Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(Ayubu 10 & 19, Yohana 1 & 12, Wagalatia 2)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Ayubu anatufundisha nini kuhusu neema na matendo? Sehemu kuu ya neema ni kwamba Mungu anatuokoa, hatuko kwenye nafasi ya kujiokoa sisi wenyewe. Kwa hakika, kisa cha Ayubu kinatuonesha kwamba hatuna uhodari wa kutosha kuweza kukabiliana na Shetani. Tafakari jinsi Mungu alivyoleta utofauti katika maisha ya Ayubu. Tuliona kwamba Ayubu alianza akiwa mtu mkuu na akamalizia kwa kuwa mtu mkuu – lakini yote haya yanatokana na Mungu. Pia tulijifunza kutoka kwa Ayubu kwamba Mungu anatutaka tutende vyema, wakati Shetani ni mchochezi wa maumivu. Hivyo, lengo la torati ya Mungu ni kutusaidia ili tuweze kuishi vizuri. Tunapomtegemea Mungu tunajifungamanisha na Yeye apendaye na mwenye uwezo wa kutubariki. Hebu tuchimbue somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi kuhusu neema!
I. Mkombozi Wetu
A. Soma Ayubu 19:25. Hebu tuangalie muktadha wa kauli ya Ayubu. Ayubu anaendeleaje kwa sasa katika hiki kisa chake? (Soma Ayubu 19:20-21. Ayubu ana hali mbaya sana kiafya.)
1. Kwa nini Ayubu anatoa kauli yake juu ya kuishi kwa Mkombozi [Mtetezi] wake katika muktadha huo? (Ayubu anaamini kuwa Mungu yupo, na kwamba katika hatua fulani Mungu atamwokoa.)
B. Soma Ayubu 19:26-27. Ayubu anawezaje kumwona Mungu “katika mwili [wa Ayubu] wakati “ngozi yake imeharibiwa?” (Lazima hii inarejea imani ya Ayubu kwamba baada ya kufa, ataishi tena, katika mwili na damu. Yote haya yatafanyika mbele za Mungu.)
1. Ayubu pia anasema kuwa atamwona Mungu, na sio mtu “mwingine.” Kuna uwezekano mdogo kwamba Ayubu anafikiri kuwa yeye pekee ndiye atakayemwona Mungu katika siku zijazo, je, unadhani Ayubu anamaanisha nini anapokana kwamba hakuna mtu “mwingine” atakayemwona Mungu badala yake?
a. Je, huwa unajiuliza kwamba “wewe,” kwa uhalisia wako, ndiye utakayekwenda mbinguni? (Nadhani hiki ndicho anachokizungumzia Ayubu. Itakuwa ni yeye, na si sehemu yake nyingine, atakayesimama mbele ya Mungu baada ya kifo chake.)
C. Soma Ayubu 19:28-29. Jambo gani jingine analoamini Ayubu kwamba litatokea baada ya kifo? (Hukumu. Ayubu anasema kuwa anapaswa kuishi huku akitambua habari za hukumu.)
1. Kwa nini ni vizuri – kuishi huku ukitambua kwamba kuna hukumu inakuja?
II. Mungu Pamoja Nasi
A. Soma Ayubu 10:2-3. Hii inaturejesha kwenye mada ya Ayubu: Sistahili yote haya, ninahitaji kusikilizwa ambapo Mungu analeta mashtaka dhidi yangu ili nami niweze kuyakanusha. Ayubu anasema maneno gani ya ziada yanayojenga msingi wa hoja ya marafiki wake wanne? (Kwamba Mungu anawapendelea waovu. Wanakosewa kwa niaba ya Mungu. Hili ni shambulizi kwenye haki ya Mungu.)
B. Soma Ayubu 10:4. Jambo gani linaendelea mawazoni mwa Ayubu linalomfanya aseme maneno haya kwa Mungu? Hii inahusianaje na mada yake na mada ya marafiki wake ambayo tumeijadili hivi punde? (Ayubu anapendekeza njia nyingine ya kuelezea kitendo cha wazi cha Mungu kutokutenda haki – Mungu haangalii mambo kwa namna ile ile wanaonavyo wanadamu. Si haki ya Mungu ambayo ina kasoro, bali ni mtazamo wa Mungu. Kamwe Mungu hajawahi kuwa mwanadamu.)
1. Hii ni hoja ambayo huwa ninaisikia mara zote. Hitimisho langu ni kwamba jambo fulani lina kasoro kwa kuwa sijawahi kupitia uzoefu kama ambao ameupitia mtu ambaye ninamhukumu. Unadhani hii ni kweli? Je, kweli huna uwezo wa kufanya uamuzi sahihi ikiwa hujapitia uzoefu wa mtu unayemhukumu?
C. Soma Yohana 1:1-5. Je, huyu “Neno” ni Mungu? (Ndiyo! Naye Neno “alikuwa “Mungu,” huyo “mwanzo” alikuwako, na “vitu vyote” vilifanyika kwa huyo. Yeye ndiye asili [chanzo] ya uzima.)
D. Soma Yohana 1:10-14. Huyu “Neno” ni nani? (Soma Yohana 1:29. Neno ni Yesu!)
E. Angalia tena Yohana 1:14. Maneno haya yanazungumziaje madai ya Ayubu kwamba mtazamo wa Mungu juu ya maisha yetu una kasoro? Kwamba Mungu haelewi uzoefu wa wanadamu kwa sababu kamwe Mungu hajawahi kuwa mwanadamu? (Kwa dhahiri hilo si kweli katika zama za leo. Yesu “alifanyika mwili” na “akakaa kwetu.”)
1. Kati ya misamiati yote ambayo Yohana angeweza kuitumia kumwelezea Yesu, kwa nini alichagua msamiati wa “Neno?” (Utakumbuka tulihitimisha kwamba tatizo la Ayubu na marafiki wake ni kwamba hawakuelewa kikamilifu kweli zote. Walikuwa wanatizama kupitia kwenye “uakisi hafifu,” au kama inavyobainishwa katika 1 Wakorintho 13:12 kwamba, “kuona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo.” Yesu alikuja kutusaidia ili “tumwone” Mungu vizuri na kwa wazi zaidi.)
2. Je, ingesaidia endapo Ayubu angeweza kusoma vitabu vya injili wakati alipokuwa akiyapitia mateso yake? (Angetambua mustakabali wake kupitia kwa Yesu. Yesu, yeye asiye na dhambi, aliteswa na kuuawa ikiwa ni matokeo ya pambano kati ya Mungu na Shetani. Ayubu aliteseka kwa sababu ya pambano hilo hilo!)
F. Soma Isaya 53:4-7. Hii inatuambia nini kuhusu mateso ya Yesu? (Ayubu anasema, “nateseka isivyo haki.” Yesu aliteseka kwa ajili ya dhambi zetu wote, zikiwezo dhambi za Ayubu.)
1. Tunapopitia mateso, tunapaswa kuwaza [kutafakari] nini?
G. Nataka kurejea katika Yohana 1:5. Ayubu anasema kuwa Mungu haelewi uzoefu wa wanadamu. Kutokuelewa kwa kweli ku wapi? (Kumo ndani yetu. Sisi ni “giza” na tunalo tatizo la kumwelewa kikamilifu Mungu wetu mkuu na mwenye utukufu.)
III. Mungu Anatuokoa
A. Soma Wagalatia 2:11-14. Inaonekana tatizo lililopo ni kwamba Petro alikuwa akila na watu wa Mataifa, lakini kutokana na mashinikizo ya kidini, aliacha. Zingatia zaidi kifungu cha 14. Ni kwa jinsi gani hili ni swali sahihi kabisa kwa Petro? Je, tatizo si kwamba Petro anarejea alikotoka kwa kuishi kama Myahudi? (Hii haileti mantiki kwangu. Ukiangalia kwa undani zaidi, Paulo anaonekana kusema kwamba ikiwa msitari kati ya Wayahudi na Mataifa umefutwa, basi hakuna sababu ya Petro kuacha kula na Mataifa au kwa kuwaambia Mataifa kuwa wanapaswa kuishi kama Wayahudi.)
B. Soma Wagalatia 2:15-16. Kwa mujibu wa kifungu hiki, Paulo anarejea “torati” gani? (Kwa dhahiri inaonekana kuwa ni sheria ya mapokeo inayoshughulikia na mtu unayepaswa kula naye na jinsi unavyopaswa kula.)
C. Soma Warumi 7:6-7. Sheria gani inarejewa hapa? (Sehemu ya Amri Kumi inayozuia “kutamani” (Kutoka 20:17).)
D. Soma Wagalatia 2:17-21. Sababu moja iliyomfanya Yesu atufie ni ipi? (Kutuhesabia haki. “tumesulubiwa pamoja na Yesu” na hivyo “hatuishi tena, bali Krisho anakaa” ndani yetu! Ahadi hii inahusika kwenye torati yote, ya aina yoyote, kwa namna yoyote ile utakayoielezea!)
IV. Mwanzilishi wa Mateso Ashindwa
A. Soma Yohana 12:30-31. Tunapoangalia kisa cha Ayubu na Yesu, ni nani aliyesababisha mateso yote haya? (Shetani.)
1. Yesu anaposema “sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje,” anamaanisha kipindi gani? “Sasa” ni lini?
2. Yesu pia anasema “sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo.” “Sasa” ni lini?
B. Soma Yohana 12:47. Utaona Yesu anasema kuwa hakuja “ili kuuhukumu ulimwengu,” bali kuuokoa. Hii inatusaidiaje kuelewa kauli ya Yohana 12:31 kuhusu kumtupa nje Shetani “sasa” na wakati wa hukumu kuwa ni “sasa?” (Kwa kuwa Yesu anasema kwamba hakuja kuuhukumu ulimwengu, lazima atakuwa anazungumzia jambo lililo nje ya ulimwengu. Nadhani Yesu anazungumzia mazingira kama ambayo tunayasoma katika Ayubu 1:6-7. Kwa kuishi maisha yasiyo na dhambi, kwa kuyashinda madai ya Shetani, kwa kuonesha kwamba katika pambano kati ya wema na uovu Mungu (wema) yuko sahihi na Shetani (uovu) hayuko sahihi, Mungu amemtupa nje Shetani kutoka kwenye baraza la mbinguni na ulimwengu umetoa hukumu juu ya kile kinachoendelea hapa ulimwenguni.)
1. Ni kwa jinsi gani Ayubu anafanana na Yesu? (Wote ni mashujaa wa wema dhidi ya uovu.)
2. Ayubu alishinda. Yesu aliishinda hukumu yote. Kwa nini ni muhimu kwako na kwangu kupitia uzoefu wa “Ayubu?” Ushindi tayari umeshapatikana? (Utakumbuka fundisho la kwanza tulilojifunza kutoka kwa Ayubu ni kwamba lazima tumtumaini Mungu. Kwa nini? Kwa sababu hatuoni vizuri taswira yote. Sina jibu la swali hili zaidi ya kusema, “Sijui kwa nini bado tunaweza kupitia uzoefu wa Ayubu, lakini kumtumaini Mungu ndilo jibu pekee la wazi.)
C. Rafiki, Mungu alishinda na kupata ushindi! Kama ambavyo Ayubu hakuweza kumshinda Shetani, vivyo hivi sisi nasi hatuwezi kufanya lolote bila Mungu. Mungu alifanyika kuwa mwanadamu. Anafahamu vizuri sana jinsi ilivyo kuishi katika ulimwengu uliojaa dhambi. Alikufa kwa ajili ya dhambi zetu na kutupatia uzima wa milele. “Najua ya kuwa Mtetezi wangu yu hai! (Ayubu 19:25.) Rafiki, je, utaipokea zawadi ya Mungu ya kuwa Mkombozi wako na kukupatia njia ya kutokea kwenye huu ulimwengu uliojaa dhambi?
V. Juma lijalo: Tabia ya Ayubu.
No comments:
Post a Comment