Somo La 9 | Vidokezo Vya Tumaini [Mwongozo Wa Kujua Biblia]

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu


(Ayubu 13)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Kaulimbiu tunayoendelea kuiona kwenye masomo haya ni kwamba tunapaswa (lazima) kumtumaini Mungu bila kujali chochote kile kinachotokea. Swali lililopo ni je, “Kumtumaini Mungu ili atende nini?” Tunachokichukulia ni kwamba tunamtumaini Mungu na kwamba atafanya mambo yote kuwa barabara. Ikiwa tunateseka, kamwe hatutapenda kumtumaini Mungu kwamba mambo yatasalia kuwa kama yalivyo au yatakuwa mabaya zaidi, sawa? Sababu moja inayotufanya tumtumaini Mungu ni kwamba mambo hayatuhusu, bali yanahusu pambano kubwa zaidi kati ya wema na uovu. Lakini, ingawa tunaweza kukubaliana kisomi kwamba “mambo hayo hayatuhusu,” tumaini letu ni kwamba Mungu anashinda hilo pambano kubwa ili kwamba wakati fulani katika siku zijazo mateso yetu yabadilike na kuwa furaha. Hilo ndilo “tumaini.” Hebu tuzame kwenye somo letu ili tujifunze zaidi juu ya tumaini!

I.                   Mtazamo wa Ayubu Juu ya Marafikize

A.                Soma Ayubu 13:1-2. Ayubu anafikiria nini juu ya mitazamo ya marafikize watatu? (Wanadhani kwamba wao wana akili zaidi au wana uelewa zaidi ya Ayubu.)

1.                  Ayubu anafikiria nini juu ya uwezo wao kiakili? (Wao wote wana akili, ikiwemo na Ayubu pia.)

2.                  Soma Ayubu 12:3. Katika sura zote mbili, yaani sura ya 12 na 13, Ayubu anatoa kauli ile ile kwamba naye ana akili kama rafikize. Je, hii inakuambia nini kuhusu mtazamo wa Ayubu? (Anadhani kuwa kweli yuko chini ya shambulizi kwenye suala hili. Unachukuliaje mtu anapokuambia katika utatuzi fulani kwamba, “Nimeshinda kwa kuwa mimi ni mwerevu zaidi yako?”)

3.                  Bila shaka hii ni hoja inayojadiliwa ulimwenguni kote kuhusu serikali. Wale wanaodhani kuwa serikali inapaswa kuwa ndogo, wanataka kuachwa peke yao ili waweze kufanya maamuzi yao wenyewe. Wale wanaodhani kwamba serikali inapaswa kuwa kubwa, wanadhani kuwa wanaweza kuisaidia serikali kuchukua maamuzi bora zaidi kwa ajili ya watu wengine. Je, kuna anayedhani kuwa watu wengine wanafanya maamuzi bora kwa ajili yao? (Ninatilia shaka kwamba mtu yeyote anadhani kuwa anapaswa kugeuzia maamuzi anayoyafanya kwa mtu mwingine. Ayubu anasema “Mimi nina akili za kutosha kufanya maamuzi yangu mwenyewe.”)

B.                 Soma Ayubu 13:3-4. Hii ni kauli mbiu ya zamani. Ayubu anaamini kuwa hakutendewa haki, na anataka ahojiane na kujenga hoja juu ya mambo yake mbele ya Mungu. Marafiki wa Ayubu wanadhani kuwa kwa dhahiri Ayubu ni mdhambi, na hiyo ndio sababu anapata mateso. Wanadhani kwamba kitendo cha Ayubu kukataa kukiri hatia yake, na kuendelea kusisitiza kwamba Mungu hamtendei haki, ni kutomheshimu Mungu. Ayubu anaiita mitazamo ya marafikize kuwa ni ya “uongo.” Unadhani marafiki wa Ayubu wanadanganya? (Hadi kufikia kusema kwamba Ayubu anastahili mateso, wanazungumza mambo yasiyo ya kweli. Hata hivyo, naamini marafiki hawa wanadhani kuwa kile wanachokisema sio tu kwamba ni ukweli, bali pia ni muhimu kukisema.)


1.                  Unadhani marafiki wa Ayubu wanafikiria nini juu ya unyofu (uaminifu) wa Ayubu? (Wanadhani kuwa Ayubu anasema uongo kuhusu hatia yake.)

2.                  Je, kuna matumaini yoyote ya kufikia suluhu kwenye huu mjadala ilhali pande zote mbili zinadhani kuwa upande mwingine unasema uongo?

a.                   Je, wao ni, kama asemavyo Ayubu, “matabibu wasiofaa?” (Ikiwa lengo ni kutatua mgogoro, basi wao hawafai chochote kwa jukumu hilo.)

C.                 Soma Ayubu 13:5. Je, hii ni kweli? (Ndiyo. Zingatia jambo hili unapojaribu kumfariji mtu.)

II.                Hoja ya Ayubu

A.                Soma Ayubu 13:6-9. Muda mfupi tu uliopita Ayubu amesema kuwa marafiki wake sio werevu. Je, ni katika eneo gani jingine marafiki wa Ayubu si bora zaidi yake? (Katika Ayubu 13:9 Ayubu anasema kuwa tabia zao si bora zaidi ya tabia yake. Hadhani kwamba wanaweza kuhimili kumwona Mungu kwa karibu. Anadhani kuwa wanajionesha kuwa na utii zaidi mbele za watu kuliko uhalisia ulivyo wanapokuwa wenyewe.)

1.                  Je, huu ndio ukweli kwa kila mtu?

2.                  Unadhani hii inasaidia kwenye hoja ya Ayubu juu ya kutostahili hali hii? (Hii inaonekana kuashiria kwamba Ayubu si mwema kama anavyoonekana kuwa.)

3.                  Utaona kwamba katika Ayubu 13:7 Ayubu anasema kuwa marafiki wake wanajenga hoja “zisizo za haki” na za “udanganyifu” kwa niaba ya Mungu. Je, hilo ni kweli? (Ikiwa kweli kwamba marafiki wa Ayubu wana dhambi za siri na wanaenenda vyema, hii inaonesha kuwa hawaamini kabisa kwamba kweli Mungu anawaadhibu wadhambi.)

B.                 Soma tena Ayubu 13:8. Inamaanisha nini kusema kuwa marafiki wa Ayubu wanamwonyesha Mungu “upendeleo?” Je, wanampendelea Mungu dhidi ya Ayubu?

1.                  Tafakari shtaka hilo. Je, Ayubu na Mungu ni wapinzani? Je, huo ni mtazamo sahihi Ayubu kuwa nao?

2.                  Je, unampendelea Mungu? (Watu wengi ni waasi dhidi ya Mungu.)

3.                  Je, madai ya Ayubu ya upendeleo dhidi ya Mungu yana mashiko (ni mashtaka halali)?

4.                  Je, tunapaswa kuangalia kama tunaonesha upendo wa kutosha kwa watu wengine, au “tuna upendeleo” dhidi ya Mungu? (Mungu anatupenda. Kuwa na “upendeleo” dhidi ya Mungu inamaanisha kwamba pia tunatakiwa kuwa na upendo dhidi ya wale wanaotuzunguka. Ayubu anaanzisha pande mbili za uongo kwa kudai kuwa upendeleo kwa Mungu huonesha ukatili dhidi yake (Ayubu).)

C.                 Hebu turuke mafungu kadhaa na tusome Ayubu 13:13-15. Kwa nini Mungu amwue Ayubu? (Ayubu anaamini kuwa anapingana na Mungu kwa kudai kwamba Mungu aelezee haki ya kile kinachomtokea Ayubu. Ayubu pia anaamini kuwa Mungu ndiye nguvu ya ulimwengu. Kwa kawaida huwa ni hatari kumpa mfalme changamoto. Hivyo, Ayubu anaamini kwamba anaweza kuwa hatarini.)

1.                  Ayubu anamaanisha nini anaposema kuwa “atamtumaini” Mungu hata kama Mungu atamwua?


a.                   “Tumaini” hili linahusianaje na Ayubu kusema kwamba atazitetea njia zake “mikononi mwa Mungu?” (Ayubu harudi nyuma kwenye madai yake kwamba hastahili kuteseka. Anadhani kwamba yuko sahihi, na Mungu hayuko sahihi, kwa kumwacha ateseke. Licha ya hayo, matumaini ya Ayubu kwa haki ya Mungu yataendelea kuwepo hata kama Mungu atamwua kwa kuwa fidhuli.)

D.                Soma Ayubu 13:16. Kwa nini Ayubu anadhani kwamba Mungu hatamwua kwa ufidhuli wake? (Ukweli kwamba Ayubu anatoa wito kwa Mungu ili amtendee haki inaonesha kwamba Ayubu ni mwaminifu kwa Mungu.)

1.                  Je, unakubaliana na mtazamo wa Ayubu? (Ndiyo, haimaanishi kutokuwa mwaminifu kwa kumwangalia Mungu kama suluhisho la tatizo unalotaka kulileta mbele za Mungu.)

E.                 Soma Ayubu 13:17-19. Hebu subiri kidogo! Ayubu anazungumzia kifo chake katika muktadha mwingine. Ayubu hazungumzii Mungu kumwua kwa kutohusiana naye. Jambo gani litasababisha kifo cha Ayubu hapa? (Ayubu anahofu kwamba ugonjwa unaomkabili utaishia kwenye mauti. Kimsingi, ana matumaini kuwa mauti yatamkumba hivi karibuni ikiwa hatathibitishwa. Kwa kuwa marafiki wa Ayubu wanajenga hoja kwamba Ayubu anateseka kutokana na dhambi ya siri, kifo cha Ayubu kitatokana na dhambi hiyo ya siri na hakitahusiana na Mungu.)

1.                  Je, hapa Ayubu anaonesha matumaini? (Ndiyo. Anasema, “Najua nitathibitishwa.”)

F.                  Soma Ayubu 13:20-22. Ayubu anamwomba Mungu mambo mawili. Ni mambo gani hayo? (Anamwomba Mungu akomeshe mateso yake na kisha ayasikilize maombi yake.)

1.                  Je, maombi mawili ya Ayubu ni ya haki? (Ikiwa unakubali kwamba mtu hana hatia hadi atakapothibitishwa kuwa ana hatia, basi Ayubu hapaswi kuwa anateseka kwa ajili ya dhambi yake hadi baada ya kushindwa hoja mbele za Mungu.)

a.                   Kuna kosa gani kwenye hitimisho letu? (Hitimisho letu linachukulia kwamba Ayubu anateseka kutokana na dhambi yake – jambo tunalofahamu kwamba si kweli.)

G.                Soma Ayubu 13:23-25. Tunaweza kujifunza nini kwenye mwendelezo wa imani potofu ya Ayubu kwamba anateseka kwa ajili ya dhambi zake? (Kwamba hatujui vya kutosha jinsi ya kujenga hoja mbele za Mungu. Hatuielewi taswira pana. Ayubu haelewi kwamba anateseka kwa sababu yeye ni mtu mnyofu, sio kwa sababu yeye si mnyofu.)

H.                Soma Yohana 16:33. Yesu amewaambia wanafunzi wake kwamba anaondoka na kwamba watu wengine watataka kuwaua. Wow! Huo ni mzigo mkubwa wa habari mbaya. Yesu anawezaje kusema “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu?” Kwa kawaida kufahamu kwamba mambo ya kutisha yanakuja sio njia ya kupata amani! (Yesu anaendelea, “Lakini jipeni moyo; nimeushinda ulimwengu.” Hapa ndipo Ayubu aliposhindwa. Ayubu anadhani kuwa anatakiwa kumshawishi Mungu kwamba hastahili kuteseka. Haelewi kwamba Mungu anakubaliana naye, Mungu hataki Ayubu ateseke. Ikiwa Ayubu atamtumaini tu Mungu, basi Mungu atatenda mambo yote kwa usahihi.)

I.                   Rafiki, nakuuliza tena, je, utakubali tu kumtumaini Mungu? Kumtumaini Mungu kutakupatia tumaini!


III.             Juma lijalo: Ghadhabu ya Elihu.

No comments:

Post a Comment