohara inatajwa.)
1.
Njia aliyoitumia Paulo inautangazaje mtazamo
wake? (Kifungu cha 5 kinathibitisha kwamba Paulo hadhani kuwa ujumbe wake wa
injili ni potofu. Badala yake, tunaona kwamba kwa kukutana na baadhi ya
viongozi kwa faragha, aliweza kuelezea mambo aliyokuwa akiyatenda Mungu kupitia
kwake. Hii inaelezea kile kinachoonekana kuwa njia ya ajabu ya Paulo. Anakaa mbali
kwa muda mrefu ili muda mwafaka uweze kufika, anakwenda kwa viongozi na ujumbe
wake kwa mkakati maalum na sio kwa makundi ya watu.)
III.
Majukumu Tofauti
A.
Soma Wagalatia 2:6. Chukulia kwamba huyu ni
mchungaji wako akiandika juu ya uongozi wa madhehebu yake. Unaweza kudhani
kwamba yeye ni bingwa wa umoja?
1.
Sababu ya Paulo kuandika kauli hiyo inayoonekana
kama ya uasi ni ipi? (Kwa mara nyingine, anao ujumbe aliofundishwa na Yesu, sio
ujumbe aliofundishwa na wanadamu wengine.)
B.
Soma Wagalatia 2:7. Unaweza kuona ujumbe wa
umoja kwenye hii kauli? (Ukiangalia kwa mtazamo mpana, unaweza kuuona umoja. Paulo
anasema kuwa anayo sehemu ya ujumbe wa kupelekwa kwa watu (Mataifa) na Petro
anayo sehemu nyingine ya ujumbe wa kupelekwa kwa watu (Wayahudi).)
C.
Soma Wagalatia 2:8. Nani anawajibika kwa
mgawanyo wa majukumu ndani ya kanisa? (Mungu. Kama ambavyo ujumbe wa Paulo
unatoka kwa Mungu, vivyo hivyo ugawaji wa majukumu unatoka kwa Mungu.)
1.
Unawezaje kutumia njia hii kufikia masuala ya
umoja leo? Kwa mfano, katika madhehebu yangu, kwa sasa kuna mgogoro juu ya
wanawake kuwekewa mikono. Vipi kama wale wanaoshadadia uwekewaji mikono
watasema kwamba Mungu ndiye aliyeelekeza msimamo wao, na kwamba Mungu ameweka
mpango kuwa katika baadhi ya sehemu hapa duniani wanawake wawekewe mikono kuwa
wachungaji na maeneo mengine ya dunia hii wasiwekewe? Je, mambo hayo
yanafanana?
a.
Kumbuka kwamba tulipojadili jinsi kanisa la
awali lilipokabiliana na mgawanyiko, uamuzi ulifikiwa wa kuizingatia kazi ya
Roho Mtakatifu? (Angalia Matendo 15:12-13.)
D.
Soma Wagalatia 2:9. Paulo anasema kuwa nini
kilithibitisha njia yake na kilithibitisha kwa msingi gani? (Hatimaye, Paulo anatuambia
kwamba “nguzo” za kanisa la awali zilithibitisha kazi yake. Hata hivyo, utaona
kwamba msingi wa uthibitisho ni “neema aliyopewa” Paulo. Tunachoona ni kwamba
viongozi wa kanisa walikiri mwelekeo ambao Mungu anauongoza.)
E.
Soma Wagalatia 2:10. Utakumbuka kwamba jambo la
kwanza kabisa ni tohara. Je, viongozi wa kanisa wanaomba mabadiliko yoyote
kwenye mafundisho ya Paulo? (Hapana.)
1.
Je, unakumbuka kwamba tangu mwanzoni mwa barua
yake kwa kanisa la Galatia, Paulo amekuwa akijenga hoja juu ya mamlaka ya
mafundisho yake? Sasa anataarifu kwamba Mungu ndiye chanzo cha mafundisho yake
na nguzo za kanisa zinakubaliana naye! Vipi kama nguzo za kanisa lako hazikubaliani
na upande wako katika mgogoro wa kimaandiko?
2.
Unadhani kwa nini viongozi wa kanisa walimwambia
Paulo “awakumbuke maskini?” Kati ya mambo yote ambayo wangeweza kumwomba Paulo,
je, hili linaonekana kama ombi lisilo la kawaida? (Ukosoaji halisi wa
kuhesabiwa haki kwa imani ni upi? Unawaruhusu watu kuendelea kulisha tamaa zao
za ubinafsi. Kuwasaidia watu wengine ni kielelezo cha moyo wa kuwajali. Na kwa
kuongezea, maskini wanaojadiliwa ni Wakristo wa Kiyahudi. Kwa kuwa na Mataifa
wakiwasaidia Wayahudi, kitendo hiki kitasaidia uwepo wa umoja.)
IV.
Kuonyesha
Dhamira/Kusema Ukweli
A.
Soma Wagalatia 2:11-12. Nini kilimsababisha Petro
atangaze msamaha kwenye uamuzi wake wa kuunga mkono mitazamo ya Paulo?
(Ushawishi wa makundi!)
1.
Fikiria migogoro ya kimaandiko unayoizingatia
sana. Kwa kiwango gani uamuzi wako unatokana na kile ambacho watu
wanaokuzunguka wanakifikiria? Kwa kiwango gani uamuzi wako unatokana na kile
kinachofundishwa na Biblia?
B.
Soma Wagalatia 2:13. Ushawishi wa makundi
(makundi rika) una nguvu kiasi gani? (Inaonekana kwamba ni Paulo pekee ndio
anaushinda ushawishi huo.)
C.
Soma Wagalatia 2:14. Changanua hoja ya Paulo. Je,
imejengwa kwenye Biblia? Unaweza kuiweka kwenye kundi gani? (Paulo anajenga
hoja kwamba Petro ni mnafiki! Anabainisha kwamba Petro alikuwa hafuati desturi
za Kiyahudi. Hivyo, itakuwa ni unafiki kwa Petro kuwalazimisha Mataifa kufuata
desturi za Kiyahudi.)
1.
Kwenye migogoro ya kimaandiko, je, tunapaswa
kujenga hoja kama hizo ili kujenga umoja? (Tutakomea hapa kwenye hoja ya Paulo,
lakini katika kifungu kinachofuata anajenga hoja iliyojengwa juu ya Biblia.)
D.
Rafiki, unaichukuliaje njia ya Paulo kwa
mustakabali wa umoja wa kanisa? Kwa nini usiombe kwamba Mungu akusaidie uione
njia madhubuti ya kuleta umoja kwa kanisa?
V.
Juma lijalo: Kuhesabiwa Haki kwa Imani Pekee.
No comments:
Post a Comment